SoC04 Mageuzi ya kiuchumi na fursa la ongezeko la watu duniani

Tanzania Tuitakayo competition threads

ZMK24

Member
May 2, 2024
6
23
UTANGULIZI
Ningependa kumshukuru Mwenyezi MUNGU kwa fursa hii adhimu, ya kuleta mapendekezo chanya kwa maendeleo ya Taifa letu. Ningependa kuanza kwa kuuliza, Je Tanzania tuitakayo ni ipi? Ni Marekani ya sasa yenye ushawishi wa kiuchumi Duniani? Au ni Dubai ya sasa yenye majengo marefu ya kuvutia? Au ni China ya sasa yenye maelfu ya biashara nyingi Duniani? Nafikiri taswira ya Tanzania tuitakayo tulikwisha ipanga kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa kufikia 2025, ambapo ililenga maeneo makuu (5).
  • Maisha bora na mazuri, kwa kila Mtanzania
  • Amani, Utulivu na Umoja
  • Utawala na Uongozi bora
  • Jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza
  • Uchumi wenye nguvu na uwezo wa kiushindani.
Nitajikita kwenye lengo namba 5 la Uchumi wenye nguvu na shindani.

HALI YA UCHUMI NCHINI
Upande mmoja wa shilingi, Toka tulipopata uhuru wetu mwaka 1961, tumebahatika kupata viongonzi werevu, hodari, na wazalendo. Lakini kwa bahati isiyo yetu tumeshindwa kuepuka mitego ya kiuchumi na kimaendeleo unaozikumba nchi nyingi zinazoendelea hasa Afrika. Mfano, hulka ya kutegemea wahisani, fikra duni za kimaendeleo na mipango mibaya ya utekelezaji, Uchumi dhaifu, mambo ambayo tuliyapinga vikali, kwenye mpango wa utekelezwaji wa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.

Katika ripoti ya mwaka 2023 ya nchi zinazoendelea (LDC’s) iliyochapishwa na UNCTAD. Tangu mwaka 2018 Nchi zinazoendelea zinatumia gharama kubwa kulipa mikopo kuliko kuwekeza kwenye sekta ya elimu na afya. Kuyaakisi hayo katika mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2024/25 Serikali itatenga shilingi za Tanzania 3,517,119,635,000 kulipa deni la nje, ikiwa ni kiasi kikubwa kuliko bajeti iliyoombwa na Wizara ya Elimu takribani shilingi za Tanzania 1,968,212,534,000 (Wizara ya Fedha).
Pia, nakisi ya urari (deficit in balance of payment) imezidi kuongezeka, kufikia dola za Marekani milioni 4,441.2 mwaka 2023, kutoka dola za Marekani 2516.1 mnamo 2022. (Wizara ya Fedha, 2023).

Upande wa pili wa shilingi, Tutoe pongezi kwa nchi yetu na uongozi wa awamu ya sita unaongozwa na Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza, kukamilisha na kuanzisha miradi mikubwa yenye tija kwenye uchumi wa taifa letu na kizazi kijacho na kuhakikisha tunakuwa na uchumi shindani na wenye nguvu. Mfano mradi wa SGR, Miradi mikubwa ya kufua umeme Julius Nyerere MW 2115, Miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ya viwango vya juu, Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Ununuzi wa ndege na uboreshwaji wa shirika la ndege na miradi mengineyo mingi.

Screenshot 2024-05-10 at 12-29-10 Microsoft Word - Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023....png

Picha (Ripoti ya Wizara ya Fedha 2023/24)



TATHMINI YA ONGEZEKO LA WATU TANZANIA, AFRIKA NA DUNIA KWA UJUMLA.
Katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania ilikuwa na watu takribani milioni 44, na kwa mwaka 2022 takribani watu milioni 64. Afrika Mashariki kwa mwaka 2012 ilikuwa na watu takribani 361,335,000 na kwa mwaka 2022 takribani watu 471,705,000, ongezeko la watu takribani milioni 110 sawa na ongezeko la 30%. (UNCTAD handbook of statistics). Kulingana na machapisho ya Umoja wa Mataifa (UN) Dunia inakadiriwa kuwa na watu wapatao bilioni 8, na kufikia mwaka 2050 kuwa na watu bilioni 9.7, ongezeko la watu bilioni 1.7. Kuongezeka kwa idadi hizo kunahatarisha ongezeko kubwa la uhitaji wa chakula. Tukilitazamia hili kama fursa tunaweza kubadilisha mtazamo na kuhakikisha Tanzania inakuwa na Uchumi wa kujitegemea na shindani kupitia uzalishaji mkubwa wa chakula.

MAPENDEKEZO
1. Kuongezeka moja kwa moja kwa uwekezaji wa kigeni (Foreign Direct Investment).

China Economic RiseWayne M. Morrison, pg 13, 2013. Ilieleza kwamba kulikuwa na takribani mashirika ya kibiashara kutoka nje 445,244 yaliyoandikishwa China 2010, na yalichangia kuajiri wazawa millioni 55.2, sawa na 15.9% ya nguvu kazi ya mjini.

History of the American Economy” toleo la 12, Gary M. Walton. Inaelezea msingi wa kiuchumi wa Amerika na mchango mkubwa uliotokana na uvamizi wa wageni, na kuongeza uwekezaji wa ndani kutoka mataifa mbali mbali kati ya 1800-1900.

Sipendekezi kwa kuiga kutoka mataifa hayo mawili, La hasha! Bali ni ukweli kuwa nchi yetu hatuwezi kuzalisha mitaji ya kutosha kuwekeza kwa teknolojia ya juu katika sekta zote tunazozilenga. Kuongezeka kwa uwekezaji wa moja kwa moja kutasaidia kutatua tatizo la nakisi ya urari kwenye biashara za kimataifa na uchumi tegemezi. Hili linawezekana kwa kufanya yafatayo.

  • Kuhakikishia upatikanaji wa malighafi kwa 100% kutoka soko la ndani, Mfano nchi yetu tunaongoza kusafirisha sana madini, kama dhahabu, almasi, chuma nakadhalika, lakini sina uhakika kama kuna kiwanda kikubwa nchini cha kutengeneza saa, mikufu na bidhaa nyingine zitokanazo na madini hayo.
  • Msamaha wa kodi kwenye uanzilishi wa biashara na uingizwaji wa malighafi nyingine zinazosaidia uzalishaji wa bidhaa husika kwa muda miaka (3-5), ili kuongeza uwekezaji.
2. Mageuzi na mabadiliko katika kilimo cha chakula.
Nafahamu ya kuwa serikali inatekeleza miradi mikubwa ya kilimo kama vile BBT (Building Better Tomorrow), na jitihada nyingine kama utoaji wa ruzuku kwenye mbolea, na kuwekeza kwenye utafiti wa mbegu. Nafikiri kwa mtazamo wangu nchi yetu inahitaji mageuzi na mabadiliko kwenye sekta ya kilimo. Nafikiri “TANZANIA TUITAKAYO” kwa miaka 25 ijayo inaweza kuwa nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula Afrika na Duniani, kama tukiwekeza nguvu kwenye kilimo cha chakula.

Nini kifanyike kwenye kilimo cha chakula:

  • Uundwaji wa sera za kiuchumi kwenye kilimo, Mfano “Kilimo Chetu, Chakula Chetu, Maendeleo Yetu”. Sera ambazo zitaamsha ari na morari kwa wakulima wadogo na wakubwa kuongeza juhudi na bidi kwenye uzalishaji wa chakula.
  • Kuwe na malengo yanayopimika “Quantitative targets” Wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Serizali za mitaa, wawatambue wakulima wote nchini wa vyakula, uwezo wao wa kuzalisha na jinsi gani wataweza kuongeza uzalishaji wao. Ili kutanua soko la ndani na nje la chakula kwa miaka ijayo.
  • Serikali ijikite moja kwa moja katika ununuaji wa mazao ya chakula na uuzaji wa ndani na nje ya nchi (Monopoly), ili kuwapa chachu wakulima ya kwamba wana soko la uhakika, Na wakulima wadogo na wakubwa waweze kunufaika na bei shindani za mazao katika soko la dunia.
HITIMISHO
Kwa ukamilifu, kama Tanzania tunaweza kuongeza uwekezaji kutoka nje ndani ya nchi yetu, na pia uzalishaji wa chakula kwa mawazo pendekezwa apo juu au mawazo mbadala naamini hatutakuwa hapa tulipo miaka 25 ijayo kwenye lengo la uchumi wenye nguvu na shindani.
 
Nafikiri taswira ya Tanzania tuitakayo tulikwisha ipanga kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa kufikia 2025, ambapo ililenga maeneo makuu (5).
  • Maisha bora na mazuri, kwa kila Mtanzania
  • Amani, Utulivu na Umoja
  • Utawala na Uongozi bora
  • Jamii iliyoelimika na inayopenda kujifunza
  • Uchumi wenye nguvu na uwezo wa kiushindani.
Ebhana eeeh! Kumbe Taifa tayari liko na tafsiri ya maendeleo ilokaa poa hivii. Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka sasa👌🏽

Tukilitazamia hili kama fursa tunaweza kubadilisha mtazamo na kuhakikisha Tanzania inakuwa na Uchumi wa kujitegemea na shindani kupitia uzalishaji mkubwa wa chakula.
Umeenda na ile kwamba watu ni soko sio janga......

  • kutanua soko la ndani na nje la chakula kwa miaka ijayo.
  • Serikali ijikite moja kwa moja katika ununuaji wa mazao ya chakula na uuzaji wa ndani na nje ya nchi (Monopoly), ili kuwapa chachu wakulima ya kwamba wana soko la uhakika, Na wakulima wadogo na wakubwa waweze kunufaika na bei shindani za mazao katika soko la dunia.
Naaam, ukilijibu suala la soko, basi tuna hatua kubwa kuelekea kukipa thamani zaidi kilimo na uzalishaji wowote. Ahsante.
 
Ebhana eeeh! Kumbe Taifa tayari liko na tafsiri ya maendeleo ilokaa poa hivii. Hii ndiyo Tanzania tunayoitaka sasa👌🏽


Umeenda na ile kwamba watu ni soko sio janga......


Naaam, ukilijibu suala la soko, basi tuna hatua kubwa kuelekea kukipa thamani zaidi kilimo na uzalishaji wowote. Ahsante.
Tuko pamoja mtaalamu, Ni kweli ya kwamba idadi kubwa ya ongezeko la watu duniani ni ngumu kulizuia.

Kuthibitisha ilo nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania zinatekeleza sera nyingi za uzazi wa mpango ilhali bado ongezeko la watu linaongezeka kwa spidi kubwa.

Tukiligeuza na kuwa fursa hasa kwenye sekta mama nchini (Kilimo) naamini tunaweza kuwa na Uchumi imara na tukaipata Tanzania Tuitakayo, sio kwa miaka 25 tu, bali karne na karne.

Kuna msemo wa kibiashara unasema "MTAJI NI WATU"
 
Back
Top Bottom