Mfumo wa Ubia Kati ya Serikali na Sekta Binafsi: Suluhisho la Kupunguza Mzigo wa Kodi kwa Wananchi

Rorscharch

JF-Expert Member
Jul 22, 2013
549
1,165
Nilipata bahati ya kufanya mafunzo ya vitendo (field) Halmashauri ya Jiji la Mwanza mwaka 2012, ambapo nilikutana na Muisraeli aliyekuwa sehemu ya exchange program kati ya halmashauri yake na Jiji la Mwanza.

Alionyesha mshangao mkubwa jinsi halmashauri zetu zinavyoshindwa kupanua vyanzo vya mapato. Alitufundisha mambo mengi, likiwemo la kuvutia sana kwamba serikali ya Israel kupitia halmashauri zake ndiyo wawekezaji wa kwanza nchini mwao. Alitolea mfano mfanyabiashara anapotaka kununua au kukodisha ardhi ya serikali. Badala ya kuuzia au kukodisha ardhi hiyo moja kwa moja, halmashauri husisitiza kuingia ubia na mfanyabiashara huyo. Halmashauri inaweza hata kuongeza mtaji wake kama hisa katika uwekezaji huo.

Alieleza kuwa mfumo huu una faida nyingi. Moja ya faida hizo ni kupunguza mzigo wa kodi kwa mwananchi wa kawaida kwa kuwa ni vigumu kwa wafanyabiashara kukwepa kodi. Serikali kama mwanahisa katika biashara hizo inahakikisha mapato yanaimarika, na hatimaye mzigo wa kifedha kwa wananchi unapungua.

Wakati wa majadiliano, mdau mmoja alionyesha kuwa hata Tanzania kuna mifano ya hali hiyo, kama ubia katika makampuni ya simu. Muisraeli hakupinga, lakini alisisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa mfumo huu katika sekta mbalimbali. Alisema hata kwa biashara ndogo kama saluni, halmashauri inaweza kuwa muwekezaji wa kwanza.

Pia aligusia jinsi mfumo huo umekuza bajeti na kusaidia maendeleo ya corporate social responsibility (CSR). Makampuni yamejenga utamaduni wa kurudisha kwa jamii kwa njia mbalimbali, kama vile kudhamini miradi ya usafi (nikawaza kwa jinsi soko kama Buguruni lingefaidi sana iwapo serikali ingekuwa mshiriki wa moja kwa moja katika maboresho yake badala ya kukusanya mapato peke yake)

Muisraeli huyo pia alikosoa maamuzi ya mipango miji yetu ambayo kwa mtazamo wake “hayana mantiki ya kibiashara.” Alishangaa kuona halmashauri zikihamisha wafanyabiashara kutoka maeneo yenye watu wengi kwenda maeneo ambapo biashara zao hushuka. Alieleza kuwa mambo kama hayo hayawezi kutokea iwapo halmashauri zingekuwa sehemu ya maendeleo ya biashara hizo.

Zaidi ya hayo, alielezea jinsi Israel inavyoshirikisha sekta binafsi kuhudumia open spaces kama mbuga za umma. Alisema, “Ukiona mbuga za umma zikiwa safi, zenye miundombinu mizuri kama sehemu za michezo ya watoto na maji ya kunywa, basi ujue sekta binafsi ndiyo inayohusika, si serikali.” Mfumo huu umewezesha hata kusaidia vituo vya watoto yatima kwa namna endelevu.

Kwa kweli, mazungumzo haya yalikuwa yenye manufaa makubwa kwangu. Nilijifunza mengi kutoka kwa Muisraeli huyo, hasa juu ya ubunifu wa mifumo ya usimamizi wa halmashauri na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
 
Back
Top Bottom