Madini yenye thamani (Blue Copper) yagundulika Tunduru!

Madini yenye thamani (Blue Copper) yagundulika Tunduru!

Informer

Platinum Member
Joined
Jul 29, 2006
Posts
1,629
Reaction score
6,812
MADINI yenye thamani kubwa aina ya shaba ya bluu(blue copper)yamegundulika katika kata ya Mbesa tarafa ya Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.Kugundulika kwa madini hayo kunaifanya wilaya ya Tunduru kuwa ndiyo wilaya pekee nchini na Afrika Mashariki kuwa na madini ya shaba ya bluu.Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amesema utafiti unaonyesha kuwa tarafa nzima ya Nalasi ina utajiri wa madini hayo ambayo yanaweza kuchangia kuinua uchumi wa wilaya hiyo,mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla wake.

"Utafiti umebaini kuwepo kwa madini ya shaba ya bluu karibu tarafa nzima ya Nalasi hadi mto Ruvuma mpakani na nchi jirani ya Msumbiji na pia madini hayo yamesambaa hadi mpakani na wilaya ya Namtumbo hii ni shaba yenye thamani kubwa '',alisema Nalicho.
Wataalamu wa madini wanaelekeza kuwa madini ya shaba ya bluu yana thamani kuzidi madini ya shaba aina nyingine zote ikiwemo shaba nyekundu ambayo inachimbwa katika nchi jirani ya Zambia.

Hivi sasa wachimbaji wadogo wadogo wa madini hayo wapo katika eneo hilo la madini tangu mwaka 2010 na kwamba utafiti kuhusiana na madini hayo bado unaendelea kabla ya serikali kupitia wizara ya madini kuanzishwa mgodi rasmi wa madini hayo.
Utafiti wa awali wa kijiolojia uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1988 katika eneo la Kata ya Mbesa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma umebaini kuwepo kwa madini mengi aina ya shaba ya bluu (Blue
copper).

blue-copper-madini-tunduru.jpg



Utafiti huo ulifanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kuonyesha kuwepo kwa madini aina ya shaba ya bluu ambapo utafiti wa karibuni uliofanyika mwaka 2010 umebaini ubora wa mashapo ya shaba ya bluu katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya madini, utafiti umebaini kuwa madini ya shaba ya bluu yanaweza kuchimbwa kwa faida na kwamba hatua hii ya utafutaji madini inahitaji utaalam, vifaa vya kisasa na fedha nyingi.

Aidha Serikali inaendelea kuimarisha STAMICO ili iweze kuwa na uwezo wa kufanya shughuli hizo za utafutaji na uchimbaji madini kwa maslahi ya Taifa badala ya kutegemea zaidi kampuni binafasi.
Hata hivyo serikali wilayani Tunduru Imetoa miezi miwili kwa kampuni ya IGA & MWAKI Co. LTD inayo fanya shughuli za uchimbaji wa madini aina ya shaba ya bluu katika Kijiji cha Mbesa Wilayani humo kukamilisha taratibu za kisheria vinginevyo itasimamishwa kuendelea kufanyakazi katika eneo hilo. Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya hiyo Chande Nalicho ametoa agizo hilo baada ya kujionea mambo mengi vikiwemo vitendo vya kuendesha uchimbaji huo huku wakiwa hawana vibali vinavyo waruhusu kuendesha shughuli hizo katika mgodi huo.

"Natoa miezi miwili ambayo mwisho wake utakuwa mwezi Julai mwaka huu muwe mmekamilisha taratibu zote za kisheria vinginevyo nitachukua hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuufunga mgodi huu'',alisisitiza.
Akifafanua taratibu zilizokiukwa na wamiliki wa mgodi huo kaimu afisa mazingira wa Wilaya ya Tunduru Eberhard Halla alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiendesha shughuli hizo bila kufanya tathimini za Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) pamoja na kutokuwa na mikataba ya kisheria kati ya Kampuni na kijiji cha Mbesa ambacho ndiyo mmiliki wa eneo linalochimbwa madini hayo.

Halla amezitaja taratibu nyingine ambazo zimekiukwa na kampuni hiyo kuwa ni pamoja na kutowapatia Wachimbaji wao vifaa vya kujikinga na madhara mbalimbali (Protective gears) yatokanayo na uchimbaji madini hayo hali ambayo inahatarisha afya zao.
Alisema kutokana na kampuni hiyo kutotimiza vigezo hivyo inakiuka kanuni na taratibu zinazo simamia sheria ya mazingira namba 20 ya mwaka 2004 ya uendeshaji wa shughuli za migodi hivyo amewataka viongozi hao kuwasiliana na ofisi za idara ya mazingira ya Halmashauri na ofisi za Baraza la mazingira la Taifa kanda ya Mtwara inayosimamia mazingira ili kukamilisha taratibu hizo.

Wakijibu tuhuma hizo kwa niaba ya Meneja wa kampuni hiyo wataalamu wanaosimamia shughuli za uchimbaji wa madini hayo katika mgodi huo Wahandisi Thomas Katto na Reymond Njota walisema kuwa kampuni hiyo ilishindwa kutimiza taratibu hizo kutokana na Wilaya hiyo kutokuwa na wataalamu walioidhinishwa kukusanya tathimini za mazingira na kutoa Cheti.

Hata hivyo walisema kampuni hiyo inayomiliki eneo la ekari 30 katika milima ya Kijiji cha Mbesa ilianza kuchimba madini hayo mwaka 2010 kwa kutumia Majembe na Sululu na kufanikiwa kuajiri hadi zaidi ya wafanyakazi 70 na kwamba kwa hivi sasa wanatumia vifaa vichache vya kisasa hali iliyosababisha uzalishaji kushuka na kupungua wafanyakazi kutoka 70 hadi 25.
Walisema kushuka kwa kiwango cha upatikanaji wa madini hayo kunatokana pia na Wilaya ya Tunduru na Kampuni hiyo kutokuwa na vifaa vya kisasa na wataalamu wa kuchoronga miamba (Geoloist) hivyo kuchimba madini hayo kwa kubahatisha.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo ina utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ambayo yakichimbwa kwa vifaa vya kisasa yanaweza kuufanya mkoa kupanda juu kiuchumi na wananchi wake wakaondokana na umasikini.
Madini yanayopatikana katika mkoa wa Ruvuma ni makaa ya mawe yaliopo katika wilaya za Mbinga na Songea,madini ya vito yaliyopo wilaya za Tunduru,Mbinga,Namtumbo na Songea, madini ya dhahabu ambayo yanapatikana Mpepo na Ruhekei wilayani Mbinga na madini ya uranium ambayo yanapatikana kwa wingi wilayani Namtumbo.

Mkuu wa mkoa mstaafu Nicodemas Banduka anasema mkoa wa Ruvuma licha ya kuwa gwiji katika uzalishaji wa mazao ya chakula hivi sasa umepata bahati ya kuwa miongoni mwa mikoa michache nchini yenye utajiri mkubwa wa madini mengi.
"Mimi baada ya kustaafu kazi serikalini nikiwa na makampuni fulani ya madini tumefanya tafiti mbalimbali za madini hapa nchini,baada ya tafiti hizo,katika vitabu vya madini vilivyopo makao makuu ya wizara ya nishati na madini, vinaonesha kuwa mkoa wa Ruvuma unaoongoza nchini kwa kuwa na kiwango kikubwa cha madini aina ya makaa ya mawe na chuma",anasisitiza.

Kulingana na utafiti huo mkoa wa Ruvuma unashika nafasi ya pili kwa uwingi wa madini ya dhahabu ambapo nafasi ya kwanza inashikwa na mkoa wa Shinyanga na kwamba madini ya chuma ambayo yameanzia Liganga na madini ya makaa ya mawe yaliyoanzia Mchuchuma yamesambaa na kuenea katika eneo kubwa la mkoa wa Ruvuma.

Chanzo: Fikra Pevu
 
Hi nchi tajiri wa asili, ila hata mimi sijui kwa nini tunakuwa maskini
 
ngoja baba rizimoko awape ndugu zake wamarekani wajichimbie madini yao, tz shamba la bibi
 
Bila manyang'au ya CCM kung'oka madarakani hayo madini si kitu. Umaskini uko palepale!!!!
 
Ni habari njema ila ni laaana kwa uongo tulio nao wa ccm
 
Wamarekani njooni mchukue na hii pia....

"Tanzania nakupenda Tanzaniax2, nami nifanyeje kijana mwenziooooo... Sishindwi na mali nninayoooo, nitakuoa Tanzaniaaaaaa".... Katuni ya O.bama @ Pikabom
 
Nimesahau chemistry kidogo.hivi hii blue copper ndio copper ll sulphate pentahydrate(CuSO4.5H2O)?
Wadau nijuzeni kidogo
 
Kwakuwa hatujui kwanini ni maskini ndio maana nchi ni maskini....

Bad leadership, ufisadi,rushwa,mikataba mibovu kuliko zote dunia watu wanasafirisha mpaka twiga na serikali wanasema haijui.....mchina anachukua madini mpaka mchanga.....wanalalamika tembo wanaisha wakati kiwanda cha kusaga meno kipo humu nchini
 
Utawaona haooo kiguu na njia eti wanaenda kutafuta wawekezaji! Hivi Jeshi letu ni la kutulipua na kusimamia interest za Marekani? Kwanini Jeshi lisitumike kuzalisha kwaniaba ya watanzania? JKT mpaka leo wanafanya mazoezi ya kufyeka na kulima kwenye mawe?! kwanini wasipewe majukumu ya kubuni miradi yenye maslahi mapana kwa Taifa?

Nchi zote zilizoendelea huwa wanatumia makampuni makubwa ya kijeshi kukuza technologia na hata kuuza bidhaa mbali mbali zinazoziingizia nchi kipato kikubwa sana...BAE wametuuzia rader, wanauza mpaka ndege za kivita, Russia, China, USA et al Jeshi kwao ndiyo kitovu na kitivo cha technologia...

Watawala muamke sasa muacha upuuzi wa kufikiri kwa kutumia vitambi vyenu, haakuna free lunch katika dunia hii, hivyo vijicent mnayowekewa huko uswis hamta weza hata kuzichukua maana ni changa la macho...Tutumie rasimilimaliwatu tuliokuwa nayo katika kutumia rasilimali zetu kwa manufaa yetu Watanzania...
 
Nadhani Mfumo wa Kuwa na majimbo utasaidia sana kwa wazawa Kuwa na nguvu za kumiliki rasilimali mahalia kuliko mfumo wa sasa wa kuchakachuliwa na serikali kuu.pili sheria zilizopo bado zinatoa mwanya Mkubwa kwa wakezejali kulipa kodi kidogo Sana,kwa hili wazawa wapewe kipaumbele ktk kuchimba na kuuza.
 
yaani hii nchi tumelalia fweza, tuseme kingine lakini Mungu katupa utajiri wa kutosha. sasa naona pia ametuzawadia watu wapumbavu, waroho, walafi, mafisadi, wabinafsi, kilichopo tuombe Mungu atuondolee hizo laana na kuondoa watu wa aina ya waliopo sasa hivi ili taifa letu liweze kuendelea. kha!
 
Bad leadership, ufisadi,rushwa,mikataba mibovu kuliko zote dunia watu wanasafirisha mpaka twiga na serikali wanasema haijui.....mchina anachukua madini mpaka mchanga.....wanalalamika tembo wanaisha wakati kiwanda cha kusaga meno kipo humu nchini

Mkuu.Umeua. Halafu bado kila siku hatujui kwanini eti sisi ni maskini?
 
Back
Top Bottom