Mahabusu ajimwagia kinyesi mahakamani

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
Mahabusu Alli Nuru (Mwasa)Mkazi wa Chang`ombe Dodoma akiwa amezungukwa na Askari polisi wa kikosi cha Mbwa wakimsihi aondoke chini ya bendera ya Taifa alipokaa jana baada ya kujipakaza mwili wake kinyesi kwenye chumba cha mahabusu cha mahakama Kuu kanda ya Dodoma

Mahakama Kuu ya Kanda ya Dodoma ililazimika kusimamisha shughuli zake jana, baada ya mahabusu Ally Nuru, maarufu kwa jina la Mwasa (30), kujipakaza kinyesi mwili mzima na kula kwa madai ya kuchoshwa kukaa rumande bila kuhukumiwa.
Tukio hilo lilitokea jana saa 2:00 asubuhi baada ya mahabusu huyo mkazi wa Chang’ombe mjini hapa anayekabiliwa na shtaka

la mauaji, kufikishwa katika mahabusu ya mahakama hiyo kuhudhuria kesi yake.
Mahabusu huyo alipofikishwa katika chumba cha mahabusu cha mahakama hiyo alibomoa choo cha mahakama na kuchukua kinyesi kisha akajipakaza mwili mzima huku akipiga kelele kuwa amechoka kukaa mahabusu bila kuhukumiwa.

Nuru, ambaye baada ya kujipakaza kinyesi na kukila, aliwazuia mahabusu wenzake kwenda kwenye chumba cha kusikiliza kesi zao, hali ambayo ilisababisha ulinzi katika eneo hilo kuimarishwa zaidi.
Hali hiyo iliwafanya polisi waliokuwa wamebeba mabomu ya kutoa machozi, silaha za moto na mbwa watatu, kumzunguka.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuvunja choo cha mahabusu ya mahakama hiyo na kuchukua kinyesi kilichokuwa ndani ya shimo na kisha kuweka kwenye kopo la maji ya kunywa lililokatwa.
Nuru baada ya kujipaka kinyesi, alivunja mlango wa mahabusu.

Hali hiyo iliwafanya mahabusu kushindwa kutoka ndani ya chumba cha mahabusu baada Nuru kusimama mlangoni na kutishia kummwagia kinyesi polisi atakeyethubutu kumsogelea.
Wakati akiwa amesimama katikati ya mlango, Nuru alimwaga kinyesi katika chumba cha mahakama kilichoko jirani.

Hali hiyo ilisababisha askari polisi na watu wengine, kumsihi kwa muda mrefu kutoka mlangoni hapo na kuahidi kuwa hawatamuadhibu kwa kosa hilo.
Tukio hilo ambalo limeshuhudiwa na NIPASHE, lilimkariri Nuru akisema: “Ni heri Polisi wanipige risasi kuliko kuteseka rumande maana nimechoka kukaa huko bila kuhukumiwa ni bora nife kuliko mateso ninayoyapata huko.”

Wakati wakimpeleka kuoga baada ya kukubali kuondoka mlangoni, Nuru aligomea chini ya bendera zilizokuwa zikipepea katika viwanja vya mahakama hiyo.
Hatua hiyo iliwafanya polisi kumsihi kwa mara nyingine, akubali kuondoka eneo hilo ili aende kuoga.
Katika tukio hilo, askari kanzu alichaniwa suruali aliyokuwa amevaa na mbwa waliokuwa wamemzunguka mtuhumiwa huyo.

Nuru alitumia mchanga uliokuwa eneo hilo kuwamwagia mbwa waliokuwa wanambwekea bila mafanikio.
Baada ya kumsihi kwa muda mrefu, mahabusu huyo alikubali kutoka na kwenda kuogeshwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kabla ya kurejeshwa tena mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mengine mawili.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, Adrian Kilimi, mahabusu huyo alidaiwa kuharibu mali za

Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makusudi, kudharau mahakama na kuzuia shughuli za chombo hicho.
Mwendesha Mashtaka, Wambali alidai kuwa mshtakiwa alifanya makosa hayo Novemba 30, mwaka huu, saa 3:00 asubuhi katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma.

Wambali alidai mahabusu huyo aliharibu mlango wa choo na thamani ya mali katika mabano (Sh. 18,000), sinki la choo (Sh. 20,000), sakafu (Sh. 90,000) na mlango wa mahabusu (Sh. 30,000).

Mshtakiwa alikana mashtaka yote na kurejeshwa mahabusu chini ya ulinzi mkali wa polisi hadi leo ambapo kesi yake itatajwa tena.
Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na shtaka la mauaji na kesi yake inasikilizwa na Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, Elias Anangise.

CHANZO: NIPASHE
attachment.php
 

Attachments

  • Mavi.jpg
    Mavi.jpg
    21.7 KB · Views: 81
Back
Top Bottom