Magufuli aivaa Tanesco | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Magufuli aivaa Tanesco

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, May 3, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 3, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli


  Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametoa siku saba kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuondoa nguzo za umeme zilizopo katika hifadhi ya barabara ili kupisha mradi wa ujenzi wa Mabasi yaendayo Kasi (Dart), vinginevyo Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) itazing’oa.

  Tamko hilo alilitoa jana jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea Dart na pia kufahamu changamoto ambazo zinawakabili katika kuendesha shughuli hiyo.

  Dk. Magufuli alifikia uamuzi huo jana alipofika eneo la Ubungo Plaza ambako kampuni ya Stra Bag ya Ujerumani ambayo imepewa kazi ya kujenga barabara ya magari yaendayo kasi, imejenga kituo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vyake vya ujenzi.

  Pia, alimtaka mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo itakayokuwa na vipande sambamba na barabara ya Morogoro, maeneo ya Kimara- Ubungo, Morocco- Magomeni, Jangwani - Fire – Kariakoo na Kivukoni, kueleza kama kuna changamoto yoyote ambayo inamkabili katika kutekeleza mradi huo.
  Mkandarasi huyo alieleza kuwa miundombinu ya umeme zikiwemo nguzo zilizopo katika mradi huo, mabomba ya maji na majengo mengine ambayo yanatakiwa kuondolewa yamekuwa ni kikwanzo katika kutekeleza mradi.

  Aidha, alisema baadhi ya vifaa vyao vimekwama bandarini hali ambayo inaathiri utendaji wa kazi na kujikuta wakifanya kazi katika mazingira magumu.

  Baada ya kusikia changamoto hizo, Dk. Magufuli alisema kuwa Tanesco inatakiwa kutoa nguzo zao kwa haraka katika kipindi hicho cha siku saba na wasipofanya hivyo Tanroads watazing’oa ili mradi huo uendelee.

  Dk. Magufuli alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Tanroad, Patrick Mfugale, kuhakikisha analisimamia suala hilo na endapo Tanesco haitatoa nguzo hizo wazitoe ili mradi huo usikwame.

  Kuhusu miundombimu ya maji, Waziri Magufuli alisema atakutana na Waziri wa Maji, kukwama kwa vifaa bandarini atakutana na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

  “Nitawafuata na kuzungumza nao endapo wakinigomea nitalipeleka suala hili kwa mkubwa wangu,” alisema bila kumtaja jina na kuongeza: Kwanini vifaa vyao vikwame bandarini na huu mradi ni maendeleo kwa wote na Rais ndiye aliyekubali mradi huo.”

  AZUNGUMZIA BOMOABOMOA

  Hata hivyo, Dk. Magufuli amewataka wananchi wote ambao wamejenga nyumba zao ndani ya hifadhi ya mradi huo waondoke kwa haraka kabla ya kubomolewa.

  Alisema hayupo tayari kuona wananchi hao wanaukwamisha mradi huo kwani hata sheria hairuhusu mtu kujenga ndani ya hifadhi ya barabara.

  Dk. Magufuli alisema kuwa hata wakikimbilia mahakamani hawatashinda kesi kwani mahakama ni chombo ambacho kinafuata sheria na wao katika suala hilo wamefanya hivyo.

  “Waliojenga ndani ya barabara waanze kuondoka kabla ya kuguswa na wajue hata wakikimbilia mahakamani hawashindi kesi, hivyo wasiucheleweshe huo mradi wa magari yaendayo kasi kwani sheria ni msumeno na haina chama,” alisema.

  Alisema mtu ambaye atalipwa fidia kwa mujibu wa sheria ni yule ambaye amekutwa na barabara na siyo aliyevamia ndani ya hifadhi ya barabara.

  Dk. Magufuli alisema kuwa mkandarasi huyo amepewa kazi ya kujenga barabara za mradi ambapo ujenzi huo utagharimu Sh. bilioni 240.

  Alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili akamilishe ujenzi huo kabla ya muda aliopewa miezi 36.

  Alisema eneo la Fire litakuwa na barabara nane na pia eneo la Kivukoni litakuwa na barabara nne huku maeneo mengine yakiwa na barabara sita.

  AKAGUA UJENZI BARABARA YA MWENGE-TEGETA

  Baada ya hapo Dk. Magufuli alizungukia ujenzi wa barabara ya Mwenge-Tegeta ambapo alimtaka mkandarasi kuhakikisha anamaliza ujenzi wa madaraja kwa wakati bila kutoa kisingizio cha mvua kunyesha.

  Alisema sababu za mkandarasi kudai kuongezewa muda kutokana na mvua kunyesha katika ujenzi wa madaraja hakubaliani nalo na kwamba wamalize kazi kwa muda uliopangwa na siyo vinginevyo.

  “Wajipange jinsi ya kufidia muda wao ili wamalize kwa wakati hayo madaraja madogo madogo 38 na sio wasingizie kuwa mvua kubwa imenyesha,” alisema.

  Aidha, alisema ujenzi wa barabara hiyo unagharimu Sh. bilioni 88 na ujenzi wa vituo saba vikubwa utagharimu ni Sh. bilioni 48.

  Dk. Magufuli alisisitiza kuhakikisha katika mradi huo ajira zitolewa kwa vijana ukiwa mkakati wa kupambana na umasikini.

  Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, alisema kuwa mradi huo utasaidia kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa na pia kuwawezesha wakazi wa Jiji kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

  Alisema jambo la msingi katika kutekeleza mradi huo ni wananchi kufuata sheria na siyo kupingana na serikali.

  Mahiza alisema vijana watakaopatiwa ajira wanatakiwa kuwa waaaminifu na kuachana na tabia za wizi kwani watakuwa wanakwamisha mradi huo.

  CHANZO: NIPASHE

   
Loading...