Mabomu yaivuruga Rufiji | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mabomu yaivuruga Rufiji

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by nngu007, May 22, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  May 22, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  [h=2][/h]JUMANNE, MEI 22, 2012 05:45 WAANDISHI WETU, DAR NA RUFIJI

  *Helkopta za polisi zatanda angani

  *Mali zaporwa kila kona, ng’ombe wachinjwa
  *Maduka, barabara zafungwa matairi yachomwa
  *Polisi wahamishwa usiku kukimbia mkong’oto  KWA siku ya pili mfululizo, mji wa Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani, umeendelea kutikiswa na mapambano makali kati ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kundi kubwa la wakulima, waliokuwa wakipinga wenzao 50, kufikishwa mahakamani.

  Katika hali ambayo haikutarajiwa jana, asubuhi mamia ya wananchi wa Ikwiriri na vijiji vya jirani walikusanyika, huku wakiwa na silaha mbalimbali na kuanza kuwapiga polisi waliokuwa wakitumia magari yao, kwa ajili ya doria kwenye maeneo mbalimbali ili kurejesha hali ya usalama.

  Hali hiyo, ilionekana kushitua uongozi wa Jeshi la polisi mkoa wa Pwani, ambao baada ya kuona wanazidiwa uliamua kuomba msaada zaidi wa FFU kutoka Dar es Salaam, ili kupambana na wananchi hao.

  Mapigano hayo, ambayo yalidumu kwa zaidi ya saa tatu, yalisababisha huduma zote muhimu za kijamii kusimama, huku barabara zote zikiwa zimetapakaa moshi mzito uliosababishwa na matairi yakichomwa na wananchi hao.

  Mbali ya kuongezwa FFU, polisi walilazimika kutumia helkopta kuzunguka mji mzima wa Ikwiriri, ili kubaini wapi wahalifu wa vurugu hizo walipojificha.

  Itakumbukwa mapigano hayo yalianza juzi, baada ya mkulima mmoja Shamte Seif Tawangala (60), kuuawa na wafugaji kutokana na kile kilichodaiwa, kupinga hatua ya wafugaji kuingiza ng’ombe wao kwenye shamba lake kwa ajili ya malisho.

  “Mapigano yalikuwa makali, kila kitu kimesimama hapa, hatujui hatma ya mji huu itakuwaje? Tunaomba jamani Serikali na wananchi wakae chini wafikirie namna ya kumaliza tatizo hili,” alisema mkazi wa eneo hilo, Abdallah Omar.

  “Kwa kweli leo (jana) asubuhi, wakati hawa watuhumiwa 50 wanapelekwa mahakamani, kulizuka tena vurugu nyingine za kuchoma matairi kutoka kwa wakulima, ambao walikuwa wanadai wenzao waachiwe huru, lakini zilizimwa muda mfupi na askari wa FFU," alisema Omar.

  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu aliiambia MTANZANIA, kuwa kumekuwa na hali mbaya kutokana na makundi ya vijana walioamua kuingia mitaani kuendesha uporaji wa mali mbalimbali.

  “Tatizo ambalo lipo pale Ikwiriri ni makundi ya vijana ambao wameamua kuingia mitaani na kuendesha uporaji wa mali mkubwa, mali nyingi zimeibwa, maduka yamevunjwa, maboma ya wafugaji yamevunjwa vibaya.

  Kibaya zaidi vijana hawa waliamua kwenda kwenye maboma na kuanza kuchinja ng’ombe wa wafugaji kwa kutumia nguvu, wamepora fedha ambazo hatujajua ni kiasi gani.

  “Huduma nyingi za kijamii karibu zote zimesimama, hakuna mtu ambaye ameweza kwenda kufungua duka au hoteli, kwa kuhofia usalama mdogo uliopo katika eneo la Ikwiriri,” alisema Kamanda Mangu.

  Alisema kutokana na hali hiyo, polisi wanatumia kila aina ya mbinu kudhibiti hali hiyo, kwani mpaka jana mchana magari ambayo yalikuwa yanaelekea mikoa ya Lindi na Mtwara, yalikuwa yakiendelea na safari zake kama kawaida.

  Kamanda Mangu, alisema jeshi la polisi limeendelea kuweka kambi katika eneo la Ikwiriri, hadi hali ya utulivu itakaporejea.

  Taarifa kutoka Ikwiriri, zinasema hadi kufikia sasa wakulima wanne wamekwisha uawa kwa nyakati tofauti.

  “Kaka hali ni mbaya huku, mapigano tangu saa nne asubuhi ni makali, helkopta za polisi na Defender za kutosha, polisi wanapiga mabomu pamekuwa kama Iraq.

  “Kinachoonekana ni kuwa wakulima wamechoka na haki zao kuishia mikononi mwa wachache, lawama nyingi zimetupwa kwa jeshi la polisi na kwa Mkurugenzi wa wilaya, kwa kuwa wao wanachukua fedha za wafugaji na kufunika kesi zao.

  “Sasa wakulima, wameamua wanachokifanya wanavamia kila nyumba ya mfugaji, (wengi Wasukuma), maduka ya pembejeo yanayomilikiwa na wafugaji wanavunja na kuharibu kila kilichopo ndani,” kilisema chanzo chetu.

  Taarifa hizo, zinaeleza kuwa nyumba ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Rufiji (OCD), ambayo alikuwa anaishi ilivamiwa na kuvunjwa huku kila kitu kilichokuwapo ndani yake kikiharibiwa vibaya.

  “Polisi wanachukua kitu kidogo (pesa kutoka kwa wafugaji), kwa kuwa wao wana fedha nyingi na hili linawaumiza sana wakulima ambao wengi ni masikini kujiona kuwa hawatendewi haki.

  “Na siyo polisi tu hata viongozi wengine wa kiserikali, mkurugenzi wa wilaya na watendaji wake, wakiwamo maofisa kilimo hawana msaada katika kutatua matatizo ya wakulima na jambo hili linaamsha hasira zaidi,” kilisisitiza chanzo hicho.

  Habari zaidi zinasema kuwa aliyekuwa Afisa Tarafa, Ali Msuya pamoja na polisi mmoja aliyejulikana kwa jina la Konstebo Mohamed, wamehamishiwa Wilaya ya Kibaha jana, chini ya ulinzi mkali wa Polisi baada ya wananchi kutaka kuwaua.

  Kuhusu majeruhi, taarifa zinasema idadi imeongezeka, lakini taarifa kutoka kwa mganga wa wilaya zilisema kuwa, hawawezi kutoa idadi kamili kwa kuwa majeruhi wengine hawajafikishwa hospitalini hadi sasa.

  Hadi juzi jioni, watu 11 waliripotiwa kujeruhiwa na 9 kati yao, wamelazwa katika Kituo cha Afya Ikwiriri, huku wawili wakihamishiwa katika Hospitali ya Misheni Mchukwi (Songa), Ikwiriri, baada ya hali zao kuwa mbaya.

  50 WAFIKISHWA MAHAKAMANI

  Katika hatua nyingine, Kamanda Mangu alisema watu 50 wanaotuhumiwa kuhusika katika vurugu hizo jana, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Rufiji, kujibu mashitaka yanayowakabili.

  Alisema watu hao, walifikishwa katika mahakama hiyo ili kusomewa mashitaka mbalimbali, likiwemo la kusababisha kifo cha mkulima wa kijijini hapo na kuipa hasara Serikali kwa kuchoma nyumba tatu za askari.

  Alisema kosa lingine ni kuchoma nyumba nane za wafugaji na duka la Afisa Mifugo wa Kata ya Umwe, aliyejulikana kwa jina moja la Lameck, ambaye anashirikiana na mfugaji Masanja Mabala.

  Alisema katika vurugu hizo watu wengine zaidi walikamatwa, lakini hata hivyo bado hawajatambuliwa kwa majina na idadi yao, hivyo na kuongeza kuwa mpaka sasa jeshi la polisi bado linaendelea na zoezi la kusaka watu wengine wanaodaiwa kuhusika na vurugu hizo ili nao waweze kuchukuliwa hatua.

   
 2. Njowepo

  Njowepo JF-Expert Member

  #2
  May 22, 2012
  Joined: Feb 26, 2008
  Messages: 9,296
  Likes Received: 381
  Trophy Points: 180
  "Kinachoonekana ni kuwa wakulima wamechoka na haki zao kuishia mikononi mwa wachache, lawama nyingi zimetupwa kwa jeshi la polisi na kwa Mkurugenzi wa wilaya, kwa kuwa wao wanachukua fedha za wafugaji na kufunika kesi zao."

  Hii tabia ni common sana maeneo ambayo kuna wafugaji nawapongeza kwa kuchukua sheria mkononi maana apo ndipo serikali itakapowaelewa.Niko na personal experience ya hayo mambo wafugai hutumia kibri ya ela kuzima kelele za wakulima.Big up kwa kutia kiberiti nyumba ya askari wahusika kama fundisho.
  Na hiyo ndio Tanzania mabayo CCM wanaijenga
   
 3. P

  Popompo JF-Expert Member

  #3
  May 22, 2012
  Joined: Nov 9, 2010
  Messages: 411
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 33
  nilipoisikia hii habari jana nilipata kutokuelewa kidogo,polisi siku hizi huwa wanatoa hukumu?na mahakama inafanya nini?sasa kwa kuwa wamepokea rushwa wakashindwa kutenda haki wacha wapate maumivu.:embarassed2::A S embarassed:
   
 4. 1800

  1800 JF-Expert Member

  #4
  May 22, 2012
  Joined: Dec 27, 2010
  Messages: 2,217
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  Huu ni ujumbe kwa serikali kua sasa wananchi sasa wamechoka,kugawa ardhi kiholela kwa wageni kwa mantiki ya kujinufaisha wao na matumbo yao itaitumbukiza nchi pabaya sana!report zinaonyesha Tanzania ni nchi inayo ongoza Africa ambayo inatoa ardhi yake kirahisi sana kwa wageni,leo ni wakulima na wafugaji,itakuja kusambaa wananchi na wawekezaji!
   
 5. M

  MERCYCITY JF-Expert Member

  #5
  May 22, 2012
  Joined: Jan 25, 2012
  Messages: 348
  Likes Received: 198
  Trophy Points: 60
  Rushwa huangamiza Taifa, Polisi na mahakama wanatupeleka pabaya. Kama hamuwezi kutoa haki wananchi watatafuta haki kwa lazima wao wenyewe.
   
 6. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #6
  May 24, 2012
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 9,223
  Likes Received: 1,412
  Trophy Points: 280
  Are you sure wafugaji walioko rufiji waligawiwa ardho na serikali?, ume/unatumia kigezo gani kuwahukumu wafugaji na serikali?
   
Loading...