Majibu ya maombi ya imani yaliyonichochea kuamini zaidi katika maombi ya imani

FaithClass

Member
Jul 16, 2023
14
114
Nilikuwa High School katika moja ya shule za Sekondari mkoani Kilimanjaro. Tukiwa shuleni, tulikuwa na kikundi chetu cha maombi. Ilikuwa ni kawaida yetu kuamka kila siku saa kumi na moja Asubuhi kwa ajili ya maombi. Tuliombea nchi, shule yetu, wanafunzi wenzetu, familia zetu, masomo yetu, n.k.

Kuna kipindi kuliibuka tatizo la wanafunzi kudondoka na kupoteza fahamu, lakini walipopelekwa hospitalini, hakukuweko na tatizo lo lote lililobainika. Waliishia kuongezewa maji na baada ya siku kadhaa waliruhusiwa kurudi shuleni.

Siku moja ya Jioni, niliitwa na mmoja wa wavulana wa kidato cha pili ambaye alikuwa ni mmoja wa wana kikundi chetu cha maombi. Aliniambia mmoja wa wanafunzi wenzake kazidiwa. Nilipofika bwenini kwao, nilikuta ndiyo wanamchukua kumpeleka kwenye matibabu kwenye kituo cha Afya kilicho jirani na shule. Sikujua kwa nini niliitwa, lakini niliamua kufuatana nao hadi kwenye kituo cha Afya alikopelekwa. Huko, niliwakuta wanafunzi wengine toka shuleni kwetu waliolazwa, lakini wakiwa wamesharejewa na fahamu.

Niliwahoji baadhi juu ya kilichowatokea, na maelezo yao yalikuwa yakifanana. Walisema kuwa waliona giza, na baada ya hapo hawakujua kilichoendelea mpaka walipojikuta hospitalini. Nilishangazwa na hiyo hali. Haikuwa kawaida kwa shule ya wavulana kukumbwa na tatizo kama hilo.

Shuleni nako, hali ya wanafunzi haikuwa shwari. Wengi walikuwa hawaingii darasani kutokana na kuwa wadhaifu. Mabweni yaligeuka kuwa kama wodi za wagonjwa.

Nilipotoka hapo kwenye kituo cha Afya, nilijisikia kujawa na HASIRA fulani, lakini hasira chanya, kutokana na hali iliyokuwa ikiendelea. Nilipata msukumo wa kufanya jambo litakalobadili hali iliyokuwepo.

Ingawa tulikuwa tukiomba kila siku Asubuhi kama kikundi cha maombi, niliamua kulichukua hilo kama jukumu langu binafsi. Siku iyo hiyo, nilifikia uamuzi wa kufanya maombi maalum kwa ajili ya hiyo hali, na nikayaanza kesho yake Asubuhi. Niliamua kufanya maombi ya kufunga kwa siku tatu, kila siku Asubuhi hadi Jioni. Kwa hiyo yalikuwa maombi ya mfungo wa nusu siku.

Kwa sababu nilikuwa nikifunga kuanzia Asubuhi hadi Jioni, kwa hizo siku tatu, ratiba yangu ilikuwa kama ifuatvyo:

1. Saa kumi na moja Asubuhi, nilikuwa nikijumuika na wenzangu kwenye maombi ya pamoja. Baada ya hapo, niliingia kwenye maandalizi binafsi kabla ya muda wa uji. Kwa sababu ya baridi, tulikuwa tukinywa uji saa kumi na mbili na nusu Asubuhi.

2. Wakati wenzangu walipokuwa wakienda kwenye uji saa kumi na mbili na nusu Asubuhi, mimi nilielekea kwenye chumba cha maombi.

3. Saa nne Asubuhi, ulikuwa ni muda wa chai. Ilikuwa ikitolewa chai tu, hakukuweko na vitafunwa. Kwa aliyehitaji kitafunwa, ilimbidi aingie mfukoni mwake, kama bado alikuwa na pocket money. Kwa hiyo wakati wenzangu walipokuwa wakienda kwenye chai, mimi nilielekea kwenye maombi.

4. Saa saba ilikuwa muda wa mlo wa Mchana, lakini kwangu ulikuwa muda wa maombi. Baada ya hapo , kulikuwa na muda mrefu wa mapumziko kabla ya kurudi tena darasani. Muda wote huo mimi niliutumia kwenye maombi.

5. Kuanzia saa kumi na moja jioni, ulikuwa ni muda wa michezo. Kwangu, ilikuwa ni fursa nyingine tena ya maombi.

Hiyo ndiyo ilikuwa ratiba yangu kwa siku tatu, nilikuwa nikimwomba Mungu aliondoe tatizo lililoikumba shule yetu la wanafunzi kuugua hovyo na wengine kudondoka na kupoteza fahamu. Wakati wa hiyon ratiba ya maombi, ilikuwa ni kawaida yangu kulitafakari kwanza Neno la Mungu kwa utulivu kabla ya kuanza maombi. Na nilipokuwa nikiomba, nilikuwa nikianza na toba kwa kumwomba Mungu anisamehe kwa uzembe nilioufanya hadi kupelekea magonjwa kupata nafasi mahali nilipokuwa, shuleni kwetu. Niliamini kwamba kama ningesimama katika nafasi yangu kwa uaminifu, hilo tatizo lisingefanikiwa kuingia shuleni kwetu. Maombi ya kimamlaka yangelikwamisha.

Kadri nilivyokuwa nikiomba, ndivyo na nguvu ya maombi ilivyokuwa ikiongezeka. Hali niliyokuwa nikiihisi wakati wa kuomba iliniaminisha kuwa maombi yangu hayakuwa maneno matupu. Kulikuwa na nguvu iliyokuwa ikiachiliwa kwayo.

Mchana wa siku ya pili, wakati nikiwa kati kati ya maombi, nilihisi kama vile Andiko la Marko 11 limedondoshwa kwenye Ufahamu wangu. Niliacha kuomba kwa muda na nikaichukua Biblia na kuanza kusoma kitabu cha Marko 11. Nilipofika Marko 11:23-24, ikawa kama vile huo ndiyo ujumbe niliotakiwa kusimama nao kwenye maombi niliyokuwa nikiyafanya. Imeandikwa, AMIN, NAWAAMBIA, YE YOTE ATAKAYEUAMBIA MLIMA HUU, NG'OKA UKATUPWE BAHARINI WALA ASIONE SHAKA MOYONI MWAKE, ILA AAMINI KWAMBA HAYO ASEAMYOYAMETUKIA, YATAKUWA YAKE. KWA SABABU HIYO NAWAAMBIA, YO YOTE MYAOMBAYO MKISALI, AMININI YA KWAMBA MNAYAPOKEA, NAYO YATAKUWA YENU. Marko 11:23-24.

Hiyo mistari ilibadilish namna nilivyokuwa nikiomba. Niliacha kumlilia Mungu, na badala yake, kama Andiko lilivyoelekeza, NILIANZA KUAMURU UGONJWA UKAUKE.

Nilikuwa nikiomba kwa kutamka hivi: ROHO YA MAGONJWA, NAKUAMURU KAUKA KATIKA JINA LA YA YESU KRISTO. KAMA VILE YESU ALIVYOULAANI MTINI UKAKAUKA, NAMI NAKUAMURU KATIKA JINA LA YESU KRISTO KAUKA SASA. WANAFUNZI MLIO HOSPITALINI, MUWE WAZIMA SASA, KWA JINA LA YESU KRISTO. WANAFUNZI MLIOLALA BWENINI KWA SABABU YA UDHAIFU, MUWE WAZIMA KWA JINA LA YESU KRISTO.

Kila nilipomaliza kuomba, nilimshukuru MUNGU kwamba kanisikia na hivyo hilo tatizo halipo tena.

Siku ya tatu ambayo ndiyo ilikuwa ya kuhitimisha maombi, niliendelea na ratiba yangu ya mombi kama kawaida. Katika maombi niliyokuwa nikiyafanya, niliyajumuisha na mahitaji mengine, lakini nilikuwa nikiyaombea mwishoni, baada ya kuombea ya shule. Nilifanya kama hitaji la ziada. Moja ya jambo nililokuwa nikiombea ni upatanisho wa wamama wawili katika ukoo wetu ambao walikuwa hawapatani kwa miaka mingi, hata kabla sijazaliwa.

Siku hiyo ya tatu, baada ya kumaliza kuombea hitaji ya shule, niligeukia la hao wamama. Nilianza kwa kutubu kwa ajli yao na kisha kuvunja roho ya mafarakano kati yao. Nilivunja kiambaza cha uadui na kupatanisha nafsi zao kwa damu ya Yesu.

Watu mbali mbali, wakiwemo wazee wa ukoo, walishajitahidi kuwapatanisha bila mafanikio. Kwa jinsi uadui wao ulivyokuwa mkubwa, walifikia hatua ya kutamkiana kuwa mmoja wao akifa mwenzake asilisogelee kaburi lake.

Jioni ya siku ya tatu, nilipoenda kwenye kipindi cha kuhitimisha maombi, kila nilipotaka kuomba, nilijikuta napata msukumo wa kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi yangu. Kwa hiyo, kipindi chote cha muda wa Jioni nilitumia kwa maombi ya kushukuru tu.

Kesho yake, nilianza kupata taarifa ambazo nilizihusianisha na maombi niliyoyafanya. Zilinipa tafsiri kuwa maombi yamejibiwa.

Kwanza, wanafunzi waliokuwa bwenini walipona na kuweza kuingia darasani. Pili, wanafunzi waliokuwa wamelazwa kituo cha Afya nao waliruhusiwa baada ya hali zao kuwaridhisha matabibu.

Mwezi wa tisa mwaka huo, baada ya kufunga shule kwa likizo fupi, nilienda nyumbani. Kesho yake, wakati nikitembelea ndugu kuwajulia hali, nilikutana na mmoja wa wale wanafamilia wa ukoo wetu waliokuwa hawapatani kwa miaka mingi. Sikumwuliza, lakini katika hali isiyo ya kawaida, aliniambia, NIMEPATANA NA... Nilipomwuliza ilikuwaje, aliniambia mmoja alimsalimia mwenzake, na mwenzake alipomwitikia, waliendelea na mazungumzo kana kwamba hawakuwahi kugombana. Hata wao wenyewe walikuwa wakijishangaa jinsi walivyopatana kirahisi wakati wamama wenzao walishindwa kuwapatanisha, na hata wazee wa ukoo.

Niliamua kuwauliza watu wengine wa karibu kuhusiana na hiyo taarifa. Nao walielezea mshangao wao kuhusu kilichojiri.

Kama haitoshi, hao wamama waliopatana bila kupatanishwa na watu, waliishia kuwa marafiki wakubwa sana, kiasi cha kusindikizana kwenye matukio muhimu na ya kawaida.

Kwa upande wa shule, hakukuweko na mwanafunzi aliyepatwa tena na tatizo la kudondoka, kwa kipindi chote nilipokuwa mwanafunzi shuleni hapo na hata baada ya kuhitimu. Miaka kadhaa baada ya kuhitimu Kidato cha sita, nilipouliza, niliambiwa kuwa tatizo kama hilo halikutokea tena.

Hizo shuhuda zilibadili kabisa mtazamo wangu kuhusu maombi. Kati ya jambo nililojifunza kuhusu maombi ni kuwa MAOMBI YA IMANI HUAMBATANA NA SHUKRANI. Kama umeomba kwa IMANI, utamshukuru MUNGU kwa IMANI, ukiwa unaamini kwa moyo wako wote kuwa Mungu kakusikia na ameshakujibu. Shukrani kabla ya kuona majibu ya maombi yako ni ishara kuwa unaamini Mungu kakusikia na amekuijbu. Na moja ya kanuni ya Imani ni mtu hupokea kwa kadiri ya Imani yake. Imeandikwa, KWA KADIRI YA IMANI YENU MPATE; Mathayo 9:29.

Na kama umeomba kwa IMANI, lazima utapata majibu. Maombi yaliyofanywa kwa IMANI hayakosi kuwa na USHUHUDA.

Ni kawaida kwa maombi ya IMANI kuleta matokeo, vinginevyo, labda, hayakufanywa kwa IMANI.

Matukio hayo mawili: la shuleni na la wamama wawili kwenye ukoo wetu, ndiyo yaliyonihamasisha kuwa na shauku ya kuijfunza zaidi kuhusu IMANI na MAOMBI. Na, kwa kadiri ya ufahamu wangu, maarifa niliyoyapata yamekuwa ya msaada mkubwa sana maishani mwangu. Ninamshukuru sana Mungu.
 
Nilikuwa High School katika moja ya shule za Sekondari mkoani Kilimanjaro. Tukiwa shuleni, tulikuwa na kikundi chetu cha maombi. Ilikuwa ni kawaida yetu kuamka kila siku saa kumi na moja Asubuhi kwa ajili ya maombi. Tuliombea nchi, shule yetu, wanafunzi wenzetu, familia zetu, masomo yetu, n.k.
Aisee!
 
Nilikuwa High School katika moja ya shule za Sekondari mkoani Kilimanjaro. Tukiwa shuleni, tulikuwa na kikundi chetu cha maombi. Ilikuwa ni kawaida yetu kuamka kila siku saa kumi na moja Asubuhi kwa ajili ya maombi. Tuliombea nchi, shule yetu, wanafunzi wenzetu, familia zetu, masomo yetu, n.k.
Mungu ni mwema na mwaminifu kweli, unajua kama huamini neno la Mungu unaweza kusema jamaa muongo, ila tunao amini na kupata uzoefu tunakubali kuwa kwa maombi ya Mtu mmoja Mungu anaweza ponya nchi nzima... Asee waombaji tukutane basi tuombee swala la DP World na bandari.. Maana tunauzwa jamani... Embu tupate hasira ya bwana tushikamane ktk kuomba🙏🙏
 
Japo sijasoma yote! Lkn mungu wetu ni mwaminifu na anatenda sawa na kuomba kwetu!

Ile baridi ya Kilimanjaro mwezi wa sita mwishoni mpaka nane mwanzoni hua inawaathiri sana wanafunzi!
 
Mungu ni mwema na mwaminifu kweli, unajua kama huamini neno la Mungu unaweza kusema jamaa muongo, ila tunao amini na kupata uzoefu tunakubali kuwa kwa maombi ya Mtu mmoja Mungu anaweza ponya nchi nzima... Asee waombaji tukutane basi tuombee swala la DP World na bandari.. Maana tunauzwa jamani... Embu tupate hasira ya bwana tushikamane ktk kuomba🙏🙏
Usihusishe siasa na imani
 
Umenikumbusha wakati nipo sekondari.Kuna msichana alikuwa anapenda sana kusali na kila kazi anayopewa alikuwa akiifanya kwa utiifu.Yule binti wengine wakienda disco yeye alikuwa anasema hawezi kwakuwa ina haribu mahusiano yake na Mungu.Ikifika kipindi cha mtihani kurasa alizokuwa anasoma ndizo zinazotoka kwenye mtihani na mtihani ukitoka amefaulu.Hivyo ikifika muda wa mtihani kila mtu atakaa karibu yake kuangalia anachosoma na ukifika kwenye mtihani unakuta kilekile.Maua yake shule nzima ndio yalikuwa yanavutia kuliko yote nakumbuka alipewa zawadi kwa ajili ya hili.Sijui yupo wapi sasa lakini na imani atakuwa mbali sana
 
Back
Top Bottom