DOKEZO Malalamiko ya vibarua (Freelancers) wanaodai malipo yao dhidi ya Kampuni ya Honora Tanzania PLC (Tigo Tanzania)

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
Rejea kichwa hapo juu, kwa niaba ya Freelancers wote Tanzania wanaofanya kazi chini ya Tigo Tanzania inayoendeshwa na kampuni mama Honora Tanzania PLC pamoja na kampuni shirika zinazosimamia Wafanyakazi huru (FREELANCERS) tunapenda kuwasilisha malalamiko yetu ya muda mrefu katika ukiukwaji mkubwa wa malipo tofauti na ulivyoainishwa na mkataba wa ulipaji wa malipo ujulikanao kama SONARA.

Kawaida FREELANCER ambaye kazi yake kubwa ni kusajili line anafanya kazi kuiwakilisha TIGO TANZANIA ambayo ni Brand name chini ya Kampuni ya HONORA TANZANIA PLC katika kusajili wateja wapya line sawasawa na muongozo wa TCRA na malipo yote ya FREELANCER yanatokana na kazi anayoifanya kama ilivyoanishwa katika mkataba wa malipo uitwao SONARA.

Aidha Mkataba wa malipo ya SONARA unaeleza yafuatayo:

1. UPFRONT COMMISSION. Freelancer atalipwa Tsh 500 pale tu atakapokamilisha kumsajili mteja line na line hiyo kuwekewa vocha ya Tsh 1000 na kuanza matumizi kwa kununua kifurushi cha kawaida chenye dakika na SMS basi freelancer atapewa upront bonus ya hapo kwa hapo ya Tsh 500 na hili mara zote limetekelezwa na kampuni kama mkataba unavyosema, kikamilifu.

2. UPFRONT DATA COMMISSION. Vile vile mkataba wa SONARA umeainisha kwamba FREELANCER atalipwa malipo ya hapo kwa hapo ya 50% ya kifurushi cha DATA anachojiunga mteja, yaani mteja akinunua Vocha ya Tsh 5000 na kujiunga na Kifurushi cha Tsh 5000 cha DATA basi Freelancer atapata Tsh 2500 kama UPFRONT DATA COMMISSION, Lakini hili lilikua halifanyiki na hivyo kwenda kinyume kabisa na mkataba wa makubaliano wa malipo kama ulivyoainishwa katika SONARA.

3. PAYMENT CYCLE. Hapa sasa ndipo ulipo msingi wa malipo ya Freelancer na freelancer wa Tigo Tanzania kama ilivyoainishwa na Mfumo wa malipo ya SONARA anatakiwa kulipwa katika CYCLE au MZUNGUKO wa AWAMU 4.

- Awamu ya kwanza (MONTH 0), Freelancer analipwa katika siku alizomsajilia mteja line kabla ya tarehe 25. Kwa kawaida malipo ya mzunguko huu wa kwanza huangalia line alizozisajili freelancer kuanzia tarehe 26 ya mwezi husika hadi tarehe 25 ya mwezi unaofuatia na freelancer hulipwa kulingana na matumizi ya vocha zilizotumika na mteja/wateja katika

Katika mkataba wa SONARA mzunguko huu umeandikwa kama (MONTH 0: au Mwezi 0) ambapo Freelancer anatakiwa kulipwa commission ya 60% (Asilimia 60) ya matumizi yote anayoyafanya mteja kwa kile tunachokiita (REVENUE SHARE) au Mgawanyo wa malipo ambapo FREELANCER anapaswa kulipwa asilimia 60 ya matumizi yote ya vocha ya mteja/wateja aliowasajili kama nilivyoainisha hapo juu

Hivyo, kwa kadri mteja anavyonunua vocha na kujiunga na vifurushi na huduma mbalimbali za Tigo basi ndivyo kadri pato la Freelancer linakua na kuongezeka na mwisho wa mwezi kulipwa commission ya 60% kwa kadri ya mteja alivyotumia vocha kama ilivyoanishwa kwenye mkataba wa malipo wa SONARA.

- Vilevile katika mizunguko mingine mitatu iliyobaki ambayo kwenye mkataba wa malipo ya SONARA umeanishwa kama (MONTH 1, MONTH 2 na MONTH 3) Freelancer anatakiwa kuendelea kulipwa 25% ya matumizi yote ya vocha anazotumia mteja/wateja aliowasajili line kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa malipo ya SONARA.

- Vilevile Tigo Tanzania wameweka bonus mbalimbali kulingana na mauzo ya line atakazozisajili freelancer, kama ifuatavyo:

Laini 50-99 zilizofanya usajili kikamilifu freelancer atalipwa Tsh 30,000.

Laini 100-149 zilizofanya usajili kikamilifu freelancer atalipwa Tsh 50,000.

Laini 150-299 zilizofanya usajili kikamilifu freelancer atalipwa Tsh 100,000

Laini 300 na kuendelea zilizofanya usajili kikamilifu freelancer atalipwa Tsh 200,000

Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na ukiukwaji mkubwa sana wa malipo kama ulivyoanishwa na mkataba wa malipo ya SONARA, bila kuletwa kwa mfumo mpya wa ulipaji wala kuwa na taarifa rasmi kwa freelancers.

Baadhi ya ukiukwaji huo ni kama ifuatavyo:
1. Bonus za papo kwa hapo za data (UPFRONT DATA COMMISSION) Bonus hizi ziliondolewa na kampuni bila taarifa rasmi kwa freelancer na hazijaendelea kulipwa kwa zaidi ya miezi minne mfululizo.

2. Kumekuwa na ukiukwaji katika kulipa freelancer mizunguko minne ya malipo kama nilivyoeleza hapo juu ambapo Freelancer anapaswa kulipwa asilimia 60 katika (MWEZI 0) na asilimia 25 kwa miezi mitatu inayoendelea (MWEZI 1, MWEZI 2, MWEZI 3) lakini kwa miezi kadhaa malipo yaliyotolewa ni ya mwanzo tu ya asilimia 60 yaani malipo ya (MWEZI 0) na malipo ya miezi mingine mitatu hayatolewi kwa ukamilifu na hakuna taarifa yoyote kutoka kwa viongozi na wala hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kuhakikisha Freelancer wanapata malipo kama ilivyoainishwa.

3. Vilevile kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa malipo katika mwezi wa 8 mwaka 2023, ambapo Freelancers wengi walifanya kazi wakijituma na kutumia mitaji yao kununua line na kusajili wateja kwa kuwapa ofa mbalimbali kama vocha za bure na line za bure kwa matazamio ya kuongeza mauzo ya line katika kampuni na kujiongezea commission ya mwisho wa mwezi ya 60% lakini commission hizo zimetoka kinyume na makubaliana ya mkataba wa malipo wa SONARA.

Mkataba umeweka wazi kwamba Italipa line zote zilizosajiliwa kikamilifu na kuwekewa vocha kuanzia Tsh 1000 na kuendelea kwa mara ya kwanza na pia Italipa vocha na matumizi ya mteja (REVENUE SHARE) kwa kadri ya matumizi ya mteja.

Kitu kilichowashtua wengi katika mwezi huu wa 8 ni kwamba malipo yameenda tofauti kabisa na mkataba.

Mfano: Mtu aliyesajili line 20 na zote zimewekewa vocha ya Tsh 1,000 na kukamilisha usajili (QGA) kwa hesabu za haraka haraka mtu huyu alipaswa kulipwa Tsh 12,000 kwa line 20 zilizoweka vocha za Tsh 1,000 hapa hatujapiga hesabu za vocha ambazo ameendelea kuweka mteja (kwa sababu hatuna taarifa za matumizi ya vocha za wateja) lakini cha kushangaza mtu ambaye alitakiwa kuwa na uhakika wa kupata Tsh 12,000 katika line alizosajilia wateja wake 20 na kuhakikisha amewawekea vocha za Tsh 1000 anapewa commission ya Tsh 700 au Tsh 900 au Tsh 1000 hii imewaumiza Freelancers wengi na kuwakatisha tamaa.

Je, tunajiuliza sisi kama Freelancers ni hesabu gani imetumika kulipa au ni mfumo gani wa malipo ulioacha kulipa asilimia 60 ya vocha za Tsh 1,000 zilizowekwa na wateja wetu tulipowasajilia line kwa mara ya kwanza ?

Aidha, sisi kama Freelancers tulijaribu sana kupiga kelele kwa umoja wetu na kuwataka viongozi kupitia malipo ambayo hayakuwa yameakisi mkataba wa malipo ya SONARA yaliyofanyika kinyume na utaratibu mnamo tarehe 30 mwezi wa 8 mwaka 2023.

Baada ya malalamiko ya karibu siku mbili mfululizo viongozi wetu walikuja na majibu kwamba tumefanya udanganyifu ambao wanatushtumu sisi Freelancers tumesajili line ambazo hapo baadae zilifanya matumizi makubwa ya vocha na kuhamisha DATA (MB).

Je, kazi ya freelancers inaendelea mara baada ya kusajili line? Au tunapaswa kusimamia na kuratibu matumizi ya wateja wetu?

Majibu ya maswali haya ni rahisi kwani jukumu zima la Freelancer ni kumsajili mteja line na kumshawishi aendele kutumia huduma mbalimbali zilizopo katika menu halali ya Tigo ikiwa ni pamoja na kununua vifurushi vya Internet, vya Tsh 10,000 na Tsh 20,000 na Tsh 50,000 na kuendelea kwa matazamio kwamba mteja huyu akitumia huduma zenye kuhitaji matumizi makubwa ya vocha basi commission ya freelancer itaongezeka.

Je, ni kosa la jinai kumshawishi mteja kutumia vifurushi vya Tigo? Ili kuongeza mauzo katika kampuni na vilevile kujiongezea malipo kama Wafanyakazi huru tunaotegemea kulipwa commission kulingana na faida mteja anayoingizia kampuni.

Je, kwa nini sasa viongozi wetu wanakuja na majibu rahisi kwamba line tulizosajili zimefanya matumizi makubwa ya vocha na data au kununua vocha na data kwa wingi.

Je, sisi kama Freelancer hatupaswi kulipwa pale wateja wanavyofanya matumizi makubwa ya vifurushi?

4. Vilevile, ukiukwaji mkubwa umejitokeza katika tarehe za kufunga hesabu za malipo na tarehe za malipo halisi, aidha jumbe zilizotumwa kwa Freelancers wote Tanzania zinaonyesha malipo yamefanyika mnamo tarehe 23 mwezi wa 8 mwaka 2023 kinyume na utaratibu kwani kazi zote za kusajili hufungwa tarehe 25 ya mwezi husika na malipo kufanyika Kuanzia tarehe 27 mpaka tarehe 29 ya mwezi husika.

Swali la kujiuliza, kwa nini jumbe zinakuja kwamba malipo yetu yote yamekamilika tarehe 23 mwezi wa 8 mwaka 2023 huku wote tumepokea malipo ya commission kwa awamu mbili yaani tarehe 30 mwezi wa 8 mwaka 2023 na baada ya malalamiko ya watu kutokuridhishwa basi wakaongeza malipo mengine kiduchu tarehe 2 mwezi wa 8 mwaka 2023.

Je, kama kampuni kuna malipo mara mbili katika mwezi ? Au ni mkataba upi wa malipo uliofuatwa kulipa Freelancers mara mbili tena katika mara zote mbili za malipo kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa huku ikiwaacha mamia ya Freelancer wengine kutokupata malipo kabisa.

Mwisho sisi kama Freelancers wa Tigo Tanzania tunaofanya kazi chini ya kampuni shiriki zinazoshirikiana na HONORA TANZANIA PLC tunaomba kutolewa tamko na Makao Makuu ya Tigo Tanzania ndani ya masaa 24 toka kupokelewa kwa waraka huu kwani maisha ya maelfu ya vijana wapambanaji yametolewa katika ramani kutokana na ukiritimba katika malipo ulienda nje ya mkataba wa malipo kama ulivyoainishwa katika mkataba wa malipo wa SONARA.
 
Wanasema mlikuwa mnaiba data na kuuza kwa vifurushi kinyume na utaratibu wa biashara! Hili lina ukweli wowote?
 
Back
Top Bottom