Mabadiliko Katiba Zanzibar: Yanaimarisha au yanabomoa Muungano?

abdulahsaf

JF-Expert Member
Aug 31, 2010
858
130



Written by Ashakh (Kiongozi) // 19/02/2011 // Habari // 7 Comments

Joseph Mihangwa
Februari 16, 2011
HATIMAYE uhasama wa kisiasa Visiwani Zanzibar uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 (tangu 1957 – 2010) umemalizika kwa vyama vikuu Visiwani humo – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kuunda Serikali ya Mseto – Serikali ya Umoja wa kitaifa.
Uhasama huo wa kihistoria umehusisha zaidi vyama vya siasa kinzani, na kwa sehemu kubwa ni Afro-Shiraz – ASP (1957) na Zanzibar Nationalist Party – ZNP (1954) ambavyo vilirithiwa na CCM [ASP] na CUF [ZNP] hadi uhasama huo ulipomalizika hivi karibuni.
Ifahamike kuwa, wakati Tanganyika na Zanzibar zikiungana Aprili 26, 1964, wakati huo Zanzibar ikiwa chini ya chama kimoja cha ASP (baada ya kufutwa kwa ZNP, ZPPP na Umma Party, Februari 1964), uhasama huo ulifichika tu kwa kiwango cha vyama, lakini uliendelea kuwapo chini kwa chini kwa misingi ya historia ya kisiasa kwa jamii ya Kizanzibari.
Kwa maridhiano ya CCM/CUF, Wazanzibari wametumia kivuli cha maridhiano hayo kurekebisha Katiba yao marekebisho ambayo baadhi ya Watanzania wanaona, ama yanabomoa Muungano kwa kuingiza mambo ambayo awali yalikuwa ya Muungano, au kwa kutoa tafsiri zinazobadili kabisa tafsiri sahihi na mtizamo wa Muungano na kutikisa mustakabali wa Muungano huo. Kuna ukweli gani kwa madai haya?. Na kama ni hivyo, kwa nini Serikali ya Muungano imenyamaza?.
Kuweza kujua kama Muungano umetikiswa au la, yatupasa kufahamu kwanza msingi na muundo wa Muungano wenyewe, kujua wapi umeguswa; bila hivyo tunavyosikia kitakuwa ni kilio cha “mbweha mbweha”, kidhihaka na kimzaha kwa mtu mwoga au mwendawazimu.
Tuambieni, Nani miongoni mwa Watanzania anayefahamu msingi na muundo sahihi wa Muungano bila kuingiza siasa na ukereketwa usio na mantiki? Na ajitokeze atuambie!
Nakuambia msomaji wangu, hakuna! Huyu atakwambia ni muundo wa serikali moja chini ya nchi moja; mwingine ataeleza ni nchi mbili zenye serikali moja; na yule pale atasema ni muundo wa serikali tatu, kwa maana ya Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano. Yote haya yanategemea ufundi wa kila mmoja wa kuchakachua siasa za Muungano.
Uchakachuaji huu umetufikisha mahali na kuazimia kwamba Muungano hauhojiki wala kuzungumzika, na kwamba kuhoji muundo wa Muungano ni usaliti kwa Muungano.
Kwa sababu hii, Muungano umebakia kuwa “fumbo la imani” kwa Watanzania, wakiuangalia ukienda mrama kwa jina la “kero za Muungano” bila kutafutiwa ufumbuzi. Rais wa awamu ya Pili Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, ilimgharimu nafasi hiyo kwa kufanya hivyo mwaka 1984.
Je, Maridhiano yametikisa vipi Muungano na Katiba ya Muungano? Ni kwa makusudi au kwa kutoelewa? Kama hivyo ndivyo, nini kifanyike katika mchakato tarajiwa wa mabadiliko ya Katiba nchini?. Hebu tuone kwanza Muungano wenyewe ukoje ili kupata majibu.
Nimesema mwanzo kwamba, muundo wa Muungano haueleweki kiasi kwamba wanasheria na wasomi wengi, kwa kushindwa kuelewa ulivyo tata, wameishia kuelezea kuwa “ni wa aina yake na wa kipekee duniani.”
Lakini pamoja na hayo, tunaweza kupata mawili matatu kwa kuudodosa Mkataba wa Muungano huo, uliotiwa sahihi na waasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Tanganyika) na Abeid Amani Karume (Zanzibar) Aprili 26, 1964 ili kuweza kujibu, angalau kwa kiwango fulani, baadhi ya maswali hayo hapo juu.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Mkataba wa Kimataifa wenye masharti yanayopashwa kuzingatiwa na kufuatwa na pande zote mbili za Mkataba huo kwa usawa, kinyume chake ni ukiukaji wa Mkataba huo kwa athari kubwa kwa uhai wa Muungano. Ni nani, na ni kipi hicho kilichoungana au kuunganishwa?.
Aprili 22, 1964, mjini Zanzibar, Waasisi wa Muungano walitia sahihi Hati (Mkataba) ya Muungano wa Mataifa yao huru. Utangulizi wa Mkataba huo unasomeka ifuatavyo:
Kwa kuwa Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na ile ya Watu wa Zanzibar …..zimekutana na kufikiria Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika pamoja Jamhuri ya watu wa Zanzibar: Na….zina shauku kwamba Jamhuri hizo mbili zitaungana kuwa dola moja ya Jamhuri [sovereign Republic, not State] kwa mujibu wa Hati [Mkataba] ya Muungano huu…..
Hapa, kuna jambo moja lililo dhahiri, kwamba Muungano huu haukufikiwa na, au kwa ridhaa ya Watanganyika na Wazanzibari, bali ulifikiwa na Wakuu wa nchi hizo kwa niaba ya Serikali zao, na si kwa niaba ya watu wao ambapo ingekuwa hivyo, ingehitajika kura ya maoni.
Ni kwa sababu hii, baadhi ya watu wamefikia hatua ya kuhoji uhalali wa Muungano kama huu ambao haukushirikisha wananchi wa nchi hizo mbili.
Lakini kuna jibu la Kisheria juu ya hoja hii; kwamba, Waasisi hao waliingia Mkataba huo kwa kuzingatia misingi na mfumo wa Sheria za Uingereza (Common Law) ambazo nchi hizi mbili zinafuata na kuzingatia. Chini ya mfumo wa Sheria hizo, Mkuu wa nchi ana ridhaa isiyohojika, kutia sahihi mikataba ya Kimataifa kwa niaba ya nchi yake; na ndivyo ilivyokuwa kwa Mkataba wa Muungano.
Kutia sahihi pekee Mkataba huo wa Kimataifa kulikuwa hakutoshi kuzalisha Muungano. Ili Muungano huo utekelezeke Mabunge ya nchi mbili hizo yalitakiwa kutunga Sheria kila moja kuridhia (to ratify) Mkataba huo (kama ulivyo na bila ya kupotosha wala kufanyia marekebisho) ili uwe na nguvu ya kisheria kwa utekelezaji.
Bunge la Tanganyika liliridhia Mkataba huo Aprili 25, 1964 kwa Sheria Namba 22 ya 1964 inayojulikana kama “Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”. Kuna ukinzani miongoni mwa Wazanzibari kuhusu kama Baraza la Mapinduzi/Baraza la Mawaziri liliridhia Mkataba huo au la. Ifahamike kuwa wakati huo, Zanzibar haikuwa na Bunge kwa jina lolote lile.
Nini kilichoungana au kuunganishwa? Ibara ya 4 ya Mkataba wa Muungano inaweka mambo 11 tu yanayopaswa kushughulikiwa na Bunge la Muungano na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (ambalo ndilo jina la Muungano, na si Tanzania), kwa maana ya Serikali ya Muungano.
Mambo hayo ni: Katiba ya Muungano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Mambo ya nchi za Nje, Ulinzi (si na Usalama ambao umeongezwa mwaka 1984 baada ya kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar), Polisi na Mamlaka yanayohusika na hali ya hatari (emergency powers).
Mengine ni Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Nje na Mikopo, Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano (si kwa Tanganyika na Zanzibar), Kodi ya Mapato, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa; na mwisho, ni Bandari, Usafiri wa Anga (wa kiraia) Posta na Simu za Maandishi (telegraphs).
Kwa mujibu wa ibara ya 6 (a) ya Mkataba wa Muungano, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano anatajwa kuwa Mwalimu Julius K. Nyerere; ambapo ibara ya 6 (b) inamtaja Sheikh Abeid Karume kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mkuu (Rais) wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.
Kwa hiyo, kwa kuwa Rais Nyerere alikuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano, ibara hiyo ya 4 ya Mkataba (kwa kutumia Katiba ya Tanganyika ambayo pia ilikuwa Katiba ya Muungano kama ilivyorekebishwa, hadi hapo Katiba ya Muungano itakapopatikana), ilimpa pia uwezo wa kuitawala Jamhuri ya Muungano (kama Rais) na uwezo pia wa kuitawala Jamhuri ya Tanganyika kama Rais pia kwa wakati mmoja.
Na kwa kutumia Katiba hiyo hiyo ya Tanganyika, kama ilivyorekebishwa, Bunge la Jamhuri ya Muungano lilifanywa pia kuwa Bunge la Muungano kuweza kutunga Sheria kwa mambo yote ya Muungano, na pia kutunga Sheria kwa ajili ya mambo ya Tanganyika.
Matakwa hayo chini ya Mkataba wa Muungano, na pia ibara ya 49 ya Katiba ya Muda ya 1964 yalisomeka ifuatavyo: Legislative power with respect to all Union matters in and for the United Republic and with respect to all other matters in and for Tanganyika is vested in the Parliament.
Kwa Zanzibar vivyo hivyo, mamlaka hayo ya kutunga Sheria yalikuwa kwa Bunge la Zanzibar. Ibara hiyo ya 54 (2) ya Katiba ilisema: Legislative power with respect to all matters in and for Zanzibar other than Union matters is vested in the Legislature for Zanzibar.
Katika kuitawala Jamhuri ya Tanganyika, Rais alitakiwa kutumia “Sheria za Tanganyika zilizopo” kwa mambo yote yasiyo ya Muungano. Na vivyo hivyo, ibara ya 3 (a) ya Mkataba, ilimpa mamlaka Rais wa Zanzibar kuitawala nchi hiyo kwa kutumia “Sheria za Zanzibar zilizopo” kwa mambo yote yasiyo ya Muungano.
Kwa mantiki hiyo, na kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, kulikuwa na Serikali tatu – Serikali ya Muungano kwa ajili ya mambo kumi na moja (ibara ya 6), Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar ambazo zingetawaliwa kwa kutumia Sheria zake ndani ya mipaka yake, Sheria ambazo hazikufa kufuatia Muungano. Neno “Sheria zilizopo” (existing laws), limetafsiriwa chini ya kifungu cha 2 na 8 cha Sheria ya Muungano kumaanisha:
“Sheria zilizoandikwa na zisizoandikwa kama zilivyokuwa mara tu kabla ya Muungano (ikiwa ni pamoja na Sheria iliyotungwa na kupitishwa siku hiyo au kabla, na kuanza kutumika baada ya siku hiyo), lakini haijumuishi Katiba ya Tanganyika kama nchi kamili (yenye mipaka yake) kwa mambo yanayohusu (yasiyo ya Muungano) Jamhuri ya Tanganyika kama nchi nje ya Jamhuri ya Muungano”.
Kufikia hapo, hebu tutue kidogo kuona na kutafakari ya hapo juu. Kwa kifupi ni kwamba: Kwanza, Marais wa Tanganyika na Zanzibar waliingia Mkataba wa Kimataifa wa kuunganisha nchi zao kwa mamlaka waliyokuwa nayo ya kufanya hivyo kwa kuzingatia misingi na mfumo wa Sheria za Uingereza unaotumika katika nchi hizo.
Pili, jina sahihi la Muungano huu, kwa mujibu wa Mkataba huo, ni “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar”, na si Tanzania. Wala majina kama vile “Tanzania Bara” na “Tanzania Zanzibar” au Tanzania, hayana msingi wa kisheria kuweza kutumika tunapozungumzia “Jamhuri ya Muungano; ni majina ya kisiasa zaidi yasiyokuwa na nguvu ya kisheria kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, japo yameingizwa kinyemela katika Katiba.
Tatu, Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuunda Jamhuri moja [sovereign Republic], kushughulikia mambo 11 ya kimuungano niliyoyataja hapo juu; na Tanganyika na Zanzibar (kama nchi), zikaachwa kusimamia mambo yote mengine yasiyo ya Muungano kwa kutumia Sheria zake zilizokuwepo, ikiwamo Katiba ya Tanganyika kwa Tanganyika, na Amri za Rais [Decrees] kwa Zanzibar ambayo haikuwa na Katiba.
Tafsiri hii haikuwa na utata hata kidogo tangu mwanzo kama inavyothibitishwa na ibara ya 13 ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1964 na ile ya 1965 juu ya Wasaidizi Wakuu (Makamu) wa Rais wa Jamhuri ya Muungano; inasema:
“There shall be two Vice – Presidents of the United Republic (who shall be styled the First Vice – President and the Second Vice – President respectively), one whom shall be the principal assistant of the President in the discharge of his executive functions in relation to Zanzibar, and the other shall be principal assistant of the President in relation to Tanganyika and the leader of Government business in the National Assembly”.
Kwamba “kutakuwa na Makamu wa Rais wawili wa Jamhuri ya Muungano…..mmoja atakuwa Msaidizi Mkuu wa Rais Visiwani Zanzibar, na mwingine atakuwa Msaidizi Mkuu wa Rais kwa upande wa Tanganyika ambaye pia atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni”.
Ibara ya 20 ya Katiba hiyo ilimpa Rais mamlaka ya kuteua Mkuu wa Mkoa kwa kila Mkoa ndani ya Tanganyika; wakati ibara ya 25 ilitamka kuwa “Tanganyika itagawanywa katika majimbo mengi ya uchaguzi kadri ya idadi ya watu….”
Lakini kwa mambo ya Muungano, Katiba hiyo ilitumia “neno” Tanzania kama vile katika ibara ya 27 kuhusu sifa ya kugombea ubunge, ibara ya 64, kuhusu tafsiri ya Katiba, ibara ya 80 kuhusu mambo ya majeshi ya Ulinzi, na kadhalika.
Kuendelea kutajwa kwa “Tanganyika” katika Katiba hii kwenye Katiba zote za 1964 na 1965 baada ya Muungano, kunathibitisha kwamba Tanganyika haikuuawa na Muungano huo. Lakini tujiulize, Tanganyika ilikufaje kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano?
Nne, kwamba, kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa haijapata Katiba yake, na ilitarajiwa kupata ndani ya miezi 12 tangu siku ya Muungano, ilikubaliwa kuwa Katiba ya Tanganyika irekebishwe na kutumika kama Katiba ya Muda kama pia Katiba ya Muungano kwa mambo 11 ya Muungano. Kwa sababu hiyo, Rais Nyerere aliitawala Serikali ya Muungano kwa njia ya marekebisho hayo ya Katiba, na aliitawala pia Tanganyika kwa kutumia Katiba ya Tanganyika kwa mambo yasiyo ya Muungano.
Sheria ya Muungano, Namba 22 ya 1964, kifungu cha 5 (2), ilimpa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuifanyia marekebisho Katiba ya Tanganyika kuingiza (si kuongeza, ambapo kufanya hivyo ni kinyume cha Mkataba) mambo ya Muungano kwa njia ya Amri (Decrees) za Rais.
Kwa mtazamo huo, ni dhahiri kwamba, Tanganyika na Zanzibar ni nchi zinazopaswa kujiongoza kwa kutumia Sheria zake (ikiwamo Katiba), bila kuingilia au kuathiri mambo yale 11 ya Muungano.
Zanzibar ina Katiba yake nje ya Muungano; na ndiyo iliyofanyiwa marekebisho kufuatia kuundwa kwa Serikali ya Kitaifa Visiwani hivi karibuni. Baadhi ya vifungu vya Katiba vilivyorekebishwa ambavyo vinatuhumiwa kukiuka matakwa ya Muungano ni pamoja na ibara ya 3 kuhusu hadhi ya Zanzibar katika Muungano. Zamani ilisomeka: Zanzibar ni Sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sasa inasomeka: Zanzibar ni nchi ambayo eneo lake la mipaka ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vinavyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano na Tanganyika ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ya 1997 kwa upande wake (tofauti na Katiba za 1964 na 1965), ibara ya 2 (1) inatamka kuwa: Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana.
Marekebisho haya, bila ya shaka yoyote yanaipa Zanzibar hadhi ya Nchi yenye mipaka yake iliyokuwapo kabla ya Muungano. Ibara ya 4 ya marekebisho hayo ndiyo inayoweka nafasi na uhusiano wa Zanzibar (kama nchi) na Jamhuri ya Muungano, inasema: Zanzibar (kama nchi) ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ibara hii haisemi wazi kuhusu Nchi hiyo ya pili (Tanganyika?) ni ipi, maana Zanzibar iliungana na Tanganyika (isiyotajwa katika Katiba zote) na haikuungana na Tanzania Bara inayotajwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kifungu kingine kilichofanyiwa marekebisho kwenye Katiba ya Zanzibar ni ibara ya 2 (2) ambayo zamani ilimpa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar, ya kuigawa Zanzibar katika Majimbo na Wilaya, na pia uwezo wa kuteua Wakuu wa Mikoa.
Lakini kufuatia mabadiliko hayo (chini ya ibara mpya ya 2A), Rais wa Jamhuri ya Muungano amepokonywa mamlaka hayo na sasa mamlaka yote ni ya Rais wa Zanzibar kwa kufuata Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi”.
Kama tutakavyoona baadaye, haya ni mawili tu kati ya marekebisho mengi ya Katiba ya Zanzibar dhidi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Hata kwa hayo mawili tu niliyotaja, na kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, msingi na matakwa ya Muungano umetikiswa au kukiukwa vipi?
……….Itaendelea toleo lijalo.
 
Back
Top Bottom