Wananchi wengine tunaojadili suala hili tunalijadili bila kuwa na uhuru. Ni kama vile tunashindana kwa misingi ya dini zetu zaidi kuliko maana na makusudi ya jambo lenyewe. Kama suala la mahakama ya kadhi lingekuwa ni suala ambalo halina maana yoyote kisheria na kisiasa bali ni suala la waislamu tu, lisingeanzishwa na Mrema ambaye ni Mkristo. Lisingekuwa katika Katiba ya Kenya ambako waislamu ni minority. Lisingekuwa katika mfumo wa sheria wa Uganda.
Jambo ambalo wengi tunasahau kulifikiria kwa uzito wake ni kwamba Tanzania ni nchi yenye mchanganyiko wa watu wa mila, desturi, dini, kabila na siasa tofauti. Serikali pamoja na mfumo wake wakisheria na utawala kwa ujumla haitoki juu. Inatoka katika jamii ya watu hao hao mkanganyiko. Siri ya mafanikio ya serikali yoyote ni kuweza kuowanisha maslahi mbalimbali kinzani ndani ya nchi bila kuathiri mshikamano wa jamii. Ndio maana leo unasikia sheria za mila ni sehemu ya sheria halali za nchi, sheria za kiislamu ni sehemu ya sheria za nchi nk. Mtu mwingine angesema kuruhusu matumizi ya sheria za kiislamu Tanzania ni udini au sheria za kimila ni ukabila. Lakini hiyo ndiyo siasa. Ndio maana Pinda japo ni mukristo safi hachoki kushirikiana na waislamu kuona namna mahakama ya kadhi inavyoweza kuundwa na kutumika bila matatizo.
Suala ambalo kwa wale wasiohusika na mahakama ya kadhi wangependa kulizingumza ni mbinu zitakazotumika ili Mahakama hizi zisiingiliane na maslahi yao na wala sio kupinga uwepo wake. Hata ile kufanya Jumapili na Jumamosi siku ya mapumziko wakati ijumaa ni siku ya kazi mtu mwenye tafsiri ya haraka haraka ya mambo kama wengi wetu tulivyo anaweza kusema udini kama yule anaedai kwamba kutumika kodi za wananchi kugharamia mahakama za kadhi ni udini. Siku mbili tunazokaa bila kazi zinalipotezea taifa kiasi gani cha fedha? Nani anaenufaika na mapumziko ya Jumapili? Nani anayenufaika na mapumziko ya Pasaka, Xmas na Idi? Xmas ni sikukuu ya waislamu, wapagani, wahindu na wasabato? Idi ni sikukuu ya wakristo, wapagani na wahindu? Hapo vipi?
Msingi wa amani, upendo na utulivu wa watanzania na jamii nyingine yoyote ya kistaarabu ni kuvumiliana kutokana na tofauti zetu za kijamii, kiuchumi, kiimani na kadhalika. Ndio maana masikini wasio na magari hawalalamiki kulipa kodi zao na zikatumika kujenga barabara japo hawana magari wala hawasafiri safiri? Mimi sipendi mpira, lakini kodi yangu inatumika kujenga uwanja wa mpira. Mimi sipendi siasa lakini kodi yangu inatumika kulipa ruzuku katika vyama vya siasa. Kwa nini? Kwa sababu japo mimi spendi mpira wapo watanzania wenzangu wengi wanaopenda mpira. Japo mimi sipendi mahakama ya kadhi wapo watanzania wenzangu wengi wanapenda. Japo mimi sipendi kutofanya kazi jumapili wapo watanzania wenzangu wengi wanapenda kuitumia siku hiyo kumuabdu mungu na kupumzika. Waislamu wangependa ijumaa iwe siku ya mapumziko, wapagani labda wangependa j tatu. Lakini siku ziko saba tu katika wiki. Kwa kuwa nchi ilizaliwa ikakuta jumapili ni siku ya mapumziko, inabidi tuache hivyo bila kuleta kinyongo kwamba wakristo wanafaidi zaidi kiimani. Huo ndio upendo bwana Yesu alitufundisha kwamba 'Mpende jirani yako kama nafsi yako". Waislamu ni majirani kwa wakristo na kinyume chao. Hata kama kuna wengine kwa tafsiri zao za haraka haraka watasema vinginevyo, maandiko pia yanasema "mpende adui yako". Hapo vipi?