Lowassa, Dk. Slaa, tusipotoshe ukweli

Lowassa, Dk. Slaa, tusipotoshe ukweli

Privatus Karugendo

MSEMA kweli ni mpenzi wa Mungu. Hivyo tunapojikuta kwenye wakati mgumu kama taifa, tunapoanza kuchanganyikiwa na kupotea njia, ni lazima tukumbuke kwamba ukweli utatuweka huru. Tusipotoshe ukweli na kuwapotosha watu. Edward Lowassa, anataka madaraka kwa gharama yoyote ile, anataka kuwa Rais wa Tanzania kwa njia yoyote ile.

Amekatwa kwenye chama chake, CCM, akakimbilia Chadema - Ukawa. Hakuwa mpenzi wa Ukawa na wala hakuwa mtetezi wa Ukawa, alikuwa mwiba wa upinzani. Amekumbatia Ukawa kama njia ya kupita kutimiza kiu yake ya kutaka kuwa Rais. Huu ndiyo ukweli, tuukubali na tusiupotoshe. Dk. Slaa, anaeleza sababu zake za kutomuunga mkono Lowassa kushika nafasi ya urais wa Tanzania. Si chuki binafsi na wala si kwa vile yeye hakupata nafasi ya kugombea nafasi hii, alisema juzi, jana na leo anasema hivyo na kesho atasema hivyo, kwamba Lowassa hana maadili ya uongozi. Huu ndio ukweli, tuukubali na tusiupotoshe.

Wanaosema Dk. Slaa, ni mtakatifu wamesema wenyewe, yeye hajasema hivyo. Na wala hoja yake si utakatifu na wenye dhambi. Hoja yake ni uadilifu wa uongozi katika taifa letu. Hoja yake ni mtu kusema ukweli ukausimamia, hoja yake ni mtu kusimamia rasilimali za taifa letu. Kuwatumikia watu, kudumisha amani na usawa katika taifa letu. Kuondoa umasikini na kuleta maendeleo.

Tumemsikia Dk. Slaa, kwa makini Mtu aliye makini ni lazima alielewa maelezo yake. Ingawa ilishangaza kabisa kwamba baada ya mahojiano yake na waandishi wa habari, waandishi wote waliouliza maswali, walionyesha kutoelewa. Tunajiuliza kama huo ndio uelewa wa waandishi wetu wa Tanzania, au waandishi hao walikuwa wamepangwa kwa malengo maalumu? Huko nyuma Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa, alisema waandishi wa Tanzania si makini, wakalalama kwamba aliwatukana! Huo ndo ukweli tusiupotoshe!

Kama waandishi hao walipangwa, basi ni upotoshaji na hizi ni dalili za kudidimiza uandishi wa habari hapa Tanzania. Waandishi watanunuliwa na kuelekezwa ya kuandika. Hii ni hatari kubwa. Lazima kupiga vita utamaduni huu kwa nguvu zote. Kama waandishi, ambao tunaamini ni wasomi, hawawezi kusikiliza na kuelewa, itakuwa vipi kwa watu wa kawaida kule vijijini? Mwandishi ambaye hakuelewa yale aliyoyasikia, ataandika nini na atawaelimisha wananchi wa vijijini na wale wanaosoma magazeti.

Dk Slaa, alimshambulia Lowassa kwa mwenendo wake juu ya maadili ya uongozi, juu ya ufisadi na tabia yake ya uongo juu ya mambo ya kuliongoza taifa letu. Hakusema chochote kuhusu maisha ya ndoa ya Lowassa na wala juu ya maisha binafsi ya Lowassa. Tunaamini Dk, Slaa kwa kiasi fulani anayafahamu maisha binafsi ya Lowassa, lakini kwa vile hoja ya msingi si maisha binafsi, yeye hakugusia jambo hili.

Sasa tumeanza kusikia upotoshaji juu ya maisha ya Dk. Slaa. Juu ya ndoa yake na maisha yake ya ukasisi. Huku ni kupotosha hoja kwa malengo fulani. Suala la msingi si maisha ya familia ya Dk Slaa. Suala la msingi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na Dk Slaa katika hoja yake aliweka wazi jambo hili na kulitetea kwa mifano na nyaraka. Hatuongelei familia na maisha ya ndoa, hatuongelei uaminifu katika ndoa, bali ni uongozi wa taifa na uaminifu juu ya rasilimali za taifa, maana kufuatana na Katiba yetu ya sasa Rais, ana mamlaka makubwa sana. Anaweza kuamua mambo mengi au ya kuliponya taifa au ya kuliangamiza. Ni muhimu tukafahamu ni mtu aina gani anataka kutuongoza. Si kuiongoza familia yake, bali kuliongoza taifa. Si kuwa mwaminifu kwa mke wake, bali kuwa mwaminifu kwa Katiba na taifa zima la Tanzania.

Maisha ya Dk. Slaa, kwenye ukasisi Maisha yake kwenye ndoa zake mbili, hayana uhusiano wa moja kwa moja na uongozi wa taifa letu au kazi yake aliyoifanya kwenye ubunge na kwenye wadhifa wa Katibu Mkuu wa Chadema. Katiba yetu, haisemi kwamba Rais awe ameoa, awe mwaminifu kwa mke wake. Haya ni maadili mazuri ambayo kila mtu ni muhimu awe nayo, lakini si masharti ya kumzuia mtu kuwa kiongozi wa taifa letu.

Dk. Slaa aliungama wazi kushiriki hatua za mwanzo za kumshawishi Lowassa kuingia Ukawa, lakini aliweka masharti ambayo si lazima sana kuyarudia kwenye makala hii. Tuliambiwa kwamba masharti hayo hayakufuatwa. Na Lowassa, akakaribishwa kujiunga na Ukawa- Chadema, bila masharti hayo kufuatwa. Hivyo wale wote wanaotetea jambo hili, tunawataka walieleze hili na wala si kukimbila kwenye maisha binafsi ya Dk. Slaa.

Tunamheshimu sana Freeman Mbowe, na sote tunafahamu juhudi zake za kukijenga chama chake, Chadema. Sote tumeshuhudia kwamba wakati wa uongozi wake chama hiki kimepiga hatua na kushika nafasi ya chama kikuu cha upinzani bungeni. Hii ni hatua kubwa na hakuna wa kuipuuza. Busara na hekima ambazo amekuwa akionyesha siku za nyuma, tulitarajia kuziona wakati huu. Hata kama ameamua kumkumbatia Lowassa, kwa dalili zake za kukipaisha chama na labda kuishika dola, tulitaraji atende haki kwa Dk. Slaa. Tunashangaa kuona hata yeye anakubali upotoshwaji unaofanywa dhidi ya Dk. Slaa. Kama kuna mtu anafahamu vizuri kabisa kwamba Dk. Slaa, hanunuliki ni Mbowe. Tunataka tusikie haya kutoka kwake na wala si hizi porojo za kununuliwa na maisha binafsi ya Dk. Slaa.

Ni wazi jinsi Chadema, inavyoendelea sasa hivi, jinsi watu wanavyovutiwa na kampeni zao, na umati mkubwa wa watu unaojitokeza kwenye mikutano yao, wanaelekea kukamata dola, hivyo wasingependa mtu kuingilia katikati na kubomoa nguvu zenye kuleta matumaini kwa upande wao. Ila wakumbuke kwamba, bila kulenga yale yale, kwa nia ya kuiondoa CCM na kuleta mabadiliko, wengine wakilenga kupata madaraka na kufurahia kuwamo madarakani, hakuna jipya litakalotokea. Si leo, na wala si kesho wakati ukifika. Mabadiliko, yanahitaji sadaka, mabadiliko yanahitaji kujitoa na kukubali kuto kukubaliana.

Tunamheshimu sana James Mbatia. Watanzania wengi wamejenga imani juu yake. Tunaamini ni mtu anayelipenda taifa letu. Hivyo hatukutarajia naye katika suala hili la Dk. Slaa na Lowassa, awe na ushabiki. Anaweza kuwa na matumaini kwa Lowassa, na hasa matumaini ya kushika dola, lakini amtendee haki Dk. Slaa.

Suala la ndoa ya Dk. Slaa na maisha yake binafsi vinajitokeza kwa nguvu, kana kwamba tunaongelea maisha ya ndoa. Kujitokeza kwa mke wake wa zamani kwenye vyombo vya habari ni jambo ambalo limetuletea mashaka. Kwa nini ajitokeze leo hii wakati wameachana na Dk. Slaa, miaka mingi ya nyuma?

Tunaamini, pale Dk. Slaa, aliposema familia yake ilikuwa inashindia mihogo, alikuwa akimaanisha familia yake na mke wake wa pili, Josephine Mushumbusi. Alisema hayo, baada ya kuelezea kwamba mke wake huyo alikuwa akitumia mshahara wake kuzunguka nchi nzima akijenga umoja wa wanawake wa Chadema. Kwa vile alitumia mshahara wake, yeye na watoto walishindia mihogo. Hakumaanisha mke wake wa kwanza ambaye amejitokeza kwenye vyombo vya habari.

Lengo ni kupotosha hoja za Dk Slaa, ambazo ni nzito na ni muhimu kwa kila Mtanzania kuzitafakari. Kama Chadema, walimshutumu Lowassa kuwa fisadi, amejisafisha kwa sabuni gani leo hii? Na je Chadema, wataendeleza vita yao kupinga ufisadi? Watanzania wanataka mabadiliko, je mabadiliko haya yanaletwa na wale wale, wenye mawazo yale yale na mfumo ule ule? Inawezekana CCM, wakatumia hoja ya Dk. Slaa, kujijenga. Si lazima Dk. Slaa, kuwa amelenga huko. Lakini wakiweza, maana ni mpaka mtu msafi, mtu mwenye maadili ya uongozi kusimama, bila kuogopa kusemwa au kukumbushwa ubovu wake, akatumia hoja ya Dk. Slaa kuisaidia CCM.

Wengi wanaamini Dk. Magufuli, ana ubavu wa kusimama na kuzungumza bila kuogopa. Labda huyu anaweza kuibeba hoja ya Dk. Slaa. Hili likitokea, Chadema wajilaumu wenyewe na wala wasimnyoshee kidole Dk. Slaa. Jambo la msingi hapa ni kukubali ukweli kwa yale yaliyotokea kati ya Lowassa na Dk. Slaa.Tusipotoshe ukweli. Tukubali ukweli utuweke huru.

Chanzo:
Raia Mwema

Kalugendo nae ni mpotoshaji tu wala kweli haiko pamoja nae,unapokuwa na watu halafu wakajiona wana akili kuliko wengine,na eti kwamba waandishi waliouliza maswali hawakumuelewa Dr.SLAA,hapo nadhani kalugendo anatudanganya mchana kweupe,hv Kalugendo hajui kwamba Dr.Slaa aliamini hakuna mwingine zaid yake.
 
Huyu PKarugendo ni mganga njaa wa ccm tusitegemee jipya anatumia taaluma yake ili mkono uende kinywani ila ukweli kwa sasa hatuangalii nani kafanya nini!Hata CCM huko ndo kumeoza wala rushwa wote ni CCM je Magufuli ni muadilifu??atwambie kama ni muadilifu.
 
Mtu mhalifu anatakiwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria ili haki ipatikane huko.
CDM ndio waliotuambia kuwa EL ni fisadi na wakadai ushahidi wanao. Imekuwaje tena waseme sasa kuwa sio fisadi??? Inawezekana kabisa EL sio fisadi ila cdm walimsingizia na kama ndio hivyo inawezekana pia hakuna ufisadi kwenye EPA, ESCROW, MEREMETA, NET GROUP NK bali ni hao hao chadema wametaka kuzusha ili serikali ionekane haifanyi kazi vyema!
Je kama CDM wanaweza kuzusha yote hayo iweje tuwaamini tuwape nchi???
Je wanataka nchi ili wafanye nini wakati wao walikuwa na ajenda ya ufisadi ambao kwa namna wanavyomtetea EL na kwa namna ''walivyomzushia'', TZ hakuna ufisadi!

wazungu wanasema MIND GAME mshatolewa mchezoni hapo ni magoli tu hahahahhhhhaaaaaa

hapo kwenye epa na ecsrow tayar mahakama ishasibitisha au hujui kama yona na mramba wapo jela vp tibaijuka na chenge si wapo ktk kamat za maadili za ccm wanahojiwa kuna nn tena inamaana wezi wanajulikana vp richmond mbona haisongi fungua akili
 
Hata Yesu alipokuja duniani hakueleweka kabisa mpaka alipokufa na kufufuka ndipo watu wakamuelewa. Kwa sasa ukweli huu hautaeleweka mpaka baada ya october 25.
 
Kwa sababu ni wao ndio waliokuwa vinara wakutuambia Lowassa ni wakufungwa ina maana pia wanatakiwa kuwa na ushaidi pia.

Hivi kesho wakiibuka na kutuambia escrow aina makosa na hakuna ushahidi utawaelewa kweli si ni wao ndio walivalia njuga na kufanya kila mtu aamini kuna watu walienda na mikokoteni kuchota hela; leo tena mara tu iwapo wahusika waliokuwa wakiwashutumu wakiamia CDM waanze kubadilisha kauli na kutaka serikari ithibitishe uoni kama ni watu wasio na principles already on what they stand for.

Tatizo sio watu kufungwa tatizo ni kuwa na kanuni usizoziamini uoni kama ao watu ni waongo tu, hivi ni nani Tanzania apewe credit kwenye kuambia umma Lowassa afai? na nani leo anataka serikari ndio ithibitishe kile kile walichokuwa wanadai wanao ushahidi wote kuhusu Lowassa.

ila na ww esrow ambayo wahisani wanagomea kutoa fedha zao ila sisi wa tz bana hiyo dili inajulikana hadi ng'ambo
 
Usipotoshe ukweli, Slaa hakumtafuta Lowasa. Yeye alitapewa Taarifa za ujio wa Lowasa ndo akaanza kuhoji anakuja kama asset au liability? Chadema ilimpuuza, na kumdhihaki kuwa yet ni abiria wa treni, si dreva wala mmilki wa train. Kwamba mmilki wa train yupo, dreva yupo, wanahiari kumpakia abiria yeyote. Kama cdm wakweli wakanushe ada ya uanachama kiasi billion 10, walicholipwa!

Kwa masikio yetu na kwa midomo na sauti ya Dr Slaa mshenga alimfuata yeye na yeye ndio alimpigia mwenyekiti nani kamtafuta hapo Dr Slaa mnafiki mzandiki muongo ndio maana hakuweza kusimama kukabiliana na miimbara ya hekalu la Mungu mwache akafilie huko marekani maana treni la ukombozi limemuacha katikati ya misitu maagizo yake yamekwama fedha za serikali ya Tanzania kupitia TISS zitamhukumu mpaka siku ya kifo chake
 
ila na ww esrow ambayo wahisani wanagomea kutoa fedha zao ila sisi wa tz bana hiyo dili inajulikana hadi ng'ambo
Hata Rich-Monduli ilipata sifa hizo hizo pia ilipojitokeza na watu wakajiuzulu kwa uwajibaki.

Hakuna tofauti hapa kutoka kwa accuser ambao ni CDM waliokuwa wakidai wana ushahidi tosha Lowassa afai, leo tena imekuwaje afadhali hata hao CCM walidai jamaa ana makando makando na utajiri usioleweka vyanzo vyake halisi. Lakini unaposema unao ushahidi wa uhusika wake kama CDM walivyokuwa wakidai miaka yote halafu tena uje kivingine ina maana wewe ni muongo tu na inapotokea mnamgeuka yule aliyekuwa kinara wa kupambana na ufisadi kwa ajili ya kupokea fisadi halafu uite hiyo ndio njia ya mageuzi na watu wakaamini kama jamii lazima tutakuwa na matatizo.

Kwanza walisema ata watu wa CCM awafai kumbe nyuma ya pazia walikuwa wanajipanga kuwapokea inataka uwe 'ndumi la kuwili' kweli kama wao ili uweze support hizi movement za kilaghai.

Kuna guarantee gani watatimiza ahadi zao za baadae wakati mpaka sasa wametuthibitishia sio watu wa kusimamia maneno yao, kusema uongo ndio misingi ya kumwamini mtu kweli.
 
CCM ni chama chenye "mfumo wa kifisadi" na ndio kimezalisha mafisadi. Sioni kama JMP anaweza kung'oa mfumo huo. Ukawa nao "wameleta fisadi" kuwa mgombea wao wa uraisi. Ni vigumu kuamini kwamba amebadilika. Kwa katiba yetu EL akishinda kuna mfumo wa kuweza kumdhibiti UKAWA/CDM kama ikibidi? KIPI hatari zaidi mfumo wa CCM au kuongozwa na EL kwa katiba hii?
 
Kilichomharibia aliyekua katibu mkuu wa cdm ni ile nguvu na msaada uliokua nyuma ya huo mpango wake wa kujitoa na maneno aliyoyasema kwenye ile press na waandishi wa habari. Hicho kimemharibia na kumshushia heshima sana yeye pamoja na wote waliokua nyuma ya huo mpango.

kuna watu wengine ni wa ajabu sana! jambo jema ni lile linalowapa faraja wao tu linalowakosoa hawapendi kusikia wala kuliona,cha ajabu hao hao kila siku wamekuwa wakiongea mabaya ya CCM , kina zitto ila kuongea mabaya ya Mbowe,UKAWA hapana sasa nyie ni watu wa anaina gani? mmekuwa malaika hata hamkosei!!!
 
Chadema imeshakubali kuwa ilijenga hoja za uongo dhidi ya Lowasa alipokuwa CCM. Kimsingi, kama Lowasa alikuwa anasingiziwa, CCM je? Haiwezekani, kwa mtu anayetumia kichwa kufikiria, haiwezekani kuamini kuwa Lowasa alikuwa anasingiziwa bali CCM ilikuwa haisingiziwi.... Yaani kwamba Sumaye alikuwa msafi, ila CCM ni chafu, kwamba Lowasa alikuwa msafi, CCM ni chafu. Ni uhuni.

Mkisema Lowasa ametubu alipokuja Chadema, ametubu dhambi gani? Hayo mamlaka ya kusamehe dhambi Chadema wameyatoa wapi? Mwenye akili hawezi kuendelea kulishabikia genge hili lililobadirika tu baada ya kunusa harufu ya ikulu - Sasa tumejua Chadema ni nini!

Unapoteza pumzi bure Mkuu, uelewa wa hawa watu ni aidha mdogo au ni ule wa watu waliojitoa ufahamu.
 
Hata Rich-Monduli ilipata sifa hizo hizo pia ilipojitokeza na watu wakajiuzulu kwa uwajibaki.

Hakuna tofauti hapa kutoka kwa accuser ambao ni CDM waliokuwa wakidai wana ushahidi tosha Lowassa afai, leo tena imekuwaje afadhali hata hao CCM walidai jamaa ana makando makando na utajiri usioleweka vyanzo vyake halisi. Lakini unaposema unao ushahidi wa uhusika wake kama CDM walivyokuwa wakidai miaka yote halafu tena uje kivingine ina maana wewe ni muongo tu na inapotokea mnamgeuka yule aliyekuwa kinara wa kupambana na ufisadi kwa ajili ya kupokea fisadi halafu uite hiyo ndio njia ya mageuzi na watu wakaamini kama jamii lazima tutakuwa na matatizo.

Kwanza walisema ata watu wa CCM awafai kumbe nyuma ya pazia walikuwa wanajipanga kuwapokea inataka uwe 'ndumi la kuwili' kweli kama wao ili uweze support hizi movement za kilaghai.

Kuna guarantee gani watatimiza ahadi zao za baadae wakati mpaka sasa wametuthibitishia sio watu wa kusimamia maneno yao, kusema uongo ndio misingi ya kumwamini mtu kweli.

CHADEMA wanajua wafuasi wake hawajielewi na ni bendera fuata upepo kwa hyo wanafanya wanavyotaka hata sasa hivi wakiambiwa Alshabab sio kikund cha kigaidi watapita wakiimba hivyo sababu tuu Mbowe kasema.
 
CHADEMA wanajua wafuasi wake hawajielewi na ni bendera fuata upepo kwa hyo wanafanya wanavyotaka hata sasa hivi wakiambiwa Alshabab sio kikund cha kigaidi watapita wakiimba hivyo sababu tuu Mbowe kasema.
Kuna kila sababu ya kusema wataamini tu si watu wa kuchanganya na zao kabisa.
 
kuna watu wengine ni wa ajabu sana! jambo jema ni lile linalowapa faraja wao tu linalowakosoa hawapendi kusikia wala kuliona,cha ajabu hao hao kila siku wamekuwa wakiongea mabaya ya CCM , kina zitto ila kuongea mabaya ya Mbowe,UKAWA hapana sasa nyie ni watu wa anaina gani? mmekuwa malaika hata hamkosei!!!

Nafikiri kuna kitu haujakielewa vizuri kwenye bandiko langu, nmesema kukosoa na wala kutofautiana sioni shida, tatizo lipo waliokua nyuma ya mpango wa huyo Dr.
 
Back
Top Bottom