Maafa ya kutisha

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
headline_bullet.jpg
Watu watano wafa kwa kufukiwa na kifusi
headline_bullet.jpg
Wananchi waua sita, mmoja kwa kuchinjwa
headline_bullet.jpg
Nyumba nne zatiwa kiberiti, familia zaokolewa



Matei%2813%29.jpg

Kamanda wa Polisi Mkoani wa Arusha, Basilio Matei.



Jumla ya watu 11 wamekufa katika matukio tofauti, watano kwa kufukiwa na kifusi, sita kwa kuuawa kikatili akiwamo kikongwe mmoja aliyechinjwa na wauaji kukimbia na kichwa huku wakitelekeza kiwiliwili chake vichakani.
Matukio hayo mabaya yametikisa mikoa ya Arusha, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam, ambayo yameshuhudia mwendelezo wa wananchi kujichukuliwa sheria mkononi kwa kuua watu sita katika majanga hayo.
Wilayani Arumeru mkoani Arusha, watu watano wamekufa baada ya kufukiwa na kifusi kwenye machimbo yaliyopo kijiji cha Kisongo.
Kamanda wa Polisi Mkoani wa Arusha, Basilio Matei, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi zaidi unaendelea.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Loserian Sabaya Mollel, alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni na kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa waliokufa, walikwenda kwenye machimbo hayo kwa lengo la kuiba kifusi.
Mollel alisema uchimbaji wa kifusi katika eneo hilo ulipigwa marufu, kutokana hatari inayotokana na uharibifu wa mazingira.
Alisema watu hao walikwenda katika machimbo hayo kwa kutumia gari lenye namba T 301 ACX lililokuwa linaendeshwa na Nicholus Dickson.
Waliokufa katika tukio hilo walijulikana kuwa ni Mzee Mashikieli, Sifaeli Boaz, Loituu Sambiti, Eliphas Lomayani na Elibariki Isaac, wote wakiwa ni wakazi wa kijiji hicho.
Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Mollel alisema kutokana na kupigwa marufuku kufanya uchimbaji wa kifusi katika eneo hilo kwa muda mrefu sasa, kuna utaratibu wa ulinzi, lakini bado watu wasiokuwa waaminifu wanafanikiwa kufanya uhalifu kwa kuiba kifusi.
Alisema wizi huo unatokea nyakati za usiku kwa vile ulinzi uliopo katika eneo hilo unafanyika mchana tu.
Afisa Mtendaji huyo alisema machimbo hayo, yamekuwa yakitumika tangu mwaka 1947.
Alisema kifusi kilichopo katika eneo hilo kina ubora wa hali ya juu na kutoa mfano kuwa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), kilijengwa kwa mchanga uliopatikana hapo.
Alisema uchimbaji uliofanyika kwa miaka mingi sasa, umesababisha uharibifu wa mazingira na kuporomoka kwa udongo wake.
Kwa mujibu wa Mollel, mtu mmoja alikufa katika machimbo hayo mwaka 2002, lakini hakujulikana kwa jina ama chanzo kilichosababisha kifo hicho.

DC atoa kauli
Akizungumzia kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Silla, aliwataka viongozi wa kijiji hicho kuhakikisha eneo hilo linakuwa chini ya ulinzi ili kudhibiti wizi wa kifusi.
“Lazima shughuli zote za machimbo zisimame ili kuokoa maisha ya watu, msimike mabango yenye kutoa tahadhari na kukataza uchimbaji, kisha muweke uzio kwani machimbo hayo yapo karibu sana na barabara,” alisema.
Alisema mbali na wizi unaofanyika, ukosefu wa uzio unaweza kusababisha hatari zaidi hasa kwa huduma za kijamii zinazopatikana ama kuwepo karibu na kijiji hicho.
Silla alisema serikali mkoani hapa, imesikitishwa na tukio hilo, pia alituma salamu za rambirambi kwa familia zilizowapoteza watu hao.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, dereva la gari lililowapeleka watu hao machimboni, anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

Mwanza: Watatu wauawa kwa kuchomwa moto
Mkoani Mwanza, watatu wameuawa kwa kuchomwa moto katika kijiji cha Nyansalala, kata ya Bukondo, wilayani Geita kutokana na tuhuma za ujambazi.
Waliouawa wanadaiwa kuwa walivamia wafanyabiashara na kuwajeruhi kisha kuwapora fedha na simu.
Kamanda wa Polisi, Mkoani Mwanza, Simon Sirro, akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana aliwataja waliouawa kuwa ni Malugu Kuboja (38), mkazi wa kijiji cha Luhuha, tarafa ya Butundwe; Didas Zacharia wa Muganza wilayani Chato na mwingine ambaye alikuwa hajatambuliwa.
Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuwavamia wafanyabiashara wa kijijini hapo na kuwajeruhi kwa mapanga kisha kupora fedha na simu za mkononi zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. 1,535,000.
Aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Sadiki Jumanne (33) na mkewe Catherine Jonathan, Nicholaus Masagati (45) na Samuel Lunyaba (75).
Alisema majambazi mengine matatu yalifanikiwa kutoroka na jeshi hilo bado linafanya msako mkali kwa kuwashirikisha wananchi ili kuwatia nguvuni.

Nyumba nne zachomwa moto
Katika tukio jingine lililotokea kwenye mji mdogo wa Katoro, nyumba za watu wanne ziliteketezwa kwa moto kwa tuhuma za kuhusika katika uporaji wa kutumia nguvu.
Nyumba hizo ni za watu wanne ambao walinusurika kuuawa baada ya kuokolewa na sungusungu.
Diwani wa eneo hilo, Maimuna Mingis, aliwataja watuhumiwa ambao nyumba zao zimechomwa moto kuwa ni Dominico Jackson, Suibona Inkama na wengine wawili waliojulikana kwa jina moja moja la Emma na Japhet.

Mbeya: Kikongwe achinjwa, wakimbia na kichwa
Mkoani Mbeya, watu wawili wameuawa, akiwemo kikongwe ambaye alikatwa kichwa na wauaji hao kutokomea nacho kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema jana kuwa tukio la kuuawa kwa kikongwe huyo lilitokea Mei 27, mwaka huu katika kijiji cha Kelalo, wilayani Rungwe.
Alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Alice Kosia (70), mkazi wa Kijiji cha Igembe, kata ya Lufingo, wilayani humo.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Nyombi alisema ilikuwa usiku wa kuamkia Mei 27, mwaka huu, kikongwe huyo akitokea kwenye klabu cha pombe alipokutana na wauaji hao.
Alisema kiwiliwili cha marehemu kiliokotwa kesho yake, saa 8:30 mchana kikiwa kimefichwa kando ya barabara.
Kamanda Nyombi alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kabla ya kuuawa, marehemu alikuwa na ugomvi wa mashamba na ndugu zake.
Kamanda Nyombi alisema hadi sasa ndugu sita wa marehemu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Wananchi waua mmoja
Wakati huo huo mwanaume mmoja asiyefahamika, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 25 na 30, ameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za wizi.
Kamanda Nyombi alisema tukio hilo lilitokea saa 8:30 usiku wa kuamkia jana katika eneo la Isesye, Jijini Mbeya.
Alisema marehemu kabla ya kuuawa anadaiwa kuwa alivunja mlango wa nyumba ya Edward Sanga (30) kwa nia ya kuiba.

Dar: Wananchi waua mmoja Mbagala
Jijini Dar es Salaam mtu mmoja anayedaiwa kuwa mwizi, alipigwa na wananchi hadi kufa katika eneo la karibu na Shule ya Sekondari Kilamba, Mbagala Rangi Tatu.
Mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jila moja la Gozila, alikutwa na mauti hayo jana alfajiri, baada ya kupigwa kwa mawe, akidaiwa kuiba seti ya runinga na simu ya mkononi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, alipoulizwa na Nipashe kuhusu tukio hilo, alisema bado halijawasilishwa ofisini kwake.
Habari hii imeandikwa na Woinde Shizza, Arusha; Renatus Masuguliko, Geita; Emmanuel Lengwa, Mbeya na Mashaka Mgeta, Dar es Salaam.





CHANZO: NIPASHE
 
Halafu tunaambiwa Bongo tambarare!!
Yaani hapa Bongo polisi ni jina tu ni afadhali hii kazi wapewe walinzi wa kwenye jumuiya "sungusungu".
Wanainchi wamechoshwa ndio maana wanachukua sheria mikononi
 
Tulipokuwa shule enzi hizo tulifundishwa katika somo la uraia kuwa moja kati ya majukumu ya serikali ni kuhakikisha usalama wa raia wake kwa kuwalinda wao na mali zao; hiyo ikiwa ni moja ya matumizi ya kodi wanazolipa. Sasa tunapofika mahala wananchi na mali zao hawahakikishiwi usalama na serikali iliyopo madarakani suluhisho lake ni nini? Leo kwa kuchoka wananchi wanajichukulia sheria mikononi na kuwaua wale wanawadhania ni wahalifu na sasa hasira zao zimehamia hata kuvichoma moto vituo vya polisi!! Je tutashangaa wananchi baadae wakichukua silaha dhidi ya vyombo vya dola?
 
Back
Top Bottom