Malezi - Anza kumjengea mwanao tabia ya kujitegemea mapema

Sema Tanzania

JF-Expert Member
May 18, 2016
251
465
Wakati mwingine, wazazi tunapata wasiwasi juu ya maisha ya baadae ya watoto wetu kwamba watakuwa na maisha ya aina gani? Watakuwa watu wazima wa namna gani? Hivi watafanikiwa kielimu? Biashara? Kimsingi, sisi wazazi ndiyo watu pekee wenye jukumu la kuhakikisha kuwa tunalea watoto wetu katika mienendo ambayo tunaona ni mema kama usemi wa wahenga usemao ‘mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo’.

Tabia ya kujitegemea kwa kiasi kikubwa huja kutokana na msukumo wa wazazi na namna makuzi yanavyotolewa. Anza kwa kumpa fursa mtoto kujifanyia vitu au mambo madogo-madogo kadiri anavyozidi kukua. Aanze kujua dhana ya kunawa mikono peke yake kuanzia umri wa miaka mitatu au mapema zaidi. Mueleze kwa nini kunawa mikono ni muhimu. Mfunde kuoga pekee yake mapema. Aanze kufua nguo nyepesi kama kanga au shati la shule mapema. Taratibu ajue akitoka shule pana kazi kadha wa kadha zinazomsubiri. Mtie moyo kwa kumsifu pindi anapojaribu kujifanyia jambo mwenyewe pasi kuambiwa. Hii itamfanya aendelee kujihusisha na jambo hilo mara kwa mara na mwishowe atavuna uzoefu katika hilo.

Heshimu mawazo ya mtoto. Watoto wetu hupenda sana kutoa maoni yao kama sehemu ya utatuzi wa changamoto za siku hata siku katika familia zetu. Zungumza na mtoto wako, kubaliana naye – lakini mpe sababu kwa nini unajua anachoshauri hakiwezekani. Unamjengea uwezo wa kusimama pekee yake katika hoja. Mpe fursa ya kuchagua nguo anayopenda kuvaa – haya mambo madogo yanatafsiri ya uhuru wa kuamua. Huku nako ni kukuza dhana ya kujitegemea.

Upo ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya wazazi huwafanyia watoto wao kila kitu majumbani mwao. Dhana ya kwamba wanawapenda sana. Lakini swali la kujiuliza ni kuwa je, utaishi na watoto wako maisha yao yote? Mapenzi kwa watoto ni pamoja na kuwaandalia kesho yao kupitia kazi kama kufagia nyumba, kufuta vumbi madirishani, kuosha vyombo, kutandika kitanda, kujipangia ratiba ya siku n.k

Mpe usaidizi wa masuala ambayo dhahiri ni magumu kwake. Namna ya kukabiliana na msiba, changamoto za kielimu, namna ya kujenga uhusiano bora wa kirafiki na watoto wengine, kuwaheshimu wakubwa, n.k. ni baadhi ya mambo ambayo yanahitaji ukaribu na miongozo ya kutoka kwako mzazi. Mtambulishe kwa ndugu wa familia tandaa – apate kujenga mahusiano na shangazi zake, wajomba zake, bibi na babu pasi wewe kuingilia-ingilia. Awasiliane nao binafsi kadiri anavyokua

Bahati mbaya sana wazazi hasa wa mijini tunatumia muda wetu mwingi kazini na hata tunaporudi majumbani hatutaki watoto wetu wamsaidie mfanyakazi wa nyumbani kazi. Wazazi wengine, mtoto akianza kupata marafiki anaambiwa akome. Ataishi vipi dunia hii bila kuhusiana na binadamu wengine? Uzoefu wa kuwa na marafiki – tabia za watu mbalimbali na mambo ya namna hii hawezi kupata ndani ya nyumba yako. Malezi ya watoto ni jambo lenye kuhitaji subira na uvumilivu. Muamini mtoto. Hatokuangusha.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia kurasa zetu wa Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org.
 
Mimi nakumbuka wakati nakua nilikuwa nauliza sana maswali, mengine ya kipuuzi sana lakini mama yangu alikuwa akiyajibu yote kadiri anavyo weza.
Hata lile swali la watoto wanatoka wapi nilijibiwa bila kudanganywa.
 
Toka nikiwa mdogo baba alinijengea tabia ya kujitegemea. Alikua ananipa pesa naenda kulipa ada mwenyewe bank. Siku naenda kuanza form one nilienda mwenyewe mara naogopa kumwambia konda anishushe basi napitilizwa hivyo hivyo mpaka nikazoea.

A level nienda mwenyewe zote hizo zilikua day. Kununua vitu kama viatu vya shule begi ananipa pesa mwenyewe naenda karume kuchukua. Maisha yangu yote sijawahi kupelekwa shule na mzazi wala school bus.

Chuo niliaply vyote mwenyewe Hadi bodi ya mikopo na nikaenda mwenyewe.

Nimesafiri mwenyewe na kuvuka boda kadhaa. Najua kero za askari wa uhamijia ( kutokana na asili yangu) na siwaogopi. Wakati nimemaliza form 4 sina kadi ya kura nina kitambulisho cha shule tu Nilishawahi kusumbuliwa na migration officer pale mbeya akataka aone nywele zangu kama ni za kibantu ndo aprove kama mimi mtanzania nikamgomea akasema nishuke nikagoma akaepa zake.

So nimezoea kua Independent hii mpaka leo hii nimekua mtu mzima nina confidence ya kwenda sehemu yoyote kufanya chochote.

Anyways wazazi acheni kulea watoto kimayai mayai. Mnawaharibu

Anyways hii independence imenifanya nigombane na wanaume wengi kisa wanataka waanze kunipangia maisha akati mwanaume alienizaa hajawahi kunipangia chochote.

Sent From Galaxy S20 Ultra
 
Back
Top Bottom