Majonzi mazito | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Majonzi mazito

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Jan 19, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jan 19, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,613
  Trophy Points: 280
  Pinda: Ni vigumu kupata mbadala wa Regia
  [​IMG] Makinda: Alikuwa mtu wa kuthubutu
  [​IMG] Mbowe: Alikuwa tunda la Chadema  [​IMG]
  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa marehemu Regia Mtema, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana.


  Vilio na simanzi jana vilitawala katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, wakati wa kuuaga mwili wa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema (32), aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Jumamosi iliyopita.

  Hali hiyo ilijitokeza kwa nyakati tofauti katika viwanja hivyo na kusababisha wingu zito la majonzi na huzuni kutanda katika eneo lote la Karimjee lilofurika waombolezaji.

  Huzuni hiyo ilianza kujitokeza wakati jeneza lililokuwa na mwili wa Regia likiwa limefunikwa kwa bendera ya taifa, kuwasili katika viwanja hivyo.

  Pia wakati Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kwa nyakati tofauti walipokuwa wakitoa salamu za kambi na chama.

  Kutokana na salama hizo ambazo zigusa maisha ya Marehemu, zilisababisha waombolezaji kububujikwa machozi, na wengine kunawa na kwikwi kutokana na kulia.

  Hali ilikuwa ni ya vile pia wakati waombolezaji walipokuwa wakitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu.

  Shughuli hiyo ilihudhuriwa na mamia ya waombolezaji, wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za serikali na zisizokuwa za serikali pamoja na wakazi wa Dar es Salaam na viunga vyake, wakiongozwa na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilali.

  Watu hao walianza kumiminika katika viwanja hivyo, kuanzia saa 1.00 asubuhi na kuketi katika eneo lililoandaliwa kwa shughuli hiyo.

  Kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda, ndivyo watu walivyozidi kumiminika katika viwanja hivyo.

  Muda wote kabla ya mwili wa marehemu kuwasili, waombolezaji walikuwa wametulia wakiliwazwa na nyimbo za dini za maombolezo, huku wengine wakitafakari kuhusu msiba huo mzito ambao umepora Watanzania mwanasiasa kijana.

  Nyimbo hizo zilikuwa zikipigwa kupitia spika zilizowekwa karibu kila kona za viwanja hivyo na ziliendelea kupigwa hadi alipowasili Dk. Bilali, ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa mwisho kuwasili kulingana na itifaki.

  Ilipofika saa 4 asubuhi, mwili wa marehemu uliwasili katika viwanja hivyo ukiwa ndani ya jeneza lililofunikwa bendera ya taifa.

  Uliwasili katika viwanja hivyo, kwa gwaride maalum la walinzi wa Bunge (Sergent-At Arms) na waombolezaji kutakiwa kusimama kama ishara ya heshima kwa mbunge huyo.

  Wakati huo mwili ulikuwa ukitoka Hospitali ya Taifa (MNH), jijini Dar es Salaam ulikokuwa umehifadhiwa, baada ya kuhamishwa kutoka Hospitali Teule ya Tumbi, iliyoko wilayani Kibaha, mkoani Pwani.

  Ile hali ya utulivu iliyokuwapo awali, ilitoweka ghafla baada ya waombolezaji wengi waliofika katika viwanja hivyo, wakiwamo wabunge, viongozi wa serikali, taasisi za umma na za binafsi, ndugu, jamaa, marafiki, majirani na wananchi wa kawaida, kuanza kuangua vilio.

  Kilichochochea zaidi na simanzi, ni wimbo wa maombolezo uliokuwa ukipigwa wakati mwili wa Regia ukiwasili katika viwanja hivyo, ambao ulivuta hisia kali za majonzi.

  Baada ya mwili huo kuwasili, shughuli za kuuaga zilianza rasmi asubuhi kwa sala fupi ya kumuombea marehemu iliyoongozwa na Mchungaji Josephat Urio.

  Ibada hiyo ilifuatiwa na kusomwa wasifu wa marehemu uliosomwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Rasilimali Watu, Ofisi ya Bunge, Kitolina Kippa na kufuatiwa na salamu za Chadema, serikali na Bunge kwa msiba huo.

  Kwa upande wa Chadema, salamu hizo zilitolewa na , Dk. Slaa, wakati upande Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, zilitolewa na Kiongozi wake, Mbowe.

  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa salamu kwa niaba ya serikali wakati Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitoa salamu hizo kwa niaba ya Bunge.

  Kila mmoja alimmwagia sifa nyingi marehemu wakati wa uhai wake.

  Akitoa salamu za Chadema, Dk. Slaa alisema Regia alijiunga rasmi na chama hicho mwaka 2005 wakati akiwa chuoni mwaka mmoja kabla hajamaliza masomo.

  Alisema baada kumaliza masomo, alifanya kazi moja kwa moja Chadema kama ofisa mwandamizi wa vijana kisha oisa wa mafunzo na baadaye akawa mbunge na wakati huo huo akateuliwa na wenzake kuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama taifa.

  “Kwa hiyo, kuna mambo ya msingi, ambayo katika kipindi chote tumeyaona kwa Regia. Tungependa tushirikiane wote katika kipindi hiki kigumu tunapomuaga mwenzetu,” alisema Dk. Slaa.

  Alisema katika nafasi alizopata, Regia alionyesha uwezo mkubwa kwani alikuwa mwepesi wa kuelewa na kutenda yale yote aliyokuwa akielekezwa na chama na viongozi wenzake.

  Pia alisema Regia daima aliamini na kusimamia ukweli kuwa hakuna kazi yoyote, ambayo mwanaume anaweza kuifanya na mwanamke asiweze kuifanya, na kusema: “Hiki kimetugusa sana.”

  Dk. Slaa alisema pia nyakati zote Regia alipigania haki za kijinsia na alikuwa akiamini kuwa kijana yeyote wa kiume na wa kike kushindwa kuwa na jambo analoliamini na kulisimamia kwa maslahi ya jamii yake, ni uzembe, ambao hautakiwi kupata msamaha na kusema: “(Regia) aliyasimamia haya kwa ukali sana.”

  Alisema Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge, Mbowe alipotambua hilo, alimteua kusimamia Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

  Hata hivyo, alisema jambo muhimu katika yote ni kwamba, Regia alipokuwa bungeni, alikuwa akilazimika kila Alhamisi kuamka saa 10.30 alfajiri ili kuwahi kupata nafasi ya kumuuliza Waziri Mkuu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni.

  “Naamini Waziri Mkuu atakuwa amekumbana na maswali ya Mheshimiwa Regia. Asichogundua ni saa ngapi Regia alikuwa akiamka pamoja na hali yake. Alikuwa akiamka saa 10.30 ili awahi kuchukua nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema Dk. Slaa.

  Alisema jambo hilo ni moja ya sababu zilizomfanya Regia ajiunge katika siasa na kuacha kazi nyingine za kuajiriwa, ambazo zingemfanya atumikie taaluma yake na kujipatia maisha mazuri na makubwa baada ya kuhitimu chuo, badala yake akachagua kujitolea katika chama cha siasa kisichomlipa mshahara na kwamba, hata posho alizokuwa akipata zilikuwa hazitoshelezi hata kwa nauli ya kwenda na kurudi nyumbani.

  Alisema aliamini kuwa katika siasa angepata nafasi ya kutoa maoni, kusikilizwa na kufanyiwa kazi haraka na kwamba, kutokana na ujasiri aliokuwa nao ulimfanya ajiamini na kuthubutu katika maisha yake.

  Dk. Slaa alisema Regia pia hakuwahi kuonekana kufikiri au kujisikia kuwa mlemavu katika hatua yoyote ya mguu.

  Alisema pia hakufikiri kwamba ulemavu huo ulikuwa ni kikwazo kwake kufanikisha malengo yake na yale ya jamii aliyokuwa akiyapigania.

  “Kwa wale tuliokuwa karibu tulishtushwa sana na jinsi alivyoweza kukwea hata kwenye lile gari letu (Fuso) na kuhutubia. Gari ambalo sisi wengine linatupa taabu, lakini Regia alikuwa akiyapanda kwa ujasiri mkubwa,” alisema Dk. Slaa.

  Alisema Regia mara zote alikuwa akisema kuwa ulemavu kwake ulikuwa ni maumbile tu na si katika kazi, na kwamba aliamini kuwa pamoja na kuwa mwakilishi wa watu ndani ya chama na bungeni, pia alikuwa ni mwakilishi wa jamii ya watu wenye ulemavu waliokuwa nyuma yake.

  Dk. Slaa alisema jambo lingine linalomuonyesha marehemu Regia kuwa alikuwa mpiganaji kuikomboa jamii yake kupitia siasa, ni pale alipoamua kujiunga na chama cha siasa bila familia yake kujua.

  Alisema ilichukua miezi miwili kwa baba yake mzazi, Estelatus Mtema, kujua kuwa mwanaye, Regia alikuwa akifanya kazi makao makuu ya Chadema.

  Kwa sababu hiyo, Dk. Slaa alisema Regia alikuwa akilazimika kuomba nauli kwa baba huyo huyo kwenda kazini bila kujua alikokuwa anakwenda na kusema: “Hiyo ni dalili ya mpambanaji anayetaka kufanya kazi ya haki.”

  Alisema alikuwa na imani kubwa sana kwa watu wake wa Jimbo la Kilombero, mkoani Morogoro, ambayo ilidhihirika katika matamshi na matendo yake akionyesha hamu kubwa ya kuwa mtumishi wao.

  Dk. Slaa alisema pamoja na kuwa mbunge wa viti maalum, Regia hakusita kusema hadharani kuwa aliamini alishinda nafasi ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2010, hivyo alipenda kujiita “mbunge wa viti maalum wa kuchaguliwa na watu.”

  “Nyota imezimika, mapambano yanaendelea,” alisema Dk. Slaa.

  Hata hivyo, alisema pamoja na Regia kuiaga dunia, ameacha wapiganaji na makamanda wenzake, hivyo, wataendelea kuyafanyia kazi yote waliyoyaamini pamoja katika kuyapigania na kuwakomboa na kuwatumikia Watanzania kwa moyo, nia na uwezo wao wote.

  Mbowe alianza kwa kusema amepata wakati mgumu sana kuzungumza kuhusu Regia.

  Hata hivyo, alisema alikutana na Regia kwa mara ya kwanza mwaka 2001 wakati huo akiwa mbunge wa Hai baada ya kutembelea Shule ya Sekondari Machame, mkoani Kilimanjaro, ambako marehemu alikuwa mwanafunzi.

  Alisema alipotembelea shule hiyo, aliyesoma risala ya kumpokea alikuwa ni Regia na kusema kuanzia hapo ukawa ndio uhusiano wa kwanza wa marehemu na Chadema.

  Alisema jambo la msingi, ambalo walioko serikalini, ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenye vyama vingine vya siasa, hawapaswi kulibeza ni kwamba, viongozi huandaliwa na viongozi makini hawazuki.

  Mbowe, ambaye ni pia Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, alisema kuna jambo hilo mara nyingi wanapopigania hayo wamekuwa hawaeleweki na hubezwa.

  Alisema Chadema wanaamini katika maendeleo ya uongozi, ambayo hatua ya kwanza ni kutambua ni wapi wenye sifa ya kuwa viongozi na baadaye hufanya kazi ya kukuza vipaji vya uongozi kwa kutoa fursa za nafasi ya uongozi.

  Mbowe alisema ni katika mpango huo, ambao umefanywa ndani ya chama chao kuona umuhimu wa kuandaa vijana wa kuja kuwa viongozi makini kwa leo na kesho wakiamini kuwa vijana ni taifa la leo na sio taifa kesho.

  Pia wakiamini wazee ni tunu ya taifa, lakini fursa kwa vijana lazima wazitengeneze kwa kuandaliwa kimkakati, kimaadili na kiutumishi.

  Alisema ni katika mpango huo, Chadema wameweza kuchukua viongozi wengi katika vyuo vikuu mbalimbali, jambo ambalo alisema lilitafsiriwa kama ni utovu wa nidhamu, kuwanyima fursa vijana kusoma na kama vile ni uchochezi.

  Hata hivyo, alisema Chadema imeweza kuandaa vijana wengi, ambao watu wote nchini ni mashuhudia kwamba, wamekuwa wachangiaji wazuri sana katika mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali taifa.

  “Kazi hii, ambayo niliiongoza mimi kama mwenyekiti wa taifa na viongozi wenzangu. Leo katika vijana viongozi kama kina Zitto Kabwe, viongozi vijana kuna kina John Mnyika, viongozi vijana kuna kina Halima Mdee, viongozi kama kina John Mrema, kina Mheshimiwa Silinde mbunge wa Mbozi, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye leo (jana) tunamuaga hawa watu kina Mheshimiwa Mtema tuliwaandaa, hawakuzuka,” alisema Mbowe.

  Kutokana na hilo, aliiomba serikali ielewe kuwa vijana katika vyuo vikuu watakapoonekana wanafanya kazi ya siasa, wasiwakwaze wala kuwafukuza, bali wawalee.

  Viongozi waliohudhuria na kushiriki shughuli hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe, Tunu Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige,

  MAKINDA: NI NYOTA INAYONG'AA

  SPIKA wa Bunge, Makinda akitoa salamu hizo, alisema Regia ni nyota inayong’aa kwani ameweza kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali tofauti za kiitikadi zilizopo katika jamii.

  “Regia ni nyota inayong’aa, ametuunganisha Watanzania kupitia upendo aliokuwa nao … ametuonyesha kuwa hizi itikadi ni za kupita tu,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya waombolezaji waliofurika katika viwanja hivyo wakiwemo viongozi wa kitaifa, mawaziri, wabunge na wananchi wa kawaida.
  Akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa marehemu, Spika Makinda alisema alimfahamu mapema wakati (yeye) akiwa mwenyekiti wa wabunge wanawake kupitia mafunzo waliyokuwa wakitoa kwa vijana kama njia ya kuhamasisha wanawake kugombea majimboni na hivyo kuongeza idadi ya wabunge wanawake.

  “Regia ni mfano kwa wanawake wengi kwa sababu alithubutu kugombea jimbo licha ya vikwazo vilivyopo ambavyo huwafanya wanawake wengi waogope kugombea majimboni… nawasihi wanawake wote muige mfano wake,” alisema Spika Makinda.

  Aliongeza: “Regia alikuwa na nyumba aliyoinunua kule Mbezi na alikuwa akiishi na watu wengi wenye matatizo, hakuwa na kazi ya maana, hakuwa na mshahara mkubwa lakini alithubutu kuwasaidia wenye matatizo. Regia ametupa fundisho, ni mtoto lakini pia ni mfano wa kuigwa na wabunge wote.”

  PINDA: ALIKUWA KIUNGO

  Waziri Mkuu, Pinda alisema ataendelea kumkumbuka Regia kwa sababu alikuwa kiungo kizuri bungeni na aliisadia serikali kupata maoni ya wananchi kwa haraka zaidi.
  “Mheshimiwa Regia ni kiongozi ambaye ataendelea kukumbukwa kwa sababu ya mchango wake… nimeongea na Mhe. Mbowe na kumwambia kwamba pengo la Regia mtaliziba, lakini hamtapata mtu wa kufanana naye kwa sababu Regia alikuwa na karama za pekee,” alisema Pinda.

  Alitoa pole kwa Chadema kwa kumpoteza mbunge mahiri na makini.

  Pia alitoa pole kwa wazazi na familia na kuwasihi wajipe moyo na kufarijiana.

  Aliwaomba wajiombee pia ili waweze kukabili majonzi ya msiba huo na akawataka waendeleze mshikamano kama familia.

  Alisema Watanzania kama jamii, kila mmoja ana jukumu la kuendeleza yale mazuri ambayo Regia alikuwa akiyasimamia.

  MSAFARA IFAKARA

  Mbali ya Kamati ya Uongozi ya Bunge na Kamati ya Huduma za Bunge, wabunge wengine watakaoshiriki mazishi ya Regia, Ifakara leo ni wabunge wote wa mkoa wa Morogoro na wabunge 10 kutoka Kamati ya Miundombinu ambayo Regia alikuwa mjumbe.

  Wengine ni wabunge sita kutoka (CCM), wabunge wanne (CUF), mbunge mmoja mmoja kutoka NCCR, TLP, UDP na chama cha wabunge wanawake.

  Serikali itawakilishwa katika mazishi hayo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Hawa Ghasia.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...