Lini utendaji wao ulikuwa juu!?

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,886
Utendaji Baraza la Mawaziri washuka
*Wananchi hawana imani na mawaziri

*Mikataba mibovu ya madini moja ya chanzo

*Utafiti waonyesha wananchi wana imani na JK

*Wakosa imani na Takukuru, Bunge, Mahakama, Polisi

Muhibu Said na Peter Edson
Mwananchi

IMANI ya wananchi kuhusiana na utendaji kazi wa serikali, Bunge na Mahakama imeporomoka huku ule wa Rais Jakaya Kikwete binafsi ukiwa si mbaya ukilinganisha na taasisi hizo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet) iliyo chini ya Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kiwango cha wananchi kuridhika sana na utendaji wa vyombo vikuu kama Baraza la Mawaziri na Bunge umepungua katika kipindi cha kati ya Oktoba mwaka jana na Oktoba mwaka huu, huku kiwango cha kutoridhika kikiongezeka mara dufu.

Katika utafiti huo, wananchi wameelezea sababu za kutoridhika na utendaji kazi wa taasisi hizo ni kuwa ni kushindwa kutofuatilia utekelezaji, kujihusisha na rushwa, kupitisha mikataba mibovu ya madini na kutokutoa mikopo au mitaji. Sababu nyingine ni kutopandisha mishahara ya wafanyakazi.

Taarifa hiyo ya Redet, inaonyesha kwamba kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa Bunge umepungua kutoka asilimia 39.2 mwaka 2006 hadi asilimia 21.8 mwaka 2007, huku kwa wananchi wasioridhika na utendaji kazi wa chombo hicho ukiongezeka kutoka 11.3 mwaka 2006 hadi asilimia 25 mwaka 2007.

Kwa upande wa Baraza la Mawaziri, kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa baraza hilo kimepungua kutoka asilimia 33.8 mwaka 2006 hadi asilimia 20.1 mwaka huu.

Katika kukosa imani ya utendaji kwa taasisi hizo, wananchi wameonyesha wasiwasi mkubwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (PCCB) ikiongoza kwa kuwa na asilimia ndogo zaidi ya utendaji kazi kati ya taasisi zote za serikali katika kipindi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mwenza wa Redet, Dk Laurean Ndumbaro, alisema utafiti huo ulifanywa Oktoba 22-28, mwaka huu, kwa kuendesha kura ya maoni kwa kuwahoji wananchi katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Visiwani.

Dk Ndumbaro alisema kulinganisha na kura ya maoni iliyofanyika Oktoba mwaka jana kutathmini mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Kikwete tangu aingie madarakani, asilimia ya waliohojiwa ambao wanasema wanaridhika sana na utendaji wake, imepungua kutoka asilimia 67.4 mwaka jana hadi asilimia 44.4 mwaka huu.

Alisema waliohojiwa, walitakiwa kutoa maoni yao iwapo wanaridhishwa au la ambapo asilimia 44.4 walisema kuwa wanaridhishwa sana wakati asilimia 35.0 walisema wanaridhika kiasi na asilimia 18.6 wakasema hawaridhiki na utendaji kazi wa Rais Kikwete.

Mbali na hilo, Dk Ndumbaro alisema pia idadi ya waliohojiwa na kusema hawaridhiki na utendaji kazi wa Rais Kikwete, imeongezeka maradufu kutoka asilimia 7.8 hadi asilimia 18.6 na kwamba, idadi ya waliohojiwa wanaosema wanaridhika kiasi, imeongezeka kutoka asilimia 23 ya mwaka jana hadi asilimia 35.

Alisema wale ambao walisema wanaridhika kiasi na wale ambao hawaridhiki, walitakiwa kueleza sababu za tathmini yao ambapo theluthi moja ya wahojiwa (sawa na asilimia 30.4), walisema Rais Kikwete ameshindwa kuboresha hali ya maisha wakati takriban asilimia 22, walisema hajatimiza ahadi na asilimia 11.6 walisema imetokana na kutofuatilia utekelezaji.

Dk Ndumbaro alisema sababu nyingine zilizotolewa na wahojiwa, ni Rais Kikwete kuteua viongozi wabovu (asilimia 9.1) na kushindwa kupambana na rushwa (asilimia 5.6).

Hata hivyo, alisema utafiti huo pia ulijaribu kutathmini kiwango cha imani ya wananchi kwa viongozi wao wa ngazi za juu na matokeo kuonyesha kwamba pamoja na Rais Kikwete kupata asilimia 44.4 ya wahojiwa waliosema wanaridhika sana na utendaji kazi wake, zaidi ya nusu ya wahojiwa (asilimia 56), walisema kwamba wana imani naye.

"Imani hii ya wananchi kwa Rais Jakaya Kikwete inajidhihirisha hata pale wahojiwa wanapoulizwa kutaja jina la mwanasiasa mashuhuri anayewafurahisha katika utendaji wake wa kazi," alisema Dk Ndumbaro.

Alisema katika swali hilo, pia Rais Kikwete anaongoza kwa kumzidi anayemfuatia ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kwa zaidi ya mara tatu.

Dk Ndumbaro alisema Rais Kikwete alitajwa na asilimia 32 akifuatiwa na Zitto aliyetajwa na asilimia 10 na Lowassa aliyetajwa na asilimia 5.8 ya wahojiwa wote na kwamba, wanasiasa wengine wametajwa kwa asilimia ndogo.

Alisema wahojiwa waliosema wanaridhika sana na utendaji kazi wa Baraza la Mawaziri, ni asilimia 20, huku Bunge likiwa na asilimia 21.8 na idadi ndogo pia kwa Jeshi la Polisi (asilimia 24), Mahakama (asilimia 21) na serikali za mitaa (asilimia 32.5).

"Maoni haya yanashabihiana na pale wahojiwa wanapoulizwa kutoa tathmini ya jumla ya utendaji kazi wa serikali nzima iliyopo madarakani. Asilimia 26.5 walisema wanaridhika sana, asilimia 39 walisema wanaridhika kiasi na asilimia 32 walisema hawaridhiki," alisema Dk Ndumbaro.

Alisema kati ya taasisi zote, PCCB inaongoza kwa kuwa na asilimia ndogo zaidi ya wahojiwa waliosema kwamba wanaridhika sana na utendaji wake wa kazi (asilimia 17), huku ikiwa na idadi kubwa ya wahojiwa waliosema hawaridhiki (asilimia 33).

Hata hivyo, Dk Ndumbaro alisema matokeo hayo yanaonyesha kwamba, wahojiwa wanaridhika zaidi na utendaji kazi wa Rais Kikwete kuliko wanavyoridhishwa na utendaji kazi wa serikali yake.

"Hii inajidhihirisha pale ambapo tunaona kwamba wakati asilimia 44 ya wahojiwa wote walisema wanaridhika sana na utendaji kazi wa Rais Kikwete, kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa serikali nzima ni asilimia 26.5 na asilimia 20 kwa Baraza la Mawaziri. Hii inaonyesha kwamba watu wengi wana imani na Rais Kikwete hata pale ambapo utendaji kazi wa baadhi ya taasisi zilizo ndani ya serikali yake haziwaridhishi sana," alisema Dk Ndumbaro.

Alisema tathmini ya utendaji kazi wa serikali nzima iliyopo madarakani, wahojiwa ambao walisema wanaridhika au hawaridhiki, walitakiwa watoe sababu za maoni yao ambapo baadhi ya sababu zilizotolewa ni pamoja na serikali kutofuatilia utekelezaji (asilimia 32.7), kujihusisha na rushwa (asilimia 24) na kupitisha mikataba mibovu ya madini (asilimia 10.9).

Dk Ndumbaro alisema kutokana na kuibuka kwa hoja mbalimbali kuhusu mikataba ya madini na maslahi yake kwa taifa, wahojiwa walitakiwa kutoa maoni yao kuhusu tathmini yao iwapo wanaridhika au la na namna serikali inavyosimamia rasilimali za nchi, hasa madini ambapo asilimia 15 ya wahojiwa wote ndio walisema wanaridihika sana wakati asilimia 16 walisema wanaridhika kiasi.

Hata hivyo, alisema karibu nusu ya wahojiwa wote (asilimia 48.4), walisema hawaridhiki kwa jinsi serikali inavyosimamia rasilimali za nchi, yakiwamo madini.

Alisema kulinganisha maoni ya wahojiwa ya Oktoba mwaka jana na yale ya Oktoba mwaka huu, utendaji kazi wa vyombo vikuu, kama Baraza la Mawaziri na Bunge, kiwango cha 'kuridhika sana', kimepungua, wakati kiwango cha kuridhika kiasi, kimeongezeka na kile kiwango cha wahojiwa wanaosema 'hawaridhiki' kimeongezeka maradufu.

Dk Ndumbaro alisema kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa Bunge, kimepungua kutoka asilimia 39.2 mwaka jana hadi asilimia 21.8 mwaka huu na kwamba, kile cha wasioridhika na utendaji kazi wa Bunge, kimeongezeka kutoka asilimia 11.3 mwaka jana hadi asilimia 25 mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Baraza la Mawaziri, kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa baraza hilo, kimepungua kutoka asilimia 33.8 mwaka jana hadi asilimia 20.1 mwaka huu ambapo kiwango cha wasioridhika, kimeongezeka kwa asilimia 10 katika kipindi hicho.

Dk Ndumbaro alisema upande wa utendaji kazi wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume, ni asilimia 35.5 ya wahojiwa wote wa Zanzibar ndio walisema wanaridhika sana, asilimia 30.6 wanaridhika kiasi na asilimia 31.5 walisema hawaridhiki.

Alisema walipoulizwa sababu za kuridhika kiasi au kutoridhika na utendaji kazi wa rais huyo, wahojiwa walitaja sababu mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuboresha hali ya maisha (asilimia 37.5), kutotimiza ahadi (asilimia 17.3), kutofuatilia utekelezaji (asilimia 11.7), kuteua viongozi wabovu (asilimia 10) na kushindwa kupambana na rushwa (asilimia 6).

Dk Ndumbaro alisema kulinganisha na matokeo hayo na yale ya utafiti wa Oktoba mwaka jana, idadi ya wahojiwa wanaosema wanaridhika sana na utendaji wa rais huyo, imepungua kutoka asilimia 47.8 Oktoba mwaka jana hadi asilimia 35.5 Oktoba mwaka huu.

Hata hivyo, alisema kuna takriban theluthi moja ya wahojiwa ambao wanasema hawaridhiki na utendaji kazi wa baraza la wawakilishi (asilimia 30.2) na serikali nzima ya SMZ (asilimia 31.9).

Kuhusu utendaji kazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, Dk Ndumbaro alisema wahojiwa waliulizwa kutoa tathmini yao na asilimia 40.7 walisema wanaridhika sana na utendaji kazi wa CCM ambapo wale waliosema wanaridhika kiasi ni asilimia 34.3 na asilimia 23.3 walisema hawaridhiki.

Alisema kwa upande wa vyama vya upinzani, tathmini ya wahojiwa ya utendaji kazi wa vyama hivyo, inaonyesha kuwa idadi kubwa ya wahojiwa hawaridhiki na utendaji wao (38.7) kulinganisha na wale wanaosema wanaridhika sana (19) au wanaridhika kiasi (30.3).

Dk Ndumbaro alisema wahojiwa waliulizwa sababu za kuridhika kiasi au kutoridhika na utendaji kazi wa CCM na kutaja kuwa hakitimizi ahadi (asilimia 19.6), viongozi wake ni wabovu (asilimia 10.8) na viongozi wake ni wala rushwa (10.1).

Alisema wahojiwa waliulizwa kutaja sababu za kuridhika kiasi au kutoridhika na utendaji kazi wa vyama vya upinzani na kutaja sababu mbalimbali, ikiwamo kuwa na migogoro (asilimia 15), kutokuwa na sera (8.6) na kutokuwa na uwezo wa kuongoza nchi (asilimia 8.4).

Dk Ndumbaro alisema kulinganisha matokeo hayo na yale ya Oktoba mwaka jana , idadi ya wahojiwa waliosema wanaridhika sana na utendaji kazi wa CCM, imepungua kutoka asilimia 60 Oktoba mwaka jana hadi asilimia 40.7 Oktoba mwaka huu na kwamba, idadi iliyoongezeka ni ya wale ambao wanasema wanaridhika kiasi (kutoka asilimia 25.5 hadi 34) na ya wale wanaosema hawaridhiki (asilimia 12 hadi 23).

"Ukiangalia kwa makini kwa upande wa upinzani, ingawa kuna idadi ndogo ya wahojiwa wanaosema wanaridhika sana na utendaji kazi wa vyama vya upinzani katika tafiti zote mbili, hata hivyo kuna mabadiliko ya maoni katika vipengele vingine. Idadi ya wale wanaosema wanaridhishwa kiasi imeongezeka kutoka asilimia 23 hapo Oktoba 2006 hadi asilimia 30 Oktoba mwaka huu. Pia asilimia ya wale ambao wanasema hawaridhiki na utendaji kazi wa vyama vya upinzani imepungua kutoka asilimia 51 hapo Oktoba 2006 hadi asilimia 38.7 Oktoba mwaka huu.

"Hata hivyo, ingawa kiwango cha kuridhika sana na utendaji kazi wa CCM umepungua kwa takriban asilimia 20, haimaanishi kwamba kiwango cha kuridhika sana na utendaji wa kazi wa vyama vya upinzani umeongezeka. Idadi ya wahojiwa wanaosema wanaridhika sana na utendaji kazi wa upinzani umeongezeka kwa asilimia 0.8 tu," alisema Dk Ndumbaro.

Alisema kati ya viongozi wote waliofanyiwa tathmini hiyo ya imani ya wananchi kwao, ni mawaziri ndio wanaopata kiwango cha chini cha wahojiwa wanaosema wana imani sana (asilimia 23.5) na kiwango cha juu cha wahojiwa wanaosema wana imani kiasi na mawaziri (aslimia 40.5) na kwamba, kiongozi anayeongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wahojiwa wanaosema hawana imani, ni mbunge ambapo asilimia 32 walisema hawana imani na mbunge wao.

Dk Ndumbaro alisema wahojiwa pia waliulizwa kuhusu imani yao kwa CCM na vyama vya upinzani na matokeo kuonyesha kwamba, wengi wao wanasema wana imani sana na chama hicho kwa asilimia 45 kuliko vyama hivyo (asilimia 14).

Alisema wale wanaosema hawana imani, ni wengi zaidi kwa upande wa vyama vya upinzani (asilimia 38 kuliko CCM (asilimia 17) na kwamba, wahojiwa wanaonekana kuwa na imani zaidi kwa Rais Kikwete (asilimia 56) kuliko CCM (asilimia 45) na hata kuliko viongozi wakuu wa serikai yake, akiwamo Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein (asilimia 46), Lowassa (asilimia 43) na wakuu wa mikoa (asilimia 36).

Dk Ndumbaro alisema wahojiwa waliulizwa kutaja tatizo moja kubwa ambalo wanaliona kama kero kwao ambalo linahitaji ufumbuzi na kuonyesha kuwa ni huduma mbaya za jamii, kama vile afya, elimu, maji, umeme na barabara ambalo lilitajwa na theluthi moja ya wahojiwa wote (asilimia 31) na kufuatiwa na kupanda kwa gharama za maisha (asilimia 28), ukosefu wa ajira (asilimia 7), rushwa (asilimia 6), viongozi walioko madarakani (asilimia 4) na mikataba mibovu/isiyo na maslahi kwa taifa (asilimia 3).

Alisema anatarajia kuwa matokeo hayo, yatatoa mwanga kwa viongozi wa serikali kuhusu uchapakazi wao pamoja na masuala ambayo wananchi wangependa yapewe kipaumbele.

Alisema maoni ya wote waliohojiwa, yalichangiwa kwa kiasi fulani na matukio makubwa yaliyojitokeza katika kipindi hicho.

Dk Ndumbaro alisema katika utafiti huo, sampuli nasibu ilitumika kuchagua wilaya moja katika mkoa na kwamba, jumla ya wahojiwa, ilikuwa ni 1,300, ikiwa ni wahojiwa 50 kutoka katika kila wilaya iliyochaguliwa.

"Lengo kuu la utafiti huu ni kuboresha shughuli za serikali kwa kuleta maendeleo kwa watu walio wengi na kuimarisha demokrasia nchini," alisema Dk Ndumbaro.

Akielezea mfumo wa ukusanyaji maoni, Dk Ndumbaro alisema utafiti huo ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. Sampuli ilichaguliwa kwa kutumia ngazi tatu ambazo ni wilaya, vijiji/mitaa na wahojiwa. Katika kila ngazi, sampuli ilipatikana kwa kutumia mtindo wa sampuli nasibu (random sampling method)

 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom