Dar es Salaam. Profesa Ibrahimu Lipumba amesema mgogoro uliopo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ukiachwa uendelee unaweza kuathiri jitihada za vyama vya upinzani kutetea mchakato wa wazi wa Katiba Mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),alisema wameanza kufanya jitihada za kukutana na viongozi wa juu wa Chadema na kuzungumza nao ili waweze kutafutia mgogoro huo ufumbuzi wa haraka.
"Umoja wetu ni kutaka mchakato wa katiba uwe wa wazi, sasa huu mgogoro wa Chadema unaweza kutukwamisha, na kwa kutambua hilo tayari tumeanza kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi ingawa hayakuwa mazungumzo rasmi lakini tupo kwenye jitihada hizo," alisema Profesa Lipumba.
Aliyazungumza hayo baada ya kuulizwa na waandishi wa habari alipokuwa akitangaza maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, ambapo alisisitiza kuwa hata hivyo wameshapanga kukutana ana kwa ana na viongozi wa Chadema kwa mazungumzo zaidi katika kuutatua mgogoro huo.
Alisema Baraza Kuu la CUF limetoa wito wa kuwepo kwa mkutano wa wadau hususan vyama vya siasa na asasi za kiraia kujadili rasmi ya mwisho ya katiba kwa lengo la kufikisha maridhiano ya mambo muhimu yaliyomo ndani ya katiba.
Profesa Lipumba alisema hatua hiyo inalenga katika kurahisisha kazi za Bunge la katiba kufikia mwafaka kuhusu vipengele muhimu vya Katiba Mpya.
Mgogoro wa Chadema unatokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya kusaliti chama.
Katika hatua nyingine Baraza Kuu la CUF limemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajiuzulu au Rais amfukuze kazi, wakidai kuwa anahusika na matokeo ya vitendo vya ukatili vilivyotokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili. "Baraza Kuu linamtaka Waziri Mkuu kuwajibika kutokana na matokeo ya operesheni hiyo."
Source: Gazeti la Mwananchi