Mabalozi wadaiwa kufadhili vurugu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mabalozi wadaiwa kufadhili vurugu

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Mwanajamii, Nov 17, 2011.

 1. Mwanajamii

  Mwanajamii JF-Expert Member

  #1
  Nov 17, 2011
  Joined: Mar 5, 2008
  Messages: 7,080
  Likes Received: 15
  Trophy Points: 0
  BAADHI ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, wanadaiwa kuunda mtandao wa kufadhili shughuli za vyama vya siasa na wanaharakati kwa lengo la kuleta vurugu, ikiwamo kwenye mchakato unaoendelea wa kupata Katiba mpya.

  Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alisema hayo jana bungeni wakati wa mjadala wa
  Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 na kuongeza, kwamba umekuwapo mtindo wa baadhi ya mabalozi kuingilia masuala ya kitaifa.

  "Naomba watuache sisi tufanye mambo yetu wenyewe, mabalozi wanawakilisha nchi zao kwetu, lakini wanapotuingilia na kutaka kutuhujumu si vizuri," alisema Ndassa.

  Alisema mbaya zaidi mabalozi hao wamekuwa wakitumia baadhi ya vyama kufanya hivyo, hali ambayo aliilaani na kuwataka kuitumia CCM ambayo ni chama tawala, iwapo wanataka kukaa na kushauriana na vyama.

  "Nchi hii tumejitawala wenyewe miaka 50 sasa, naomba msituingilie," alisema huku akishangiliwa na wabunge wengine.

  Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), alisema kuna chama kimoja hivi karibuni kilipokea ufadhili kutoka nchi fulani (hakuitaja) na sasa chama hicho kinaeneza
  mambo ya uongo.

  Alisema huenda ufadhili huo ulikuwa na masharti kwa chama hicho, ndiyo maana kimeanza kufanya shughuli hizo za kueneza uongo.

  Aliongeza kuwa haiwezekani kikundi cha watu wachache kiwe na haki na uzalendo wa kutaka mawazo yao pekee ndiyo yathaminiwe na kuwakilisha Watanzania zaidi ya milioni 42, hali ambayo alisema inatia shaka kutokana na watu wengine kutumikia mabwana wawili.

  "Nakubali kuwa haiwezekani hata siku moja Watanzania milioni 42 wote tukakubaliana kuwa na wazo moja, lazima kutakuwa na tatizo, ila kinachotakiwa ni kila mmoja kuheshimu mawazo ya mwenzake na si kung'ang'ania kuwa wazo lako ndilo sahihi," alisema.

  Alisema kitendo cha Chadema kutaka Muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza wakati tayari ulishawasilishwa mara ya kwanza na sasa umefanyiwa marekebisho, ni sawa na kuanza safari, gari liharibike badala ya kuendelea na safari urejee nyuma na kuanza upya.

  Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), alisema kuna watu wengine hoja zao zina walakini na
  hivyo kuzihusisha na masuala ya ufadhili.

  "Nawaomba Watanzania wenzangu tusisahau uzalendo wetu, kwa sababu ya ufadhili, na katika hili naiomba Serikali ifanye uchunguzi na watakaobainika kutumiwa na wafadhili kutuvuruga, wachukuliwe hatua," alisema.

  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, alisema Chadema katika hotuba zao, walisema iwapo wakishinda watatengeneza Katiba ndani ya siku 100, lakini wakati mchakato huo ukiendelea, wamedai kuwa unakwenda haraka.

  Alisema sababu za kutoka wabunge hao bungeni na kutojihusisha na mjadala wa Katiba, zinalenga kupotosha wananchi kwa kuwa madai yote wanayoyatoa hayana ukweli.

  Alisema jambo linalosikitisha ni kwamba wapo baadhi ya wasomi wanaodai kuwa kinachojadiliwa kwa sasa bungeni ni Katiba, jambo ambalo si kweli kwani kinachojadiliwa ni
  Muswada wa kutunga sheria ya kutafuta Tume itakayosimamia mchakato wa Katiba.

  Aidha, alisema madai kwamba wananchi hawajashirikishwa kwenye Muswada huo si ya kweli, ambapo alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyesema:"Ukikuta mtu mzima anadanganya watu wazima wenzake, ujue kuna mawili, akili yake imeharibika au anadharau wenzake."

  Aliwataka Watanzania kufahamu kuwa nchi yao ni moja na wote wanaishi humo na iwapo kutokana na upotoshaji unaoendelea Katiba ikikosekana, watakaoikosa ni Watanzania na si watu wengine.

  Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), aliwataka Chadema watafakari msimamo wao potofu, kwani suala hilo la Katiba linahitaji muafaka kwani hoja yao ya kutaka Muswada huo usomwe kwa mara ya kwanza, kikanuni haikubaliki na hata yeye kama mwanasheria anaikataa.

  Alitaka Bunge likatae mtindo ulioibuka bungeni wa kikundi cha watu kuzusha hoja ambazo zinasisitiza na kuhamasisha wasikilizwe huku wakisingizia kuwa wametumwa na wananchi.

  Mbunge wa Viti Maalumu, Stella Manyanya (CCM), alihoji utendaji wa asasi zisizo za serikali (NGOs) ambazo zimeonekana kutoa maoni yao na kuegemea upande mmoja, huku mambo mengi yanayohusu wananchi yakitokea bila zenyewe kuchangia lolote.

  "Kuna matatizo mengi yanaikabili nchi hii, likiwamo tatizo la bei ya mafuta ambalo chanzo chake ni matatizo yanayotokea katika nchi zinazozalisha mafuta hayo, lakini NGOs hizi zimekuwa mstari wa mbele kuilaumu Serikali, mbona kwenye hili hazizungumzi?" Alihoji.

  Hata hiyo, aliiomba Serikali katika Muswada huo kifungu kinachomlinda mwananchi wa kawaida, kwani sasa wamekuwa wakitumika hovyo na kushirikishwa kwenye maandamano bila hata kujua nini kinaendelea na matokeo yake kupotoshwa.

  Mjadala kusogezwa Katika hatua nyingine Muswada huo, huenda ukapitishwa leo au
  kesho baada ya kusogezwa mbele kutokana na kujitokeza kwa idadi kubwa ya wabunge wanaotaka kuuchangia.

  Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, hadi jana walishachangia wabunge takribani 40 na kwa mujibu wa orodha ya walioomba ni 60.

  "Tunachotaka angalau kutokana na umuhimu wa mjadala huu, wachangie wabunge 50, na ili nafasi hiyo ipatikane kwa leo (jana) hauwezi kupita inabidi usogezwe mbele, ili waliobaki wapate nafasi," alisema Joel.

  Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alitaarifiwa kuwa siku ya kupitishwa Muswada huo imesogezwa mbele, lakini hakuwa amefahamishwa lini utahitimishwa.

  Katiba milioni 5 kugawiwa Wakati huo huo Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya,
  itachapisha nakala milioni tano za Katiba ya sasa kwa ajili ya kuwapa wananchi wakati itakapoanza kazi.

  Lengo la kutolewa kwa Katiba hiyo ni kusaidia wananchi kutumia kama mapitio wakati wa kutoa maoni.

  Waziri Kombani alisema kiuhalisia, asilimia ndogo ya Watanzania wameisoma na kuielewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

  Sambamba na hilo, tayari Serikali inachapisha nakala 200,000 na zitagawiwa katika wizara zote, vyuo, shule za sekondari na NGOs.

  Maelezo hayo ya Kombani yalitokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba (CCM), aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kusambaza Katiba ya sasa kwa Watanzania, ili waijue na kufanya mapitio wakati wa kuijadili.

  Chadema warudi bungeni Wakati huo huo, Chadema imeahirisha mkutano wake wa Kamati
  Kuu uliotarajiwa kufanyika leo, ili wabunge wa chama hicho wahudhurie vikao vilivyobaki na hasa wasikie tamko la Kamati Maalumu kuhusu sakata la Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.

  Akizungumza Dodoma jana, Katibu wa Wabunge wa chama hicho, John Mnyika, alisema chama hicho kimebaini kuwa ratiba ya Bunge inaonesha matukio yaliyobaki ni muhimu na si vizuri wabunge wa chama hicho kuyakosa.

  "Tuliomba mkutano wa dharura wa Kamati Kuu na tumekubaliwa, lakini tumeomba ufanyike Jumapili, ili wabunge wa chama hiki waweze kushiriki mijadala iliyobaki," alisema.

  Kwa mujibu wa ratiba leo kutakuwa na maendeleo ya mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Biashara 2011, taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini na Tamko la Kamati Teule ya Bunge.

  Alisema baada ya Bunge kuahirishwa iwapo kutakuwa na shughuli nyingine za wabunge
  keshokutwa, wabunge wa Chadema hawatashiriki kwa kuwa wote wataondoka siku hiyo kwa msafara kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mkutano.

  chanzo: Habari Leo.
   
Loading...