La Lipumba na kitisho dhidi ya CUF

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Historia ya maisha yangu kisiasa si refu kulingana na umri wangu wa miaka 43. Pamoja nakuzaliwa kwenye mazingira ambayo siasa hupikwa, ikatiwa nazi na hatimaye kuliwa au kukorogewa sukari na kisha kunywewa, makuzi yangu kwa kiasi kikubwa hayakuwa kwenye jamii yangu ya asili, na ndio maana sehemu kubwa ya maisha yangu sikupata kushiriki au kufanya siasa za kwetu, Zanzibar.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba sina uweledi wa siasa za Zanzibar. Hapana. Siasa ni sayansi iruhusuyo mtu kuifahamu bila mipaka ya kijografia na ndio sababu ukawepo uwezekano wa mtu kuishi Afrika, lakini akaisasambura siasa ya Marekani hata kama haishi huko.

Nilianza rasmi kujihusisha na siasa mara baada ya kurejeshwa tena mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Uchaguzi wa kwanza wa mfumo huu mnamo mwaka 1995 ndio ulionipa fursa ya mimi kupiga kura kwa mara ya kwanza nikiwa katika ardhi ya Tanganyika niliko kulia na kuishi sehemu kubwa ya maisha yangu. Ukija kulinganisha na chaguzi zilizofuatia hapo baadaye, unaweza kusema kuwa uchaguzi huu haukuwa na msisimko mkubwa sana, kwani bado uligubikwa na koti la chama kimoja kwa upande wa Tanganyika. Hali hiyo ilikuwa tafauti kwa upande wa Zanzibar, ambako siasa haijawahi kuwapo doro tangu hata hivyo vyama vingi havijarejeshwa. Kwa Zanzibar, kila siku ni siku ya siasa, pawe na vyama vingi au kimoja, pawe na uchaguzi au usiwepo!

Na Ahmad Abu Faris
Na Ahmad Abu Faris
Kama nilivyosema, ni uchaguzi huu wa mwaka 1995 ambao ulinipa fursa ya kushiriki kumchagua niliyempenda na kumuamini kwamba alikuwa na uwezo wa kuiletea maendeleo nchi yangu. Ni uchaguzi huu ambao, kwa mara ya kwanza, ulitowa fursa kwa wengi wetu kuhisi tunachagua kutokana na kushirikisha wagombea wengi wenye umaarufu kielimu na kisiasa. Ni uchaguzi huu ambao uliondoa timbwa za watu kushiriki uchaguzi wa kuchagua baina ya mtu au ukuta kama tulivyoshuhudia za kabla ya hapo. Pamoja na ufinyu wa demokrasia, uchaguzi huu ulianza kutoa mwanga mpya kwa kizazi cha baadaye juu ya vile kitakavyoshiriki chaguzi mbalimbali zilizofuatia hapo.

Ni uchaguzi wa mwaka huo ndio pia ulioyaibuwa majina mapya kwenye siasa za Tanzania. Wanasiasa kama Profesa Ibrahim Lipumba, Marehemu Christopher Mtikila, Marehemu Emmanuel Makaidi, Augustino Mrema, Benjamin Mkapa, mbunge Dk. Walid Aman Kabouru wa Kigoma Mjini na Dk. Masumbuko Lamwai wa Ubungo walikuja juu wakati huu. Wengine wamezama na kupotea kwenye ramani ya kisiasa, na wengine wameendelea kutajika hadi leo hii.

Binafsi nilishiriki kupiga kura ndani ya viwanja vya Shule ya Buguruni, wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Nilishiriki huku nikijua ninachotimiza ni wajibu na haki yangu ya kikatiba, lakini ndani yangu nikiamini kwamba sikuwa na ubavu wa kutoa hata diwani kupitia chama nilichokiamini moyoni mwangu sambamba na wagombea wake wa ngazi zote. Niliamini hivyo kutokana na mazingira ya wakati ule kisiasa kwa upande huu wa Tanganyika. Kama nilivyoeleza, Watanganyika walikuwa bado kwenye blanketi la mfumo wa chama kimoja, ambalo wengi waligubikwa bila kufurukuta na kiongozi wanayemuamini kama nabii wao, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, kiasi cha kuuona mfumo wa vyama vingi kama laana ya kuwaletea vita na sio neema.

Kabla ya uchaguzi wenyewe, nakumbuka mikutano ya kwanza ya kampeni za vyama ilifanyika. Jangwani kikawepo Chama cha Mapinduzi (CCM), Mnazi Mmoja kikawepo Chama cha Wananchi (CUF) na Shule ya Uhuru wakawawepo NCCR MAGEUZI. Ambapo kule Jangwani alisimama Benjamin Mkapa, Mnazi Mmoja alisimama Prof. Lipumba na Shule ya Uhuru akaunguruma Augustino Mrema. Kulikuwa na ushiriki wa vyama vingine kwenye mbio hizi za mwaka 1995, lakini hivi vitatu ndivyo pekee ambavyo vilionekana kuwa na uhai na mjengeko wa kiuongozi tofauti na vingine ambavyo vilikuwa dhaifu mno, kikiwemo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hata hivyo, niweke wazi kwamba sehemu kubwa ya wafuasi wa vyama hivi iliegemea zaidi kwenye makabila, dini na maeneo wanayotokea viongozi wa juu wa vyama hivyo au wagombea wao. Kwa hivyo, haikushangaza kwamba sehemu kubwa ya wafuasi wa Mrema ni wale wenye asili ya kaskazini mwa Tanzania, wengi wao wakiwa wenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro na huku idadi kubwa wakiwa Wakristo, huku CUF ikiungwa mkono na Wazanzibari na wenyeji wa mikoa ya Pwani na kusini, wengi wakiwa Waislamu, na CCM ambayo ilikuwa na fursa ya kuwa chama tawala kinachomiliki kila taasisi na kila nyenzo kikitaka kionekane kuwa chama pekee cha kitaifa, ingawa ukweli ni kuwa hakikuwa tafauti sana na hao wengine.

Nakumbuka mkutano wa mwanzo aliofanya Prof. Lipumba pale Mnazi Mmoja, ulihudhuriwa na wanachi wengi wenye asili ya Zanzibar na wenyeji wachache wa mikoa ya Pwani. Huu ulikuwa mwanzo wa chama hiki kuitwa chama cha Wapemba na baadae kutokana na kukubalika kwake sana kwenye mikoa ya Pwani, kikaitwa chama cha Waislamu. Hata hivyo hili jina la chama cha Waislamu likawa na athari kubwa kwa CCM, kwani ni kweli Waislamu wa Tanganyika walimiminika na kukikubali mno kiasi cha CCM kujutia kosa hili!

Hapa ndipo nilipoanza kumfahamu Prof. Lipumba na uwezo wake mkubwa kwenye eneo lake la utaalamu wa uchumi. Huyu ni mwanasiasa aliyemvutia kila mtu aliyejipa nafasi kumsikiliza kiasi cha kujizolea umaarufu muda mfupi wa ushiriki wake kwenye siasa. Kwa hakika, Prof. Lipumba hakuwa mwanasiasa hasa kwa maana ya wanasiasa waliozoeleka. Yeye alikuwa na bado ni mchumi bingwa wa kimataifa, hivyo hotuba zake zilijikita zaidi kwenye data na takwimu lakini kwa lugha ya mtu wa kawaida kiasi ambacho kilimfanya msikilizaji wake kuvutika kifikra na kutochoka kumsikiliza. Ni mtu ambaye aliwazidi wote walioshiriki kama wagombea wa urais mwaka huo, akiwemo hata Mkapa, ambaye alikuwa anajivunia tu ufasaha wa kuzungumza, lakini si uwezo wa kuelezea matatizo makubwa ya uchumi na umasikini na suluhisho lake. Wagombea wengi wa vyama vingine walimkwepa kwenye midahalo na wale waliokubali kushiriki wakaonekana viroja. Hakika kiongozi huyu aliweza kuwavutia wengi na akapelekea kuimarika kwa CUF na kuibua hamasa kubwa kwa upande wa Tanganyika, kama alivyoweza kuibua hamasa hizo Maalim Seif Sharif Hamad kwa upande wa Zanzibar.

Hata hivyo, wengi hawajuwi tofauti iliyopo kwenye mjengeko wa kisiasa baina ya Tanganyika na Zanzibar. Kwamba wakati Wazanzibari wamekataa kujenga mfumo wa kugawa ushindi kirahisi kwa chama tawala, Tanganyika wameuasisi na kuujenga mfumo huu toka kuanza upya kwa mfumo wa vyama vingi. Hadi muda naandika makala hii, ushindani pekee wa kisiasa kwa Zanzibar ni baina ya CUF na CCM, wakati kule Tanganyika kuna utitiri wa vyama mpaka vya mtu na mkewe! Kuna vyama ambavyo uwepo wake husikika kipindi cha uchaguzi pekee na si baada ya hapo. Kuna vyama ambavo toka kusajiliwa kwake havijawahi kufanya mkutano mkuu wa kuweka au kubadilisha viongozi!

Hapa nitoe hongera kwa Wazanzibari kwa namna walivyofanikiwa kuasisi mfumo wenye nguvu na usioruhusu mgawanyiko wa kura usio na tija kwao, badala ya kuwa neema kwa chama tawala ambacho kina dalili za wazi za kuchokwa na walio wengi, lakini hakiondoki kwa kuwa wananchi wanaokipinga wamegawika.

Kuelekea uchaguzi wa mwaka 2015, ukiwa ni uchaguzi wa tano wa vyama vingi, siasa za Tanganyika ziliingia kwenye awamu nyengine, ambayo ilikuwa na mazuri na mabaya yake. Ubaya wake ni kuwa vyama vya kimageuzi vikapigwa na dafrau kutokana na kimbunga kilichojiri kwenye CCM. Wakati CUF ikipata pigo la kujivua uenyekiti kwa kiongozi aliyekubalika na wengi kwenye chama hicho, Prof. Lipumba na CHADEMA iliachwa mkono na katibu wake mkuu na mtu mahiri kwenye siasa za Tanzania, Dk. Wilbroad Peter Slaa. Wote wawili, Lipumba na Slaa, walisema sababu za kujiondoa ni ujio wa Edward Lowassa aliyekuwa CCM kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulioundwa na vyama hivyo na vyengine viwili.

Lakini kuja kwa Lowassa kwenye UKAWA hakukuwa na madhara kwa CUF na CHADEMA tu. Mtikisiko wa hatua yake hiyo hautosahauliwa kamwe ndani ya CCM kwenyewe, kwani kwa mara ya kwanza chama hicho tawala na kikongwe kilipasuka vipande vipande huku tukishuhudia wazito kadhaa wakikikimbia kumfuata Lowassa kule alikokukimbilia. Ni mtikisiko ambao umezibadili mno siasa za Tanzania kupita wakati mwingine wowote ule ndani ya miongo hii miwili na nusu ya vyama vingi.

Binafsi sikuuona ubaya wowote wakati Prof. Lipumba alipoamua kujivua uenyekiti wa chama chake cha CUF. Pengine sikuuona kwa vile hadi leo madharaya uamuzi wake hayajawa makubwa kiasi cha kukifanya chama chake kugawanyika na kutoa ishara za kusambaratika. Pengine kuondoka kwake kwenye nafasi hii na kisha kuwa kwake kimya au kujitokeza mara kadhaa hadharani kuzungumzia mambo mbalimbali ya kuikosoa serikali akiwa ndani ya ofisi za chama chake pale Buguruni, kulisaidia kutuliza hali ya taharuki iliyojaa kwenye mioyo ya wana-CUF walio wengi. Pengine hili liliwapa matumaini na kuendelea kuwa wastahamilivu, huku wakiamini kwamba kuna siku kiongozi wao huyu angelirejea tena mapambanoni kwa lengo la kukipeleka mbele chama chao.

Na kweli, Kama ndoto Prof. Lipumba akajitokeza hadharani na kutangaza kufuta uamuzi wake wa kujizulu uwenyekiti miezi minane iliyopita na akaeleza kuwa tayari kurejea kwenye nafasi yake ya awali, nafasi ambayo ni wazi kwamba alijaa na kuenea mno kwenye kiti chake. Na huu sasa ndio mtihani mkubwa na mzito zaidi kwa chama hiki kuliko hata ule wa kujiuzulu kwake. Naamini endapo watu watashindwa kusahau yaliyopita na kuamua kuganga yajayo, basi mtafaruku mzito unaweza kukikumba chama hiki kwa upande wa Tanganyika.

Nimejipa muda kujadili suala hili kwa maslahi mapana ya chama na kama mtu niliyetumia muda mwingi kushiriki siasa za Tanganyika. Hivyo nazielewa tabia za wengi kwenye uwepo wao kwenye siasa. Wenzetu wengi wa Tanganyika wameingia kwenye siasa za vyama vingi kutokana na mtiririko wa kimapokeo pamoja na kufuata mkumbo. Wengi hujenga mapenzi kwa mtu kwa vile rafiki yake au kaka yake ni mpenzi wa mwanasiasa fulani. Wengi hawana muda na hawajui katiba za vyama vyao. Wengi kwanza ni mashabiki wa mtu fulani na chama baadaye. Nalisema hili nikiamini kwamba wengi bado mnakumbuka namna ujio wa Lowassa katika upinzani ulivyobadili siasa za Tanganyika.

Ni huyu ambaye baina ya mwaka 2006 na 2013 upinzani ulitumia muda mwingi kumjadili kwa ubaya hadi kufikia mahala pa kumuingiza kwenye ile “Orodha ya Mafisadi” iliyozinduliwa viwanja vya Mwembeyanga, ambapo Dk. Slaa na Tundu Lissu waliusasambura ufisadi mkubwa, wakimuwekwa Lowassa kwenye nafasi za juu. Lakini pamoja na yote hayo, hatimaye ni huyu huyu aliyeihama CCM na kuleta nguvu kubwa kwenye upinzani ambao hadi jana yake ulikuwa unamuona kama fisadi. Kuna wanaokosoa hatua hiyo ya UKAWA kama ukigeugeu, lakini ukweli ni kuwa hii ndiyo aina ya wapigakura wengi wa Tanganyika, na ndio maana kwa mara ya kwanza upinzani ukavuuka asilimia 40 ya kura za uraisi na zaidi ya viti 100 vya wabunge, kutokana na kuja kwa Lowassa. Kama hukuwa makini na ukaongozwa na busara, unaweza ujiweke kwenye mazingira tata kisha wapigakura wasiwe na habari na wewe!

Bado kichwani mwangu ningali nakumbuka kisa alichonisimulia Juma Duni Haji, mgombea mwenza wa Lowassa kwenye uchaguzi wa 2015, kuhusu safari yake ya kazi ya kuimarisha chama chake cha CUF mkoani Mbeya. Kule alishangaa kuona kila mahali alipopita kukitangaza chama chake, watu walimsikiliza kwa makini na hamasa, lakini mwisho wa mahubiri yake, walimuuliza suali moja: “Sasa mheshimiwa tumekusikia, lakini unatuachaje?” Maana yake watu walikuwa wanaulizia anawaachia kiasi gani cha fedha au takrima ili wamuunge mkono.

Huo ndio utamaduni uliotawala sehemu kubwa ya siasa za Tanganyika. Kwamba watu wengi hawajajua umuhimu wa kuleta mabadiliko. Badala yake, hata mtu yule yule aliyewakwamisha na kuwadhikisha kwa miaka yote, hawaoni sababu wala hawajipi muda wa kumshughulikia kwa kumyima kura, bali akiwaendea na kibuyu cha mbege au gongo, anakuwa mtu safi wa kumpa tena nafasi ya kuwaumiza zaidi.

Hivi sasa, siasa zimehamia mitandaoni na tumeshuhudia taarifa mbalimbali juu ya uamuzi wa Prof. Lipumba wa kufuta barua yake ya kujiuzulu. Ndani ya taarifa hizo tumeziona kambi tatu za suala hili: wale wanaomuunga mkono Prof. Lipumba kurudi kwenye nafasi yake bila ya kupitia hatua za uchaguzi kama ulivyo utaratibu wa chama chake, na wale wanaompinga moja kwa moja kwamba hafai tena kuwa kiongozi wa CUF na wale wanaotaka arejee lakini kwa kupitia taratibu zilizowekwa na chama hicho.

Licha ya kuwa siwaungi mkono wanaotumia mitandao kama njia ya kushinikiza maamuzi ya CUF kwenye suala hili, mimi naona kwamba hakuna haja ya waliowahi kuwa viongozi wa juu wa chama hicho na hata viongozi wa sasa kujiingiza kwenye malumbano haya. Nalisema hili huku nikiamini kwamba wengi wa watakaoonekana kumuunga mkono kiongozi yeyote kwenye kundi lolote kati ya yaliyopo si wenye chama chao, bali ni wachochea utambi wapendao kuiona CUF ikiripuka na kusambaratika vipande vipande!

Kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, lakini ni muhimu kufanya utafiti wa kutosha juu ya athari au faida za kile wanachokiwasilisha mitandaoni, hasa kwa viongozi ambao wamewahi kufanya na Prof. Lipumba.

Binafsi sipendi kuona chama hiki kikisambaratika, lakini pia sipendi kuona uimara wa chama hiki uko kwenye kutegemea nguvu za wengine, badala ya kujikita na kujijenga kwa watu kama taasisi yenye kujitegemea. Wna_CUF wengi walifadhaika kuona mtu aliyetumia muda mwingi kuimarisha chama akiwaacha kwenye mazingira tata kipindi ambacho walimuhitaji sana, lakini kama alivyosema mtu mmoja: “mtu mzima akikosa na kulikiri kosa lake, si lazima awaombe radhi watot wake. Vitendo vyake vinatosha kumfahamu kuwa ametubu.” Naamini kuna kundi kubwa la wana-CUF ambao wataumia na kukata tamaa zaidi ikiwa kiongozi huyu ataundiwa mazingira ya kutorejea kwenye nafasi yake bila ya hoja za msingi.

Kama nilivyosema awali, siasa za Tanganyika – ambako ndiko nilikokulia na kuishi sehemu kubwa ya maisha yangu – zina tofauti kubwa na siasa za kwetu, Zanzibar, nilikozaliwa. Tanganyika unaweza ununuwe kura kwa glasi ya gongo au kapelo. Kwa hivyo, suala la Prof. Lipumba lisipelekwe kihasirahasira bali busara itumike ili chama kiendelee kuwepo kwa makabwela wa Buguruni, Vingunguti, Lindi na Mtwara yake.

Nahofia sana kuja kuiona milingoti ya chama hicho ikija ikipandishwa bendera ya vyama ambavyo twaviona rafiki chini ya UKAWA, huku ajenda nyuma ya pazia dhidi ya CUF zikiwa za kuitengezea mazingira ya kusambaratika ili yao yawendee!

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Ahmad Abu Faris, ni mwandishi wa habari anayeishi kisiwani Pemba. Anapatikana kwa nambari ya simu +255 774 581 264.

Zanzibar Daima

Chanzo MzalendoNet
 
Unasema Lipumba asiundiwe zengwe la kumuondoa bila sababu za msingi wakati huo huo makala yako imeainisha sababu za msingi kwa nini Lipumba hafai.... Sasa tukueleweje au hujui umeandika nini?
 
Makala imara na nzuri sana. Ila umemaliza kwa fumbo kuwa sehemu ya bendera za CUF zaweza kupandishwa bendera za vyama vingine chini ya muungano wa UKAWA!! kwa maneno mengine ndani ya UKAWA kuna chama kinachochea kuni moto uwake? Binafsi Prof Ibrahim Lipumba hakuna haja ya kuendelea kuwa M/kiti wa CUF, CUF ina watu imara ebu wapeni nafasi ya kufanya siasa za kizazi hiki na cha kesho. Aendelee kuwa mwanachama na mshauri basi licha makando kando ila toeni nafasi kwa wengine.
 
Back
Top Bottom