Georgie Smith mtoto wa kiume anayepigania kubadili jinsia kuwa mwanamke Tuesday, November 24, 2009 6:22 AM
Mama mmoja nchini Uingereza amewashangaza watu wengi kwa kupigania mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 14 afanyiwe operesheni ya kubadilisha jinsia yake akidai amezaliwa katika umbile la kiume kimakosa. Mtoto wa mama huyo aliyejulikana kwa jina la Georgie Smith inadaiwa alitaka kuwa mwanamke tangia alipokuwa na umri wa miaka miwili.
Kitengo kinachosimamia huduma za afya nchini Uingereza (NHS) kimemtaka Georgie kusubiri hadi atakapovuka atakapofikisha umri wa miaka 18 ndipo aanze matibabu ya kubadilisha jinsia yake kuwa mwanamke.
"Nina umri wa kutosha kujua nini ninataka, nataka kuwa mwanamke", alisisitiza Georgie.
Mama yake Georgie, Carole mwenye umri wa miaka 41, aliilamu NHS kwa kuzuia matibabu ya kubadilisha jinsia ya mwanae mpaka atakapevuka kwani kwa kusubiria mpaka wakati huo mwili wake utakuwa umejijenga na kumfanya aonekane kama mwanaume.
Carole ambaye ni mama wa watoto watatu alisema kuwa Georgie alitaka kuwa mwanamke tangia alipokuwa na umri wa miaka miwili na aliwahi kujaribu kujiua mara mbili akipinga kuendelea kuwa mwanaume.
Alipokuwa na umri wa miaka minane alikiri mbele ya mama yake kuwa anataka kuwa mwanamke kama mtangazaji wa kipindi cha watoto katika luninga Tracy Beaker.
Kutokana na tabia yake ya kujipodoa na kuvaa nguo za kike, Georgie alikuwa akisumbuliwa na wakati mwingine kuzomewa na wanafunzi wenzake tangia alipokuwa shule ya msingi na alipoingia sekondari alikataliwa kuvaa nguo za kike na kumfanya awe anavaa nguo za kiume lakini akiendelea kujipodoa kama mwanamke.
Carole anasema kuwa aliwahi kufikiria kumpeleka Georgie Marekani kuanza matibabu ya kubadilisha jinsia yake lakini hana uwezo wa kulipa gharama za matibabu zinazokadiriwa kufikia dola 30,000.
Miezi michache iliyopita wanafunzi wawili wa kiume wa shule mbili tofauti za kusini mwa Uingereza walirudi shuleni toka likizo wakiwa wamebadilisha jinsia zao kuwa wanawake na kusabisha mjadala mkubwa kuhusiana na kuongezeka kwa idadi ya wavulana wanaotaka kubadili jinsia kuwa wanawake.
http://www.nifahamishe.com/NewsDetails.aspx?NewsId=3604398&&Cat=2