Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,411
UKAGUZI wa hesabu za fedha za Halmashauri ya Jiji la Arusha uliofanywa na Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor) umeibua ‘madudu’ ya baadhi ya watendaji wa Jiji hilo, ikibainika kuchotwa kwa mamilioni miezi minne tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Ukaguzi huo umefanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni za fedha za serikali za mitaa (LAFM) ya mwaka 2009 na (LAAM) ya mwaka 2009 na kanuni za ununuzi za mwaka 2013, sambamba na maelekezo ya kamati ya fedha.
Kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi huo ambao Raia Mwema imeona nakala yake, fedha zilizopotea ni zaidi ya milioni 500, kati ya mwezi Julai 2014 na Juni 2015, ikiwa ni miezi minne kabla ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba, mwaka jana.
Hali hiyo inatokana kinachoelezwa kuwa ni udhaifu mkubwa wa wakala wa kukusanya mapato ya halmashauri ambaye ni kampuni maarufu ya Max-Malipo inayojishughulisha na biashara fedha kwa njia ya mtandao.
Kampuni hiyo ya Max-Malipo iliingia mkataba unaodaiwa kuwa na utata mkubwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha Julai mwaka jana, kwa shinikizo kubwa la Mkurugenzi wa Jiji, Idd Juma, pamoja na baadhi ya madiwani wakiwamo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa wakati huo.
Mapato yalivyopotea
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu, imegundulika kuwa mapato yanayokusanywa na mashine za maxcom yalishuka badala ya kuongezeka.
“Wakati wa ukaguzi na ukusanyaji wa mapato kwa vyanzo vinavyokusanywa na mashine za maxcom, masoko, vituo vya mabasi, vyoo na machinjio mapato yamepungua kwa asilimia 40 tofauti na kipindi cha awali makusanyo yalipokuwa yanafanywa na mawakala,” inasomeka sehemu ya taarifa ya ukaguzi huo.
Inaendelea zaidi: “Mapato yanashuka kutokana na wakusanya mapato kutotoa stakabadhi za mashine kwa wateja na kusababisha makato hayo yasiyokatiwa stakabadhi kutoingia halmashauri, kinyume cha kanuni za fedha za serikali za mitaa”.
Pamoja na taarifa hiyo ya ukaguzi, habari kutoka ndani ya Jiji zinadai kuwa halmashauri imeingia hasara kubwa ya kupoteza mapato yake kutokana na mfumo huo na mkataba ambao unadaiwa kuwa umejaa utapeli.
Akitoa mfano wa hasara hiyo, mmoja wa watumishi wa halmashauri aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alieleza kuwa kabla ya kuingia mkataba na Max-Malipo wakala aliyekuwa akisimamia choo cha Soko la Kilombero alikuwa anawasilisha kiasi cha shilingi milioni 1.5 kwa mwezi.“Kwa Max-Malipo mapato yameshuka na pia halmashauri inalazimika kulipa gharama za uendeshaji kama maji na umeme kila mwezi kati ya shilingi 500,000 na 800,000 pamoja na mshahara wa msimamizi, hivyo kukosa mapato kwa asilimia 50,” alidai mtoa taarifa huyo.
Takwimu za ukaguzi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya Machi ,Aprili na Mei mwaka 2015 kabla ya kuingia mkataba na Max-Malipo Halmashauri ya Jiji la Arusha ilikuwa inakusanya wastani wa shilingi 95,225,018 kwa mwezi.Fedha hizo ni kutoka vyanzo vya mapato vya vituo vyote vya mabasi, vyoo vya umma, machinjio na masoko yote ya Jiji.Taarifa hiyo inabainisha kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu kampuni ya Max-Malipo ilikusanya wastani wa shilingi 56,768,104 na 83,296072, hivyo halmashauri kupoteza zaidi ya shilingi milioni 100.
Ufisadi Arusha Meat
Aidha ufisadi mkubwa umebainika katika ukaguzi huo, katika kampuni tanzu ya Arusha Meat inayomilikiwa na Jiji ambayo inasimamia machinjio ya Jiji na kiwanda cha kusindika nyama cha Arusha Meat.Ukaguzi huo unaonyesha kuwa kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za matumizi ya fedha za serikali kutokana na usimamizi mbovu wa Mkurugenzi wa Jiji, mweka hazina na watumishi wa kiwanda hicho.
Miongoni mwa mfano wa matumizi mabaya ya kanuni za fedha ni kukosekana kwa hati za malipo (Invoice) yenye thamani ya shilingi 178,164,308 kati ya Julai 2014 na Juni 2015.
Ukaguzi unaonyeha kuwa katika kipindi hicho malipo yenye thamani ya shilingi 64,604,574 pia yalikosa uthibitisho na viambatanisho halali kinyume cha sheria namba 10 ya kifungu cha 2 (d) cha mwaka 2010, kinachohusiana na usimamizi wa fedha za serikali za mitaa.
Pia ilibainika kuwa fedha za mauzo ya duka la nyama la kampuni hiyo lililopo eneo la Nanenane katika Jiji la Arusha kiasi cha shilingi 9,614,000 hazikuwasilishwa benki kinyume cha sheria ya fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2010, namba 37 kifungu cha tatu.
Mkaguzi huyo anafafanua kuwa hatua ya kutopelekwa kwa fedha hizo benki kumesababisha kampuni hiyo kukosa uwazi na kuzua upotevu wa fedha za umma.
Ukaguzi huo umeendelea kubainisha kuwa kampuni hiyo ya nyama pia imepoteza kiasi cha shilingi 16,635,320 kati ya Julai 2014 na Juni 2015, kabla ya kuwasilishwa benki na hakukuwa na vielelezo vyovyote vya matumizi ya fedha hizo.
Aidha pia imebainika kuwa kati ya siku 4 hadi 54 daktari msimamizi wa ukaguzi wa nyama katika kiwanda hicho hakuwasilisha benki malipo ya shilingi milioni 15,770,000, kinyume cha sheria ya fedha za serikali za mitaa namba tano na 50 ya mwaka 2009.
Katika idara nyingine za halmashauri, ukaguzi unaonyesha kuwa katika kipindi cha Julai 2015 na Septemba 2015 kiasi cha shilingi 12,280,750 zimelipwa kwa wadai mbalimbali (creditors) ambao hawako katika orodha ya wadai wa Jiji.
Taarifa hiyo inaendelea: “Pia hati za malipo zenye thamani ya shilingi 339,044,587,22 katika idara mbalimbali za halmashauri zilikosekana kati ya Julai 2015 na Septemba 2015”
Pia watumishi 49 wa Jiji walishindwa kurejesha masurufu wala kuingizwa katika rejista yenye thamani ya shilingi 144,777,100.45, wakiwamo maofisa wa ngazi za juu katika Jiji hilo.
Majina ya watumishi hao 49 na kiasi cha fedha za masurufu ambayo hayakurejeshwa zimembatanishwa katika taarifa ya ukaguzi huo.
Kwa ujumla ripoti hiyo ya ukaguzi imejaa ‘madudu’ mengi yanayofanya halmashauri hiyo kuendeleza rekodi yake ya muda mrefu kuwa halmashauri inayoongoza kwa vitendo vya kifisadi pamoja na kuwa na vyanzo lukuki vya mapato.
Ufisadi huo mpya ni tofauti na upotevu wa fedha zinazokadiriwa kufikia shilingi bilioni 22 baada ya halmashauri kushindwa kukusanya kodi ya pango katika maduka na vizimba zaidi ya 286 kati ya mwaka 2006-2016.
Taarifa hizo za ufisadi ziliripotiwa na gazeti hili katika toleo lake la wiki iliyopita ambapo imebainika kuwa maduka hayo yanamilikiwa na baadhi ya viongozi wa serikali na Halmashauri ya Jiji, makada wa CCM wakiwamo, pia baadhi ya madiwani walioshindwa katika uchaguzi wa mwaka jana.
Maduka hayo yanajumuisha maduka 27 yaliyokuwa chini mfanyabiashara maarufu Morris Makoye ambaye pia ni diwani wa kata ya Ukaoni, katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini na pia alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kati ya mwaka 2010-2015.
Kauli za viongozi wa Jiji
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Idd Juma hakupatikana kufafanua juu ya taarifa hiyo ya ukaguzi, ikielezwa kuwa alikuwa safarini kikazi mkoani Dodoma.
Msemaji wa Jiji, Ntegejwa Hosea, hakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa gazeti hili baada ya kueleza kuwa angetoa taarifa ya maandishi kuhusu tuhuma za ufisadi na uzembe wa watumishi wa Jiji.
Hata hivyo hadi mwishoni mwa wiki hakuna taarifa yoyote ya maandishi iliyolifikia Raia Mwema na msemaji huyo hakupokea tena simu yake kila alipotafutwa.Kwa uapnde wake Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema hana taarifa ya ukaguzi huo kwa kuwa haijawasilisha bado katika vikao vya Baraza la Madiwani hivyo asingeweza kuizungumzia.
“Ningekuwa katika nafasi nzuri kama ingewasilishwa mbele ya vikao vyetu na tukaijadili, hivyo siwezi kuizungumzia taarifa hiyo kwa sababu hatujaijadili,” alisema Meya Lazaro. Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Kampuni ya Max-Malipo, Juma Rajab, pia hazikuweza kufanikiwa hadi mwishoni mwa wiki.
Ukaguzi huo utakapowekwa hadharani unaweza kumweka katika wakati mgumu Mkurugenzi, Idd Juma, pamoja na watendaji wake wa juu kutokana na msimamo mkali wa madiwani wa Jiji la Arusha linaloongozwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Chanzo: Raia Mwema