Serikali yamjibu Slaa:
Yawatetea watu wanaotuhumiwa
na Mwandishi Wetu
WIKI mbili tangu wapinzani watoe tuhuma nzito za rushwa dhidi ya viongozi waandamizi serikalini na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), serikali imetoa tamko ikitoa majibu yake.
Serikali katika tamko lake hilo lililotolewa kwa upendeleo maalumu kwa vyombo kadhaa vya habari leo hii, inakanusha tuhuma takriban zote zilizotolewa na wapinzani, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
Katika tamko lake hilo, serikali, inaziita tuhuma zote za Slaa, kuhusu Benki Kuu (BoT), Kampuni ya Tangold na nyinginezo kuwa ni za kizushi na ambazo zimetolewa pasipo kufanyika kwa utafiti wa kutosha.
Kuhusu Benki Kuu, serikali katika taarifa yake hiyo inasema; Baada ya kufuatilia kwa kina kuhusu tuhuma hizi, serikali inatoa tamko kuwa ni za uzushi na upotoshaji wa makusudi wa ukweli. Aidha, tuhuma kuhusu majina ya wanaodaiwa kuingiza fedha za kigeni nchini na baadaye kulipwa na Benki Kuu, ni vyema ieleweke kuwa wadai wanaozungumziwa hawakuingiza fedha za kigeni nchini, bali walilipa fedha za Kitanzania kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kama malipo ya kuagiza bidhaa kutoka nje katika miaka ya 80.
Aidha, katika hilo serikali inasema BoT ilishindwa kufanya malipo hayo wakati huo, baada ya kupokea fedha kutoka NBC kutokana na kutokuwa na fedha za kigeni enzi hizo.
Bila ya kutaja wakati, serikali inaeleza katika taarifa yake hiyo kuwa, baada ya tuhuma za uwezekano wa kuwepo kwa malipo yasiyo sahihi kupitia akaunti hii kujitokeza, ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kuteua mkaguzi wa kimataifa (International Auditing Firm) kwa utaratibu wa wazi wa zabuni ili kufanya uchunguzi maalumu na kuwasilisha taarifa yake serikalini.
Uchunguzi huo unaendelea na serikali inasubiri ukamilike ili kuamua hatua muafaka. Mhe. Dk. Slaa na wenzake wanafahamu vizuri hatua zilizochukuliwa na serikali katika suala hili, kwani serikali ilitoa taarifa kwenye vyombo vya habari na imetoa maelezo ya hatua za utekelezaji wake bungeni mara kadhaa, inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kuhusu madai mengine ya wapinzani kwamba, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuhusu hesabu za Benki Kuu kwa mwaka 2005/06 kuonyesha mapungufu makubwa, serikali katika tamko lake inasema imepitia taarifa ya ukaguzi wa hesabu hizo, lakini haikuona hoja za ukaguzi zinazodaiwa kutolewa na CAG.
Mbali ya hilo, serikali inasema, taarifa ya hesabu za Benki Kuu kwa mwaka 2005/2006, ziliwasilishwa katika Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge mapema mwaka huu na kukubaliwa na kamati hiyo na kwamba (kamati hiyo) iliwasilisha taarifa yake bungeni na Bunge likairidhia.
Serikali inaeleza katika tamko lake hilo kwamba, kwa nyakati tofauti, Kamati ya Fedha ya Uchumi ya Bunge pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) zimepata nafasi ya kutembelea miradi ya ujenzi wa majengo ya Benki Kuu ya Dar es Salaam na Zanzibar ili kupatiwa maelezo ya kutosheleza, kuhusu utekelezaji na gharama za miradi hiyo, hali ambayo inaifanya hoja ya Slaa kuonekana kuwa ni ya kubuni na yenye nia mbaya.
Nia mbaya ya Mheshimiwa Dk. Slaa na wenzake katika kutoa tuhuma hizi, inadhihirishwa na upotoshaji wa makusudi wa takwimu zilizo katika hesabu hizi, ili kupindisha ukweli. Kwa mfano, anaituhumu Benki Kuu kutumia shilingi 522,459,255,000 (Bilioni 522.5) kwa ujenzi wa Twin Towers mjini Dar es Salaam. Ukweli ni kwamba kiasi hicho ni thamani ya mali zote za kudumu za Benki Kuu hadi tarehe 30 Juni, 2006. Taarifa hizi ziko wazi katika nyaraka zilizowasilishwa bungeni na zinaweza kuthibitishwa na mtu yeyote kutokana na Taarifa ya Benki Kuu ya Mwaka 2005/06 iliyosambazwa kwa umma, inasema taarifa hiyo ya serikali.
Aidha, serikali katika tamko lake hilo, imewatetea watumishi wake wanaotajwa kuwa miongoni mwa mafisadi katika orodha ya Dk. Slaa, ikisema kuwa kwao wakurugenzi katika Kampuni ya Tangold Limited, kunatokana na uamuzi wa serikali na kuwa kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia 100 na serikali.
Wakurugenzi wa Tangold wameteuliwa na Serikali ya Tanzania, wote ni watumishi wa umma ambao ni pamoja na wale ambao Mheshimiwa Slaa anawatuhumu katika tamko lake.
Watumishi hao wameteuliwa kuwa wakurugenzi wa Tangold kutokana na nafasi zao katika utumishi wa umma. Kuwa mkurugenzi katika chombo cha umma hakusababishi mgongano wa kimaslahi, kwani ni sehemu ya utumishi wa umma, inasomeka sehemu moja ya tamko hilo la serikali.
Mbali ya hilo, tamko hilo la serikali linasema wakurugenzi hao wa Tangold hawana hisa katika kampuni hiyo, kwa sababu hisa zake zote zinamilikiwa na Mfuko wa Udhamini wa Maendeleo (Tanzania Development Trust) kwa niaba ya Watanzania wote.
Kwa maana hiyo, wakurugenzi wa Bodi ya Kampuni ya Tangold hawana maslahi yoyote binafsi zaidi ya kusimamia maslahi ya Watanzania, inasema taarifa hiyo.
Serikali katika tamko lake hilo, imekanusha madai mengine ya wapinzani, kwamba kulikuwepo na shinikizo kwa Kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington, Marekani, kupewa kazi ya kukagua hesabu za kampuni za uchimbaji dhahabu.
Serikali katika tamko lake inasema, kampuni hiyo ilipatikana kwa kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi wa umma na hakukuwa na shinikizo lolote.
Hata hivyo, kuhusu tuhuma zilizoelekezwa katika sekta ya madini, serikali katika tamko lake hilo imesema kutokana na unyeti wa suala lenyewe, inakusudia kulitoa tamko rasmi kuhusu jambo hilo katika taarifa nyingine maalumu kwa lengo la kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu sekta hii.
Sekta ya madini ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu. Kutokana na unyeti wa sekta hii na tuhuma nzito zilizotolewa dhidi ya serikali juu ya sekta hii, serikali inaona ni vyema kutoa maelezo ya ufafanuzi zaidi. Hivyo, serikali itatoa taarifa maalumu na ya kina kuelezea wananchi juu ya sekta hili, linasema tamko hilo.
Akizungumzia hoja za serikali katika tamko lake hilo, Dk. Slaa aliyejibu kwa maandishi kipengele kwa kipengele, anasema majibu takriban yote ya serikali yana mapungufu makubwa na akasema bado alikuwa akisubiri hatua za kisheria ili akatoe ushahidi alionao kuhusu madai yake mahakamani.
Katika sehemu moja ya majibu yake, Dk. Slaa anaeleza kusikitishwa na tamko la serikali linalozungumzia uchaguzi wa mwaka 2005 na kushindwa kwa upinzani, kuwa ndiyo sababu kuu ya wapinzani kujaribu kuwahadaa wananchi ili wawachague wao siku zijazo.
Hoja hii ni ya watu walioshiwa, na wamebaki na fikra mgando. Nani kati yetu kipindi chote hiki amezungumzia masuala ya uchaguzi? Ni kazi yetu ya kikatiba kuelezea Watanzania pale ambapo serikali imefanya makosa. Si kazi ya upinzani kuipigia makofi serikali. Kazi ya kambi ya upinzani duniani kote inajulikana. Na ndiyo maana tuko kikatiba, anasema Slaa katika majibu yake.
Aidha, Dk. Slaa anaitaka serikali kujieleza kwa wananchi ili ieleweke, badala ya kutafuta mchawi, na akasisitiza kuwa leo hii wananchi wanalalamika kila kona ya nchi maisha bora hayajaonekana, na kwamba vyama vya upinzani vina wajibu wa kuhoji kwa niaba ya wananchi kutaka kujua kuhusu rasilimali za taifa.