Mabadilishano ya Utamaduni-Vichekesho

Feb 13, 2021
5
5
Kuna tofauti gani baina ya vichekesho vya Kichina na Kiswahili? Tafadhali lete baadhi ya vichekesho vya Kiswahili hapa, tuvilinganishe.


1.NZIGE

Wakati Bwana Bababa alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Kilolo, mwaka mmoja kulitokea jua kali, nzige walionekana kila mahali, bali mkuu wa Wilaya ya Utata alimlaghai mkuu wa mkoa kwa kumwambia:
“Hakuna nzige katika wilaya yetu.”

Siku kadhaa baadaye, palitokea kundi la nzige katika Wilaya ya Utata. Wakati mkuu wa mkoa alipomlaumu mkuu huyo wa Wilaya ya Utata, hakuwa na la kujibu, lakini baada ya kufikiri kwa nukta chache tu alipata jawabu akasema:
“Hapo awali wilaya yetu haikuwa na nzige. Hao nzige walikuja kutoka Wilaya ya Kilolo.”

Basi mkuu wa mkoa alimpelekea Bababa waraka na akamwambia ashughulikie kazi ya kuwaua nzige kwa jitihada iIi wasiruke na kwenda kwenye wilaya ya jirani.

Baada ya kupokea waraka huo, mara Bwana Bababa alimwandikia barua mkuu wa Wilaya ya Utata:
“Nzige ni msiba wa jamii, si kosa langu. Ukisema nzige wametokea kwetu, basi tafadhali uwarudishe!”
aliyesikia alicheka sana.


2.TAJIRI BAHILI

Palikuwa na tajiri mmoja bahili aliyeitwa Chachacha. Siku moja, kaka yake alikuja kumsalimia kutoka kijijini kwao. Alipofika ndipo wakati wa chakula cha jioni. Tajiri Chachacha alipanga kumnyima kaka yake chakula akamwagiza kitwana amwambie kaka yake kwamba ametoka. Kaka wa Chachacha akakaribishwa katika chumba kidogo amngojee tajiri na njaa .

Pale uani pa Chachacha, mbwa alifukuzana na kundi la kuku. Mara Chachacha akamfokea mbwa wake: “Uss! Wacha ukorofi!”
Kwa kusikia makelele ya tajiri, kaka yake akauliza:“Didi upo nyumbani?”
Chachacha akajibu haraka: “Mimi sipo, mke wangu yupo.”
(Katika Kichina “didi” ni ndugu wa kiume mwenye umri mdogo kuliko wewe.)


3. KUSHONA SURUALI

Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Fufufu katika Wilaya Ufefe, naye alimpa mke wake kitambaa kimoja kipya na kumwambia amshonee suruali.

Mke wake alimwuliza amshonee suruali ya mtindo gani. Fufufu alisema, "Sawa na mtindo wa ile suruali kukuu."'
Mke wake alikumbuka maneno yake na alishona suruali moja mpya kwa kuiga suruali kukuu. Kwa ajili ya kuwa sawa kabisa, yeye alichanachana kwa makusudi ile suruali mpya na kutia viraka.
2021/03/05


4. KUUMA PUA

Gugugu na Huhuhu waligombana. Gugugu aliikata pua ya Huhuhu kwa kisu na ikaanguka ardhini. Huhuhu akivumilia maumivu alimshika Gugugu na kumpeleka kwenye korti. Hakimu alitaka kumpa Gugugu adhabu.
Gugugu alisema, " Pua ya Huhuhu ilikatwa na mdomo wake mwenyewe, si na mimi. "

Hakimu alimwuliza "Pua ya mtu iko juu,mdomo uko chini, mdomo wa mtu unawezaje kuikata pua yake na kuanguka chini?"
Gugugu alijibu, "Huhuhu alisimama juu ya kitanda na kuikata pua yake kwa mdomo wake."


5. KULIPA DENI KWA MAISHA YAKE BAADA YA KUNIUA

Mlevi alimshika mzee Kukuku barabarani na kumpiga kwa nguvu. Mzee alijishika nyonga kwa mikono miwili na kusimama pale akihiari kupigwa na mlevi bila ya kusema cho chote wala kumrudishia.
Wapita njia waliona ajabu, wakamwuliza, "Mlevi anakupiga,
mbona husemi cho chote wala kumpiga pia?"
Mzee alijibu, " Akiniua lazima alipe deni kwa maisha yake, Mimi ndiyo ninangoja aniue ili alipe deni kwa maisha yake."


6. MACHO YA JARIBOSI
Kulikuwa na ofisa mmoja aliyeitwa Lululu, alimwita mchoraji aje
amchoree picha.
Mchoraji alipomaliza kuchora picha ya ofisa kwa kufuata sura yake,
akamwonyesha. Baada ya kuona picha hiyo, ofisa alighadhibika , akamlaumu mchoraji, " Juzi ulipochora chui niliona kuwa ulibandika macho yake kwa jaribosi; mimi ni ofisa mkubwa namna hii, kwa nini hukubandika macho yangu kwa jaribosi?"

7. WALI MWEKUNDU NA WALI MWEUPE

Mumumu alifiwa na mama yake. Siku moja, alikula mlo mmoja wa wali uliopikwa kwa mchele mwekundu. Msomi mmoja ashikiliaye kanuni alimwona akamlaumu: "Mtu aliyefiwa, haifai kula wali mwekundul."
Mumumu alimwu1iza sababu. Msomi ashikiliaye kanuni alijibu, "Rangi nyekundu ni rangi ya furaha."
Mumurnu alimwuliza, "Kama ulivyosema ni sawa, basi mtu ye yote
anayekula wali mweupe amefiwa nyumbani?"

8. MSOMI ALIYESTIRI AIBU

Kulikuwa na msomi maskini aliyeitwa Nununu, alipenda kustiri aibu yake. Mara kwa mara alikuwa akisifu kuwa familia yake ina fedha nyingi.
Mwizi mmoja alisikia maneno yake na akadhani kuwa familia yake kweli ina fedha nyingi. Usiku wa siku moja mwizi huyo alikwenda nyumbani kwake kuiba.
Mwizi huyu aligundua kuwa si kama nyumbani kwake hakukuwa na pesa tu bali pia hakukuwa na kitu cho chote cha thamani. Msomi Nununu alisikia manung'uniko ya mwizi, basi alipapasa na kuchukua hela kadhaa alizokuwa nazo tu kutoka mchagoni na akamkimbilia mwizi akamkabidhi huku akisema, " Umekuja kwangu lakini hukupata cho chote, nakuomba uniwie radhi. Ukifika nje tafadhali nistiri aibu yangu, usiambie mtu ye yote
kuwa familia yangu ni maskini hata haina kitu cho chote cha thamani.

9. MGANGATAPELI

Makabwela wengi wa Mji Uzeze walisadiki mgangatapeli mmoja. Palikuwa na jemadari mmoja aliyeitwa Jujuju, naye aliwachukia watu wa ukoo wake ambao waliamini mgangatapeli huyo lakini hakuwa na njia ya kuwafanya wasimwamini. Siku moja, Jujuju aliwaghuri jamaa zake kwa kuficha korosho kadhaa kinywani na akasema kuwa shavu lake lilikuwa limevimba na kumwuma. Siku hiyo nzima hakula chochote ila kupiga kite tu na kulala kitandani. Mke wake aligaya, basi akaenda kumwalika mgangatapeli huyo aje kumtibu. Baada ya kufika, mgangatapeli alisema,“Mume wako amepatwa na ugonjwa wa banguzi, kwa kuwa siku za kawaida hakumheshimu Mungu, kwa hivyo Mungu hakumlinda.”Jamaa wa Jujuju walimzunguka mgangatapeli huyo na kumsujudia, kisha walimwomba amsaidie Jujuju, hatimaye mgangatapeli alikubali.
Jujuju alijifanya kama kwamba alikuwa akiumwa na alipiga kite kitandani, baada ya muda aliwaambia jamaa zake,“Ugonjwa wangu hauwezi kuponyeshwa bila ya kumwalika mgangatapeli aingie chumbani kuniokoa." Baada ya kuingia chumbani mwake, mgangatapeli alibonyeza shavu lake ambalo lilikuwa gumu, wakati mgangatapeli alipotaka kupayuka Jujuju alitema nje polepole zile korosho na kumwonyesha mgangatapeli ili aone. Jujuju hakusema chochote akashika nguo ya mgangatapeli na kumpiga makofi kwa nguvu kwenye mashavu yake mawili, halafu alimfukuza hadi nje ya mlango huku akimtukana. Kuanzia hapo, watu wa ukoo wake hawakuamini mgangatapeli huyo tena.


10. KUMBEBA MDAIWA
Palikuwa na mtu mmoja aliyekopa fedha nyingi kutoka kwa marafiki zake. Bwana Sisisi, mmojawapo wa marafiki hao, alikuja kwake mara nyingi kudai haki lakini mtu huyo hakumlipa. Bwana Sisisi alikasirika, akamtuma mtumishi wake kwenda njiani kumngojea mdaiwa ili akimwona ambebe hadi nyumbani na kumpiga. Mtumishi huyu baada ya kufanikiwa kumpata alimbeba mdaiwa huyu. Alisafiri naye nusu masafa, akachoka, akamweka chini kupumzika.
Mdaiwa alimhimiza, "Twende upesi, usipumzike hapa, ama sivyo nikichukuliwa na mdai mwingine usije ukajuta."


11. KUMKEJELI MGENI

Mgeni mmoja alikuja kumtembelea Bwana Dedede. Walikunywa akari pamoja tangu adhuhuri mpaka jioni, lakini kwa sababu akari ni ya dezo, mgeni huyu bado hakutaka kuondoka. IIi kumkejeli, Bwana Dedede alisimulia hadithi moja, "Katika wilaya fulani palitokea chui mmoja ambaye alikuwa akila watu mara kwa mara. Mfanyabiashara mmoja aliyeuza mitungi ya kuwekea akari alikuja kuuza mitungi yake wilayani humo. Siku moja, alipotembea mlimani ghafla alikutana na chui huyo. Chui alitaka kumvamia. Wakati huo, mfanyabiashara aliamua kuchukua mtungi mmoja na kumtupia lakini chui hakuondoka, halafu alichukua mtungi mwingine na kumtupia tena, chui bado hakukimbia. Hivyohivyo mpaka kukabakia mtungi wa mwisho. Mfanyabiashara alisema kwa sauti kubwa,'Mnyama wee! Uondoke usiondoke, huu ndio mtungi wangu wa mwisho!'"

12. KITI KIFUPI

Mzee Zuzuzu alikuwa na kiti kifupi nyumbani kwake. Kila alipokaa juu yake alikuwa akiweka vigae chini ya miguu ya kiti hicho. Siku moja, alijihisi kufanya hivyo kunampa shida, basi alifikiri njia nyingine. Alimwagiza mjakazi wake akihamishe kile kiti hadi ghorofani. Wakati alipokaa juu ya kiti hicho aliona kilikuwa kifupi kama hapo awali, basi alisema kwa hasira, "Watu husema nyumba ya ghorofa ni ya juu, kumbe ni upuuzi mtupu." Baada ya hapo, Mzee Zuzuzu aliwaambia watumishi wake waivunje ghorofa ya nyumba yake hiyo.

13. KUSIMAMA KWA KUKABILIANA

Kulikuwa na watu wawili, baba Fafafa na mwanawe. Wao wote walipenda kuwashinda watu wengine na kutokubali kushindwa.
SIku moja, Fafafa alimwalika mgeni kuja nyumbani kunywa piwa. Fafafa alimtuma mwanawe kuingia mjini kununua nyama. Mwanawe alinunua tayari nyama humo mjini, akarejea nyumbani.
Alipofika mkabala na lango la mji, mbele yake alikuja mtu mmoja aliyependa kuwashinda wengine pia. Lango lilikuwa limekaribia kufungwa, mwanya mdogo tu ndio uliokuwa umebakia. Watu hao wawili, kila mmoja hakukubali kumpisha mwingine. Walisimama kwa kukabiliana huku wakikodoleana macho bila ya kujali utumwa wake.
Fafafa alipoona mwanawe harejei baada ya kumngoja kwa muda mrefu, akaenda nje kumtafuta. Alipofika kwenye lango la mji tu alimuona mwanawe akiwa amesimama kwa kukabiliana na mtu mwingine, akamwambia mwanawe kwa haraka, "Kwanza peleka nyama nyumbani na kula chakula pamoja na mgeni, mimi nitasimama kwa kukabiliana naye badala yako!"


14. KALENDA

Siku ya mwisho ya mwaka fulani, mgeni mmoja alikuja kumtembelea Ninlni . Mgeni huyu alimtunukia kalenda ya kusherehekea Mwaka Mpya. Ninini pia alimpa mgeni huyo tuzo ya kumshukuru — kalenda kukuu ya mwaka huohuo. Mtumishi wa Ninini alijisemea, "Nafikiri kalenda hii kukuu haitafaa kitu."
Bwana Ninini naye akasema, "Hata nikiibakiza nyumbani pia haitafaa kitu."


15. CHOO
Hapo kale palikuwa na ndugu wawili waliokuwa wakiishi pamoja. Kaka aliitwa Pipipi; didi① aliitwa Ririri. Hawa wawili walitengana baada ya baba yao kufariki dunia.
Pipipi alikuwa mwerevu na Ririri alikuwa mjinga zaidi. Kaka Pipipi alijenga choo kimoja kwenye njia panda. Kila mtu aliyetumia choo hicho alitozwa kiasi fulani cha fedha.
Tangu hapo kila mwaka Pipipi alipata fedha za kutosha kumwendeshea maisha yake. Kwa sababu ya mapato hayo mke wa Ririri alimwonea wivu Pipipi, kwa hivyo alikuwa akimlalamikia na kumtukana mumewe Ririri mara kwa mara kwa kuwa anadhani Ririri hana maarifa ya kutafuta pesa.
Hatimaye, ilimbidi Ririri naye vilevile alijenga choo kimoja kwenye njia panda nyingine. Alichemsha ubongo wakati wa kujenga choo hicho ili kumshinda kaka yake. Alipaka chokaa nyeupe na kuchora picha nzuri juu ya kuta za choo. Choo hicho kilionekana safi na cha kuwapendeza watu, hata wapitanjia wengi walidhani kuwa choo hicho kilikuwa hekalu. Ingawa watu waliopita mbele ya choo hicho walikuwa wengi lakini hakukuwa na mtu hatammoja aliyeingia ndani kujisaidia.
Siku ya pili, Ririri alikaa kando ya mlango wa choo chake. Aliwaomba wapitanjia waingie chooni lakini hawakuingia. Giza lilipoingia Ririri alimshika mpitanjia mmoja na kumwomba, "Karibu chooni!"
Mpitanjia huyu alisema huku akitabasamu, "Ahsante, sina haja."
Ririri hakuweza kuvumilia, akasema kwa hasira, "Kama huna haja kubwa, basi jamba ushuzi mmoja kisha uondoke!

_____________________________________________________
  • " Didi " hurejelea ndugu wa kiume aliyezaliwa baada yako; " meimei " huashiria ndugu wa kike aliyezaliwa baada yako katika China.

16. MWANAMKE MZEMBE

Hapo zamani za kale, palikuwa na mwanamke mmoja mzembe aliyeitwa Momomo. Kazi zote za nyumbani zilifanywa na mume wake Lololo. Yeye mwenyewe alijua tu kuinyoosha mikono wakati alipovalishwa nguo, na kufunua kinywa wakati alipoletewa chakula.
Siku moja, mume wake alitaka kwenda nje kusafiri na baada ya siku tano atarudi. Mume wake alihofia kuwa mkewe atashinda na njaa, basi alimkaangia chapati moja kubwa iliyomtosha kula kwa siku tano, halafu akaitoboa katikati ya chapati na kumvisha shingoni, kisha akafunga safari bila ya jakamoyo.
Mpaka Bwana Lololo aliporejea nyumbani, aligundua kwamba mke wake Momomo alikuwa amesha kufa kwa njaa. Bwana Lololo alishituka sana baada ya kuona kuwa mke wake alikula sehemu ndogo tu ya chapati ambyo ilikuwa karibu na mdomo wake na hakuwahi kuizungusha chapati hiyo hata kidogo.


17. KUWAHI KITI

Palikuwa na bwana mmoja aliyeitwa Sososo. Alikuwa na madeni mengi. Siku moja, wadai wengi walikuja kwake kudai haki zao, hivyo viti vyake vilikuwa vimeenea watu. Mmojawao alikuwa Tototo, ambaye alikosa kiti na aliamua kukaa juu ya kizingiti. Bwana Sososo alimsogelea karibu na kumnong'oneza sikioni mwake, "Kesho asubuhi njoo mapema zaidi ili uwahi kabla ya wenzako."
Tototo alifikiri, "Bila shaka Bwana Sososo anataka kunilipa fedha zangu kwanza." Basi alifurahi moyoni na mara akawaambia wenzake, "Turudi makwetu kwanza, tumwache atushughulikie fedha zetu. Kesho asubuhi tuje tena!" Wadai hawakuwa na mbinu nyingine, iliwabidi warudi makwao.
Siku ya pili kulipopambazuka tu Tototo alifika na kubisha hodi kwenye nyumba ya Bwana Sososo. Mlango ulipofunguliwa, Tototo alimwuliza Bwana Sososo maana ya kumwambia aje mapema.
Mdaiwa Bwana Sososo akajibu, "Jana nilisikitika sana kwa kukulazimisha ukae juu ya kizingiti, kwa hivyo nilikuambia uje mapema leo ili uweze kuwahi kiti."


18. MARADHI YANAYOFANANA

Siku moja, Bababe alitengeneza kitanda kipya ambacho mtindo wake ulikuwa mzuri. Aliwaza, "Ikiwa Chachache ataweza kukiona kitanda changu, nitaona fahari iliyoje!" Basi alijifanya kama amepatwa na ugonjwa. Akalala kitandani kungoja Chachache aje kumfariji na ataweza kumwonyesha kitanda hicho.
Wakati huo, sadfa Chachache alikwisha shonesha suruali maridadi, kwa hivyo alitamani pia kutia maringo mbele ya Bababe. Chachache aliposikia Bababe amepatwa na ugonjwa alifurahi moyoni na mara alikwenda kumtembelea.
Chachache alikuja ubavuni mwa kitanda cha Bababe, akaketi juu ya kiti na kupania joho lake ili kuweza kukoga suruali yake mpya na maridadi, halafu alipachika mguu wake wa kulia juu ya mguu wa kushoto, akatikisatikisa mguu wake wa kulia bila ya kusita kusudi kumvuta Bababe aangalie, akasema, "Mguu wangu huu unauma, nisipoutikisatikisa sioni raha." Baada ya kusema maneno haya, alimwangalia mwenzake kidogo na kisha akatupa macho kwenye kitanda cha Bababe, akamwuliza, "Je, mwenzangu umepatwa na ugonjwa gani?"
Bababe alitupa jicho kwenye suruali mpya ya Chachache na akasema kwa tabasamu, "Ugonjwa wangu karibu ni sawa na wako."


19. MTU ANAYETUMIA JINA LA MTU MWINGINE

Hapo kale palikuwa na ofisa mmoja wa serikali aliyeitwa Hahahe, naye aliishi kwenye Mkoa Uhoho. Siku moja alijiwa na bwana mmoja aliyeitwa Jajaje kumtembelea. Jajaje alitoa shairi moja na kumpa Hahahe ili asome huku akamwambia kuwa shairi hilo lilitungwa naye.
Baada ya kusoma shairi hilo, Hahahe alishituka, akasema, "Huu ni muswada nilioandika zamani, kwa nini unaniletea nisome?"
Jajaje alitahayari kwa kuwa hakupata kufikiria kwamba shairi hilo alilojifanya kuwa yeye ndiye mtunzi, limesomwa na mtunzi wake halisi, basi aliamua kujipurukusha, kwa hivyo akasema, "Muswada wako ulikuwa mikononi mwangu kwa muda mrefu, leo nakuja kwa makusudi ya kukurudishia muswada huo."
Hahahe alijibu, "Muswada wangu huu wa zamani hautafaa kitu, kwa hivyo nakutunukia basi."
Jajaje alimshukuru.
Baada ya dakika Hahahe alimwuliza Jajaje, "Sasa unakwenda wapi?"
Jajaje alimjibu, "Nakwenda mjini Ulili kumtembelea Bwana Waziri wa Fedha. Yeye ni bamkwe wangu."
Hahahe alimwuliza tena, "Jina la Bwana Waziri wa Fedha ni nani?" ,
Jajaje alijibu, "Anaitwa Lalale,"
Baada ya kusikia jibu lake, Hahahe aliangua kicheko, akasema, "Sasa hivi ulinighilibu kwamba wewe ni mtunzi wa muswada wa shairi langu, sasa unanilaghai tena kuwa una bamkwe aitwaye Lalale lakini hujui kwa kweli Waziri wa Fedha Lalale ndiye bamkwe wangu!"


20. Hirizi ya Kufukuza Mbu

Hapo zamani za kale, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akiuza hirizi za kufukuza mbu. Alisema kuwa mtu yeyote aliyenunua hirizi zake, akizibandika nyumbani, mbu hawatathubutu kuingia.
Mamame alinunua hirizi moja na kuibandika nyumbani, lakini mbu hawakupunguka hata kidogo. Mamame alikwenda kwa muuza hirizi na kumlaumu,"Mbona hirizi yako haifanyi kazi!"
Muuza hirizi alijibu, "Umekosea kuibandika hirizi mahali pake."
Mamame alimwuliza, "Kwa kufuata mawazo yako inafaa niibandike wapi?"
Muuza hirizi akamjibu:"Inafaa uibandike ndani ya chandarua." 2021/03/31


21. KUBADILI MABUTI

Rarara alikuwa na jozi moja ya mabuti yenye soli nene na jozi nyingine ya mabuti yenye soli nyembamba.
Siku moja asubuhui, alikosea kuvaa mabuti. Alivaa buti moja lenye soli nene na buti jingine lenye soli nyembamba. Baada ya kutoka nje alijihisi kuwa mguu mmoja ulikuwa mrefu na mwingine ulikuwa mfupi. Alisema kwa mshangao, "Ni ajabu, mbona leo miguu yangu hailingani, mmoja mrefu na mwingine mfupi?"
Njiani mtu mmoja aligundua, akamwambia, "Umekosea kuvaa mabuti."
Baada ya kusikia maneno hayo, mara alirejea nyumbani kuyabadili. Alipofika kwake aliyaona yale mabuti yaliyokuwa yamebaki. Alifikiri kitambo na kusema, "Sitabadili, kwani naona mabuti haya yaliyobaki nyumbani pia buti moja lina soli nene na jingine lina soli nyembamba."


22. DOMO NA KAYA

Hapo zamani palikuwa na ndugu wawili: Domo na Kaya, ambao walikuwa wanapiga porojo kutwa nzima bila ya kufanya kazi yoyote, hata ikawa hawawezi kushinda siku moja wasiwadanganye watu.
Siku moja, kaka Domo alimwambia didi yake Kaya, "Sisi husema uwongo na watu wanatuchukia. Naona bora tukoge katika bahari ili tukajitakase. Waonaje?"
Didi yake Kaya alijibu, "Sawa, kaka."
Domo alivua nguo zake akajitupa baharini na mkononi mwake ameshika kisirisiri kipande cha nyama ya kuchomwa. Punde si punde Domo akatoka majini huku akitafuna nyama kwa furaha. Kaya alishangaa na kumwuliza, "Kaka, umepataje nyama hii?"
Domo alisema, "Nilipokoga majini, nilimkuta Mfalme Joka wa Baharini akiwaandalia karamu kabambe askari wake kambakoche na majemadari kaa. Huyo mfalme amenizawadia nyama hiyo baada ya kujua kwamba nimeazimia kuacha tabia ya kusema uwongo. Lo, nyama yake tamu sana."
Didi Kaya alimezea mate akavua nguo na kupiga mbizi baharini. Bahati mbaya, akajigonga kwenye mwamba, akatoka majini halahala huku damu ikichuruzika usoni pake.
Domo alimwuliza, "Kaya, imekuwaje?"
Kaya akajibu, "Mfalme Joka wa Baharini alinikaripia kwa kuwa nimechelewa kuhudhuria karamu na akanipiga kwa nyundo. Lo, nyundo hiyo ya Mfalme Joka wa Baharini ni nzito kwelikweli!"


23. NYENJE-MTI WASIOKULA WALA KUVAA

Paukwa? Pakawa. Hapo kale, palikuwa na bwana mmoja ambaye aliwanyima vikali vitwana wake, hata vitwana wake walikuwa mara kwa mara wanaishi na njaa na baridi.
Siku moja, nyenje-mti walikuwa wanaimba mitini. Kitwana mmoja alimwuliza bwana wake kwa makusudi, "Bwana, ni wadudu gani wanaoimba?"
"Aa, hao wanaitwa nyenje-mti."
"Bwana, wanakula nini?"
"Hawali chochote ila kufyonza maji tu."
"Wanavaa nini?"
"Hawavai chochote."
Kitwana akasema, "Naona bora uwachukue nyenje-mti kuwa watumishi wako."


24. MTABIRI NA AFKANI

Kulikuwa na afkani mmoja. Siku moja, alimwona mtabiri akifafanua utabiri wake.
Mtabiri alisema,“Mwanamume akiwa na mkono laini, nyumbani huwa na mali nyingi; mwanamke akiwa na mkono kama tangawizi, chakula chake hujaa ghalani.”
Baada ya kusikia maelezo yake, afkani alisema kwa furaha,“Mkono wa mke wangu kama tangawizi.”
Mtabiri alimwuliza:“Wewe umejuaje mkono wake ni kama tangawizi?”
Afkani akajibu,“Jana alinipiga kofi, mpaka sasa shavu langu bado linawaka moto.”


25. KIDONDA CHA MGUUNI

Palikuwa na mkorofi mmoja ambaye alikuwa anapenda kuwachimbia wengine. Siku moja, mkorofi huyu aliumwa vikali na kidonda cha mguuni mwake. Punde si punde alipata nia moja. Alitoboa ukuta wa jirani yake, halafu akaupenyeza mguu wake wenye kidonda hadi chumbani mwa jirani.
Mtu mmoja alimwuliza,“Jamaa, unafanya nini?” Mkorofi akajibu,“ Leo kidonda kimenisumbua kwelikweli na sasa nacho kinaanza kuwasumbua jirani yangu.”
2021/04/03


26 KUBADILISHANA PIPI KWA NYWELE

Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa . Alipoona watu wengine waliweza kubadilishana pipi kwa nywele, basi alifikiri kwamba watu pia wanaweza kubadilishana kitu kingine kwa nywele.
Siku moja alikwenda kilabuni kunywa pombe huku akiwa na nywele zilizokwisha katwa mkononi. Baada ya kumaliza kunywa ugimbi, alimpa mtumishi nywele zake na kutaka kuondoka. Mtumishi alimzuia na kusema kwa tabasamu:“Nywele hizi zinawezaje kutumiwa kama pesa?”
Pupupu alimjibu kwa hamaki:“Wengine wanaweza kuzitumia nywele kama pesa, kwa nini mimi siwezi?”
Baada ya kusema maneno hayo Pupupu alitaka kuondoka tena.
Mtumishi alimvuta nywele za kichwani mwake na kutomruhusu aondoke.
Pupupu alimwuliza:“Hukubali kupokea nywele nilizokupa, kwa nini unadai nywele za kichwani mwangu!”


27 MAHARAGWE

Bwana Bobobo alimwalika Bibi Chichichi kula chakula nyumbani kwake. Bwana huyo alimpikia mgeni ubwabwa na maharagwe tu. Wakati wa kula chakula Bwana Bobobo alijisemea mwenyewe:
“Maharagwe ni kama maisha yangu. Napenda kula maharagwe. Naona ladha yake ni bora kuliko vitoweo vyote vingine duniani.”
Siku saba baadaye, Bwana Bobobo alialikwa kwenda nyumbani kwa Bibi Chichichi kula chakula. Bibi Chichichi alikumbuka kuwa Bwana Bobobo alipendelea kula maharagwe, basi alimpikia maharagwe, samaki na nyama, lakini wakati wa kula chakula Bwana Bobobo alikula samaki na nyama tu, bali hakugusa maharagwe.
Bibi Chichchii alimwuliza:“Si wewe uliyesema kuwa maharagwe ni kama maisha yako, kwa nini leo huli?”
Bwana Bobobo alimjibu:“Baada ya kuona samaki na nyama hata maisha ninayatupa upande.”



28 SABINI NA TATU NA THEMANINI NA NNE

Bwana Nenene alikuwa mchoyo. Alipomwandalia mgeni wake karamu alimwagizia mhudumu: “Wakati wa kula chakula usipoteze gongo ovyo, subiri mpaka ninapogonga meza ndio uje kummiminia mgeni mara moja. ”
Lakini Bwana Nenene hakutarajia kuwa maongezi yao yalisikiwa na mgeni. Wakati wa kunywa gongo, mgeni alimwuliza Bwana Nenene kwa makusudi:“Mama yako ana umri wa miaka mingapi?”
“Miaka sabini na tatu.”
Mgeni alisema huku akigonga meza:“Ni adimu kufikia umri mkubwa kama huu! Ni adimu sana!”
Mhudumu alisikia sauti ya kugonga meza, akaja na kummiminia mgeni gongo.
Baada ya muda si mrefu, mgeni alimwuliza Bwana Nenene tena:“Baba yako ana umri wa miaka mingapi?”
“Miaka themanini na nne.”
Mgeni aligonga meza tena huku akasema:“Ni nadra sana tena sana!”
Mhudumu alikuja tena kummiminia mgeni gongo.
Dakika chache baadaye, mwenyeji aligundua kuwa hii ilikuwa kitimbi cha mgeni, basi alimlaani kwa hasira:“Usijali wao ni sabini na tatu au themanini na nne, kwa namna yoyote umekwisha kunywa gongo kwa kiasi cha kutosha!”


29 KUMTUKUZA MKE

Hapo kale palikuwa na mzee mmoja mwislamu ambaye baada ya kutajirika alianza kujivuna. Siku moja, mke wake Mamama alifariki dunia. Mzee huyo alikwenda kwa imamu kumwomba amsaidie kuandika maneno ya kumtukuza mke wake kwenye jiwe la kumbukumbu lililokuwepo mbele ya kaburi. Imamu alifikiri kwa muda mrefu lakini hakupata maneno yaliyofaa. Mwishowe ilimbidi aandike maneno yafuatayo:
“Kaburi la bikizee Mamama ambaye ni jirani wa Sususu, Mkuu wa Chuo Kikuu, Ph. D., LL.D..”



30 SHETANI
Watu wa nchi ya Ususu walikuwa wakiabudu mashetani. Mtu yeyote akipatwa na ugonjwa hakukosa kuwatambikia mashetani na kuomba kuponyeshwa ugonjwa wake. Usiku wa siku moja, kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Sasasa ambaye alikuwa akitambika nje ya mlango wa kaskazini wa mji, kwa bahati kijana mmoja mtundu alimuona. Basi mtundu huyo alijificha kimyakimya kichakani, halafu alitupa kijiwe pale mahali pa kutambikia. Sasasa alishtuka kwa hofu, akakimbia kwa haraka, lakini kabla ya kwenda mbali alisimama na kuangaza huku na huko. Kijiwe kilimrukia tena. Sasasa aliogopa mno na safari hii akakimbilia mbali zaidi. Kila alipozidi kukimbilia mbali ndivyo kadiri vijiwe vingi zaidi vilimrukia. Wakati mtundu alipoona kuwa Sasasa amekwisha kimbilia mbali akaanza kula sadaka iliyotolewa kwa tambiko.
Baada ya tukio hilo, Sasasa aligundua kwamba sadaka aliyotoa kwa tambiko ilitoweka, akadhani kuwa kutambika kwake kumeleta alilotaka. Hivyo watu waliokuja kutambika waliongezeka zaidi na zaidi. Kuanzia wakati huo, mahali hapo pa tambiko pakazidi kujulikana. Baadaye watu wakiona vitu vyao vilivyotolewa kwa tambiko vilikuwa salama na wao hufikiri kuwa mashetani hawakuwa wamekula, kwa hivyo watu hao hawakufurahi. 2021/04/05


31 Maini ya Farasi

Mgeni mmoja alimwambia mwenyeji wake Bwana Nanana kuwa maini ya farasi yana sumu kali.
Baada ya kusikia usemi huo Nanana alisema huku akicheka:
“Mgeni wangu, labda unanichenga. Farasi amekuwa na maini tumboni mwake tangu kuzaliwa, mbona hafi?”
Mgeni alijibu kwa utani: “Kwa sababu farasi ana maini, ndiyo maana hawezi kuishi hadi umri wa miaka mia.”
Baada ya kusikia maneno hayo ya mgeni, Nanana alisadiki. Alipasua tumbo la farasi wake na kutoa maini yake. Punde si punde farasi alikufa. Nanana alikita kisu chini na kusema:
“Maneno ya mgeni huyu ni sawa. Kweli maini ya farasi yana sumu. Nimeyatoa maini tu farasi amekufa, sembuse ningeacha maini yake ndani ya tumbo lake!”



32 KUOGOPA MBWA

Palitokea mtu mmoja aliyeitwa Yoyoyo. Siku moja, mgeni alikuja kwake kumtembelea. Yoyoyo alipenda kujifanya tajiri, basi aliazima kijakazi mmoja kutoka kwa jirani yake. Wakati kijakazi huyu aliposhika sinia ya vikombe vya chai na kutaka kuingia sebuleni, ghafla alisimama mbele ya sebule, halafu akarandaranda pale. Kuona hayo, Yoyoyo alimwuliza kwa sauti kubwa:
“Ebo! Mbona huingii ndani?”
Kijakazi alijibu:
“Ninaogopa mbwa mkali wa kwenu.”



33 Ni Shida Kuigiza Shani za Kimaumbile

Baba alimwambia mwanawe Gagaga:“Kila neno lako na kila kitendo chako, huna budi kujifunza kutokana na jinsi mwalimu wako anavyofanya.”
Baada ya kusikiliza maneno ya baba yake, Gagaga alikwenda kwa mwalimu wake na alitaka kujifunza kutoka kwa mwalimu wake. Mwalimu alipokula Gagaga alijifunza jinsi yake alivyokula; mwalimu alipokunywa Gagaga alijifunza jinsi yake alivyokunywa; mwalimu alipogeuza mwili wake upande yeye pia alijifunza jinsi yake alivyogeuza mwili. Mwalimu alipoona Gagaga akimwiga kikasuku namna hivyo alicheka bila ya kujizuia na kujiwa na chafya cha ghafla. Gagaga pia alitaka kujifunza kupiga chafya lakini kwa vyo vyote vile hakuweza kufaulu. Hakuwa na njia akainamisha kichwa mbele ya mwalimu na kusema: “Hakika, shani ya kimaumbile ni shida kuigika!”


34 SHILINGI ELFU

Tatata na Vavava walikuwa marafiki. Siku moja, Tatata alipatwa na ugonjwa, uso wake ulikuwa umekunjwa. Vavava alikwenda kwake kumjulia hali na kumwambia:“Kaka yangu mpendwa, umepatwa na ugonjwa gani? Ukihitaji kitu cho chote niambie, nami nitajitahidi kutafuta njia ya kukipata.”
Tatata alijibu kwa sauti ya chini: “Sihitaji cho chote kingine ila shilingi elfu moja tu. Ugonjwa nilio nao ni ukosefu wa fedha.”
Baada ya kusikia maneno hayo, Vavava mara alijifanya hakusikia na kumuuliza kwa makusudi:“Umesema nini?”


35 KUBISHANIA BEI

Kulikuwa na mfanyabiashara mmoja aliyeitwa Yayaya, ambaye alitaka kwenda Mji Tanono kununua bidhaa. Mtu mmoja alimfundisha:
“Watu wa Tanono wanapouza vitu hudai bei maradufu ya thamani. Akidai kiasi cha fedha, basi unapigania nusu ya bei aliyoitaka.”
Mfanyabiashara huyu aliamini kabisa maneno yake. Baada ya kufika Mji Tanono, Yayaya aliingia katika duka moja la kuuzia hariri. Kila mwuza duka alipodai shilingi mia nne Yayaya aliomba aheri na kutaka kutoa shilingi mia mbili tu; na mwuza duka alipodai shilingi mia moja aliomba aheri ili atoe shilingi hamsini tu.
Mwuza duka alihamaki akisema:“Ukiomba aheri hivyo, basi bora usinunue, nitakutunukia majora mawili.”
Yayaya alisema bila ya kukawia“Sithubutu, nitachukua jora moja tu.”


2021/04/10

36 YAI LILILOPIKWA KWA CHUMVI

Zazaza na Bebebe walikuwa wajinga wawili. Siku moja, Zazaza alikula yai lililopikwa kwa chumvi. Alipoona ladha yake si ya kawaida alishangaa na kusema:
“Mimi niliwahi kula mayai lakini yote niliyokula yalikuwa hayana ladha ya chumvi. Mbona yai hili lina ladha ya chumvi?”
Bebebe akamjibu,
“Mimi ni mwerevu kuliko wewe. Naweza kukuambia sababu yake. Yai hili lenye ladha ya chumvi ni yai lililotagwa na bata aliyepikwa kwa chumvi.”


37 MKUU WA MKOA

Kulikuwa na Mkuu wa Mkoa mmoja aliyejulikana kwa jina la Bwana Checheche, alikuwa na tabia ya uchoyo na ubahili.
Siku moja, mjakazi wake alimwambia kuwa viatu vyake vimechakaa. Mara alimwita ofisa mmoja mdogo aliyevaa viatu vipya aje ofisini mwake, akamwamrisha aparamie mti kuchuma matunda, kisha akamkonyeza mjakazi wake aviibe vile viatu vipya vya ofisa huyo mdogo na kuvipeleka nyumbani kwao. Ofisa huyo mdogo alipoteremka kutoka mtini hakuona viatu vyake, basi akamwuliza Checheche:“Mkuu wa Mkoa, unaweza kujua viatu vyangu viliko?”
Bwana Checheche alijibu:“Mimi ni Mkuu wa Mkoa, siyo mtu wa kukulindia viatu!”


38 KUPIKA POMBE KWA BIA

Bwana Fefefe na Bwana Gegege waliafikiana kupika pombe kwa bia. Fefefe alimwambia Gegege:
“Wewe utoe mchele, nami nitatoa maji. Unaonaje?”
Gegege alimwuliza: "Mchele wote ni wangu. Baada ya kumaliza kupika pombe tutagawana vipi?”
“Mimi kwa kweli sina uchoyo. Pombe itakapoiva uichuje na nirudishie yale maji yataniridhisha, vitu vingine vyote vitakavyobaki vitakuwa mali yako.”


39 JANI LA KUFICHA MWILI

Hapo zamani, palitokea mtu mmoja aliyeitwa Wowowo. Alipotembea njiani alipewa jani moja na kuambiwa:

“Jani hili linaitwa‘Jani la Kuficha Mwili". Mtu yeyote akishika jani hili watu wengine hawataweza kumwona.”

Bwana Wowowo alisadiki.
Siku moja, alitembea mtaani huku akishika jani hilo mkononi. Ghafla alipora hela za mtu na kukimbia nazo. Mwenye hela alipotanabahi, akamshika na kumpiga ngumi. Wakati huo Bwana Wowowo alimwambia:
“Hata kama utanipiga namna gani, kwa vyovyo huwezi kuniona.”


40 KUZIBA MATUNDU YA PAA

Yalikuwa majira ya masika na mvua ilinyesha bila ya kusita. Paa la chumba cha Bwana Hohoho lilivuja kama chekecheke. Usiku mzima Hohoho alihamishahamisha kitanda hapa na pale lakini hakupata sehemu kavu hata moja. Mke na watoto wake wote walimlaumu.
Kulipopambazuka Hohoho alikwenda haraka kwa waashi ili waje kumsaidia kuziba matundu ya paa la vigae. Aligharimia fedha nyingi na siku hiyo alichoka sana. Baada ya kufanya matengenezo, mvua ilisita ghafla na mwezi mzima uliofuata haikunyesha tena. Siku moja, Hohoho aliinua kichwa kuangalia dari huku akisema:
“Bahati yangu mbaya iliyoje! Nilipomaliza kutengeneza chumba changu tu mara mvua ikasita. Kumbe nimetoa gharama bure!”

2021/04/15



41 MANENO YA NUKSI

Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Jejeje ambaye alizoea kusema maneno ya nuksi, kwa hivyo watu wengine walimchukia.

Tajiri mmoja alijenga nyumba mpya. Jejeje alikwenda kuiangalia kwa kuimezea mate. Alipofika mlangoni alibisha hodi lakini hapakuwa na mtu aliyemwitikia, basi alianza kutukana kwa ghadhabu:

“Mbona mlango huu wa gereza umefungwa sana? Bila shaka watu wote waliomo ndani wamekwisha kufa!”

Baada ya kusikia maneno yake, tajiri alitoka na kumlaumu:

“Niligharimia shilingi elfu kumi kuijenga nyumba hii, kwa nini unaifananisha na gereza?”

Jejeje akamjibu:

"Ala, uligharimia shilingi elfu kumi kuijenga nyumba hii mbovu? Ukiiuza hasahasa unaweza kupewa shilingi elfu tano tu.”

Tajiri alimfokea:

“Sikusema kuwa ninatafuta dalali wa kuniuzia nyumba hii. Nani aliyekuambia uikadirie bei ya nyumba yang;u ?”

Jejeje alisema:

“Ni jambo zuri kukupendekeza kuiuza nyumba hii, ama sivyo ikishika moto, haitakuwa na thamani hata senti moja.”

Maneno yake yalimghadhibisha mno yule tajiri ambaye alishindwa hata kutamka.

※ ※ ※

Kulikuwa na familia nyingine ambapo mzee wa familia alibahatika kupata mwanambee alipofikia umri wa miaka 50. Katika siku za mwanzo majirani na marafiki walikwenda kwake kumpa hongera. Jejeje pia alitaka kuwa miongoni mwa watu waliotaka kwenda. Rafiki yake alimshauri:

“Kwa kuwa wewe husema maneno ya nuhusi, afadhali usiende.” Jejeje akamjibu:

“Ninakuahidi kwamba sitasema lolote. Unaonaje?”

Rafiki yake alimjibu:

“Ikiwa hutasema lolote, basi nitakubali kuongozana nawe.”

Walifika nyumbani kwa mzee. Rafiki yake alimpa mzee hongera kwa niaba ya Jejeje, halafu walikula chakula na kunywa chang'aa pamoja. Muda wote huo Jejeje hakusema neno. Rafiki yake aliridhika.

Baada ya kula chakula waliagana na mwenyeji. Ndipo hapo Jejeje alisema kwa mwenyeji:

“Leo sikusema hata neno moja. Baada ya mimi kuondoka, ikiwa mtoto wako atakufa kwa kupatwa na pepopunda, msinilaumu!”



42 NATAMANI KUPATA KIDOLE CHAKO

Hapo zamani, kulikuwa na malaika mmoja aliyeweza kugeuza jiwe kuwa dhahabu. Siku moja, alishuka duniani. Alitaka kujaribu mioyo ya watu ili kupata mtu mmoja asiyekuwa na choyo na kumsaidia kuwa malaika.

Ingawa alitafuta kila mahali lakini hakumpata. Kila mtu aliyemkuta aliona dhahabu iliyogeuzwa kutoka jiwe ilikuwa ndogo. Mwishowe malaika huyo alimkuta mtu mmoja aliyeitwa Mememe. Malaika alielekeza kidole kwenye jiwe moja na kumwuliza:

“Nikigeuza jiwe hili kwa kidole changu liwe dhahabu, halafu nikupe, unasemaje?”

Mememe alijibu:

“Sitaki kipande hicho cha dhahabu.”

Malaika aliwaza kuwa labda mtu huyu anaona jiwe hili ni dogo, basi akaelekeza kidole chake kwenye kipande kingine kikubwa na kumwuliza:

“Nigeuze kipande hiki kikubwa kiwe dhahabu halafu ukichukue.” Mememe alitikisa kichwa kuonyesha kukataa.

Malaika aliwaza moyoni kuwa mtu huyu hana choyo hata kidogo. Ni nadra sana kumkuta mtu wa namna hii, basi akaamua kumsaidia kuwa malaika.

Hapo alimwuliza swali la mwisho:

“Vyote hutaki kupokea, kipande kikubwa wala kipande kidogo, basi unataka kitu gani?”

Mememe akamjibu:

“Sitaki kitu chochote kingine ila tu naomba nibadilishane kidole chako kwa kidole changu, ambacho sasa hivi ulitumia kuligeuza jiwe kuwa dhahabu, maana nikipata kile kidole chako nitaweza kugeuza jiwe Iolote kuwa dhahabu kama nipendavyo.”



43 KUCHORA PICHA

Palitokea mchoraji mmoja aliyeitwa Gigigi. Hapakuwa na mtu hata mmoja aliyekuja kwake kumwomba amchoree chochote. Rafiki yake alimshawishi achore picha yenye sura yake na ya mkewe halafu aitundike mlangoni, wapitanjia wakiiona picha hiyo watajua kuwa anafanya kazi ya uchoraji. Bwana Gigigi alifanya kama rafiki yake alivyoshauri.

Siku moja, baba mkwe wa Bwana Gigigi alikuja kumtembelea. Alipoona picha hiyo alimwuliza: “Huyu mwanamke ni nani?”

Bwana Gigigi alijibu: “Ndiye binti yako.”

Baba mkwe alimwuliza tena: “Mbona amekaa bega kwa bega na mtu huyu mgeni?”



44 KUFA MAJI


Zamani kulikuwa na mzee mmoja aliyeitwa Mimimi. Mzee huyo alikuwa bahili . Siku moja, ilinyesha mvua kubwa. Maji ya mto yalifurika. Mzee Mimimi alitaka kuvuka mto huo lakini hakupenda kutoa fedha ya kivuko, kwa hivyo alijaribu kuvuka kwa miguu. Alipofikia katikati ya mto aliangushwa na mkondo mkali wa maji na kuchukuliwa nusu kilomita.

Mwanawe alitafuta mtumbwi harakaharaka kando ya mto ili kumwokoa. Mwenye mtumbwi alitoza shilingi kumi lakini mwana wa mzee Mimimi hakukubali. Alikubali kulipa shilingi tano tu. Kutokana na kupatana nauli walipoteza wakati mwingi. Mzee Mimimi aliposikia mabiishano ya nauli, aligeuza kichwa na kupiga makelele kwa mwanawe: “Mwanangu, akikubali shilingi tano niokoe, asipokubali niache nife!”

Baada ya maneno hayo kadiri alivyozidi kuelea mbali ndivyo sauti yake ilivyozidi kuwa hafifu. Hatimaye alikufa maji.



45 BABA KABWERA AHUDHURIA KARAMU YA TAJIRI

Siku moja, kabwera Wiwiwi alikwenda kuhudhuria karamu ya mjomba wake tajiri. Ilikuwa majira ya baridi na baba Wiwiwi alikuwa hana nguo nzito na rasmi, ikawa alihudhuria karamu akivaa shati tu. Alihofia watu watacheka umaskini wake akachukua kipepeo mkononi. Alipofika aliwaambia wageni: “Mimi naogopa joto na nimezoea kupunga kipepeo hata katika siku za baridi.”

Mjomba wake tajiri alijua Wiwiwi hana chochote ila anajidai tu. Baada ya karamu, mjomba tajiri akataka Wiwiwi akae nyumbani kwake usiku uleule na arudi siku ya pili. Usiku mjomba tajiri alimwandalia mkeka na mto wa mwanzi, na akakiweka kitanda uani kando ya kidimbwi. Usiku wa manane, upepo wa baridi ulivuma, Wiwiwi alitetemeka kwa baridi na akatafuta mahala pa kujisetiri. Gizani hakuona njia sawasawa akajitumbukiza ndani ya kidimbwi. Mjomba tajiri aliamka na kumwuliza kumetokea nini. Wiwiwi alijibu: “Naona joto na nimezoea kukoga kwa maji ya baridi hata usiku wa manane!”
2021/04/20



46 JUHA NA JOHO LAKE

Hapo kale palikuwa na afisa mmoja aliyeitwa ZAZAZA katika nchi fulani.

Siku moja, alikwenda kuonana na diwani akijipakia kwenye mashua.

Alipofika diwani alimwuliza, "Umeegesha mashua wapi?

ZAZAZA alijibu, "Mashua yangu iko mtoni."

Diwani akahamaki na kumfokea kwa sauti kubwa: "Juha wee!"

ZAZAZA alifikiri diwani anauliza habari za joho lake akajibu bila

kukawia: "Joho langu pia liko kwenye mashua."



47 HUDUMA ZA CHAPUCHAPU

Hapo kale, palikuwa na askari mmoja aliyeitwa ZEZEZE ambaye alijeruhiwa mgongoni kwa kupigwa mshale akatoka vita. Baada ya kurudi kambini akaenda kwa daktari. Daktari alichunguza jeraha lake na kusema: “Usiwe na wasiwasi, litapona tu. Ni kazi rahisi kuutoa mshale.” Daktari aliposema hayo alichukua mkasi mmoja mkubwa akakata kijiti cha mshale kilicho nje ya ngozi. Baada ya kupata malipo daktari alitaka kuondoka. ZEZEZE alisema: “Ebo daktari, yeyote anafahamu namna ya kukata mshale kwa mkasi. Sasa kichwa cha mshale kingali bado kimo mwilini mwangu na kukitoa nje ndiyo kazi yako. Bado hujamaliza tiba!” Daktari akajibu kwa ubayana:“Mimi nashughulikia tu huduma za chapuchapu. Kazi yangu imekwisha. Sasa nenda ukaonane na daktari anayeshughulikia maradhi ya ndani.”


48 KISIMA CHA POMBE

Hapo zamani alikuweko mzee mmoja aliyeitwa ZIZIZI ambaye alikuwa huja kunywa pombe katika mkahawa ulioendeshwa na mama mmoja. Kila akimaliza pombe yake, aliinuka akaenda zake bila ya kulipa hela na mama mwenye mkahawa naye hakudai malipo. Baada ya siku nyingi, mzee ZIZIZI alimwambia mama huyo: “Mimi hunywa pombe bila kulipa, sasa nataka kukushukuru kwa dawa. Ukiitia dawa hii kisimani utapata pombe safi na baadaye huna haja ya kugema pombe tena.” Mzee akatoa vidonge viwili vya dawa akavitupa ndani ya kisima akaondoka.

Siku yake ya pili, huyo mama alichota maji kutoka kisimani akapata pombe tamu, ambayo inashinda ile aliyogema. Watu wakaisifu pombe hiyo kuwa pombe ya malaika. Tangu hapo mama huyo akatajirika. Baada ya miaka 30, siku moja mzee ZIZIZI akaja tena akalakiwa vizuri na mama huyo na akamwuliza: “Shilingi ngapi umejichumia tangu ulipopewa kisima cha pombe?”

Mwenye mkahawa akajibu kwa kubabaisha: “Kisima hicho hutoa pombe tamu, lakini minazi yetu imekaa bure. Na hayo ndiyo masikitiko yetu.”

Mzee ZIZIZI hakusema chochote. Akanyoosha mkono kwenye mdomo wa kisima, vidonge vile viwili vya dawa vikaruka na kutua mkononi mwake. Mzee akavitia mfukoni mwake akaondoka na kisima kikawa kama cha hapo awali.



49 KULUNGU NA SWALA

Siku moja, katika nchi fulani mgeni mmoja aliyeitwa ZOZOZO alimletea Waziri Mkuu zawadi ya kulungu na swala, ambao walifungwa ndani ya tundu kubwa. Hapo pia alikuwepo mtoto wa Waziri Mkuu aliyekuwa na umri wa miaka kadha tu. Mgeni ZOZOZO alimwuliza mtoto:“Je, unaweza kumtambua yupi ni kulungu na yupi ni swala?”

Kusema kweli mtoto huyu hakuweza kuwatofautisha lakini baada ya kufikiri kwa muda alijibu:“Naona kando ya kulungu ni swala na kando ya swala ni kulungu.” Kutokana na jibu hilo mgeni ZOZOZO alishangazwa na werevu wa mtoto huyo.


50 Kubadilishana Hila

Kulikuwa na muuza dawa mmoja aliyeitwa ZUZUZU katika Mji wa Ulinlin aliyekuwa akibeba sanamu ya mungu. Kila alipoonana na mgonjwa alikuwa akijaribu kumpa kidonge kimoja cha dawa. Lakini iIkiwa kidonge hicho cha dawa kitakuwa kimepitia moja kwa moja kwenye mkono wa mungu bila ya kusimama atampa mgonjwa na kumruhusu kukila; ikiwa kidonge hicho cha dawa hakitapitia moja kwa moja atakirudisha dawa hiyo na kutompa mgonjwa. Baada ya siku kadhaa aliweza kujikusanyia mapato makubwa kutokana na tiba yake.

Kulikuwa na kijana mmoja ambaye alikuwa akiibia jambo hili kwa pembeni ili apate uganga wa namna hiyo. Baada ya watazamaji wote kuondoka, alimwalika muuza dawa ZUZUZU waende pamoja mkahawani kunywa pombe. Baada ya kunywa pombe waliondoka bila ya kulipa na watumishi wa mkahawani hawakushituka wala hawakuwasemesha kitu. Walifanya vivyo hivyo kwenye mikahawa minne tofauti na kuwa ndio tabia yao. Muuza dawa ZUZUZU alistaajabu na kumuuliza kijana kwa mshangao:“Tafadhali niambie huu ni uganga wa namna gani?"

Kijana alijibu:“Uganga wangu ni mwepesi,ukikubali ninaweza kubadilishana na wako!”

Muuza dawa ZUZUZU akamwambia:“Uganga wangu hauna shani yoyote. Mkono wa mungu ulitengenezwa kwa sumaku, dawa isiyo na chembechembe za chuma hupita na ile yenye chembechembe za chuma huvutwa na kugandamizwa.”

Kijana akamjibu:“Hali kadhalika uganga wangu hauna chochote cha ajabu. Kabla ya kunywa pombe nilikuwa nimetangulia kulipa na niliahidiana na muuza duka kuwa akituona sisi wawili tumekuja asithubutu kutuuliza chochote.” 2021/04/28


51 USHURU

Hapo kale wafanyabiashara wa nchi fulani walitozwa ushuru mkubwa. Katika mji mkuu wa nchi hiyo ulitokea ukame kwa miaka mitatu mfululizo na kuwapa wananchi dhiki ya maisha. Safari moja,

Mfalme aliwaandalia maofisa wake karamu kubwa katika kasri yake. Wakati wa kula chakula Mfalme aliwauliza maofisa wake:“Mikoa mingine yote ilinyesha mvua isipokuwa mji mkuu tu. Sijui ni kwa sababu gani?”

Waziri Mkuu YAYAYA alijibu kwa ucheshi: "Mvua haithubutu kuingia mji mkuu, inaogopa isitozwe ushuru!”

Baada ya kusikia jibu la Waziri Mkuu, Mfalme alicheka bila ya kujizuia. Kisha aliamua kupunguza ushuru usio wa lazima.




52 MTOTO ALIYEZALIWA AKIWA NA MIEZI SABA

Kulikuwa na mama mmoja, ambaye alijifungua mtoto kwa mimba ya miezi saba. Mume wake aitwaye YEYEYE alihofia kuwa huenda mtoto huyo hataweza kukua na kufikia utu uzima. Hivyo kila alipokutana na mtu alimwuliza jambo hili. Siku moja,alitaja jambo hili alipokuwa akiongea na rafiki yake. Rafiki huyo alimwambia:“Mtoto aliyezaliwa akiwa na miezi saba hatapatwa na matatizo yoyote. Babu yangu pia alizaliwa akiwa na miezi saba.”

Mume huyo YEYEYE aliuliza kwa mshangao:“Kama ni hivyo, je babu yako alikua mpaka akafika kuwa mtu mzima?”




53 KUOTA NDOTO

Mwalimu mmoja alilala usingizi darasani wakati wanafunzi wake walipokuwa wakitahiniwa. Baada ya kuzinduka ilimbidi awapige uwongo wanafunzi wake:“Nilikwenda kuonana na Mungu ndotoni.”

Siku ya pili yake, mwanafunzi YIYIYI naye alijifunza kutokana na mwalimu wake, pia aliamua kulala darasani. Mwalimu alimwamsha kwa kumgonga kwa fimbo, halafu akamwuliza kwa hamaki:“Mbona unalala darasani?”

“Mimi pia nilikwenda kuonana na Mungu ndotoni.” Mwanafunzi YIYIYI alijibu.


“Je Mungu alisema nini?” Mwalimu alimwuliza tena.

“Mungu aliniambia kuwa jana hakukuona.” Mwanafunzi YIYIYI alimjibu bila woga.



54 Chapati na Asali

Hapo zamani za kale, alikuweko sufii aliyeitwa YOYOYO. Siku moja,sufii huyo alitaka kula chapati. Basi alikwenda mtaani akanunua chapati 12 na chupa moja ya asali, halafu alijificha chumbani akala peke yake kwa siri. Baada ya kula chapati nne na kushiba, aliweka chapati 8 zilizobakia ndani ya bakuli na kuificha chupa ya asali mvunguni mwa kitanda, kIsha YOYOYO akamwambia sufii mdogo;“Linda chapati zangu kwa makini zisije zikapotea, ndani ya chupa iliyopo chini ya kitanda mna sumu kali mno,kama mtu akila atakufa.”

Baada ya kusema maneno hayo alitoka nje. Sufii mdogo alipoona sufii haonekani,bila ya kuchelewa alichukua chupa ya asali, akapaka asali kwenye chapati,akala moja baada ya nyingine mpaka akashiba. Akambakizia chapati mbili tu.

Muda si mrefu sufii YOYOYO alirejea. Mara alikwenda kuangalia chapati zake,akagundua kuwa zimebakia mbili tu na asali ilikuwa imemalizika,akaghadhibika na kumfokea sufii mdogo:“Kwa nini ulikula chapati na asali yangu?Sema upesi!”

Sufii mdogo alijifanya anagwaya sana kwa hofu. Alijibu huku akitetemeka:“Baada ya wewe kuondoka,nilizilinda chapati kwa makini. Niliponusa harufu nzuri sikuweza kujizuia nikachukua moja na kuila. Baada ya kula moja nilitamani kula ya pili,baada ya kula ya pili nilitamani kula ya tatu. Nilihofia kuwa utanichapa,niliona afadhali nile sumu na kufa kuliko kufa kwa kupigwa. Wakati ule nilitarajia nife mara tu baada ya kula sumu,lakini wapi!Mpaka sasa bado niko hai.”


Sufii YOYOYO alikasirika na kumwambia:“Ulikula jinsi gani?Uliwezaje kula chapati nyingi namna ile kwa muda mfupi?”

Bila ya kukawia sufii mdogo aliunyoosha mkono wake na kuchukua chapati kula kwa haraka, halafu akamjibu:“Nilikula kama ninavyokula hivi sasa.”

Sufii YOYOYO alipiga makelele kwa hasira. Sufii mdogo alipoona hali inazidi kuwa mbaya aliamua akimbie upesiupesi.



55 MWIZI

Usiku wa manane,mwizi mmoja alijipenyeza ndani ya chumba cha mtu maskini baada ya kutoboa ukuta. Alipoona hakukuwa na cha kuchukua, alifungua mlango na kutoka kwa maringo, akauacha mlango wazi. Kumbe mwenyeji YUYUYU alimwona akiwa amelala kitandani pake, bila ya kukawia alisema kwa sauti kubwa:“Hebu, bwana,nifungie mlango wangu halafu uondoke!”
Mwizi alijibu baada ya kugeuza kichwa chake: “Mbona wewe mvivu sana! Si ajabu huna chochote ndani ya nyumba yako!”
Mwenyeji maskini YUYUYU alimjibu huku akijinyoosha nyoosha kitandani na kugeuza ubavu:”Unaota ndoto nini! Unataka niwe na bidii za kazi ili nikipata utajiri uje uniibie, siyo?“ 2021/05/01


56 NIMESAHAU

Mpishi Wawawa alipokuwa akikatakata nyama nyumbani kwake alificha chinyango moja kifuani. Bibi mwenye nyumba alipoona vile alimkaripia:
“Hii ni nyama yetu. Mbona unaifanya hivyo?“
Wawawa alijibu: "Nimesahau.”


57 KUNG'ANG'ANIA KUDAI PESA

Kulikuwa na msafiri mmoja Wewewe, ambaye alikuwa akirejea watani wake akiwa amebeba mzigo. Alipopitia Mkoa wa Ushasha alikuta ukame mkubwa, watu walibanwa na njaa na wengi walikufa. Hoteli zote zilifungwa na kutofanya kazi. Wewewe hakuwa na mahali pa kula wala kulala, ilimbidi alale katika hekalu moja la kale. Baada ya kuingia aliona majeneza kadha upande wa mashariki,na kwenye upande wa magharibi kulikuwa na jeneza moja tu. Baada ya saa nne, kutoka kila jeneza kulitokeza mkono mmoja,mikono yote ya upande wa mashariki imekondeana, ila mkono wa upande wa magharibi ulikuwa mnene na mweupe. Wewew alikuwa ni mtu jasiri,alitumbatumba na kuangalia huku na huko, halafu aliangua kicheko bila ya kujizuia:“Mashetani wakubwa nyie maskini, huenda nyote mnakosa pesa, ndio maana mnanyoosha mikono kuomba pesa kwangu,siyo?” Kisha akachukua pesa kutoka mfukoni mwake na kumpa kila shetani senti moja. Mikono ya mashetani wa upande wa mashariki ilirudi haraka lakini mkono wa shetani wa upande wa magharibi ulikuwa bado umenyooshwa. Wewewe alisema:“Senti moja haiwezi kukuridhisha, basi nitakupa zaidi.” Aliongeza moja baada ya nyingine mpaka ikatimia shilingi moja, lakini mkono wa shetani huyo ulikuwa bado umenyooshwa. Wewewe alicharuka kwa hamaki na kusema:“kiumbe wa namna gani, labda una choyo!” Basi alichukua shilingi 20 na kuziweka mkononi mwake,hivyo shetani huyo aliurudisha mkono wake. Wewewe alipata mshangao kidogo,hivyo aliinua kandili na kumulika kwenye pande zote mbili, akaona kuwa katika kila jeneza la upande wa mashariki kumeandikwa jina la mtu ambaye alikufa kwa njaa, ila katika jeneza la magharibi kumeandikwa jina la hakimu wa wilaya fulani.

58 KUBWEKA

Mtu mmoja aitwaye Wiwiwi alimwuliza ombaomba:“Kwa nini kila mbwa anapowaoneni hubweka?”
Ombaomba alijibu:“Tutakapokuwa tumevaa mavazi mazuri mnyama huyu atatuheshimu.”


59 KULA CHAKULA KWA SIRI

Kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Wowowo, ambaye alimwachia mgeni sebuleni na yeye mwenyewe aliingia ndani akala chakula kimyakimya. Mgeni alisema kwa sauti kubwa: “Sebule hii nzuri iliyoje! Lakini inasikitisha kuwa nguzo yake imeliwa na mdudu.”
Baada ya kusikia maneno hayo Wowowo alitoka kwa haraka na kumwuliza:“Mdudu yuko wapi?”

Mgeni alimjibu: “Nitawezaje kufahamu, kwani mdudu huyo anaila nguzo kwa kuipekecha kwa ndani.”


60 ITAKAYOOZA NI SINIA

Hapo zamani za kale kulikuwa na ofisa mmoja aliyeitwa Wuwuwu, ambaye alipopata cheo aliweka nadhiri kwa Mungu:“Nikiomba shilingi kwa mkono wa kushoto, basi mkono wangu huo utaoza na nikiomba shilingi kwa mkono wa kulia, basi mkono wangu wa kulia utaoza.”
Baada ya muda si mrefu,mtu mmoja alikuja na fedha ili atoe rushwa. Ofisa Wuwuwu alitaka kupokea huku akiogopa asije akavunja nadhiri aliyoweka hapo awali. Baada ya kufikiri kwa muda, ghafla alipata akili na akajisemea mwenyewe: “Mimi nitaleta sinia tupu na kumwambia huyo mtu aweke fedha yake kwenye sinia, halafu nitamwita mjakazi wangu aje na kuipeleka ndani. Siku ile niliweka nadhiri, nilisema kuwa sitapokea shilingi, lakini iliyoletwa leo ni fedha bali siyo shilingi. Zaidi ya hayo,sitatumia mkono wangu, kama itaoza,basi itakayooza ni sinia. Sinia na mimi hatuna uhusiano.“ 2021/05/12


61 KUMTUKANA ALIYEFUSA

Hapo kale kulikuwa na watu kumi ambao walikuwa wanaongea pamoja. Ghafla mtu mmoja miongoni mwao aliyeitwa Vavava alifusa na hewa ikachafuka. Baada ya kunusa harufu ya ushuzi wote walimshuku bwana Veveve. Walimtukana bwana huyo huku wakimwelekeza kidole. Kwa kweli Veveve maskini hakufusa, lakini hakujitetea wala hakusema chochote ila alicheka kwa dharau tu. Wengine waliona mshangao na kumwuliza: ”Unacheka nini? Tuambie.“
Veveve alisema:”Ninamcheka yule aliyefusa pia amenitukana pamoja na wenzake.“


67 MAVAZI NA TAJI YA MFALME

Hapo zamani za kale palitokea ombaomba mmoja aliyeitwa Vivivi, alirudi kutoka mji mkuu. Baada ya kurudi alijisifu na kujigamba kuwa alimwona mfalme.
Mtu mmoja alimwuliza:“Mfalme amejipambaje? ”
Vivivi alijibu,“Mfalme amevaa taji iliyochongwa kwa almasi na kanzu iliyotengenezwa kwa dhahabu.”
Mtu yule alimwuliza tena:“Kama akivaa kanzu iliyotengenezwa kwa dhahabu,basi atawezaje kusalimiana na watu kwa kujiinamisha?”
Ombaomba alitema mate kwa dharau na kusema, “Wewe ni mjinga kwe likweli, iwapo atawasalimia watu wengine kwa kujiinamisha atakuwa mfalme wa namna gani?”


68 NJIA YA KUMCHOMBEZA MTOTO

PaliKuwa na yaya mmoja aliyeitwa Vovovo, alikuwa akipatishwa taabu na ulezi wa mtoto, kwa kuwa kila alivyojitahidi kumchombeza mtoto huyo ili alale alishindwa. Ghafla yaya huyo alimwambia baba wa mtoto amletee kitabu kimoja.
“Unataka kitabu cha kufanyia nini?”
Yaya Vovovo alijibu:”Niliwahi kukuona kuwa kila ulipokisoma kitabu ulikuwa ukishikwa na usingizi.
Nafikiri nikimwonyesha huyu mtoto kitabu atapata usingizi kwa haraka.”

69 HAIWEZEKANI

Zamani za kale palitokea msomi mmoja aliyeitwa Vuvuvu, alipenda kujifunza lugha. Kila aliposikia msomi mwingine akisema “Haiwezekani”alivutiwa na alipenda kurudiarudia sentensi hiyo mara kwa mara.
Safari moja, Vuvuvu alipokuwa akivuka mto alipanda mashua ya jamaa mmoja. Kwa kuwa alishughulika, akasahau sentensi hiyo, basi alizungukazunguka ndani ya mashua na kuitafuta. Mwenye mashua alimwuliza:“Umepotelewa na nini?”
Vuvuvu alijibu:“Sentensi moja.”
Mwenye mashua alishituka na kusema:“Sentensi pia inaweza kupotea?Haiwezekani!" Baada ya kusikia maneno yale msomi huyo alifurahi kwani alipata sentensi hii bila ya kutarajia, basi akamwambia:“Kanama uliiokoa sentensi hii, Mbona hukuniambia mapema na unaniacha nikihangaika!“ 2021/05/20

70 KUSHONA NGUO

Hapo zamani kulitokea mshonaji mmoja maarufu katika mji mkuu. Jina lake liliitwa. Mavazi yote aliyoshona yaliwafaa wateja. Safari moja, meya wa mji mkuu alimjia kutaka amshonee shati moja. Tatata alimwuliza meya:”Tafadhali niambie umeshika cheo cha meya kwa miaka mingapi?”
Meya alistaajabu na kumwuliza:“Kuna haja gani kujua jambo hili wakati mimi nimetaka unishonee nguo?
Tatata alijibu:”Kijana alipopata cheo kikubwa huwa na majivuno makubwa,kwa hivyo siku zote huonekana kifua mbele. Inanibidi nimshonee nguo ambayo kipande cha mbele ni kirefu na kipande cha nyuma ni kifupi; alipofikia makamo ujeuri wake hupungua, wakati huo inanibidi nimshonee nguo ambayo urefu wa mbele na wa nyuma ni sawa; mpaka aliposhika cheo cha ofisa kwa miaka mingi huonekana mnyenyekevu na huwa anafikiri mambo kwa kuinamisha kichwa,nguo yake ya wakati huo ilibidi iwe sehemu ya mbele fupi na sehemu ya nyuma ndefu. Kwa hivyo ndio maana siwezi kukushonea shati bila ya kujua kwanza umeshika cheo cha meya kwa miaka mingapi.“

71 MBILIKIMO

Mbilikimo Tetete alikuwa msomi. Aliwahi kukutana na jambazi. Jambazi lilimnyang'anya fedha zake na kutaka kumwua. Wakati jambazi liliponyanyua upanga, Tetete huyo aliongea kwa ucheshi: “Watu wananiita‘mbilikimo' ukikata kichwa changu si nitakuwa mfupi mno?” Jambazi lilicheka bila ya kujizuia na kuuteremsha upanga.

72 KUFICHA NGUO YA MWIZI

Siku moja mwizi alipenya katika familia ya mzee Tititi, lakini bahati mbaya familia hii ilikuwa maskini. Chumbani hamkuwa na kitu chochote ila chungu cha mchele kikiwa kimewekwa kando ya kitanda. Mwizi aliwaza: "Lakini hata hivyo si vibaya kuiba mchele huu kuliko kuondoka mikono mitupu. Baada ya kurejea nyumbani nitaweza kupika ubwabwa.”
Basi alivua shati lake na kulitandaza chini. Kumbe mke na mume wa familia hii walikuwa wamelala kitandani. Tangu mwizi alipoingia chumbani, mzee Tititi alizinduka kutokana na mchakacho na kuona vitendo vyake vyote kwa kutegemea mbalamwezi. Wakati mwizi alipokwenda kuchukua chungu hicho, mzee Tititi alinyoosha mkono polepole, akachukua shati la mwizi na kulificha mgongoni. Baada ya kugeuka, mwizi aligundua kuwa shati lake halipo. Wakati huo mke wa mzee Tititi aliamka pia. Alimwuliza mume wake kwa haraka:“Sikiliza, sauti gani hiyo? Labda kuna mwizi?”
Mzee Tititi alimjibu: “Niliamka kitambo lakini sikumwona mwizi yeyote. Usiwe na wasiwasi .”
Mwizi aliposikia maneno ya mzee alisema kwa sauti kubwa: “Nani kasema hakuna mwizi? Nilipoweka chini shati langu tu, mara lilitoweka.”

73 HAKIMU ANAYEKULA RUSHWA

Alikuweko hakimu aliyeitwa Tototo, ambaye alipenda kula rushwa. Siku moja alikuwa anatoa hukumu ya kesi moja. Kabla ya kuhukumu mdai alimpa hongo ya shilingi hamsini, hakimu akazipokea. Baada ya mdaiwa kujua jambo hilo naye alimpa hongo ya shilingi mia, nazo pia hakimu alizipokea.
Wakati kesi hiyo ilipoanza tu, mara hakimu huyo alitoa amri kumpiga mdai fimbo 50. Mdai alisema: “Mimi nina hoja,” huku akionyesha vidole vyake vitano kusudi kudokeza kwa hakimu: “Niliwahi kukuhonga shilingi 50!”
Hakimu alifahamu maana yake lakini alicheka kwa kejeli, halafu alionyesha kidole kimoja kwa mdaiwa na kusema: “Yeye ana hoja zaidi kuliko wewe!” Baada ya kusema akanyoosha vidole vyake kumi vya mikononi kusudi kudokeza kwa mdai: Hongo aliyonipa mdaiwa ni maradufu ya hongo yako!

74 KUPIGA MARIMBA MTAANI

Hapo zamani palitokea mpiga marimba aliyeitwa Tototo, naye alitamba kwa ufundi wake. Siku moja, alipopiga marimba yake mtaani wakazi wengi walikuja kusikiliza, lakini waliposikia kuwa muziki wenyewe si mali kitu, wakaanza kuondoka mmoja baada ya mwingine. Mwishowe alibakia ajuza mmoja tu aliyekuwa amesimama kando yake. Bwana Tototo alifurahi na kuongeza ufundi, hatimaye alisema: “Vyema sana. Kwa vyovyote vile nina mwenzi mmoja anayependa muziki wangu. Kusikiliza kwako hapa kunanifariji. Jambo hili linathibitisha kuwa sikufanya bure mazoezi ya kupiga marimba kwa miaka nenda.”
Ajuza alimkata kauli: “Kama nisingesubiri kuichukua meza yangu uliyowekea marimba, ningeondoka zangu kwenda nyumbani mapema zaidi.”

75 KUISHI MILELE

Shaibu Sasasa aliwakaribisha wageni wengi kuhudhuria katika sherehe yake kwa ajili ya kukumbuka siku yake ya kuzaliwa. Mmojawapo wa wageni alimpa pongezi kwa kusema: “Nakutakia maisha marefu kama msonobari!”
Baada ya kusikia maneno yake shaibu Sasasa alikunja uso na kusema bila ya furaha:“Lakini mbona iko siku ambayo msonobari utakauka?”
Akatokea mtu mwingine na akampongeza shaibu huyo: “Nakutakia maisha marefu kama mlima!”
Baada ya kusikia pongezi yake mzee alikunja uso tena na kusema:“Iko siku pia mlima utamomonyoka.”
Watu hao wawili walimwuliza kwa kauli moja: “Mzee Sasasa, huna habari kuwa mti na mlima vinadumu sana, lakini mbona bado hujaridhika! Tafadhali tuambie unataraji kuishi miaka mingapi?” Shaibu Sasasa alisema huku akiinamisha kichwa chake:“Afadhali niweze kuishi milele.”

76 AKARI YA“KUTOKUFA”

Kulikuwa na mtu aitwaye Sesese ambaye alimpa Mfalme mtungi wa akari. Jina la akari hiyo ni“KUTOKUFA”. Baada ya kusikia habari hii Waziri Mkuu wa ufalme huo, alikunywa kwa siri akari hiyo. Baada ya mfalme kusikia vile alichukia na kutaka kumwua Waziri Mkuu wake. Waziri Mkuu alisema: “Akari niliyokunywa ni akari ya ‘KUTOKUFA’. Kama ukiniua bila shaka sitakufa; kama nitakufa basi akari hii haitaitwa ‘KUTOKUFA”. Mfalme alicheka na kumsamehe.

77 USIUZE KWA MKOPO

Kulikuwa na mshamba aliyeitwa Sisisi, ambaye alikuwa na ubahili mpaka shingoni. Alipokaribia kufa Sisisi alimpa mke wake wasia: “Nilijitahidi kwa nguvu na jasho langu mpaka kuwa na utajiri kama huu. Baada ya kufa kwangu jaribu kujifunza njia yangu ya kuendeleza maisha. Usipoteze mali yoyote bure. Nakuambia:“Nikifa, chuna ngozi yangu uiuze kwa fundi wa ngozi; kata nyama yangu uiuze kwa mwenye bucha na safisha mifupa yangu uiuze kwa mwenye duka la rangi.” Baada ya kusema maneno hayo alisubiri jawabu la mke wake akiwa amelala kitandani, lakini mke wake hakusema chochote kwa sababu ya majonzi. Baada ya kuzimia kwa dakika mbili, Sisisi alipata fahamu tena, akasisitiza tena maneno aliyosema dakika mbili zilizopita, japo hivyo bado hakuweza kutuliza moyo, akaongeza:“Hivi leo watu wote hawaaminiki. Kumbuka, kwa vyovyote vile usikubali kuwauzia kwa mkopo.”

78 KUPENDA SIFA

Palitokea mkuu wa wilaya. Jina lake lilikuwa Sososo, ambaye alipenda kusifiwa na wengine. Kila alipotangaza amri, wafuasi wake wakimsifu yeye, naye akaona furaha; wasipomsifu atachukia. Mtumishi wake alitaka kujipendekeza kwake, basi alisema kwa makusudi nyuma ya mgongo wa Sososo:“Maofisa wote hupenda kusifiwa na watu wengine isipokuwa mkuu wetu wa wilaya. Yeye huwadharau wale watu wanaombembeleza.”
Maneno hayo yalifika upesi kama umeme masikioni mwa Sososo, naye alimwita huyo mtumishi haraka, akamsifu huku akimpigapiga bega lake: “Ha, ha, ha, anayenifahamu vizuri ni wewe peke yako tu. Wewe ni mtumishi wangu mwema kwelikweli!”

79 KUAZIMA NGUO

Siku moja, mvua ilikuwa inanyesha chapachapa. Mzee afkani Sususu aliazima nguo kwa rafiki yake, akaivaa na kufunga safari pamoja na mhudumu wake. Barabara ilikuwa na matope mengi. Mzee Sususu aliteleza na kuanguka. Mkono wake mmoja ukavunjika na nguo aliyovaa pia ilichafuka. Mhudumu wake alikwenda haraka kumwinua na kupapasa mkono wake aliokuwa ameumia. Mzee Sososo alimzuia: “Lete maji kwanza, usafishe nguo hii, usijali mkono wangu ijapokuwa umevunjika.”
Mhudumu wake alimwuliza: “Mbona huujali mwili wako bali unajali tu nguo iliyochafuka?”
Mzee Sususu alijibu:“Mkono ni wangu mwenyewe. Nani atakuja kuudai?”

80 KILEMBA CHA UKOKA

Hapo zamani kulikuwa na wanafunzi wawili ambao baada ya kufuzu masomo yao watakwenda kushika vyeo vya ofisa. Siku ya kuondoka walikuja kwa mwalimu wao Rarara kumwaga. Mwalimu aliwaambia: “Katika dunia ya leo mnapoonana na mtu yeyote bora mumvishe kilemba cha ukoka, ama sivyo hamwezi kufaulu.”

Mmojawapo kati ya wanafunzi hao wawili alisema: "Maneno ya mwalimu ni sawa kabisa. Katika dunia ya leo wako watu wangapi wasiopenda kuvishwa kilemba cha ukoka kama mwalimu wetu!”
Mwalimu Rarara alifurahi baada ya kuyasikia maneno hayo. Baada ya kuagana na mwalimu na kutoka nje, mwanafunzi huyo alimwambia mwenzake: “Nimefanikiwa kumvisha mwalimu wetu kilemba kimoja cha ukoka.”
2021/05/21


81 KUCHEZA BAO

Palitokea mchezaji wa bao Rerere, ambaye alijigamba kuwa alikuwa mchezaji hodari. Aliposhindana na mtu mwingine Rerere alishindwa raundi tatu. Siku iliyofuata, mzee mmoja alimwuliza:
“Je, jana ulishindana na yule mtu raundi ngapi?”
“Raundi tatu.”
“Matokeo yalikuwaje?”
“Raundi ya kwanza sikumshinda, raundi ya pili hakushindwa, raundi ya tatu niliomba nitoke sare lakini kwa vyo vyote vile hakukubaliana nami. ”


82 VIFO VILIVYOLETWA NA UBAHILI

Katika Mkoa wa Ushasha kulikuwa na kabaila mwenye choyo ambaye aliitwa Ririri. Karibu na kwake kulikuwa na hekalu la kale. Katika hekalu hilo walikuweko sufii wawili ambao waliheshimiwa na wanakijiji, nao waliishi kwa kutegemea sadaka. Kila sufii walipokwenda nyumbani mwa Ririri mke wake alikuwa akiwapa baadhi ya sadaka. Safari moja, mke
wa Ririri alipokuwa akiwapa sufii sadaka aligunduliwa na Ririri aliyewachukia sufii hao moyoni, akataka kuwaadhibu.
Siku moja, sadfa sufii hao wawili walikuja tena kwa jambo jingine. Mara hii Ririri alijifanya ni mwenye ukarimu mno. Alipokuwa akiwakaribisha akamwambia mhudumu wake faraghani kuwa aende kupika chapati nne chapuchapu na kuzitia sumu ndani ya chapati. Baada ya kumaliza kupika chapati, Ririri alizitoa na kuwakaribisha wageni. Kwa kuwa sufii hao wawili walikuwa wamekwisha kula chakula muda mfupi uliopita, hivyo hawakuweza kula chapati zile, basi walizitia katika mifuko na kurejea hekaluni. Ririri akasema moyoni: " Ni bora zaidi mnakula chapati hizo katika hekalu, kwani mkifa sitakuwa lawamani.”
Asubuhi ya siku ya pili, watoto wawili wa Ririri walikwenda hekaluni kucheza wakiwa wamevaa mavazi mazuri. Baada ya kuwauliza watoto hao, sufii wakafahamu kuwa wao walikuwa ni watoto wa kabaila. Mara walimwambia sufii mmoja mdogo aende kuwaletea chakula kitamu. Sufii huyo mdogo alitafuta chakula kwenye kila chumba lakini hakupata chakula chochote kitamu. Mwishowe aligundua chapatti nne mezani ambazo zilikuwa ni zile chapati walizoleta kutoka nyumbani kwa Ririri, basi akampa kila mtoto chapati mbili. Watoto hao wawili hawakuweza kujua kuwa ndani ya chapati hizo mlikuwa na sumu. Kila mtoto alikula chapati moja na kutia chapati iliyobaki mfukoni, halafu wakarejea nyumbani kwao .
Walipoingia nyumbani tu mara walianza kupiga makelele kuwa walikuwa wanaumwa na matumbo, kisha wakaanguka chini. Muda si muda, walikutakuta mikono na miguu na wakakata roho. Ririri alikuja mbio lakini hakujua sababu ya kifo chao. Alimwuliza mhudumu, mhudumu naye pia hakujua kitu. Ririri alichunguzachunguza miili ya watoto, akagundua chapati mbili.
Baada ya kugundua kuwa zilikuwa ni zile chapati walizopikiwa sufii,
Ririri alijua watoto walikufa kwa kula sumu. Hakuwa na la kufanya ila kunyamaza tu na kulia. Ingawa alilia sana na mara kadhaa alikaribia kupoteza fahamu lakini hakuthubutu kusema wazi kiini cha kifo chao.
Niliwahi kumwambia bahili mmoja kuwa anafanana kidogo na kabaila huyo, lakini hakuridhika na kusema haraka haraka: "Unasema kabaila huyo alipatwa na mkasa kwa sababu yeye ni bahili. Kwa mujibu wa maelezo yako, mimi naona kuwa kabaila huyo si bahili hata kidogo. Mimi ningekuwa kabaila huyo, hata zile chapati nne nisingaliwapa wale sufii, hivyo mkasa wa namna hiyo ungewezaje kutokea?”


83 KUPELEKA WARAKA

Zamani za kale, mkuu wa mkoa fulani alipomtuma tarishi wake Rororo kupeleka waraka muhimu kwa mkuu wa wilaya nyingine, alimwambia tarishi huyo aende kwa kupanda farasi ili aweze kupeleka waraka upesi zaidi. Tarishi huyu hakumpanda farasi, bali alitembea kwa miguu huku akimfukuza yule farasi nyuma yake.
Buda mmoja alimwuliza Rororo:“Shughuli yako ni muhimu na ya haraka, kwa nini hupandi farasi? Ukipanda farasi si utaweza kumaliza shughuli yako mapema zaidi?”
Rororo alijibu:“Si vyepesi zaidi Kutembea kwa miguu sita kuliko kutembea kwa miguu minne?”



84 KANZU INAWAKA MOTO

Palikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Papapa ambaye alikuwa mtaratibu. Siku moja, hali ya hewa ilikuwa baridi. Alikuwa akiota moto pamoja na rafiki yake. Alipoona badani ya kanzu ya Rafiki yake inaungua, alisema polepole:“Kuna jambo moja ambalo nimeliona kwa muda. Nataka kukuambia lakini naogopa pengine utakuwa na haraka, maana wewe ni mwepesi. Kama nisipokuambia pia nahofia kuwa utapata hasara kubwa. Sijui nifanyeje. Niseme au nisiseme?”
Rafiki yake alimwuliza: “Jambo gani?”
Baada ya kuwaza na kuwazua kwa muda mrefu, mwishowe Papapa alisema taratibu maneno aliyotaka: “Badani ya nyuma ya kanzu yako imewaka moto.”
Rafiki yake alivua kanzu yake kwa haraka na kuizima, halafu alilalamika kwa hasira: “Maadamu umeona kwa muda mrefu, kwa nini hukuniambia mapema?”
Papapa alisema:“Poa moto! Nilisema sasa hivi kuwa wewe ni mwepesi. Tazama jinsi unavyokuwa sasa!”



85 KUAZIMA NG'OMBE

Siku moja, mkulima Pepepe alikwenda kwa mzee tajiri kuazima ng'ombe kwa njia ya barua. Alipofika alimkuta mzee tajiri akiwa na mgeni wake. Bila ya kusema chochote alimkabidhi barua. Mzee tajiri aliipokea na kuifungua barua hiyo mbele ya mgeni wake kwa kuwa hajui kusoma na hakupenda mgeni wake afahamu hivyo, alijifanya anaisoma barua kwa kupitisha macho na kumumunya mdomo hali akiinamisha kichwa kwa kukubali, kisha akasema kwa mkulima huyu: “Nimekwisha elewa shida yako. Nitakuja mimi mwenyewe baadaye.”


86 KIUMBE KINACHOFANANA NA KUTOFAUTIANA NA BINADAMU

Hakimu Pipipi alipoanza kazi yake alimwamuru tarishi wake aende kukikamata kiumbe kinachofanana na kutofautiana na binadamu na kukifikisha mahakamani. Tarishi huyo aliona muhali. Baada ya kurejea nyumbani alishauriana na mke wake kuhusu jambo hilo.
Mke wake alimwambia: "Kuna shida gani kutafuta kiumbe hicho? Mvalishe nyani mmoja mavazi na kofia, kisha mpeleke mahakamani na kusema: 'Nimekuletea kiumbe kinachofanana na Kutofautiana na binadamu.'“
Kwa kufuata shauri la mkewe, tarishi huyo alimpamba nyani mmoja na kumpeleka mahakamani kuonana na hakimu. Baada ya kukiona kiumbe hicho, hakimu
Pipipi alifurahi, akamtunukia nyani matunda. Naye nyani alikuwa mtiifu. Hakimu alipoona kuwa nyani huyo alipendeza kiasi kile, alimwambia tarishi ampeleke nyani huyo karamuni. Baada ya nyani huyo kunywa ugimbi unyama wake ulianza kujitokeza, akavua kofia, akararua nguo, akaanza kurukaruka na kulialia ovyo. Hakimu Pipipi alimtukana:“Nyani wee! Huna adabu. Kabla ya kunywa ugimbi ulishabihiana na binadamu, lakini baada ya kunywa ugimbi hushabihiani tena na binadamu.”


87 KICHEKO CHA KIPOFU

Kulikuwa na kipofu aliyeitwa Popopo, aliishi na marafiki zake wenye macho. Siku moja, alipokuwa akiongea nao, wenzake waliona jambo fulani la kuchekesha, wakaangua kicheko kwa pamoja. Popopo kusikia vile naye alicheka pia. Wenzake walimwuliza: “Unacheka nini?”
Kipofu aliwajibu: “Nimesikia kicheko, bila shaka nami nikicheka sikosei.”


88 KICHWA LAINI

Kinyozi Pupupu alipomnyoa mteja wake, bahati mbaya baada ya muda mfupi alikuwa amekwisha mjeruhi kichwa cha mteja mara kadha wa kadha. Kwa hivyo ilimbidi asiendelee kumnyoa kwa kuhofu kwamba atashindwa hata kuona mahali pa kupitisha wembe. Pupupu alipoagana na mteja huyo alimwambia: “Kichwa chako bado laini, siwezi kukigusa kwa wembe. Afadhali uende na urudi wakati kichwa chako kitakapokuwa kigumu.”

89 KUMKIMBIA MDAI

Kulikuwa na bwana aitwaye Nanana, ambaye alikuwa na madeni mengi kiasi kwamba yalimshinda kulipa na kuamua kutumia hekima kuwakwepa wadai.
Siku moja, mdai mmoja alikuja kudai haki yake. Bwana huyo alimlaghai: “Enhe, umefanya vizuri kuja, kuna mjane mmoja tajiri, natarajia kumwoa, lakini sina fedha za mahari. Ukinisaidia baadhi ya fedha leo hii, baada ya ndoa, si kama nitaweza kulipa deni lako tu bali pia nitaweza hata kukukopesha fedha nyingi.”
Mdai alisadiki, akamkopesha shilingi elfu saba zaidi.
Baada ya kupata shilingi hizo, Nanana alipamba nyumba yake ili kumdhihirishia mdai. Mdai alipoona vile alizidi kuamini maneno yake.
Siku moja, mdai alipopita mbele ya nyumba yake, alipiga hodi, akasikia mwanamke mmoja anajibu kutoka ndani: “Mume wangu ametoka kidogo.”
Tangu siku hiyo mdai alikuja mara tano, kila mara alisikia jibu lilelile na mlango haukuwahi kufunguliwa hata mara moja.
Siku nyingine, udadisi ulimfanya mdai atamani kujua ukweli wa jambo hili, basi alikwenda mbele ya dirisha la mdaiwa, akachungulia ndani kwa siri, hakuona mwanamke wala nini ila mdaiwa tu akiwa anabana pua yake ili kuigiza sauti ya mwanamke. Mdai alipoona hali hiyo alighadhibika. Ghafla alivunja dirisha na kujipenyeza ndani. Alimshika mdaiwa na kumpiga ngumi. Kwa sababu mdaiwa allizoea kuigiza sauti ya mwanamke kwa muda mrefu, hakuweza kubadilisha tabia hiyo kamwe, kwa hivyo alikuwa bado akibana pua yake na kusema kwa sauti ya kike: “Ni mume wangu aliyekopa fedha kwako, bali siye mimi. Mimi ni mwanamke, jambo hili linanihusu nini?


91 USISEME MANENO YA UAMUZI

Alikuweko baba mtu aitwaye Nenene, alimfundisha mwana wake: “Unaposema, usiseme maneno ya uamuzi.”
Mwanawe aliuliza: “Nini maana ya kutosema maneno ya uamuzi?”
Wakati walipozungumza, Sadfa jirani mmoja alikuja kuazima vitu . Nenene alimwambia mwanawe akimwonyesha jirani huyu: “Kwa mfano, jirani huyu amekuja kuazima vitu. Tusiseme kwamba vyote anavyotaka vipo wala tusiseme vitu vyote havipo, bali inafaa tuseme pengine vipo nyumbani na pengine havipo nyumbani. Jambo lolote tunaweza kusema namna hiyo.”
Mwana alikumbuka maneno hayo moyoni. Siku moja, alikuweko mgeni aliyekuja mbele ya nyumba akauliza: “Baba yako yuko nyumbani?”
Mwana alijibu, “Pengine yupo na pengine hayupo.”

92 MJUKUU

Mzee Ninini alikuwa na mjukuu ambaye alikuwa na umri wa miaka kumi na zaidi. Lakini kwa bahati mbaya mjukuu huyo alikuwa mzembe na alipenda kucheza badala ya kujifunza vizuri. Mzee Ninini alikuwa akimpiga mara kwa mara kwa fimbo, bali mjukuu huyo hakubadilisha tabia yake hata kidogo. Baba wa mtoto huyo alikuwa na mtoto huyo mmoja tu kama roho, kwa hivyo alikuwa akihangaika, si kama aliogopa kuwa mtoto wake hawezi kuvumilia kupigwa tu bali pia alihofu kuwa mtoto wake akifa hatakuwa na mirthi. Hivyo kila wakati mzee Ninini alipomwadhibu mjukuu wake, baba wa mtoto alikuwa akimsihi mzee huku akilialia na kusema kuwa asimpige mtoto wake.
Mzee Ninini alimjibu kwa hamaki:“Ninakufundishia adabu mtoto wako, ama unaona si vema kufanya hivyo?” Basi aliendelea kumpiga mjukuu wake vibaya. Baba wa mtoto hakuwa na la kufanya hata kidogo.
Asubuhi ya siku moja ilianguka theluji kubwa. Mjukuu huyo alicheza mchezo wa kutengeneza mpira wa theluji. Mzee Ninini alipomwona hakusema chochote, akamvua mjukuu wake mavazi yake na kumwamuru apige magoti thelujini. Jinsi mjukuu wake alivyotetemeka kwa baridi iliwafanya wengine wamwonee huruma.
Baba wa mtoto hakuthubutu kusema chochote ila alivua pia mavazi yake mwenyewe na kupiga magoti kando ya mtoto wake. Mzee Ninini alimwuliza baba wa mtoto kwa mshangao: “Mtoto wako anastahili kuadhibiwa hivyo, kwa sababu ana makosa, kwa nini wewe pia unapiga magoti hapa?”
Baba wa mtoto alisema huku machozi yakimtiririka mashavuni:“Kwa kuwa unafanya mtoto wangu apigwe na baridi na mimi ninamfanya mtoto wako apigwe na baridi pia!”
Mzee Ninini aliangua kicheko na akaamua kumsamehe mjukuu wake.


93 MASHARUBU YA MANJANO

Palikuwa na mtu aitwaye Nonono, ambaye masharubu yake yalikuwa ya manjano. Alikuwa akijisifu mbele ya mke wake:“Kati ya watu wenye masharubu ya manjano hakuna mnyonge. Hawawezi kunyanyaswa na wengine hata kidogo”
Siku moja, Nonono alipigwa na mtu mwingine. Baada ya kurejea nyumbani mke wake alimkejeli kwa kumkumbusha maneno aliyosema hapo awali. Hata hivyo Nonono alijitetea: “Unajua nini mke wangu! Masharubu ya mtu yule ni mekundu kabisa!”


94 KULA UPEPO NA KUVAA MAJANI YA MITI

Palitokea mjakazi aitwaye Nununu, ambaye alikuwa akinyanyaswa mara kwa mara na bwana wake. Kila siku alikuwa anapewa chakula kidogo.
Siku moja, Nununu alipofungua kinywa na kutega upepo bwana wake alimwona akashangaa na kumwuliza: “Nununu Unafanya nini?”
“Mimi huwa na njaa, hivyo ninajifunza njia ya kula upepo. Nikifaulu nitafanya kazi tu, sitakula chakula chenu.”
Baada ya kusikia maneno hayo bwana wake alifurahi na kumwambia bila ya kukawia: “Kazana kujifunza! Nimeweka akiba ya majani mengi ya miti, leo nitakushonea nguo kwa kuyatumia majani hayo. Ukifaulu kujifunza njia hiyo utakula upepo badala ya chakula, kama sitakushonea nguo, wengine watasema sina utambuzi.”


95 KUTOMWALIKA MGENI

Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Mamama ambaye alikuwa bahili. Mamama hajawahi kualika mgeni hata mmoja tangu kuzaliwa kwake. Siku moja, jirani yake aliazima ukumbi wake ili kuandaa karamu. Buda mmoja alistaajabu akamwuliza mtumishi wa Mamama:“Leo bwana wako atamwalika mgeni?”
Mtumishi huyu alijibu: “Ukitaka kumwona bwana wangu akialika mgeni, inakubidi usubiri mpaka siku ile atakayozaliwa upya.”
Bila kutegemea Mamama aliyasikia maneno hayo, akasema kwa hamaki:“Kwa nini ulimwahidi tarehe!”


96 USIKATE MWILI WA CHUI

Mememe alikuwa amebanwa kinywani mwa chui. Mtoto wake alikuwa na shoka mkononi, alimfuata chui huyu kwa haraka ili kumwokoa baba yake.
Wakati Mememe alipoona mwanawe anataka kuukata mwili wa chui alipiga kelele kwa sauti kubwa:“Mwanangu, usikate mwili wake, kata miguu tu, kwa sababu ngozi ya chui ina thamani kubwa. Ukiuza utapata fedha nyingi.”


97 KULIMA KWA USHIRIKA

Kulikuwa na ndugu wawili walioamua kulima ngano kwa ushirika. Baada ya kuvuna mazao walijadiliana jinsi ya kugawana. Kaka Mimimi alimwambia didi yake:“Nitachukua sehemu ya juu na wewe uchukue sehemu ya chini.”
Didi alishangaa baada ya kusikia maneno haya yasiyokuwa na usawa.
Mimimi alimwambia didi yake bila ya kuchelewa:“Hamna shida. Mwaka ujao utachukua sehemu ya juu na mimi nitachukua sehemu ya chini.”
Wakati wa kupanda ngano ulipowadia, didi alimhimiza kaka yake wapande mapema.
Mimimi alisema: “Naona mwaka huu bora tupande majimbi.”


98 MUNGU WA SHABAHA

Hapo zamani za kale ofisa Momomo aliwaongoza askari wake kwenda kupigana vita. Wakati alipokaribia kushindwa ghafla jeshi la mungu lilishuka kutoka mbinguni kumsaidia. Mwishowe Momomo alipata ushindi. Momomo alipiga magoti mbele ya mungu na kumwomba amwambie jina lake. Mungu alimjibu: “Mimi naitwa mungu wa shabaha.”
Momomo akaendelea kumuuliza mungu wa shabaha: “Niliwahi kukupa manufaa gani hata ukaja kuniokoa?”
Mungu wa shabaha alimjibu: “Nakushukuru kwa vile siku za kawaida hukuwahi kunijeruhi hata mara moja wakati ulipofanya mazoezi ya kulenga shabaha uwanjani.”


99 Daftari ya Kuchangia Hela

Palikuwa na askari aitwaye Mumumu, ambaye siku moja alikwenda kutembelea hekalu moja maarufu. Kwa kuwa alivaa mavazi ya kiraia, mtumishi wa hekalu alifikiri huyu ni mtu duni, hakumtendea kwa adabu njema. Askari Mumumu alimwuliza mtumishi:“Naona hekalu lenu linahitaji matengenezo. Kama mkipungukiwa hela, basi lete daftari nitaandika.”
Mtumishi alifurahi akaleta chai kwa kumshukuru mtalii huyo. Kwa unyenyekevu na adabu nzuri alimpa mtalii daftari na kalamu. Mtumishi wa hekalu alipoona mtalii akiandika “makao makuu ya jeshi”, mtumishi alifikiri huyu pengine ni ofisa mwandamizi, akapiga magoti mbele ya mtalii. Chini ya mstari wa kwanza, mtalii akaongeza “askari wa batalioni ya kwanza ya rejementi ya kwanza.” Mtumishi alipoona huyu ni askari tu, akainuka na uso wake ukakunjamana. Mtumishi alipomwona mtalii akiandika “nachangia”, alifikiri pengine atachangia hela nyingi, akapiga magoti tena. Mumumu alipoandika “senti 30”, mtumishi akainuka kwa hasira hali uso wake umekunjamana tena.



100 ASKARI MGENI

Askari mgeni Lalala alifika kambi ya jeshi. Afande wa kambi hiyo alikuwa akitumia ujanja wa namna kwa namna ili kupata fedha kutoka kwa askari wake.
Siku moja, afande na Lalala walitoka nje ya kambi kutembea. Afande alimwambia askari Lalala kwa makusudi atangulie mbele. Lalala alitii amri yake, lakini baada ya kutembea hatua kumi tu afande alimtukana: “Tukitembea hivyo, si itakuwa ninafuata nyuma ya matako yako?”
Kisha alimwamrisha Lalala amfuate. Askari Lalala alimtii, lakini hakutarajia kuwa afande angemtukana tena:“Tukitembea hivyo, si itakuwa mimi ninakutembeza?”
Lalala alivunjika moyo, hakujua la kufanya, ilimbidi apige magoti na kumwuliza:“Afande, inanipasa nitembee namna gani?”
Afande alimjibu: “Kila mwezi nipe kiasi fulani cha fedha, nitakuachia huru utembee utakavyo.”

2021/05/25
 
Back
Top Bottom