Malezi: Mambo 8 ya kuzingatia ili kuwa baba bora

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Mtandao wa MenCare uliwahi kuwahoji washirika wake 100 wakiwemo akina mama, akina baba, wanaharakati na watafiti katika malezi kutoka nchi 50 kutoa ushauri kwa wazazi wakiume. Mambo manane yafuatayo yalishauriwa kwa akina baba wote wanaohusika moja kwa moja katika maisha ya watoto iwe wanafamilia, walimu, makocha, n.k.

Kama baba, unaweza kuwa mlezi kamili. Unaweza kumpatia mwanao malezi kamili kama mwenza wako afanyavyo. Hivyo akina baba msisite kutimiza majukumu yenu kwa kufanya kazi za kujikimu pamoja na kuwatunza watoto, wenza wenu na wengine ndani ya familia. Usiache imani za kijinsia juu ya malezi ziathiri dhamira na uwezo wako wa kumtunza mwanao, malezi ya mtoto na changamoto zake zimekuwa zikiaminiwa kuwa ni jukumu la mwanamke peke yake jambo ambalo huwanyima wazazi wa kiume nafasi ya kutoa mchango wao katika malezi na makuzi ya mtoto. Tafiti zimeonesha kuwa, ushiriki wa baba kikamilifu katika malezi una mchango mkubwa katika afya na ustawi wa mtoto.

Shiriki sawa na mwenza wako katika shughuli zote za malezi ya watoto wenu. Usiogope kutumia muda wako vizuri na mwanao wa kike au wa kiume na kufanya kazi zote kama vile kunepisha, kupika, kucheza nao na kuwabembeleza wanapolia. Watoto siku zote hukumbuka matendo haya na hivyo kujenga upendo kati yenu na kuzidisha amani kwa familia. Ni vyema kuhamasishana wake kwa waume ili kila mmoja wetu ajione ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya malezi na kutafuta pesa kwa pomoja.

Wajengee wanao uwezo wa kutekeleza majukumu bila kujali mipaka ya kijinsia. Wapende wanao na uwakubali walivyo, usitumie nguvu kuwabadli. Jitahidi kuwapa malezi yenye kuondoa mila potofu na kuleta usawa wa kijinsia katika majukumu kwa wewe kuwa mfano.

Jijengee heshima na upendo kwa watoto wako na siyo nguvu na umangi-meza. Kila mtu hufurahia kupenda na kupendwa na unaweza kupata upendo wa watoto wako kwa kuwapenda na si kwa kuwaonesha mabavu na umangi-meza. Ubabe unaambulia nidhamu ya uoga na sio heshima na utii wa kweli. Hivyo ni vyema kwa wazazi wa kiume kuonesha upendo, heshima na uwajibikaji kwa watoto, mwenza wako na familia kwa ujumla. Kumbuka kwa kufanya hivi unajenga msingi wa tabia za mwanao unayemtaka kwa miaka kadhaa ijayo. Yakupasa kuishi kama mfano wa kuigwa kwa watoto wako kwa kupitia malezi unayowapa, matendo unayotenda kwa familia, jinsi unavyotatua migogoro baina yako na mwenza wako, lugha unayotumia n.k. Mabinti na vijana wakimuona baba yao katika hali ya utu, heshima, asiyetumia ukatili na mwenye mahusiano yenye usawa huiga na kurithisha usawa katika vizazi vyao.

Kuna kuteleza na kuanguka katika kutekeleza jukumu la malezi. Usikatishwe tamaa na chanagamioto unazokumbana nazo au makossa yanayojitokeza katika jitihada zako za kulea. Kulea hakujawahi kuwa rahisi lakini tunajifunza siku hadi siku.

Kuwa baba ni zaidi ya kucheza na mwanao. Kuwa baba na kutekeleza jukumu la malezi huanza mtoto angali tumboni. Huhusisha ushiriki wako katika kutunza mimba, kumsaidia mwenza wako katika kipindi hiki na kumuonesha upendo kwa kumsaidia majukumu ya malezi. Ingawa kucheza na mwanao ni muhimu, vivyo hivyo kushiriki kazi za nyumbani na malezi ya watoto, hujenga ari ya kujituma na kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto wa kiume na kumjengea mtoto wa kike uwezo wa kujitegemea na kujiamini. Tafiti zimeonesha kuwa mabinti waliolelewa na baba wanaojihusisha na shughuli za nyumbani wana nafasi kubwa ya kuwa wachapakazi na kujikita katika ajira zenye maslahi makubwa.

Mazungumzo na mijadala ya wazi kati yako na mwenza wako ni nguzo ya malezi. Mara zote zungumzeni kuanzia mambo madogo na hata mipango mikubwa katika familia. Namna hii mnawasaidia watoto wenu kujua umuhimu wa kufikia maamuzi kwa mazungumzo. Kukubaliana na kutokukubaliana.

Wasikilize watoto wako, jadiliana nao na wawezeshe kupitia sauti zao. Jambo muhimu ambalo akina baba wengi wanapaswa kuzingatia ni kuwasikiliza watoto wao kwa makini. Kuyapa uzito mawazo yao na kushirikiana nao katika kufanya maamuzi. Walee wanao katika namna ya kujihisi kuwa na uwezo wa kupambana na changamoto na kujiskia wamewezeshwa. Ukiwafunza wanao kuwaheshimu watu wote na kuwatendea usawa basi unawajenga kuwa wanastahili kesho bora yenye fursa na usawa.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom