NMB Foundation leo imefungua rasmi dirisha la pili wa ufadhili wa masomo na usimamizi kwa mwaka 2023/24 kwa Wanafunzi wanaojiunga na Vyuo Vikuu kupitia Programu ya NMB Nuru Yangu Scholarship and Mentorship ambayo itafadhili Wanachuo 65 mwaka huu na 65 wa mwaka jana kwa kiasi cha Sh. Bilioni 1.
Ufadhili huo unatolewa kupitia Asasi ya Kiraia ya NMB Foundation iliyo chini ya Benki ya @nmbtanzania ambayo imejikita kusimamia na kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Sekta za Kilimo, Elimu, Afya, Mazingira na Ujasiriamali…. kwa mwaka jana pekee ilifadhili Wanafunzi 65 ambao hadi sasa wanaendelea na masomo katika vyuo vikuu mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa dirisha la maombi linaloanza Septemba 15 hadi Oktoba 8, 2023, Meneja Mkuu wa NMB Foundation, Nelson Karumuna alitaja sifa za Waombaji kuwa ni ufaulu wa kidato cha sita wa daraja la kwanza pointi 3 hadi daraja la kwanza pointi 7, pia kwa Wanafunzi wenye mazingira magumu na wenye changamoto.
“Ufadhili huu ambao unaenda katika maeneo ya ada, nauli, posho, stationary, mafunzo ‘field’ na laptop, unatolewa kwa Wanafunzi wanaojiunga chuo katika fani za hesabu na takwimu, biashara, uchumi, teknolojia, habari na mawasiliano, uhasibu, uhandisi, mafuta na gesi, sayansi pamoja na udaktari"
“Mwaka huu tutafadhili wanafunzi 65, hivyo kuifanya NMB Foundation kuwa na wanafunzi 130 hadi Mwaka wa Masomo wa 2023/24 utakapoanza, tunawahamasisha Watanzania wote kufikisha taarifa hizi kwa Wanafunzi waliomaliza ‘form six’ mwaka huu ambao wanajiandaa kujiunga Vyuo vikuu, kutembelea tovuti yetu ya
www.foundation.nmbbank.co.tz wajaze fomu kwa usahihi ili kuepuka makosa yanayoweza kuwatoa kwenye mchakato wasomi wenye vigezo,” alisema Karumuna.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation, Bi. Ruth Zaipuna, aliweka msisitizo kauli ya Meneja Mkuu wake akiwataka waombaji wahakikishe wanajaza fomu zao kwa usahihi, ili kuepuka makosa kama yaliyochangia kutopata Wanafunzi 100 waliowahitaji mwaka jana badala yake wakapata 65 tu.