Makala: Tanzia: Mwana mapinduzi Ernesto Cardenal

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Kwaheri compañero Ernesto Cardenal

-Mwana mapinduzi aliyekuwa tayari kutokubaliana na Kanisa kusimamia alichokiamini

NA MOHAMMED ABDULRAHMAN

Maisha yake yote alijitolea walio wengi, watu wavtabaka la masikini. Alifahamika kama kasisi wa kikatoliki, mshairi na mwanasiasa. Alama yake kubwa ilikuwa ni kofia nyeusi aina ya Beret, ambayo kwa wakaazi wa Amerika Kusini ni alama ya mwanaharakati mwenye fikra za kimapinduzi. Huyo hakuwa mwengine, ni Mwana mapinduzi kutoka Nicaragua, taifa la Amerika Kati, Ernesto Cardenal Martinez aliyefariki dunia hivi karibuni Machi mosi.

Cardenal alizaliwa kutokana na familia tajiri ya kibwanyenye , mtu aliyegeuka msomi na sauti ya mapinduzi ya wanicaragua yalioongozwa na chama cha ukombozi. Alikuwa mfuasi wa theolojia ya ukombozi, iliochanganyika na falsafa ya Marx ikipigania haki ya jamii ili kuwawezesha walio masikini, tabaka la pangu pakavu.

WaSandinista wakiongozwa na Chama cha Sandinistas cha Ukombozi wa Taifa –FSLN, walitawala kwanza 1981 hadi 1990 na utawala wao ulikuwa mfano wa kuigwa baada ya Cuba, panapohusika na kupambana na ujinga kwa kufanikisha kampeni ya kujua kusoma na kuandika na kuwekeza zaidi katika huduma ya afya na usawa wa jinsia.

FSLN kilifanikiwa kuwashinda waasi wa Contras, kundi lilioundwa 1981 , kugharimiwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na Shirika la Ujasusi la Marekani-Cia, wakati wa utawala wa Ronald Reagan, kuitia msukosukoserikali ya Sandinista.

Mapinduzi hayo yaliotukuzwa na wafuasi wa mrengo wa kushoto takriban sehemu nyingi duniani yakaanza kwenda kombo. Kiongozi wa Nicaragua Daniel Ortega akaanza kulewa madaraka na kusahau malengo ya Wasandinista waliyoyapigania na kuamua kuchukua silaha kupambana na utawala wa dikteta Anastasio Somoza, waliyempindua 1979.

Safu ya usoni kumpinga Ortega na kukosoa vikali kupotea dira kwa FSLN alikuwa Kasisi Ernesto Cardenal. Cardenal aliyeyaunga mkono Mapinduzi na kuteuliwa Waziri wa utamaduni katika serikali ya kwanza ya Wasandinista, pia alitafautiana na Kanisa Katoliki lililomtenga na Pope wa wakati ule John Paul II ( Yohanna Paulo wa pili ) kuwapiga marufuku makasisi na viongozi wengine wa Kanisa kutoshika nyadhifa zozote za kisiasa.

Hasira za Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki dhidi ya Cardenal zilidhihirika wakati Papa alipoizuru Nicaragua 1983. Alipochutama. Alipiga magoti kutaka kumbusu mkono, Papa alimnyooshea kidole ishara ya kumuonya na akawambia,” unapaswa kujirekebisha.” Ulikuwa mwaka ule ule 1983, baada ya ziara hiyo ambapo Cardenal alisimamishwa shughuli zote za ukasisi. Adhabu hiyo ikamkumba pia ndugu yake Fernandoaliyekuwa Waziri wa Elimu.

Theolojia ya ukombozi ilianza Amerika Kusini mnamo miaka ya 1950 na mwanzoni mwa 1960, kuzpigania haki za masikini. Kanisa likikosolewa vikali kwa kile kilichoonekana ni kushirikiana na tawala za Kidikteta au kunyamaza kimya wakati wa madhila yaliyoukumba umma katika nchi mbali mbali za Amerika Kusini na Kati.

Cardenal hakukubaliana na msimamo wa kwamba kanisa lijitenge kabisa na siasa . Aliamini kwamba siasa na dini ni sehemu ya maisha ya binadamu na ni jukumu la Kanisa kusimamia haki popote inapokandamizwa, kwani waumini ni watu na wao ndio wenye kuunda taifa. Kwa maneno mengine pamoja na kwamba dini haipaswi kuingizwa moja kwa moja katika mwenendo wa kisiasa, lakini inasimama kuwa sawa na darubini kuhakikisha haki inatendeka. Amerika Kusini ndilo eneo lenye waumini wengi Wakatoliki duniani.


Miaka mingi baada ya kupeyana mgongo na Ortega, kujiuzulu uwaziri, kutokuwa tayari kushika wadhifa wowote wa kisiasa na kujitenga na Wasandinist 1987 , mwana mapinduzi huyo aliendelea kushika uzi wake ule ule ule kwamba wapiganaji hao wa zamani wameugeuza uongozi wa taifa hilo kuwa mali ya chama badala ya wananchi. Cardenal alianza kuziona dalili na mapema na hasa Ortega aliporudi tena madarakani 2006 baada ya muda mrefu kufuatia kushindwa na Violeta Barrios de Chamorro katika uchaguzi wa 1990.

Ortega alipigania kwa kila njia kurudi tena madarakani akisaidiwa na ndugu yake Humberto Ortega aliyekuwa Waziri wa ulinzi katika serikali ya kwanza ilioongozwa na pia ya Chamorro. Kutokana na hayo Cardenal na kuonya juu ya hatari ya Nicaragua kuelekea kwenye kile alichokiita, udikteta wa kifamilia. Niliyakumbuka maneno hayo ya tahadhari ya Comrade Cardenal 2016 , pale Rais Ortega alipomteuwa mkewe Rosario Murillo kuwa mgombea wake mwenza na akawa Makamu wa Rais baada ya mumewe kuchaguliwa kwa muhula wa tatu.

Alisisitiza kwamba Wanicaragua walichokipigania ni “Jamhuri ya Kidemokrasi” na kuuasa upinzani kwamba kuzungumza na Oretega hakutakuwa na maana bali ni kupoteza wakati. “ huwezi kuzungumza juu ya demokrasia na mtu asiyeiheshimu na kuidhamini.” Utawala wa Sandinista ulihakikisha unamyamazisha na hata alipotimia umri wa miaka 90, siku hiyo ilisherehekewa kwa hafla maalum nchini Mexico, alikoishi na kusoma alipokuwa kijana.

Ilikuwa Februari mwaka jana 2019 pale Papa Francis ambaye Cardenal aliuunga mkono msimamo wake , alipoiondoa amri ya kumpiga marufuku mfuasi huyo wa theolojia ya mapinduzi. Ilikuwa hatua kubwa kwake. Amefariki akiwa amepatana na Kanisa lililomrudishia hadhi yake kama kasisi. Lakini ameiaga dunia, akiendelea kuupinga utawala Ortega , lakini akisimama kidete kusimamia maadili na malengo ya mapinduzi ya Sandino. Kujitoa kimasomaso, wapinzani wake walitangaza siku tatu za maombolezi, kuuenzi mchango wake wakati wa ukombozi, ingawa kuna wachache walioendelea kushambulia wakimtaja kuwa msaliti.

Kifo cha Kasisi Cardenal kilifuatiwa siku nne tu baadaye na kile cha mwanadiplomasia mashuhuri kutoka Peru na Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Javier Perez de Cuellar. Mwanadiplomasia huyo , alihudumu nafasi ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mihula miwili hadi Desemba 1991. Kabla ya hapo aliokuwa naibu Katibu mkuu anayehusika na masuala maalum ya kisiasa. Alikuwa mgombea wa maridhiano aliyekubaliwa kujaza nafasi ya Kurt Waldheim kutoka Austria alipomaliza muhula wake wa pili katika kinyanganyiro dhidi ya mgombea aliyesimamiwa na Afrika na kuungwa mkono kwa nguvu zote na mataifa ya Ulimwengu wa tatu Dr Salim Ahmed Salim wa Tanzania.Ulikuwa ni wakati wa mvutano wa vita baridi na hata baada ya duru 16 za kupiga kura maridhiano hayakuweza kupatikana.

Marekani chini ya utawala wa Ronald Reagan, ilitumia kura ya turufu kumuwekea kikwazo Dr Salim na China ikampinga Wadheim na ndipo Perez de Cuellar alipopitishwa baadaye akiwa mgombea wa maridhiano. Mwanadiplomasia huyo na pia waziri mkuu wa zamani anakumbukwa kwa kufanikisha kupatikana suluhisho lililomaliza vita kati ya Iraq na Iran 1988 ,mkataba wa amani nchini El Salvador, kuondoka majeshi ya uvamizi ya Urusi nchini Afghanistan na kusimamia mchakato uliopelekea Uhuru wa Namibia kutoka Afrika Kusini. Alifariki mjini Lima akiwa na umri wa miaka 100.

Taarifa ya kifo cha Ernesto Cardenal aliyeaga dunia mjini Managua tarehe 1 mwezi huu wa Machi akiwa na umri wa miaka 95, ilipokelewa kwa masikitiko makubwa . Miongoni mwa maandishi yake yakuvutia yakiwemo mashairi, ni kitabu nilichokisoma binafsi alichokipa jina “ Nchini Cuba”, ambapo anasimulia mazungumzo yake na vijana wafanyakazi wa sekta mbali mbali aliokutana nao, huku akijiuliza Cuba leo ingekuwa wapi pindi Marekani isingeiwekea vikwazo?


Atakumbukwa kuwa mwadilifu aliyewakosoa wale wasio kuwa Tayari kukosolewa.


Ernesto Cardenal ameondoka duniani, akiwa mmoja wa mashujaa, akijiunga na kundi la wana mapinduzi wakubwa wa Amerika Kusini, wajina wake Ernesto Che Guevara, Fidel Castro, Hugo Chavez na Salvador Allende.


Adios y Descanse en Paz Camarada Ernesto Cardenal, ( Kwaheri na Upumzike kwa Amani Comrade Ernesto Cardenal ) .


Chanzo:Raia Mwema

Baruapepe:mamohamed55@. hotmail.com


IMG-20200313-WA0032.jpeg
IMG-20200313-WA0033.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nimevutiwa sana na Ushupavu wake Asante Muandishi wa Rai Bw.Mohamed Abdulrahman... Nina-Report uzi huu uvushwe kule Idara ya Historia. SIJUI kama Kizazi hiki kutatokea Mashujaa wa namna hii...
Mwanzoni tuliwaona sasa hivi....
Tuanze na hawa...
1.Polepole
2.Prof.Palamagamba Kabudi.
3.Prof.Bashiru Ally
4. Dr Slaa
5. Kitila Mkumbo
6. Zitto

.LIST NI NDEFUU

Mpaka sasa
Tundu Lissu anakaribia japo kapita JARIBIO baya kabisa.

RIP Mawazo Aphonce
#Bringback Saanane
#Bringback Azory Agwanda nk

Cc. Anna Mghwira
 
Back
Top Bottom