MsemajiUkweli
JF-Expert Member
- Jul 5, 2012
- 13,171
- 23,991
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza mawaziri kwa kuanza utendaji kazi vizuri, ikiwemo kutumbua majipu.
Amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, itaendeleza dhamira yake ya dhati ya kupambana na ufisadi na rushwa hadi itakapojiridhisha kuwa mambo yanakwenda sawa.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka mawaziri hao kutambua kuwa cheo na uongozi ni dhamana, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa umma kwa vitendo bila upendeleo wala kuhitaji ujira zaidi ya wajibu wao. Alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya mawaziri na naibu mawaziri kuhusu sheria, mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na utekelezaji wa ahadi ya uadilifu Ikulu, Dar es Salaam jana.
Alisema Rais John Magufuli alipoingia madarakani, aliweka wazi msimamo wake juu ya mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa. Alisema wakati Rais Magufuli akizindua Bunge mjini Dodoma, alisisitiza kuhusu mapambano hayo na kubainisha kuwa tiba yake kuu ni uzingatiaji wa Sheria ya Maadili katika nyanja zote.
“Alitaja maeneo hayo kuwa ni ucheleweshaji wa utoaji huduma, upendeleo, ubinafsi, rushwa na ufisadi lakini pia matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Majaliwa.
Alisema kutokana na jitihada za kukabili hali hiyo zinavyoonekana tangu waingie madarakani, inadhihirisha namna ambavyo Rais hakutoa ahadi hiyo kwa sababu ya kuwarubuni wananchi kupata kura zao au sifa, kwa kuwa serikali imeanza kuchukua hatua.
“Nawapongeza waheshimiwa mawaziri kwa kazi nzuri mliyoanza kuifanya, nasisitiza kuwa bado tutaendelea kuchukua hatua tatizo hili la ufisadi na rushwa, hatutamvumilia mtumishi yeyote atakayeenda kinyume cha maadili kwani hali hii imewanyima kwa muda mrefu wananchi haki na kuipotezea Serikali mabilioni ya fedha,” alisisitiza.
Alisema mawaziri hao tangu walipoteuliwa kushika wadhifa huo, wameanza vizuri kufanya kazi yao na kuzingatia maadili hivyo mafunzo hayo ya sheria, mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na hati ya uadilifu, yataimarisha zaidi utendaji wao.
Alisema mafanikio hayo ya awali katika kudhibiti tatizo hilo la ufisadi na rushwa, bado wapo watu wachache wasiofurahia jitahada hizo ikiwemo utendaji mzima wa Serikali hiyo ya Awamu ya Tano. “Sasa tunasema wanaokasirika ni wachache na wengi wanafurahia tutaendelea na kasi hii hadi tuone mambo yanakwenda sawa,”alisema.
Aidha alisema kutokana na kasi ya kutumbua majipu inayoendelea kupitia mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali hiyo, kuna baadhi ya watumishi wa umma wamedai kuwa na hofu ya kufanya kazi. “Mimi nadhani mtumishi anayefuata maadili ya kazi yake na kuwajibika hapaswi kuwa na hofu. Wale wote walio na hofu ni wale wasiozingatia maadili,” alisema.
Aliwataka mawaziri hao kujenga tabia ya kuzingatia maadili kama heshima pekee, ambayo wananchi wangetamani ionekane kwa kila kiongozi na mtendaji aliyepewa dhamana. “Maadili ni tunu inayoweza kumtofautisha mtu na mtu. Maadili yanachochea kujenga tabia ya upendo, umoja na mshikamano hali itakayoleta maendeleo katika taifa. Maadili ni nyenzo muhimu katika ujenzi wa taifa lenye watu wachapakazi, wastaarabu na wanaotanguliza maslahi ya nchi yao mbele,” alisisitiza.
Alisema historia ya maadili nchini, haikuanza leo kwani imetajwa katika nyaraka mbalimbali za Serikali ikiwemo Katiba, Sera ya Menejimenti ya Umma ya mwaka 1999, Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Ilani ya Chama cha Mapindizi (CCM) ya mwaka 2015 na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
Akikariri Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la Pili la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Dar es Salaam, alisema maana ya maadili ni mwenendo mwema. “Kwa maana hiyo huwezi kusema maadili mabaya, maadili yanaonyesha kuzingirwa na tabia mbaya ndio tunapata changamoto kuhusu utendaji usioridhisha,” alisema.
Aliwataka viongozi hao kutambua kuwa kiongozi yeyote, hubeba dhamana ya umma au ya watu anawaongoza hivyo kwa kuwa wameshakubali kuwa viongozi wa umma maana yake wawajibike kwa umma. “Hii inanikumbusha kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa cheo ni dhamana. Uongozi ni cheo chenye wajibu. Kwa tafsiri sahihi kiongozi huwajibika kwa matendo yake kwa wale anaowaongoza… Pamoja na kuwa sisi ni watumishi wa umma, tunapaswa kuwahudumia watu wanaotuzunguka bila upendeleo wala uhitaji wa ujira zaidi,” alisisitiza.
Alibainisha kuwa sheria ya maadili imeweka masharti maalum kwa mawaziri, naibu mawaziri na wakuu wa mikoa, ambayo baadhi yake ni viongozi hao hawatakiwi kufanya jambo lolote linalopingana na dhana ya uwajibikaji kuhusu Sera ya Serikali. Pia hawatakiwi kupinga hadharani au kujiondoa binafsi katika uamuzi wowote, unaofanywa na Baraza la Mawaziri, kutoa hadharani matamshi ya kumkosoa kiongozi mwenzake mwenye madaraka ya waziri na kutoa nje taarifa zisizoruhusiwa za mijadala, uamuzi au nyaraka za baraza la mawaziri.
Alipongeza utendaji na uaminifu, uliooneshwa na baraza hilo la mawaziri, akisema tangu liingie madarakani hakuna waziri yeyote aliyevunja kifungu hicho cha sheria.
Chanzo cha dhana ya utumbuaji majipu ni hotuba ya Rais Magufuli alipofungua rasmi Bunge mjini Dodoma Novemba 20, mwaka jana.
Chanzo: Habari Leo