Hali si shwari kati ya CUF na Chadema, kutokana na vyama hivyo sasa kuamua kuoneshana ubabe hadharani.
Hatua hiyo inatishia usalama wa Watanzania kisiasa, kutokana na vitendo ambavyo vinadaiwa kufanywa au kusababishwa na wafuasi wa vyama vya siasa katika mikutano ya hadhara.
Na kama hali hii itaacha iendelee huku nchi ikielekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, kuna hatari ya wananchi kudhuriana na kufanya mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini kuonekana balaa kwa Taifa.
Baada ya vurugu kutokea katika mikutano ya Chadema chini ya Operesheni Sangara na kusababisha vifo vya watu wawili Morogoro na Iringa hivi karibuni, sasa kumezuka mtafaruku baina ya chama hicho na CUF.
Jana CUF iliituhumu Chadema na kuihadharisha, kuwa falsafa yake ya ‘ngangari' iliyokuwa ikiendeshwa dhidi ya Polisi inaweza kuhamishiwa dhidi ya Chadema na kusababisha ikose pa kukaa.
Tamko la CUF linatokana na kile ilichodai kwamba wafuasi wake walipondwa mawe na wale wa Chadema walipokuwa wakiendelea na shughuli za kutangaza mikutano inayoendelea mjini Arusha.
"CUF inatoa onyo kali kwa viongozi wa Chadema, kwamba hali hii ikiendelea, wajue hawataweza kufanya shughuli zao sehemu yoyote Tanzania, kwani uwezo wa kuwafanya tutakavyo tunao na kwa sababu wameanza tunaweza kumaliza," Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya alisema hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Taarifa hiyo iliendelea kumnukuu: "Ile ngangari kwa Polisi tunaweza kuwahamishia wao na wakose pa kukaa, ila hatupendi tufike huko na kama wana busara na ni wanasiasa kweli wenye nia ya kutumia hoja badala ya vurugu kumkomboa Mtanzania, watafakari hilo."
Kwa mujibu wa Kambaya, CUF inaona Chadema kama chama kisichoweza siasa za ustahimilivu, haijiamini na ni changa kisiasa. "Hii inadhirishwa na kutoelewa maana ya demokrasia na uhuru wa Mtanzania kuamua kujiunga na chama chochote atakacho.
"Bado hawajakomaa kisiasa kama CUF ilivyokomaa kisiasa hatudhuru chama chochote kinapofanya siasa maeneo yoyote hapa nchini," alisisitiza.
CUF inatuhumu viongozi wa Chadema Arusha kushawishi wafuasi wao kuwaponda mawe wafuasi wake wanaoendelea na mikutano ya kisiasa tangu mwanzoni mwa wiki hii.
Kambaya alimtuhumu Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema kwamba juzi akihutubia wafuasi wa chama chake kwenye viwanja vya stendi ya Nduruma alisema ‘CUF wametuvamia' na kuwasihi kwa usemi wa ‘kamata mwizi men' uanze kutekelezwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya CUF, vijana wao walipondwa mawe jana wakiwa mtaa wa Kilombero kata ya Levorosi. Inasema kutokana na vurugu hizo, gari la matangazo la CUF lilipondwa na mwanachama mmoja aliyetajwa kwa jina la Athumani Abdulrahman kujeruhiwa jicho na kwamba taarifa ziko Polisi.
Chama hicho kilisisitiza, kwamba kitaendelea na siasa Arusha hususan Operesheni Mchakamchaka na mikutano. "Kama wao ni wababe kweli na wanatumia hoja ya vurugu, waendelee na mipango yao ya hujuma na tutawafundisha siasa, kwani bado hawajakomaa," ilisisitiza taarifa ya Kambaya.
Gazeti hili lilimtafuta Lema ambaye alipata kuwa mbunge wa Arusha Mjini kabla ya Mahakama Kuu kubatilisha ubunge wake, kwa ajili ya kujibu shutuma za kushawishi vijana kuwafanyia vurugu wana CUF, lakini hakupatikana.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa alipotafutwa kujibu shutuma hizo za CUF dhidi ya chama chake, alisema yuko mkoani Mwanza hafahamu suala hilo. Alimtaka mwandishi kuwasiliana na viongozi wa chama walioko Arusha.
Aidha, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema hana taarifa ya suala hilo na akaomba apewe muda apate ukweli kabla ya kutoa majibu juu ya shutuma hizo za CUF.