Kwanza Kilimo?

David Nkulu

Member
Jul 25, 2008
53
1
Wana JK

Hotuba za Waheshiwa Raisi wa JMK na mawaziri wa fedha na kilimo walizozitoa hivi karibuni bungeni zinaonyesha kuwa serikali ina mpango wa kukitilia mkazo kilimo, TENA. Hili ni jambo zuri ila inabidi wote tuliangalie kwa makini. Ikumbukwe kuwa serikali ya awamu ya kwanza ilichambua njia za uzalishaji mali nchini kwa wakati ule na kukitambua kilimo kuwa ni njia pekee (sic!) itakayoweza kuingiza pesa za kigeni kwa kuuza mazao nje. Azimio la Arusha limekitaja kilimo kuwa ni moja ya misingi ya maendeleo ya nchi. Tatizo ni kuwa Azimio la Arusha halikuweka mpangilio wowote ambao ungeweza kuleta maendeleo ya kilimo kwa kiwango cha kimataifa zaidi ya kupendekeza kuanzisha vijiji vya ujamaa, na kuongezea kutilia mkazo “juhudi” na “maarifa”. Matokeo mahususi ya sera hizo sina lazima ya kuyarudia hapa.
Waheshimiwa watajwa hapo juu wametangaza kuwa serikali imetenga pesa kwa ajili ya kunufaisha shughuli za ukulima, ikiwemo Benki ya Rasilimali. Kiasi kilichotengwa kinaanzia shilingi bilioni 50 kwa TIB na shilingi bilioni 460 kwa bajeti ya 2008/09. Waziri wa fedha hakusita kutaarifu kuwa pesa hizo hazijumuishi misaada ya wadau na mashirika ya nje. Ifahamike kuwa kutenga pesa peke yake hakutaleta mafanikio tunayoyatamani kama watanzania. Achilia mbali hoja kwamba pesa hizo ni kama tone la maji kwenye bahari ya mahitaji! Ili pawe na matokeo mazuri, na ili kilimo chetu kiwe na faida kwa wakulima na kuleta tija kwa nchi nzima, inabidi patokee mabadiliko ya mfumo mzima wa kilimo. Ni lazima tubuni mfumo endelevu wa muda wa kati hadi muda mrefu ujao utakaojenga misingi ya kuwa na wakulima mahususi wenye sifa zote zinazohusiana na uzalishaji mali kwa kilimo cha kisasa.
Ukichunguza hotuba kwa uangalifu utagundua kuwa serikali haina mpango maalum kama huo unaowalenga wakulima wenyewe. Kama ni “kwanza kilimo” basi inabidi tuanze kwa kuhakikisha kuwa mkulima anabadilishwa na kupewa mkazo na huduma zote ambazo dola inapaswa kumhakikishia mkulima kama raia mzalishaji mali. Na siyo kuirudia hoja kuwa serikali haina fedha. Kubuni sera, mifumo na mazingira mazuri ya maendeleo ni jukumu la Serikali, na kwa sehemu kubwa hakuhitaji fedha za kutisha.
Miongoni mwa huduma ambazo raia mkulima anapaswa ategemee kupata kutoka kwa serikali yake anayoipigia kura kwa karibu miaka hamsini sasa ni hizi:
a)Elimu ya kutosha ya kilimo ya kiwango kinacholenga uzalishaji bora kwa nyenzo za kisasa
b)Huduma zilizotengwa kwa mkulima na kilimo zitakazowawezesha wakulima kurahisishiwa “uwekezaji” na ujasiriamali kwa kiwango endelevu cha juu.
c)Huduma za afya, bima, akiba ya uzeeni n.k zitakazowalenga wakulima ili kukidhi mahitaji na mazingira yao kama wakulima.

Kwa mtazamo wangu ili mtu aitwe mkulima na apewe huduma hizo, lazima awe amejikita kwenye kilimo kwa asilimia mia moja. Asiitwe “mkulima” mtu ambaye ana kazi ya ziada isiyohusiana na uzalishaji mali kwa kilimo.
Mabadiliko ya mfumo wa kilimo (cha kisasa) lazima yahusishe mambo yafuatayo:

1.Wakulima wenye elimu ya kilimo cha kisasa inayojumuisha

- Matumizi ya nyenzo za kisasa za kulimia
- Matumizi ya “best practices” za kilimo zinazotokana na uchunguzi na maendeleo (R&D) ya kilimo cha kisasa.

Inabidi kuanzisha / kushirikisha shule na vyuo vya kilimo, wataalamu wa kilimo katika ngazi mbalimbali ambao wangeelimisha wakulima na hasa vijana wanaokusudiwa kuwa wakulima kukiwa kumewekwa lengo maalum linaloeleweka la kulifikia kutokana na matakwa na mahitaji yetu kitaifa.

Serikali na vyombo vya dola viwe wabunifu, wasimamizi wa kisheria / kimuundo kwa mbali na isijiingize kwenye uzalishaji kwani kazi hiyo si yake na ilishatushinda huko nyuma!

2.Wakulima hao wawezeshwe kumiliki ardhi kubwa kutosheleza aidha kwa kupewa ardhi kwa masharti au kukopeshwa pesa za kuwawezesha kumiliki ardhi inayohusika.
3.Kuwepo kwa mikopo nafuu ya muda mrefu kwa wakulima watakaotimiza masharti 1 na 2 hapo juu itakayowawezesha kumudu gharama zote za uendeshaji wa shughuli za kilimo ikiwemo:
- Ununuzi, ukopeshwaji wa nyenzo za kisasa za kulimia, kupandia, kutibu, kumwagilia maji na kuvunia mazao.
- Ununuzi wa mbolea, dawa za kupigana na wadudu, ujenzi wa maghala ya vifaa na mazao yao.
- Ununuzi wa vifaa au vyombo vya kusafirishia mazao yanapovunwa.

Lengo la 2 na 3 hapo juu ni kujenga / kutayarisha “thamani” (value) ya uzalishaji ikiwa kama msingi wa uwiano baina ya mkulima / wakulima na vyombo husika vitakavyokuwa vinasimamia ukopeshaji wa pesa na vifaa kwa kazi nzima za ukulima.

Kupiga mbiu kwenye mikutano ya hadhara kuwa watanzania walete matrekta hakuleti manufaa, bila kuwepo mpangilio wa mfumo mzima wa kilimo na mazingira yake.

4.Kuwepo kwa mfumo na mpangilio wa kuwawezesha “ku-process” au kusindika mazao yao na kuwa bidhaa kamili na kuuza kwa bei yenye faida kwa wakulima katika soko badala ya kuuza kama “mali ghafi” kwa bei inayopangwa na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Serikali na vyombo vya dola itilie mkazo kitengo cha kuzalisha bidhaa kamili kutokana na mazao ya wakulima hapa hapa kwetu nchini na kuwezesha kuuza bidhaa kamili nje kitu ambacho kinatufanya tukose sauti kwenye upangaji wa bei za bidhaa zetu wenyewe kwani tunakuwa tunategeme kuziuza kama mali ghafi.

5.Kuwepo mpango wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa kupitia vyombo vya dola kama “chambers of commerce” na njia nyingine za soko huria kama
- Kushiriki kwenye maonyesho ya taifa na kimataifa ya kibiashara.
- Kufuatilia na kutumia “trade quotas” ambazo nchi zetu zinapewa nafasi hiyo na nchi kama za jumuiya ya ulaya, SADC, na masoko mengine ambazo hatuzitumii ipasavyo.

6.Kuwepo utaratibu mahususi wa kuhakikisha kuwa mikopo ya ardhi na au/pesa inarudishwa kwa misingi ya soko huria kwa uwiano wa soko la bidhaa na thamani ya pesa. Kuwepo vitengo maalum vya dola vitakavyosimamia msululu mzima wa mpangilio wa ufuatiliaji wenye lengo la kumrahisishia mkulima sheria na vikwazo tangu mwanzo wakati wa matayarisho ya uzalishaji, wakati wa uzalishaji na baada ya uzalishaji.

Serikali inabidi itambue kuwa kwa kumuelimisha na kumuwezesha mkulima mzalendo mmoja kuwa “mkulima wa kisasa”, mwenye malengo yanayoeleweka na kukubalika kijamii na kitaifa, itakuwa inajenga msingi imara wa kilimo endelevu cha kuzalisha mazao ambayo yatasaidia kuhudumia jamii ya watanzania wa kizazi hiki na vizazi vijavyo wakati huo huo itakuwa inaongeza pato la nchi kwa ujumla. Mwekezaji anayetoka nje ya nchi, japo anavutia kwa kuja na pesa zake, hatoleta faida ya muda mrefu kwa nchi hii, na itabidi ahakikishe kuwa anapata faida ambayo daima atataka aitoe nje ya nchi.

Kutokubali kuleta mabadiliko ya mfumo mzima wa kilimo, ambao ungelenga kumtambua upya “mkulima wa kisasa” ni kukubali kuwa tunarudia makosa yale yale tuliyoyafanya baada ya (na kwa) kutangaza Azimio la Arusha na Azimio la Dodoma. Jitihada za serikali zitakuwa hazina manufaa kwa wakulima, wananchi kwa jumla na nchi nzima kama tunavyokusudia. Hii itasababishwa na fedha hizo kutumiwa na wajanja wachache ambao siyo wakulima wa kweli, bali ni wachuuzi na wafanya biashara waliokwisha kujichomeka kwa niaba ya wakulima. Tutagundua hili baada ya kupita miaka kadhaa isiyokuwa na tija kwetu wote. Kilimo Kwanza itabaki kuwa “slogan” tupu, sawa na slogans zilizopita miaka ya nyuma zilizohusiana na kuwalenga wakulima.

David N.


P.S: Sitarajii kuwa serikali ya JMT itayafuata niliyoyaandika hapa. Hilo si lengo langu. Serikali zetu zina historia ya kutosikiliza mawazo na maoni ya wananchi wake. Kusudi langu ni kupata mawazo yenu, tushauriane, tukosoane na kubadilishana mawazo.. Lengo hasa ni kupanda mbegu ya mawazo na mabadiliko ya mtazamo ili kujaribu kupata suluhisho la matatizo sugu tunayokabiliana nayo, matatizo ambayo siku hadi siku yanaonyesha kuendelea kutuzidi nguvu!

Watanzania tuko zaidi ya milioni 40, na kila mmoja bila shaka ana mtazamo wake. Kwa kujadiliana tutakuwa na mwelekeo wa nadharia na kifikra nini tunapaswa tufanye. Huenda siku kama hiyo, siku moja itatokea!

Karibuni kuchangia
 
Nakubaliana na hoja yako kwamba "kilimo kwanza" bila mikakati ya kimiundombinu na wakulima kuandaliwa vya kutosha ni kaulimbiu isiyo na strategy hivyo itabaki midomoni mwa hayo mawazili na wabunge ambao wengi wao tangu kuzaliwa kwao hawajui jembe linashikwaje?
Hivi huyo mkulo anashamba huko kwao Moro au anajisemea tu mambo ya kilimo? amisha onja hasara wanazopata wakulima wa kibongo?
Badala ya kuwafidia wakulima eti wanawapa hela wafanyabiashara wa mazao,mafisadi wenzao eti wasifilisike! Hii ni akili kweli?
Wanawaiga wenzao wa ulaya ambao tayari wanaruzuku kwa wakulima wao. Hivi hii nchi inakwenda wapi? Inanitia uchungu sana!!!!!
 
Nakubaliana na hoja yako kwamba "kilimo kwanza" bila mikakati ya kimiundombinu na wakulima kuandaliwa vya kutosha ni kaulimbiu isiyo na strategy hivyo itabaki midomoni mwa hayo mawazili na wabunge ambao wengi wao tangu kuzaliwa kwao hawajui jembe linashikwaje?
Hivi huyo mkulo anashamba huko kwao Moro au anajisemea tu mambo ya kilimo? amisha onja hasara wanazopata wakulima wa kibongo?
Badala ya kuwafidia wakulima eti wanawapa hela wafanyabiashara wa mazao,mafisadi wenzao eti wasifilisike! Hii ni akili kweli?
Wanawaiga wenzao wa ulaya ambao tayari wanaruzuku kwa wakulima wao. Hivi hii nchi inakwenda wapi? Inanitia uchungu sana!!!!!

Rumenyela,
Nakuelewa mkuu. Uchungu unaoupata nina hakika ni wengi tunajisikia hivyo. Ni aibu kukuta kuwa ktk karne ya 21, isiponyesha mvua sehemu fulani nchini kwetu basi watu wanakufa kwa njaa!
Hali hii haitosita ikiwa lengo la wahusika wenye jukumu la "kutupanga" wanajali kupitisha bajeti ya mwaka husika, na matatizo sugu yanpigwa chenga ya mwili. Hali hii ndiyo iliyotufanya tujikute imepita miaka 49 baada ya uhuru na adui njaa na umasikini wako "njangari!!"
 
Back
Top Bottom