Umejaribu kujenga hoja yako bila kufikiri inavyotakiwa.
Kwanza cheti sio mwisho wa matatizo! Hata wanaohitimu elimu za darasani wanajua kupata cheti sio tiketi ya ajira au utaalamu wa hali ya juu.
Cheti cha ndoa na cha kitaaluma havijatofautiana malengo! Vyote vina kazi moja tu; kuwatambulisha wahusika kwenye jamii kwamba wao ni wataalam/wanandoa ili kupata haki stahiki kutokana na hadhi zao.
Cheti cha ndoa kinakutambulisha kwamba wewe ni mme/mke wa fulani, hii inasaidia kupata haki zako hata za kiaheria pindi unaona kuna mtu anakuchukulia mme/mke wako, sawa na kwenye taaluma, cheti ndicho kinahalalisha ujuzi ulio nao wakati unatafuta ajira! Bila cheti hata uwe mtaalamu vipi huwezi kupata ajira kwenye taasisi inayoamini kwenye elimu ya darasani/taaluma/vyeti.
Kwa utangulizi huo naamini umeelewa cheti ni nini na nini kazi yake. Kuhusu hoja ya kupewa cheti kama ufaulu kabla ya mtihani, nimeelezea kwenye hapo chini.
Kabla ya ndoa kuna hatua ambazo wahusika wanapitia kabla ya kuhalalishwa kama wanandoa kwa kupewa vyeti kama ilivyoelezwa kwenye mada.
Hatua kubwa inayojulikana ila haileweki vyema ni uchumba. Hatua hiyo ndio mtihani wenyewe, ukiona unapewa cheti basi maana yake ulishinda kwenye hatua hizo kwa kuvuka vikwazo vyote, hata hivyo kiuhalisia ni wengi sana wanaopewa vyeti bila kuruka vikwazo vilivyopo kwenye uchumba, na kwa kuwa sio kazi ya mchungaji, sheikh au padri kuchunguza mahusiano yenu, wao hawana sababu ya kutokukupa cheti, maana ndoa yako ni yako, wao haiwahusu.
Nimesema hapo juu kwamba, uchumba ni hatua kubwa isiyoeleweka kwa sababu, watu wengi hawajui madhumuni yake au wanapuuza, ndio maana tunashuhudia ndoa nyingi zikiwa zinaenda kombo kwa kuwa wahusika waliruka ngazi ya kwanza hadi ya tatu bila kukanyaga ya pili.
Uchumba upo kwa dhumuni la kuchunguzana tu kujua ikiwa fulani anafaa kuwa mke/mme au hafai. Katika uchumba huo ndipo unapopimwa uvumilivu, upendo, heshima na adabu, mapenzi ya dhati, ukarimu nk. Kwa siku za sasa maana ya uchumba imepindishwa! Watu wanafikiri uchumba ni kushiriki ngono kitu ambacho si cha kweli na hakitakiwi kwenye hatua ya uchumba.
Hivi unawezaje kujua ikiwa mme/mke wako wako ataweza kustahimili vishawishi vya mwili(ngono) ukiwa upo mbali naye labda masomoni nje ya nchi au hata shughuli za kazi/biashara ikiwa wakati wa uchumba umekuwa ukishiriki naye kwenue ngono?
Utawezaje kujua mke wako atakuwa mvumilivu pale utakapopungukiwa pesa au kufilisika ikiwa katika uchumba wenu umekuwa ukimpa pesa anapokuomba au hata pale asipokuomba?
Nimalizie kwa kusema hivi; uchumba ndio darasa lenyewe ambapo nadharia zote za mapenzi ndipo zinapokuwa. Umakini wako kwenye hatua hiyo(uchumba) ndio unaamua ndoa yako iwe vipi sio cheti. Ukikosea uchumba utakuwa umekosea ndoa/kuoa pia kwa sababu mitihani inayoitwa ya ndoa kimsingi inaonekana wazi kwa wale wanaojua uchumba nini, na ndio maana kwa wakristo inasemwa kwamba, ikiwa unaona hamuendani mkiwa kwenye uchumba ni bora kuvunja uchumba mapema ili kuepuka matatizo kwa sababu ndoa ya kikristo haivunjwi popote pale.