Binafsi nina kigugumizi. Siku moja utotoni mwangu, jamaa mmoja aliniudhi sana kwa kunitukania Mama yangu, basi tukapanga kupigana baada ya shule kwisha kwa ile siku. Tukaenda uchochoroni huku mie nikiwa na hasira ile mbaya, wapambe kibao walijaa kwani walikuwa wanajuwa mimi nikipigana lazima nimtoe ngebe mwenzangu, yaani sina msamaha hata kidogo na nilikuwa najulikana mpaka kuitwa 'Bud Spencer' enzi hizo. Wapambe wakachota mchanga na kutuambia tupute, nikaanza mimi kuputa...mwenzangu akawa anaogopa kwani alikuwa anajuwa muziki wangu au ni uwoga wake tu ulimzuia. Kwa kuwa nilikuwa na hasira sana, kigugumizi kikanishika na kuongea kumwambia jamaa apute mchanga siwezi. Kuangalia kando nikaona mpambe mmoja kashika kifuu anakifukia nikajuwa ni yeye ndiye kanifanya nishindwe kuongea. Ee bwana, nilimwacha yule jamaa niliyetaka kupigana naye na kumvamia mpambe, nilimtandika ile mbaya, nilimtwanga vichwa mpaka akapasuka midomo na kuvunja pua yake. Usiku nashangaa wanakuja yeye na Mama yake na polisi kuja kunikamata kunipeleka polisi. Nikaruka ukuta na kukimbilia Tandale kwa wahuni. Sikuonekana nyumbani wiki nzima kwani nilijuwa nakwenda kufungwa jela ya watoto.