Kwanini Bageni amehukumiwa kunyongwa peke yake kati ya watu 13 alioshitakiwa nao...

Bashir Yakub

Member
May 27, 2013
84
1,561
KWANINI BAGENI AMENYONGWA PEKE YAKE KATI YA WATU 13 ALIOSHITAKIWA NAO ?.

Na Bashir Yakub
+255 784 482 959.

Walioshitakiwa walikuwa 13, SP Christopher Bageni, ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed Makele, PC Noel Leornard, WP 4593 Jane Andrew, CPL Nyangerela Moris, PC Michael Shonza, CPL Abeneth Saro,DC Rashid Mahmoud Lema, CPL Emmanuel Mabura,CPL Felix Sandys Cedrick , CPL Rajab Hamis Bakari, na CPL Festus Philipo Gwabisabi.

Kwanini wameshitakiwa watu wote hawa halafu mtu mmoja ndiye aliyepatikana na hatia na akahukumiwa kunyongwa, tutaona hapa.

Kwa kumbukumbu kesi hii ilianzia mahakama kuu ya Tanzania mbele ya Jaji Massati JK.
Wakati upande wa mashtaka ukifunga kesi yao mahakama ikawaondoa watuhumiwa watatu PC Noel Leornard, CPL Nyangerela Moris na CPL Felix Sandys Cedrick kwa kuwaona hawana kesi ya kujibu na hivyo ikaona hakuna haja ya kuwataka kujitetea na kuendelea kuwa katika kesi.

Kwahiyo wakabaki 10 ambao sasa walikutwa na kesi ya kujibu na hivyo kesi ikaendelea na hao 10 ikiwemo Bageni.

Wakati wameanza kujitetea mmoja wao hao 10 DC Rashid Mahmoud Lema alifariki na hivyo kesi yake ikaishia hapo na sasa idadi ikabaki 9.

Mwisho wa kesi hapo mahakama kuu Jaji Massati aliwaachilia huru watuhumiwa wote 9 waliokuwa wamebaki kwa kuwaona hawana hatia. Moja ya hoja kubwa ya kuachiliwa kwao huru ilikuwa kwamba kati ya wote hao 9 waliobaki katika kesi hiyo hakuna hata mmoja kati yao iliyefyatua risasi na kuua.

Ikumbukwe aliyefyatua risasi na kuua ni CPL Saad ambaye hakuwahi kufikishwa mahakamani baada ya kutoroka mapema liliposanuka. Kwahiyo mahakama kuu iliona kutokuwepo kwa CPL Saad ili atiwe hatiani kwa kuua au amtaje mtu mwingine aliyempa amri ya kuua ili wote wahukumiwe kwa kosa moja, iliona ni udhaifu ambao unatosha kuwaachilia watuhumiwa wote 9, na iliwaachilia wote huru.Kwa ufupi iliona hakuna kinachowaunganisha na mauaji zaidi ya tu kuwa walikuwa kwenye tukio.

Serikali/Jamhuri haikuridhishwa na uamuzi huo na hivyo ikakata rufaa mahakama ya rufaa ikipinga hukumu hiyo dhidi ya watuhumiwa wote 9 walioachiliwa. Rufaa ikasajiliwa kwa namba 358/2013. Rufaa ilipangwa kwa majaji watatu Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na Jaji Kaijage.

Wakati rufaa inapangwa kusikilizwa serikali/Jamhuri ikawafutia rufaa watuhumiwa watano WP 4593 Jane Andrew, CPL Emmanuel Mabura, PC Michael Shonza, CPL Abeneth Saro na CPL Festus Philipo Gwabisabi.Kwahiyo kwenye idadi ya wale 9 wakabaki wanne ACP Abdallah Zombe, SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makele na , CPL Rajab Hamis Bakari.Hivyo rufaa ya mahakama ya rufaa ikaendelea na hawa wanne.

Rufaa ilisikilizwa na mwisho mahakama ikawaondoa watatu ACP Abdallah Zombe, ASP Ahmed Makele na , CPL Rajab Hamis Bakari kuwa hawana hatia na ikawaachilia huru, ikabaki na mmoja SP Christopher Bageni ambaye ilimkuta na hatia na ikaamuru kunyongwa kwake hadi kufa.Kumbuka mahakama kuu ilimwachilia huru. Ni mahakama ya rufaa iliyobadilisha maamuzi haya kutoka kuachiliwa huru hadi kunyongwa.

KWANINI BAGENI ANYONGWE NA WENZAKE WAACHILIWE HURU.

Mahakama Kuu.

Kumbuka mahakama kuu ilimuachilia Bageni kwasababu kuu mbili. Kwanza siye aliyefatua risasi, na pili yule aliyefyatua risasi CPL Saad hakufika mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyemuamrisha kupiga risasi ili wote wawe na hatia sawa.

Hii ni kwasababu kwa mujibu wa Kifungu cha 22 cha Kanuni za Adhabu aliyetenda kosa kama vile CPL Saad alivyopiga risasi, na aliyeamrisha(saidia) kutendwa kosa wote hatia yao ni moja. Kama ni kunyongwa ni wote na kama ni kifungo ni wote.

Kwa msingi huu mahakama kuu haikumuona Bageni akifyatua risasi kwasababu sio yeye aliyefyatua risasi na hivyo upande huo akaondolewa, lakini pia haikumuona akiamrisha risasi kufyatuliwa kwasababu aliyefyatua hakuwapo mahakamani kumtaja kuwa ndiye aliyemwamrisha kufyatua na hivyo upande huo pia nako akaondolewa.

Mwisho akaonekana haingii popote kwenye kosa basi akaachiliwa huru.

Mahakama ya Rufaa.

Mahakama ya rufaa haikukubaliana na uchanganuzi huo wa mahakama kuu na hivyo ilimuona Bageni ana hatia. Ilisema ni kweli Bageni siye aliyefyatua risasi, lakini kifungu cha 22 cha Kanuni za Adhabu kuhusu kutoa kwake amri kinamuingiza hatiani.

Ilisema kwamba ushahidi wa kimazingira unathibitisha wazi kuwa alitoa amri. Ushahidi wenyewe wa kimazingira uliionwa na mahakama ya rufaa ni kama ifuatavyo ;

KWANZA, katika askari wote waliokuwa kwenye tukio yeye ndiye aliyekuwa na cheo kikubwa kuliko wote na hivyo yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa amri zote katika matukio yote yaliyotokea eneo hilo hata pasingekuwepo na shahidi wa kusema alimuona anatoa amri.

PILI, walipokuwa wamewakamata wafanyabiashara waliouliwa katika barabara ya SAM NUJOMA yeye ndiye aliyeamrisha msafara wa magari mawili Defender na Pajero kuelekea msitu wa PANDE(ushahidi wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari ).

TATU, mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari anasema walipofika msitu wa PANDE Bageni alishuka kwenye gari akamuachia radio call . Wakati amekaa ndani ya gari akiwa amebaki na dereva kwa jina FRANK alisikia kupitia radio call aliyoachiwa milio ya risasi.

Ikabidi ashuke kuelekea Bageni alikoelekea. Alipowakaribia alimuona CPL Saad akiwa anamalizia kumpiga risasi mfanyabiashara wa mwisho,wengine wakiwa wameshauliwa wamelala chini huku Bageni akiwa amesimama anatazama.

NNE, baada ya wafanyabiashara kuuliwa, ni Bageni aliyeamuamrisha dereva SGT James kubeba maiti na kuzipeleka Muhimbili(ushahidi wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari na Sgt James ).

Kwa mazingira haya mahakama ya rufaa ikaona kwa vyovyote vile hata kama CPL Saad hayupo mahakamani kumtaja Bageni kuwa ndiye aliyetoa amri ya kuua, bado mazingira yote yanaonesha yeye ndiye aliyetoa amri na hivyo kuwa na kosa sawa na CPL Saad aliyekimbia.

Zaidi, mahakama ya rufaa ikazingatia haya kwa Bageni ;

MOJA, kwanini Bageni aamrishe wafanyasbiashara kupelekwa huko mbali kote PANDE tena kwenye msitu ambako hakuna nyumba wala kituo cha polisi. Nia ya kuwapeleka huko ilikuwa nini hasa. Jibu likawa ni mpango wa kuwadhuru tu bila shaka.

MBILI, Bageni alisema kuwa walikuwa wakijibizana kwa risasi na marehemu maeneo ya Sinza kwenye ukuta wa Posta. Ushahidi na mashahidi wote akiwemo shahidi wa 20 Kisa Mohammed mlinzi wa ukuta huo wa posta alithibitisha kuwa hakuna majibizano yoyote ya risasi yaliwahi kutokea eneo hilo. Swali lilikuwa uongo huo ulitungwa kwa lengo lipi.

TATU, Bageni alionesha makasha tisa ya risasi na kusema kuwa maganda hayo yalitokana na risasi zilizotumika katika majibizano na wafanyabiashara waliouliwa maeneo ya Sinza.

Wakati ushahidi wa mtuhumiwa wa 4 CPL Rajab Hamis Bakari unaonesha kuwa maganda hayo yalitokana na risasi zilizofyatuliwa hovyo hewani maeneo ya Bunju na zilifyatuliwa na CPL Saad na DC Rashid na baada ya kufyatuliwa Bageni aliwaamrisha wamkabidhi maganda hayo ambayo ndiyo aliwasilisha mahakamani. Swali kwa mahakama ni lengo la kufyatua risasi hovyo hewani na kuchukua maganda lilikuwa ninini.

Kwa kuzingatia haya na hayo niliyotangulia kueleza mahakama ya rufaa ikapigilia msumari kuwa Bageni si tu alitoa amri ya kuuliwa wafanyabiashara bali pia aliandaa mazingira ya ushahidi ili kukwepa mkono wa sheria.Kwa shahidi hizi mahakama ya rufaa ikafuta uamuzi wa mahakama kuu wa kumuona Bageni hana hatia, na ikatangaza uamuzi mpya wa kumkuta na hatia ya kuua kwa kukusudia na hivyo kuamuru anyongwe hadi KUFA.

BAGENI AOMBA UAMUZI WA KUNYONGWA KWAKE KUREJEWA.

Hii ndo ile ya juzi ambayo mlisikia. Basi ni hivi, mahakama ya rufaa ndiyo mahakama ya mwisho katika kutoa maamuzi. Hakuna rufaa nyingine baada ya maamuzi yake inakuwa imetosha na imetosha. Umeridhika, hukuridhika uamuzi ukitoka hapo biashara imekwisha.

Hata hivyo, Sheria Mamlaka za Rufaa, Sura ya 141 kifungu cha 4(4), pamoja na Kanuni za Mahakama ya Rufaa zaMwaka 2009 , Kanuni ya 66(1)( a ) ( b ) zinatoa nafasi ya mwisho kwa mtu ambaye hakuridhika na maamuzi ya mahakama ya rufaa kuomba MAREJEO hapohapo mahakama ya rufaa.

MAREJEO ni maombi ya kuiomba mahakama ileile iliyotoa hukumu kupitia tena maamuzi yake ili kujiridhisha na nukta kadhaa ambazo muombaji atakuwa ameziainisha.

Utaiomba mahakama chini ya majaji wengine tofauti na wale waliotoa uamuzi wa kwanza kurejea tena na kuangalia vile vitu ambavyo unadhani umeonewa.

Kesi ya BABU SEA nayo ilifikia hatua hii lakini ikashindikana.Kwa Mawakili wanajua kuwa hii ni hatua isiyowezekana siku zote labda iwe vinginevyo.

Kwahiyo hukumu mliyoisikia juzi ni matokeo ya MAREJEO yaliyoombwa na Bageni ambayo ni namba 63/2016 chini ya majaji wengine watatu Jaji Mugasha, Jaji Wambali, na Jaji Kerefu.
Bageni alikuwa na hoja kuu mbili za kurejea, kwanza kuwa hakupewa nafasi ya kusikilizwa na pili kuwa mahakama ya rufaa wakati inasikiliza rufaa yake iliibua vitu vipya ambavyo havikuwa sehemu ya kesi kule mahakama kuu.
Kwa ufupi majaji hawa walimsikiliza hoja zake kupitia kwa wakili wake Gaudiosus Ishengoma, na wakasikiliza hoja kinzani kutoka upande wa serikali/Jamhuri uliowakilishwa na Wakili Ladislaus Komanya na kusema kwamba Bageni hana hoja za msingi na anacholalamikia hakina mashiko.

Kwa uamuzi huu majaji hawa Jaji Mugasha, Jaji Wambali, na Jaji Kerefu wakakubaliana na uamuzi wa majaji wa mwanzo wa mahakama hiyohiyo Jaji Luanda, Jaji Mjasiri na Jaji Kaijage kuwa Bageni anastahili kunyongwa hadi KUFA.

Hivi ndivyo SP Christopher Bageni alivyobaki peke yake kati ya watu 13 alioshitakiwa nao.

Katika kuweka kumbukumbu sawa, tarehe 14 / 1 / 2006 wafanyabiashara wanne wa madini Ephraim Sabinus Chigumbi,Sabinus Chigumbi, Juma Ndungu na Mathias Lunkombe waliuliwa na kuporwa madini na fedha taslim walizokuwa nazo katika msitu wa PANDE Kinondoni Dar es salaam, mauaji yaliyotekelezwa na watuhumiwa waliotajwa humu kwa kisingizio kuwa wafanyabiashara hao ni majambazi.
 
Polisi kuwa muuaji ni kosa kubwa sana kwenye jamii kwani yeye ndio anategemewa kutoa ulinzi wa Mali na maisha ya RAIA na sio ushenzi kama wa Bageni na wenzake.
Ni kwa vile sheria inasema hukumu ya muuaji ni kunyongwa hadi kufa, lakini Hugo Bageni na wenzake akiwamo Zombe walistahili adhabu ya kukatwa viungo hadi wafe ili liwe fundisho kwa polisi wenye tabia za kijambazi.
 
Hii kesi naona kuna mkono wa mtu. Inanikumbusha ya Ditopile alivyofia uraiani wakati aliua live!!

Zombe alitangaza kuwa hao majambazi waliuawa Kinondoni, baadaye ikadhihirika waliuawa Mabwe.
Mhusika mkuu ambaye alitakiwa atoe siri zote, alikufa kifo cha kutatanisha pale Muhimbili. Zombe kuachiwa kwake kulitia wasi wasi lakini wenye nguvu walikuwa nyuma yake.

Vito vilivyochukuliwa na pesa ziliishia wapi ikiwa waliouawa walionekana ni raia wema lakini baada ya kuuawa?

Hii ni kesi ya Ngedere na huyo Bageni atatoka tu karibuni ni danganya toto. Nilipishana na Zombe siku moja anakwenda kwa advocate wake, karibu nimtemee mate ila nikaogopa asinido na mimi.
 
Asante sana kwa ufafanuzi nina maswali;

1.Hivi majaji wa Mahakama ya Rufani wanakua na elimu na busara zaidi kuzidi wa Mahakama kuu au inakuaje?maana naona sababu za kumkuta na hatia Bageni zina mashiko tofauti za wenzao wa Mahakama kuu waliomwachia huru.

2.Je nini nafasi ya Mahakama ya Afrika mashariki kama akiamua kwenda huko?

Ahsante
 
Back
Top Bottom