Kuthibitisha hilo tuangalie viashiria. Afrika inakadiriwa kumiliki karibu asilimia 48 ya akiba ya madini yote duniani. Kimsingi, Afrika bado ni mzalishaji mkubwa wa mali ghafi [yakiwamo madini] kwa ajili ya viwanda vya nchi zilizoendelea.
Kwa mfano, kati ya mwaka 1970 – 1975, utafiti na uchimbaji wa mafuta barani Afrika ulichukua asilimia 54.5 ya sekta zote ambapo sekta ya madini ilichukua asilimia 20.3, na viwanda asilimia 9.6 tu. Lakini kati ya 1990 – 2002, uwekezaji katika madini ulipaa kufikia asilimia 54 wakati sekta ya mafuta iliporomoka hadi asilimia 26, na ile ya viwanda kushuka hadi asilimia 5.2 ya sekta zingine.
Kwa Tanzania, tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa, kati ya Kilometa 945,087 za mraba za nchi hii, Kilometa 886,037 za mraba zina utajiri wa madini mbalimbali, na eneo la Kilometa 59,050 lililosalia ni maji, lenye utajiri mwingine wa rasilimali.
Kwa hiyo, kama uvunaji wa madini na rasilimali zingine utaruhusiwa kwa kasi ya sasa, kwa kuwekwa mikononi mwa wawekezaji wa kigeni kwa kile kinachoitwa "kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji", muda si mrefu Tanzania itakuwa koloni la Wazungu kupitia makampuni ya kimataifa ya kuhodhi, yanayowakilisha matakwa ya nchi za Magharibi.
Licha ya utajiri mkubwa wa madini, Afrika bado ni moja ya mabara masikini sana duniani. Kwa mfano, hadi miaka ya karibuni, Angola, Botswana, Jamhuri ya Afrika ya Kati [CAR], Ghana, Liberia, Namibia, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tanzania na DRC, zilizalisha karibu asilimia 70 ya almasi yote duniani, lakini bado ni kati ya nchi masikini, zenye kutembeza "bakuli la omba omba".
Kwa madini ya dhahabu, shaba na vito vingine, Afrika inashikilia asilimia 51 ya soko la dunia, lakini haijaweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kwa nini?
Tofauti na mikataba ya kilaghai ya karne ya 19, mikataba ya sasa ya madini inahusisha ndoa kati ya siasa [wanasiasa] na rushwa kubwa za kimataifa ili kuwapora wananchi haki zao.
Ni kwa sababu hii sasa tunaambiwa na viongozi wetu kwamba mikataba hiyo ni siri ya serikali wakati ni haki ya kila mwananchi kuijua. Kwa nini mikataba mingine ya kimataifa inatangazwa kwa mbwembwe na tafrija ila ya madini tu? Tofauti yake ni nini?
Vivyo hivyo, taarifa za mapato ya sekta hiyo, zenye kukinzana, zinaashiria ufisadi au kuficha ukweli. Kwa mfano, tunaambiwa, kati ya 1992 na 2000, uvunaji wa dhahabu nchini uliongezeka kwa asilimia 266.7; yaani kutoka kilo 409 hadi 15,000 ambapo uzalishaji wa almasi uliongezeka kutoka karati 67,300 hadi 354,500.
Lakini, licha ya ongezeko hilo, chini ya wawekezaji wa kigeni, sekta ya madini ilichangia asilimia 2.5 tu ya pato ghafi la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 15 waliyochangia wachimbaji wadogo wadogo kabla ya kuenguliwa na Wazungu. Hii inaonyesha dhahiri kwamba kuna hujuma inayolindwa.
Serikali nayo, ama haina uhakika na kinachozalishwa au inaficha ukweli kwa hila. Kwa mfano, wakati Wizara ya Mipango ilisema kuwa mauzo ya madini yaliingiza dola milioni 396.1 mwaka 2002, Wizara ya Madini ilidai mauzo yalifikia dola milioni 432.3. Na wakati Wizara ya Mipango ilisema mauzo yalifikia dola milioni 491.1 mwaka 2003, Wizara ya Madini na Nishati ilidai yalikuwa dola milioni 560.2.
Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji dhahabu baada ya Afrika Kusini na Ghana, lakini inasaga meno kwa umasikini, licha ya utajiri mkubwa huo.
Kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya hujuma inayofanywa kwenye sekta ya madini, hatimaye Novemba 22, 2007, Serikali iliunda Tume ya Jaji [Mark] Bomani kuchunguza mikataba hiyo. Matokeo yake ni kuwa, "Ukishangaa la Mussa, la Firauni je?" Hapa ndipo "umangungo" [ujinga] wa Watanzania unapozidi ujinga wa watu wengine, kama inavyothibitishwa na ukweli ufuatao.
Mwaka 2008 uzalishaji dhahabu ulifikia wakia [ounces] 1,170,000. Kwa bei ya dola za Kimarekani 900 iliyotumika. Thamani ya dhahabu iliyouzwa ilikuwa dola bilioni 1,053 tu.
Na kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hulipa mrahaba [kodi] kidogo, kiwango cha asilimia tatu tu ya faida [net back value] kwa sasa, serikali ilipata [kama kweli imelipwa] dola 15,970,500 tu kutokana na uwekezaji huo!
Na kama serikali ingekubali na kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Bomani ya kuongeza kiwango cha mrahaba kufikia asilimia 50 ya faida ya mwekezaji, kama zifanyavyo nchi zingine za Kiafrika, serikali ingeweza kujipatia dola 52,650,000, sawa na Shs. 68,445,000,000.
Ujinga wetu unajidhihirisha pale tunapokubali kudanganywa na makampuni kwamba, gharama za uzalishaji ni kubwa kiwango cha dola 445 kwa wakia. Ujinga huu umetukosesha mapato ya dola 36,680,000, sawa na Shs. 47,680,000,000 kwa mwaka 2008 pekee; ambazo zingetumika kuleta maendeleo kwa wananchi wetu.
Ujinga wetu unakwenda mbali zaidi: Wakati tumekubali kudanganywa kuwa bei ya dhahabu katika soko la dunia ni dola 900 tu kwa wakia, wanunuzi kutoka India, Pakistani na wengineo wanalipa kati ya dola 1,200 na 1,300 kwa wakia huku tukijifanya kutolijua hilo. Kwa nini? Eti tunaweka "mazingira mazuri kwa wawekezaji".
Ilivyo sasa, nchi yetu hainufaiki hata kidogo na sekta ya madini; wanaonufaika ni hawa Wazungu wanaopora utajiri wetu, na sisi kuachiwa mashimo na mazingira yaliyoharibiwa kama urithi wetu.