Lowassa; Goli la kichwa, apiga Tiktaka kwa madoido

Lowassa; Goli la kichwa, apiga Tiktaka kwa madoido

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Joined
Dec 26, 2012
Posts
1,016
Reaction score
2,195
Too much cinnamon is harmful. Huu ni msemo wa Kiingereza, ukiwa na maana kwamba hata mdalasini ikitumiwa kupita kiasi una athari kwa afya. Mdalasini ni kiungo katika chakula, sifa zake zenye faida kiafya ni nyingi sana lakini matumizi yake ni kwa kiasi.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa, nyuma ya kufeli kwa jaribio lake la kuteuliwa kuwa mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu 2015, kuna matokeo ya msemo huu. Nyongeza kubwa ya vionjo na mikogo ni sababu ya kuenguliwa, japo yeye anaona ameonewa.

Lowassa alisifiwa kuwa ni mwenye kasi ya kiwango cha juu kwenye kukimbia, matokeo yake alikimbiza upepo mpaka akapitiliza kwao. Alipambwa kwamba ndiye mwenye sifa zote za kupeperusha bendera ya CCM katika mbio za Urais, akakoleza mbwembwe mpaka akavuka mahitaji ya chama. Hakukumbuka kuwa "mtaka nyingi nasaba hupata mwingi msiba."

Alisahau msemo wa Kiingereza "Leave well alone! You won't improve matters by going on tinkering", kwamba kiache kizuri kijioneshe, huwezi kukiongezea thamani kwa nakshi na mapambio. Ndege, helikopta, mabasi, msululu wa magari pamoja na mamia ya wapambe kila alipokwenda, zilikuwa mbwembwe tu lakini hazikuwa na mantiki kwenye kuongeza ujazo wa sifa za Lowassa kuteuliwa.

Pengine Kamati ya Maadili ya CCM ilikuwa na sababu tofauti na zile nizifikiriazo wakati wa kumkata Lowassa, maana hazijatamkwa! Wala siamini kama hoja pekee iliyotumika ni ile kashfa ya Richmond, sidhani! Ila kwa macho ya kawaida tu, mbio za Lowassa katika kile alichokiita Safari ya Matumaini, zilijaa vitimbi na vioja, vyenye dhihaka ya hali ya juu kwa chama.

Zipo nyakati niliogopa, maana ni kama vile Lowassa alikuwa amekizidi nguvu chama. Ilidhihirika bila shaka kuwa alikuwa anakilazimisha chama kione hakina ujanja wa kumuengua. Ilikuwa anakionesha chama wazi kwamba yeye ndiye chaguo la wananchi, na kutompitisha yeye kungesababisha chama kupasuka, nchi kuyumba. Unajua CCM ndiyo chama tawala, hakiwezi kuvurugika pasipo kusababisha athari ya kisiasa kwa nchi!

Ni picha wazi kuwa Lowassa alijua mapema kuwa upo uwezekano mkubwa wa kukatwa. Kabla, zilishakuwepo taarifa za Lowassa kuenguliwa kisha kuhama chama. Pamoja na yote hayo, aliamua kujaribu bahati yake. Hivyo, michezo mingi ya maonesho ambayo aliifanya wakati wa mchakato wa kuwania uteuzi, ililenga kujenga picha ya hofu kwa viongozi wa CCM, kusudi wamwache autawale mchezo mpaka Ikulu.

CCM ndiyo chama tawala, vilevile ni kikubwa, chenye ubavu wa kushinda Urais bila shaka. Kwa maana hiyo, kwa maonesho ambayo Lowassa aliyafanya, kama angevuka salama kisha kuteuliwa kuwa mgombea Urais, ilikuwa anaandika dira mpya, kwa hiyo yeyote ajaye, ataanza kujipanga kwanza kifedha kabla ya chochote kile.

Mbwembwe nyingi tu na matumizi makubwa ya fedha kuliko washindani wengine, hiyo ndiyo ingekuwa dira. Bila kujalisha zinapatikana vipi hizo fedha, atapitishwa tu. Ni uwezo wa kununua wajumbe, na kutekeleza anasa nyingi za kushtua taifa kisha chama kione wewe ndiye kiboko yao.

Tungefika mahali watu wenye fedha chafu, yaani mafisadi wanaopiga fedha serikalini, wauza madawa ya kulevya, watakatisha fedha haramu, majambazi wa mabenki, wafilisi mali za umma na wengineo, wangefanya vikao vyao na kupanga Rais wao atakayeweza kurahisisha kazi zao na kulinda usalama wao katika kipindi cha utawala wake.

Hayo si ajabu kutokea kama tu fedha ingeruhusiwa kuwa kielelezo cha kuteuliwa kuwa mgombea Urais 2015. Na kwa eneo hili, CCM kwa mara ya kwanza, imefanya jambo la heshima sana kuwaengua wote waliofanya matumizi makubwa ya fedha kuielekea tiketi ya kuwa mgombea Urais. Ni Dk. John Pombe Magufuli, aliyefanikiwa kupewa tiketi ya kupeperusha bendera ya chama hicho na wengine wachache ndiyo hawakufanya ghasia za matumizi ya fedha, ila wengi wao kila mmoja alijikuna alipofikia.

Siyo uongo kwamba Lowassa hajakubali kushindwa. Na anasubiriwa kuamua chochote ambacho kwa jinsi minong'ono ilivyokithiri, ni wazi hakitashtua tena. Yaani atafanya kinachosemwa sana. Pengine asipofanya chochote ndipo kutakuwa na mshangao wenye kuambatana alama ya kuuliza ni kwa nini ameamua kutulia?

Hilo likisubiriwa, ni vizuri sasa kumkumbusha mambo kadhaa ambayo kwa namna moja au nyingine yalimvurugia mwenyewe. Kutangaza nia, kuchukua fomu, kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini na hata kurejesha fomu, alifanya madoido mengi yaliyoharibu. Alitenda mithili ya mcheza mpira mpenda sifa, katika mchezo wa fainali, ilipotimu dakika ya 89 alipiga chenga wachezaji wote mpaka golikipa lakini badala ya kufunga akaanza kucheza danadana.

Mara ainue mpira na kuutuliza kifuani, akaushusha chini na kuupandisha juu kwa kichwa, mwisho mabeki wa timu pinzani wakaokoa. Dakika ya 90 mpira ukiwa langoni kwa mchezaji mpenda sifa, akapewa pasi, badala ya kuokoa, akaanza danadana zake, mara kichwani, mara kifuani, mwisho mpira ukagusa mkono, refa akaweka penalti, goli na mpira ukaisha. Lowassa alishika mpira golini kwake kwa mbwembwe zake, ikapigwa penalti, akafungwa!

Kwanza; Unaweza kujiuliza ni nini kilikuwemo ndani ya ubongo wa Lowassa mpaka kushindwa kuheshimu mamlaka za chama. Yanayokatazwa aliyafanya bila uoga. Hakuogopa sheria za uchaguzi. Hakuona aibu kutumia mtindo wa kitajiri, kuomba ridhaa ya maskini.

Pili; Matumizi makubwa ya fedha yalimtisha kila aliyeshuhudia. CCM ingempitisha kuwa mgombea Urais, ingekuwa sawa na kuruhusu aina mpya ya kusaka uongozi kwa kiburi cha fedha.

Tatu; Pengine kwa msemo wake "huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono", alikuwa na maana ya mbali zaidi, kwani alicheza rafu za wazi kwa kiburi kuwa hakuna mwenye kuweza kumzuia.

Nne; Badala ya kuwa na timu ya washauri, yeye aliunda kundi kubwa la wapambe, matokeo yake pale alipohitaji kushauriwa au kukosolewa, alishangiliwa, hivyo kumfanya avimbe kichwa. Alipewa matumaini hakuna wa kukata jina. Naye akapaza sauti "hakuna mwenye ubavu wa kukata jina langu." Kweli ni safari ya matumaini!

Tano; Angejua mapema angejitenga na matamshi mabaya yaliyokuwa yanazungumzwa na kikosi chake cha Team Lowassa au Friends of Lowassa. Mengi yalimharibia kwa kumchonganisha na wagombea wenzake pamoja na mamlaka za chama badala ya kumsaidia.

Mathalan, yalisemwa maneno kuwa Rais Kikwete hana ubavu wa kumzuia kuwa Rais kwa sababu hata Rais Benjamin Mkapa hakumtaka JK, vilevile Mkapa hakuwa chaguo la Rais Ali Hassa Mwinyi, lakini hakuna aliyezuia. Hizi sauti zilikuwa na kelele nyingi na kwa hakika, zilitosha kumshtua mkuu wa nchi na kujipanga kukabiliana na upinzani. Hili ni kosa kubwa la kiufundi kwa upande wa Lowassa na kambi yake.

Hapa kwenye kambi ndipo palipotia shaka kubwa. Kwanza alizungukwa na watu ambao uadilifu wake ulitia shaka hasa. Pamoja na yote hayo, bado kukawa na hali ya kujiaminisha, ikiwemo kumtunishia msuli Rais Jakaya Kikwete, pasipo kuzingatia ukweli kuwa huyo ndiye Mwenyekiti wa CCM, yaani kwa lugha rahisi ndiye mwenye chama (Chama Tawala), vilevile ndiye Amiri Jeshi Mkuu.

Huyohuyo ndiye unataka akuachie uongozi kidemokrasia, wakati huohuo unamfanyia vitimbi, huku ukimuonesha waziwazi kuwa siku ukiwa madarakani, kuna uwezekano ukamfanya ajute kuzaliwa Tanzania, vinginevyo akimbie nchi. Sijui kama JK alitumia ‘undava' kumkata Lowassa kutokana na hofu hiyo, ila kwa heshima na usalama wa mkuu wa nchi anayemaliza muda wake, Mr. Monduli alistahili kukatwa!

Wanasema "ukichezea tope litakurukia", Lowassa limemrukia na kumchafulia joho lake jeupe. Hakika yupo kwenye maumivu makubwa sana pengine kuliko yoyote yale kuwahi kumtokea kwenye maisha yake. Huwezi kuwa unanyoosha nguo, halafu unashika pasi katika upande wa kunyooshea, si utakuwa unataka kuona kama inaunguza? Pasi ya CCM imemuunguza Lowassa, imemuunguza sana!

Lowassa angeweza kuwa mnyenyekevu kwa chama na kwa viongozi waliopo mdarakani, pengine hata matokeo yaliyotokea yasingekuwa na maumivu makali kama yanavyomtesa kwa sasa. Kilichojiri Dodoma angekichukulia kama sehemu ya mchezo. Majina yalikuwa 42, mara 38 waliorudisha fomu, nafasi iliyowaniwa ni moja tu, kwa unyenyekevu angesema haikuwa raziki.

Ameumia hasa, ndiyo maana mpaka leo hajatoa tamko japo la kumpongeza Magufuli kwa kuteuliwa. Wenzake wote walishafanya hivyo kwa nyakati mbalimbali. Hata Bernard Membe ambaye naye alivimba kichwa kuwa ni mteule wa ‘bwana mkubwa', alikubali yaishe na kutoa pongezi zake. Kwa Lowassa imeshindikana, yupo kimya anatunga sheria, pengine alishatunga, anasubiri muda tu ili afunguke.

Kelele za kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, zimekuwa na maelezo yenye kutafsiri ukimya wa Lowassa, kwamba hajakubali matokeo ya mchezo ndani ya chama. Mzee kila baada ya muda anatoa matamko ya kulaani Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na mchakato mzima wa kumpata mgombea Urais wa CCM kuwa haukuwa wa kidemokrasia.

Kingunge, anatetea kuwa Lowassa siyo fisadi kwa sababu kashfa ya Richmond alisingiziwa. Anachoamini Lowassa hakukatwa kwa sababu nyingine zaidi ya skendo ya kampuni hiyo ya kufua umeme na wizara ya nishati na madini, kipindi akiwa waziri mkuu. Zile kufuru za kifedha hakuziona wala washirika wabaya waliopo nyuma yake.

Mbaya zaidi, hoja ya Kingunge imekaa kibinafsi sana kwa sababu lawama zake kwa Kamati ya Maadili kuwa ilijitwalia mamlaka ya Kamati Kuu, ni kwa sababu tu Lowassa alikatwa. Hazungumzii wengine ambao nao walienguliwa kwa sababu za kiusalama wa chama na nchi kwa jumla. Ni Lowassa tu, kwa nini Lowassa akatwe?
Shida kubwa inayoonekana hapa ni kuwa Lowassa na timu yake waliingia kwenye kinyang'anyiro kwa mapambano ya kufa au kupona. Ndiyo maana kitendo cha kuondolewa jina lake, kimechukuliwa na kambi yake kuwa ni mpango wa kumuua kisiasa.

Tatizo siyo kuanguka, hoja ni wapi umeangukia. Kuna kuanguka na kujikung'uta vumbi kisha safari inaendela lakini kuna kuanguka kunakomaanisha kifo. Lowassa lazima akiri kuwa kuna makosa mengi yamefanyika ndani yake na watu wake wenyewe. Pengine anaweza kukiri na kuangalia nini anaweza kufanya kwa sasa kuendelea kulinda heshima yake.

Zaidi, Lowassa alikuwa na nafasi nzuri ya kufunga goli, mpira ulikuwa rahisi sana kuusukumiza wavuni kwa kichwa chepesi tu lakini kwa madoido akataka kupiga tiktaka, badala ya kufunga, akafungwa yeye. Mchezo wenyewe ilikuwa gombania goli, uwezo wa mchezaji kufunga, goli moja, kipa mmoja.

Imeandikwa na Luqman Maloto


(Makala haya yametoka kwenye Gazeti la Raia Mwema)
 
11692582_10207219414544370_4095211305826421859_n.jpg
 
kweli huna kazi ya kufanya mimi kusoma makala yako tu nimetumia dakika 20 wewe ulieandika je? tafuta kazi ya kufanya acha majungu hao washafanya yao nawe fanya yako
 
Ww nae kama mganga wa jadi, huna tofauti, UNATAFSIRI HALI BAADA YA KUTOKEA... acha ujinga..

Subiria sasa, aende ukawa ndio mtaliona joto...
 
Ni kweli kabisa, LOW HASA alivimba kichwa na kujiona yeye ni zaidi ya chama, haya sasa na aende huko anakotaka kwenda ili chama kibaki salama!
 
Back
Top Bottom