LinkedIn, nafasi tosha ya kutunisha misuli ya IT

LinkedIn, nafasi tosha ya kutunisha misuli ya IT

Kilongwe

JF-Expert Member
Joined
Feb 7, 2008
Posts
423
Reaction score
116
linked_in_kwa_tanzania.png




Kipindi cha kiangazi (summer) kinapoingia, moja ya biashara zinazofaidika kwa sana ni ile ya vyumba vya kufanyia mazoezi (gym). Biashara hii huwavutia watu wengi kwa sababu muda huo,wake kwa waume hupendelea kwenda kujenga muonekano wa maumbo yao. Wanamume wanataka kujenga misuli huku wanawake wanataka kuondoa vitambi ili waweze kupendeza zaidi pindi wanapovaa nguo za kujinafasi.Ingawa lengo la wengi ni kujenga maumbo yenye kuvutia, ila wakati wa ujenzi huu, pia huwasaidia kujenga afya bora kutokana na mazoezi wanayoyafanya. Hivyo kama walenga walivyosema "kuua ndege wawili kwa jiwe moja".

Wafanya mazoezi hawa hushindwa kujizuia kuuliza pindi wanapokutana na wenzao waliofaulu (ama wenye misuli minene ama walio na maumbo mazuri yenye kuvutia), hupenda sana kujua siri za mafanikio yao.Ukiachana na hayo, hakuna kitu kinachokatisha tamaa ukiwa gym kama unapokuwa peke yako, kwani ukiwa peke yako hauna uwezo wa kujitathmini, hii ndio sababu wengi wetu hupenda kwenda gym na marafiki zetu ili kupata mtu ama wa kuoneshea utofauti ama kuwekea malengo ili nawe uwe kama yeye.

Katika vitu ambavyo huleta amasa kwa wafanya mazoezi ni pale unapokutana na mtu akakuambia, duh bwana Nyoni umejazia mkono ile mbaya, pia huleta changamoto sana pale mtu anapokuambia jamaa umezajia juu kinoma ila una miguu kama njiti. Unaposikia haya, kesho yake ukienda gym, basi utafanya mazoezi ya kukuza miguu. Hii ndiyo hulka ya binadamu na siri ya Gym.

Katika ulimwengu wetu wa IT, moja ya vitu muhimu kuliko vyote ni kukua kifani. Hii inamaanisha, kila siku ni siku ya mazoezi kwako kujenga misuli yako ya IT, haijalishi unataka kujijenga katika eneo gani ndani ya IT, mazoezi ni kitu cha lazima. IT ama kwa lugha ya matani (Inayo Tiririka) ni moja ya fani ambazo inabadirika kila siku, yaaani IT inabadirika kila kukicha, hivyo pindi unapokubali kuwa mwana IT basi ni lazima ukubali kujifunza na kujitathmini.
Katika Kujifunza na kujitathmini, ni dhahiri kuwa unahitaji kujumuika na watu mbalimbali, kwani kijifunza ni kupata maarifa mapya ambayo ama tulikuwa hauyajui ama haujayashika balabala. Kujitathmini, ni kitendo ya kujiangalia wewe mwenyewe unaonekanaje kwa watu wengine? Utakapofanikiwa kwenye haya mambo mawili, basi utafanikiwa kwenye IT. Na kama utaona kuwa wewe tayari umeshafika unapotakiwa kufika, basi jua kifo chako kwenye fani kipo karibu.Swali linakuja, je utajifunza na kujitathmini vipi?

Uzuri wa IT ni uwezo wake wa kujiendeleza yao yenyewe na kujikamilisha kwake, yaani ndani ya hiyo IT, kila kitu kipo ndani yake. Utajifunza na utajittathmini. Kuna njia nyingi sana za kujifunza na kujitathmini, ama kwa njia ya mitihani, ama kwenda kwenye semina, workshop nk. Ila kuna njia moja ambayo ipo mikononi mwetu. nayo si nyingine bali ni kwa kutumia mitandao jamii. Ndio, kama jina lake linavyojieleza, mi mitandao ya wanajamii, na sisi tunajifunza toka kwa wanajamii. Mitandao hii ipo mingi sana, kuanzia Facebook, Twitter, LinkedIn nk. Ila kila mtandao umeanzisha kwa lengo lake mahsusi. Kwa mfano, Facebook ni kwa ajili ya mahusiano ya kirafiki, ule wa Twitter ni kwa ajili ya kusasisha (update) juu ya maono, maisha nk na huu wa LinkedIn ni kwa ajili ya kifani (professionalism) zaidi. Hivyo leo hii tutazama hapa kwenye LinkedIn.

LinkedIn-Logo.jpg



LinkedIn kama ilivyo mitandao mingine ya kijamii, inakuwezesha kutengeneza mtandao wa wanajamii kulingana na matakwa yako. Ndani ya mtandao huu sio tu utaweza kuungana na wale mulisosoma wote, muliofanya kazi wote, muliofanya biashara wote bali pia hata wali mulio katika idara moja au kuhusiana kwa mtindo fulani. Pia inakuwezesha kutanua wigo kwa kupata marafiki wa marafiki na kuweza kuwa marafiki zako.Ingawa wengi wetu wamekuwa wakitumia LinkedIn, lakini wengi bado wakiwa hawajajua umuhimu wa hii LinkedIn. Kuna wengine bado wanafikiria LinkedIn ni Facebook nyingine hivyo hakuna haja ya kuwa huko. Ukweli ni kuwa, LinkedIn ina ufanano na Facebook ikiwa ni mitandao jamii bali ina utofauti mkubwa sana na Facebook. Utofauti huu upo kwenye nyanja nyingi, ila nitagusia chache.

Aina za watu:Watu wengi wanaotumia LinkedIn hujali taarifa na matendo yao ndani ya LinkedIn, mfumo wa mtandao huu huwakimbiza wengi wanaokuja kwa sababu zisizo na mashiko hivyo siku ya mwisho, wengi (SIO WOTE) wa watumiaji katika LinkedIn huwa ni walio makini na kuthamini taarifa zao humo huku wakijua lengo lao la kuwa humo. Tofautio na Facebook ambapo wengi hufuata mkumbo huku wakiwa na akaunti nyingi zinazotumia majina bandia, picha bandia nk.

Taarifa:Kwenye Facebook kama nilivyoeleza ni mtandao wa urafiki wa mahusiano, iwe kwa wanafamilia, iwe kwa wapenzi ama wanafunzi, hivyo taarifa nyingi zilizo kwenye Facebook ni zile za aina hizo, ingawa Facebook inaweza kutumiwa vyema kama chombo cha kuelimisha jamii, biashara nk ila wengi wa watumiaji (haswa kutoka Tanzania) kwa wao Facebook ni sehemu ya kupotezea muda, majungu na kupashana. Hivyo, kwa watu wa aina hii Linked kamwe sio kwao kwani taarifa hizi, kule hazihitajiki. Siku ya mwisho watu kama hawa wataishia tu kuwa na Profile halafu wakapotea (watoto wa mjini wanasema wakasepa).

Gharama:
Facebook ni mtandao ambao huduma zote ni bure ukiondoa zile za viwango vya juu, ila akaunti zote ni bure. Kule kwenye LinkedIn, akaunti za kawaida n bure (kwa wengi, akaunti hii inatosha kabisa), ila kama unahitaji akauti za VIP ambapo utakuwa unapata huduma zaidi toka kwao basi inabidi kulipia. Hii inafanana na zile huduma za kulipia za facebook.

Baada ya kuangalia ufanano na utofauti, hebu sasa tujikite nini unaweza kufanya kwenye LinkedIn wewe kama mwana IT.Kupata muelekeo wa ajira.Mara nyingi nimekuwa nikiongea na vijana wanaomaliza vyuo vikuu, wengi hadi mwaka wa mwisho wamekuwa hawajui nini wanahitaji na wapi ni muelekeo wao, hili sio kwa Tanzania peke yake bali ni kwa nchi nyingi sana zinazoendelea. Mfumo wa Elimu kwenye nchi hizi nyingi umekaa kutomuandaa mwanafunzi kwenye fani husika. Hivyo kwa kutumia LinkedIn, sio tu utaweza kuelewa mielekeo (Career path) toka kwa watu wenye ufananao na wewe, bali pia utaweza kufahamu kwa undani mambo muhimu kwenye kila uelekeo.
skills.jpg

Kujijenga kwenye uelekeo husika.

Kama unataka kuwa na uwezo mzuri ndani ya IT, ni lazima uchague muelekeo na kujijenga huko, kwenye kila muelekeo unatakiwa uchague shemu moja ambayo unaona wewe unaiweza na unaishika. Uata uanakuja pale unapokuwa haujiamini ama kutojielewa ndani ya uelekeo wako. Kumbuka, kuna baadhi ya mielekeo inahitaji kufahamu idara nyingine zaidi na zaidi, kwa mfano ili uwe IT Auditor mzuri, ni lazima uwe umepitia idara nyingi sana za IT, sheria na hata zile za fedha.Je utaweza kujijua vipi kama umewiva au kwa sasa unafaa kwenda huko? LinkedIn inaweza kukusaidia kwenye hili kwa kuwauliza marafiki zao juu ya tathmini yao kwako. Kwa mfano, binafsi baada ya kumaliza degree ya pili ya mambo ya Uchumi wa IT na Utawala (IT Economics & Managaement) nilikuwa ninataka kujikita ndani zaidi kwenye sehemu moja, hivyo nilitaka kujua kutokana na kazi nilizofanya, tathmini ya watu je ni eneo gani linanifaa kwa kina? Nilitumia huduma moja ya LinkedIn inayoitwa endorsement ambapo marafiki zako wanaweza kukutathmini kwenye kila idara. Siku ya mwisho niliweza kufikia suluhisho la kuchagua wapi pa kujikita ndani zaidi na zaidi.


expert.jpg

Kujua hatua uliyofikia.
Kwa kutumia mtazamo wa marafiki, taarifa zako nk, LinkedIn inaweza kukutathmini na kujua hatua uliyofikia, ama unayeanza, expert nk. Kitu cha muhimu kuzingatia ni kuwa , hakikisha marafiki wanauku endorse ni wale tu wanaojua nini wanachokifanya na sio kwakuwa wewe ni rafiki zako. Kumbuka, tathmini hii haiwezi kuwa 100% kwani mara nyingi huathiriwa na uhusiano (friendship) pia uwezo kiufundi (Professionalism). Kwa mfano, chukulia mtu anakuendorse kwenye ITIL wakati hata hajui ni kitu gani, hivyo kuwa makini, usigubikwe na misifa isiyo na manufaa, ooh.

Ulinganishi.Mashindano ni moja ya njia nzuri za kujiendeleza kifani, akhsante LinkednIn, kuna hii feature ambayo inakuwezesha kujilinganisha na watu wengine ambao ama mupo kwenye kampuni moja, ama marafiki ama mulio kwenye fani moja. Hii itakuwezesha kuona ubora wako, mvuto kifani kulinganisha na wengine (kwani utaweza kuona uwiano wa utembelewaji wa kurasa yako kulinganisha na mwenzako).

Kuvutia waajiri.Siu hizi, waajiri wote (WALIO MAKINI) hutumia mitandao jamaiii kuangalia ubora (potential) ya muajiriwa. Moja ya mitandao ambayo ni chaguo la kwanza kuangalia fani ya mtu ni LinkedIn wakati facebook ni kwa ajili ya kuangalia matendo / tabia.Hivyo kumbuka, LinkedIn ni zaidi ya kuwa na kurasa, hakikisha unakuwa na kurasa iliyoshiba na yenye mvuto.

Kutanua Wigo.Kwakuwa kwenye LinkedIn unaweza kujenga mtandao wa marafiki kifani, hivyo itakuwezesha kuwa na wigo mpana wa kifani utakaokuwezesha kuwa na uwanja mpana zaidi. Kumbuka, tunaishi kwenye dunia ya utandawazi, hivyo usijikusanye sehemu moja. Jitawanye na jinfunze zaidi.

common.jpg

Elimu na Maarifa Chanya.
Kitu ambacho ninakipenda kwenye LinkedIn ni makala zenye mlengo chanya. Niliwahi kuwa mwanachama kwenye moja ya kundi la Facebook, kuna watu wengi sana kule. Ila binafsi nilijitoa kwakuwa ilifika wakati kila kitu kinachoongelewa kule ni chuki chuki chuki. Machache mno ya kujenga, yaani ni siasa zisizo na msaada kwa taifa letu masikini la Tanzania. Nikiwa kama wana IT wengine wengi ambao kwao maendeleo kwanza, ninapenda kusoma taarifa zenye kujenga na sio kubomoa. Huku LinkedIn, makundi mengi yamekaa kifani zaidi, hivyo kwa kujiunga kwako utaweza kupata makala mbalimbali zenye muelekeo chanya tena zenye uhusiano. Ukiachia makundi uliyojiunga, LinkedIn hutuma makala kulingana na muelekeo wa fani yako hivyo utajifunza zaidi.

Pata taarifa za kazi, semina nkLinkedIn ina hii feature inayokuwezesha kujiunga kwenye makundi, kampuni na vijikundi mbalimbali. Kwa kujiunga kwako, utaweza pokea taarifa muhimu zinazoendeleo humo, iwe za kazi, maarifa au nyinginezo.Ili kupunguza mlundikano wa taarifa, unashauri kujiunga kwenye makundi / kmapni chache uwezavyo.
Yapo mengi ila uzuri wa mambo ni machache yenye kueleweka, hivyo shime wana IT wa Tanzania, tutumie LinkedIn kujinoa pia tuepuke kuweka fanitusizozijua au kuipamba kurasa yako kwa vitu usivyoviweza kwani hii haikusaidii badala ya kukudidimiza. Tujenge utamaduni wa kujifunza na kuepuka kuchanganya IT na siasa chafu.
Kama hauna Linked In Jiunge kwa kutembelea Hapa.

Mkata Nyoni
Chief Business Development Office - Dudumizi
LinkedIn ID: Mkata Nyoni Facebook ID: nyonim
 
Back
Top Bottom