Alichosema Lissu kuhusu Muungano ni hiki hapa.
Mheshimiwa Spika,
Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba inapendekeza pia kwamba Katiba Mpya ipatiwe nguvu na uhalali wa kisheria kwa kupitia kura ya maoni itakayoratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Tume hizi mbili kwa mashauriano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar - ndizo zitakazotengeneza swali litakaloulizwa kwenye kura ya maoni. Utaratibu utakaotumika katika kura ya maoni ni ule unaotumika katika chaguzi za kawaida katika nchi yetu, yaani Sheria ya Uchaguzi wa Taifa, Sura ya 343, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, 1984. Ijapokuwa kura ya maoni itaamuliwa kwa wingi wa wapiga kura (simple majority), Rasimu ya Muswada inapendekeza kwamba ili kura hiyo iwe halali ni lazima angalau 65% ya wapiga kura wote waliojiandikisha Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar washiriki katika kupiga kura. Rasimu ya Muswada inapendekeza kwamba Rais ndiye atakayeamua, kwa namna atakavyoona inafaa, kuanza kutumika kwa Katiba Mpya!
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi kama Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba ndio inawakilisha msimamo wa Serikali juu ya mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya. Kama ni hivyo, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka wazi msimamo wake Muswada huu haukubaliki hata kidogo. Kwanza, Kambi Rasmi ya Upinzani haikubaliani na mamlaka makubwa yanayopendekezwa kupewa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar chini ya Muswada huu. Urais wa Kifalme kama kanuni kuu ya kikatiba na kisiasa ndiyo ambayo imetufikisha hapa tulipo leo: taifa lenye wananchi maskini, lililojaa ufisadi, lisilojali demokrasia na haki za binadamu na lenye kuongozwa na watawala wasiowajibika kwa wananchi au kwa vyombo vya uwakilishi vya wananchi. Mfumo huu hauwezi kutumika tena kulipatia taifa letu Katiba Mpya ya kidemokrasia itakayokidhi mahitaji ya karne hii na nyingine zijazo.
Pili, Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Rasimu ya Muswada hayakubaliki kwa sababu yanaweka mchakato wa Katiba Mpya kwenye huruma na/au fadhila ya Rais wa Zanzibar na siasa za Zanzibar kwa ujumla. Kwa mapendekezo haya, Rais wa Zanzibar asipokubaliana na jambo lolote linalohitaji ridhaa yake basi mchakato mzima utasimama au kusitishwa. Aidha, endapo katika kura ya maoni inayopendekezwa, theluthi mbili ya Wazanzibari hawatakubaliana na Katiba Mpya basi Katiba hiyo haitapitishwa hata kama inakubaliwa kwa kiasi kikubwa na wananchi wa Tanzania Bara. Mustakbala wa taifa letu hauwezi kuwekwa tena rehani kwenye siasa za Zanzibar na kwenye matakwa ya Wazanzibari kwa kiasi hicho. Kuhusiana na jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba Rais wa Zanzibar ahusishwe tu katika masuala ya kikatiba ambayo ni ya Muungano tu. Nje ya masuala hayo, Rais wa Zanzibar hana sababu yoyote ya kuhusishwa na mchakato wa kikatiba unaohusu mambo ya Tanzania Bara.
Aidha, wajumbe wa Tume ya Mapitio ya Katiba ambao watatoka Zanzibar wahusike tu katika mchakato wa masuala ya kikatiba ambayo ni ya Muungano tu. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza wananchi wa Zanzibar washiriki katika kura ya maoni inayohusu mfumo mpya wa Muungano tu. Hii ndio kusema kwamba, kama vile ambavyo viongozi, wawakilishi na wananchi wa Tanzania Bara hawajashirikishwa katika mchakato wa kikatiba wa Zanzibar kwa sababu ulihusu mambo yasiyokuwa ya Muungano, vivyo hivyo viongozi, wawakilishi na wananchi wa Zanzibar wasishiriki katika mchakato wa kikatiba wa mambo yasiyokuwa ya kikatiba kwa upande wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuzingatia historia halisi ya Muungano wetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba wakati umefika kwa wananchi wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuamua - kwa mara ya kwanza katika historia yetu na kwa uhuru kabisa - kama wanataka kuendelea kuwa na Muungano na wa aina gani. Hili halijawahi kufanyika na ndio maana Muungano umeendelea kuwa kero kwa wananchi wengi wa nchi hizi mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba suala la ridhaa ya wananchi ni la umuhimu mkubwa na ni lazima lishughulikiwe kwanza kabla ya mchakato unaopendekezwa na Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba kuanza na/au kupitishwa.
Aidha, kwa kuzingatia historia yetu halisi ya kikatiba na kisiasa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mfumo mpya wa kutunga Katiba Mpya ambao hautatawaliwa na kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme. Kikubwa hapa ni kwamba, badala ya wajumbe wa Tume ya Katiba kuteuliwa na Rais kama inavyopendekezwa na Rasimu ya Muswada, wajumbe hao wateuliwe kutokana na mapendekezo ya vyama vya siasa, hasa hasa vile ambavyo vina uwakilishi Bungeni, taasisi zisizokuwa za kiserikali na za kitaaluma, makundi maalum ya kijamii pamoja na Serikali yenyewe. Aidha, badala ya Sekretariati ya Tume kujazwa warasimu wa Serikali ambao ni wateuliwa wa Rais kama inavyopendekezwa, Sekretariati hiyo itokane na wajumbe watakaoteuliwa na Tume yenyewe na ambao watawajibika moja kwa moja kwa Tume yenyewe badala ya kuwajibika kwa Rais kama ilivyo sasa.