Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Sianzi na ashakumu, leo ninawatukana,
Mwaufanya uwazimu, na mambo yaso maana,
Huu si ubinadamu, pia sio uungwana,
Ben wetu yuko wapi?
Ben hakuwa mzimu, vipi asionekane?
Kama karuka sehemu, uhamiaji wanene,
Na kama ni marehemu, mwili wake tuuone,
Ben wetu yuko wapi?
Bavicha machakaramu, Katambi una laana,
Siku saba zishatimu, Desemba mwaka wa jana,
Nyumbu twataka fahamu, komeni kulaliana,
Ben wetu yuko wapi?
UTG zenu salamu, mlipo muitikie
Sina pesa hali ngumu, fulana siniuzie,
Lengo si kuwalaumu, ila nanyi mtwambie,
Ben wetu yuko wapi?
Serikali naheshimu, ila kwa hili hapana,
Mloona kwenye simu, sasa yawekwe bayana,
Tunataka kufahamu, naye walopigiana,
Ben wetu yuko wapi?
Mboe ni mtu muhimu, ana kubwa sana dhima,
Ela naye kala ndimu, hataki hata kusema,
Kiasi ni mtuhumu, ameufanya unyama,
Ben wetu yuko wapi?
Nimtaje Jeyi Pi Emu, tuliyempa dhamana,
Mjuwe namuheshimu, ela namna hakuna,
Nahisi anayo damu, ya huyu wetu kijana,
Ben wetu yuko wapi?
Kalamu naomba koma, miye sina roho mbili,
Siniletee nakama, nikenda fichwa mahali,
Kisha niwe madhuluma, athama ni hili swali,
Ben wetu yuko wapi?
Shairi langi lingine.
Ana mazonge mfalme
31 January 2017 Jumanne.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whats app 0622845394 Morogoro.