Kwa rasimu hii muungano tunaunusuru au tunaudidimiza?

fellali

Member
Aug 14, 2013
17
2
Na Felix Mutalicious Lugeiyamu; 0712246001/ flugeiyamu@gmail.com

Ni kitambo sasa tangu suala la mchakato wa uundaji katiba mpya uwekwe wazi masikioni mwa watanzania. Suala ambalo watanzania waliahidiwa katiba mpya kupatikana ifikapo mwaka 2014 au kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mwanzoni lilianza kimasihala lakini sasa limepamba moto na kuonyesha uhalisia wa kupatikana kwa katiba mpya hiyo. Kimsingi ni kweli kabisa kuwa katiba iliyopo sasa inahitaji mabadiliko makubwa; lakini ni kweli tulihitaji kubadili katiba nzima? Lakini pia ni kweli watanzania walikuwa tayari kuibadili katiba yao?

Nauliza hivi kwasababu ni wazi kabisa kuwa asilimia kubwa ya watanzania hawa ambao wanaishi vijijini, ambao hawajui hata katiba iliyopo sasa inasemaje au inazungumzia nini ndio ambao mwenyekiti wa kuandaa rasimu ya katiba anadai amewahoji na kutoa maoni yao ya kimsingi? Wamejadili nini iwapo hata katiba iliyopo hawaijui?

Au ndo ilie ya kuelekezwa kitu gani waseme kama ilivyo kuwa kwenye baadhi ya maeneo ambapo wajumbe wa tume hiyo walipita? Au tuseme ndiyo wamesema hicho wanacho kijua swali linakuja je, walisema wanataka katiba yenye kuugawa muungano?

Kwa mujibu wa ripoti ya mwenyekiti wa tume ya kuaandaa rasimu ya katiba aliyoitoa mnamo tarehe 30/12/2013 inaonyesha kuwa takribani 61% kutoka Tanzania bara waliunga mkono hoja ya serikali tatu na 60% kutoka Zanzibar walipendekeza Muungano wa mkataba; ni wazi kuwa ripoti hiyo haionyeshi kiuhalisia wa jumla ya watanzania waliohojiwa na kutamka kwa vinywa vyao kuwa wanataka muundo wa serikali tatu.

Kwa mfano ripoti inasema "kwa Tanzania Bara wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni yao kuhusu Muungano na karibu 27,000 walizungumzia Muundo (Hawakusema kama wanataka serikali tatu).

Kwa Zanzibar karibu wananchi wote waliotoa maoni walijikita kwnye suala Muungano. Kati ya wananchi karibu 38000 waliotoa maoni, wananchi 19,000walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano (hawakusema kama wanataka serikali tatu)".

Sasa swali linalojitokeza ni je, hizi aslilimia zinzoonyesha kuwa idadi kubwa ya watanzania wanataka muundo wa serikali tautu inatoka wapi? Ukweli wa mambo unaonyesha kuwa, kimsingi ni kweli kamati teule iliwahoji watanzania takribani 333,516; kati hao watanzania 16,470 walipendekeza muundo wa serikali tatu, kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni yao kuhusu Muungano, 27,000 walizungumzia Muundo.

Kwa Zanzibar wananchi 19,000 walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano na wengi wakipendekeza muungano wa mkataba. Takribani wananchi 287537 hawakuzungumzia suala la muungano au muundo wa serikali tatu.

Sasa je, asilimia 61% inatoaka wapi amabyo inaunga mkono hoja ya muundo wa serikali tatu? Ni watanzania wapi wengi ambao wameonyesha nia ya kuwa na muundo wa serikali tatu?

Kimsingi tatizo langu hapa siyo tu serikali tatu, mbili au moja, ila je, kwa rasimu hii tuanalenga kuimarisha taifa letu lililo chini ya muungano au tunalenga kulibomoa? Na je kwa kuruhusu mfumo wa serikali tatu tutaweza kuondoa uozo uliopo?

Tusitumie siasa kwenye jambo ambalo linagusa uhuru na mustakabali wa taifa letu, maisha ya watanzania na maendeleo ya watanzania eti kwa lengo la kumfurahisha mtu au kikundi cha watu Fulani.

Ni suala lililo wazi kabisa kwamba kwa muundo huu wa katiba tuko tunaandaa mazingira ya kuuvunja muungano wetu uliodumu kwa muda mrefu sana na hivyo kulijengea taifa letu sifa lukuki mbele ya mataifa.

Ni kweli kabisa kuwa kwa muundo wa katiba hii tunaondoa U-tanzania na kurudisha U-tanganyiaka na U-zanziabar ambapo mwisho wa siku hatutauona U-zanziabar wala Utanganyika bali tutauona U-unguja na U-pemba, huku bara tutakuta U-zaramo na U-chaga na makabila mengineyo.

Sasa tukifikiapo, tutakuwa tumejenga au tumebomoa? Hivi waasisi wa muuungano huu wangekuwepo wangekubaliana na kinachotokea sasa?

Wangeuafiki muundo wa serikali tatu? Maana tusiwadanganye watanzania kwa maneno matamu ya kilaghai huku wakiukumbatia moto. Ni suala lililowazi kuwa Zanzibar ipo kwasababu ya Tanzania, vile vile Tanganyika ipo kwasababu ya Tanzania, nje ya jina TANZANIA kuna ukabila! na ndani ya ulabila hakuna nchi tena.

Hadi kufikia hapo mitafaruku, ugomvi na vita vitatuandama. Ikifika hiyo hatua Mzaramo haomruhusu mchaga afanye biashara kwake na ikiwa hivyo msemo wa kisiwa cha amani hautokuwepo tena bali kisiwa cha mitafaruku na vita ndiyo utapamba moto.

Hivi tujiulize, kwasasa tuko chini kofia ya Muungano wana Mtwara wanataka gesi iwanufaishe wao, sasa tukiwa nje ya Muungano tunafikiri mwana mtwara ndo atabadilisha mawazo? Mwalimu Nyerere aliwahi kulizungumzia suala hili na kimsingi hoja zake ziko sahihi kwani si tunaona ya Sudani Kaskazini na Kusini?

Bila shaka yalianza kama ya kwetu, Sudani kusini ikadai taifa huru kutoka Sudani ya Kaskazini lakini kilichotokea baada ya hapo nini? Hadi leo vita inashika hatamu. Nchi ya marekani imekuwa na nguvu na mabavu iliyonayo kutokana na Muunganiko wa nchi zaidi ya hamsini nab ado wako chini ya utawala wa Rais mmoja!

Na bado nchii inaendelea kuwa na nguvu kuliko taifa jingine lolote duniani kwasababu hakuna mmarekani hata mmoja anayetanguliza ubinafsi wa jimbo lake bali wote kwa nia moja wanatanguliza masilahi ya taifa zima la Marekani.

Wanania mamoja na kufanya mambo yao kwa umoja. Vipi ulaya; kama Marekani kama Ulaya. Tusidhani kwa kurejesha U-tanganyika na U-zanzibar kuwa tunauimarisha muungano au tunaleta maendeleo bali tutambue kabisa kuwa tunaibomoa nchi yetu wenyewe kwa mikono yetu wenyewe sawa na maandiko matakatifu yanavyosema "mwanamke mjinga huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe".

Kwa matazamo wangu sidhani kama watanzania waliowengi wanaafiki suala la muundo wa serikali tatu eti kwasababu mwenyekiti wa tume amesema. Sidhani kama takribani watu 16,000 elfu wanaweza kubeba haki za watanzania walio wengi.

Pengine hao wanaounga mkono muundo wa serikali Tatu ni wanasiasa amabo wameshindwa kushika hatamu kwa muundo uliopo hivyo wanatafuta njia mbadala ya kuwasaidia kufikia malengo yao binafsi?

Au pengine ni mkono wan chi bepari wanaolenga kuibomoa nchi yetu ili watutawale kiulaini kama ilivyokuwa Libya? Au pengine ni wanasiasa wanaolenga kuzimiliki mali asili za watanzania na hivyo wanaandaa mazingira kwa kuwatenganisha na kuwasambaratisha watanzania ili waweze kuzimiliki kwa urahisi? Au tunaandaa mazingira ya kuukaribisha ukoloni mambo leo?

Maswali haya yanajitokeza kutokana na hoja kuwa kwa kurejesha U-tanganyika na U-pemba na U-unguja ni sawa kurejesha ukabila. Japo, ni kweli kabisa kuwa kuna baadhi ya vitu vya kuendeshwa kisiasalakini siyo moyo wa taifa yaani KATIBA. Hivi kuna uharaka gani katika suala hili la uundwaji wa katiba mpya? Kwani lazima iwe kabla ya 2015?

Kwani isipokuwa tayari 2015 nini kitatokea? Kwani hili taifa linaama kwa hiyo tuseme kuwa tufanye haraka kabla halijaondoka? Tuwaache watanzania wajadili rasimu hii kwa undani na umakini sana ili wapate kutoa maoni yanayokidhi haja zao.

Kimsingi kuna baadhi ya vitu havijawekwa wazi kwenye rasimu hii ikiwa ni pamoja na serikali ya Tanganyika ambayo haipo na kama ilikuwepo awali tiyari imeishapotea na hivyo inahitaji kuandaliwa upya, na haijulikani muundo wake utakuwaje?

Rasimu mpya inasema kuwa serikali hii itakuwepo iwapo tutaafiki suala la serikali tatu,. Hivi ni binadamu anayeweza kuambiwa aamue kwa ajili ya jambo ambalo hajui mwanzo wala mwisho wake utakuwaje?

Kama tume ingetaka serikali tatu ni vyema ingejikita kwenye pande zote kama ilivyojadili kwa Zanzibar. Hivi kweli watanzania hapa inatupasa kuwa makini kwamba tunaambiwa kuwa hadi 2015 katiba mpya itakuwa tayari, wakati huo huo tunaambiwa itachukua mwaka mmoja hadi katiba ya Tanganyika ikamilike na kuanza kutumika, sasa je kama uchaguzi unafanyika 2015, Tanganyika itamchagua nani na kwa katiba ipi?

Je ataongoza kwa kusimamia misingi ipi? Atakuwa katika ofisi zipi (Ikulu ipi)? Atachaguliwa ili aiongoze serikali gani? Labda tuachane na hilo, vipi kuhusu Jeshi kwa maana ya Jeshi la Wananchi na lile la kujenga Taifa? Ni ukweli usiopingika kuwa majeshi yaliyopo sasa yapo chini ya kivuli cha muungano. Sasa je, iwapo tukiwa na serikali tatu, majeshi haya yatagawanywa kwa uwiano sawa kwa serikali tatu au yatabaki chini ya kivuli cha muungano na hizi serikali mbili zitaunda majeshi yake?

Maana hakuna maana ya kuwa na serikali kama huna jeshi lolote la ulinzi, yaani haileti maana eti Tanganyika iwe ni nchi yenye raisin a katiba lakini haina jeshi la ulinzi vile vile kwa Zanzibar! Au utakuwepo mchezo wa kuazimana majeshi pindi inapohitajika? Na mfumo wa mahakama utakuwaje? Kama haitoshi, tujiulize Ikulu ya Tanganyika itakuwa wapi?

Tutajenga mpya au Rais wa Jamhuri ya Muungano atatumia ofisi moja na wa serikali Tanganyika? Makao makuu ya serikali ya Tanganyika yatakuwa wapi na Muungano wapi? Lakini tusisahau kuwa majengo mengi sasa yanayotumika kwa ajiri ya wizara na taasisi za kiserikali zipo chini ya kivuli cha muungano, sasa je, nje ya muungano tunajenga upya miundo mbinu ya seriakali ya Tanganyika ambayo haipo sasa?

Hivi kipato cha kuandaa miundo mbinu kwa ajili ya serikali ya Tanganyika kitatoka wapi? Sanjali na hili tukumbuke kuwa serikali yetu iliyo madarakani sasa ipo chini ya kivuli cha muungano na ukweli usiopingika kuwa ina dimbwi la madeni, sasa je, dimbwi hilo la madeni atabebeshwa nani? Ni serikali ipi kati ya tatu itahusika kulipa madeni hayo? Na itayalipa kwa mfumo gani?

Kimsingi maswali ni mengi sana juu ya rasimu hii ya katiba na kiukweli kila swali moja linazaa swali jingine na hivyo kuongeza sintofahamu ndani ya vichwa watanzania wenye fikra kama zangu.

Ni mtazamo wangu uliowazi kabisa kuwa, rasimu hii ya katibaisingejikita zaidi kwenye muundo wa serikali tatu badala yake ingesisitiza kwa zaidi maswala nyeti kama vile mali asili za taifa na mgawanyo wake kwamba nani atafaidika na nini, haki za binadamu, majukumu ya Rais hasa kwenye uteuzi.

Lakini pia lingekuwa jambo la busara iwapo rasimu hii ingependekeza mfumo wa majimbo badala ya mikoa ili kutengeneza mfumo ambao ungelenga kudumisha muungano kwa kupendekeza mfumo wa serikali moja badala ya tatu kama inavyopendekeza.

Ni imani ya mtazamo wangu kuwa, ni heri kuwa na mfumo wa serikali moja yenye Rais moja na makamu wa Rais wawili yaani mmoja bara mwingine visiwani na majimbo ambayo yangewakilishwa na mbuge mmoja kutoka kila jimbo au maseneta sawa na marekani ilivyo. Unajua ni ngumu sana kuwa na tawala mbili ndani nchi moja.

Maana wananchi itafika wakati wananchi watashindwa kuelewa wamsikilize yupi? Lakini pia hata viongozi wenyewe itafika wakati watashindwa kuelewana. Hoya yangu ya msingi ni kwanini serikali tatu? Kwanini siyo moja?

Tusitake kudanganyana hapa, bajeti zetu za kila mwaka zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya bajeti inajikita kwenye matumizi ya serikali kuliko maendeleo, na hapo tukumbuke niserikalimbili tu, je, zikiwa tatu?

Labda najiuliza maswali yote haya kwasababu asilimia kubwa ya watnzania tumezaliwa ndani ya muungano na tunaishi ndani ya muungano na hivyo kusindwa kutambua nje ya muungano kuna nini? Ni hofu hiyo inayonipa mtazamo wa kwamba katiba yetu ingelenga kuuboresha muungano na siyo kuusambaratisha ili kudumisha amani iliyopo sasa.

Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa dini wamenukuiwa wakipinga suala la Muundo wa serikali tatu, baadhi ya wanataaluma na wananzuoni wamenuuiwa pia kwenye vyombo vya Habari wakipinga suala la muundo wa serikali tatu, hata baadhi ya wananchi wamenuuiwa wakipinga suala hili la mfumo wa serikali tatu; sasa je, mwenyekiti wa tume ya rasimu ya katiba anaripo vipi kuwa watajwa hapo juu wanakubali suala la muundo wa srikali tatu?

Binafsi, ni imani yangu kuwa watanzania walio wengi hawapo tayari kuishi nje ya muungano au ndani ya muundo wa serikali tatu. Kwahiyo, wanasiasa wasitumie maslahi yao binafsi katika kuwashawishi watanzania waliowengi kuwasaidia katika kutimiza ndoto zao. Ni vyema tutanguliza maslahi ya utaifa hasa muungano kuliko jambo linguine lolote.

Hivi tujiulize kama mtu ameshindwa ndoa ya mke mmoja atawezaje kuimiliki ndo ya wake wawili? Huu ndiyo wakati muafaka wa watanzania kufanya maamuzi yaliyo sahihi kwa kutenganisha jema na baya.

Tusilaghaiwe na maneno matamu ya kisiasa au ya wanasiasa maana yakianza kutukuta wao hawatakuwepo kutusaidia nap engine watakuwa ughaibuni.

Kama mwalimu Nyerere alivyosema "mchawi anaekula nyama hawezi kuacha hata siku moja"; tulianza kwa kutupa kando Azimio la Arusha, tukatupia mbali baadhi ya misingi ya Taifa na sasa tuaelekea kulivinja na kulisambaratisha Taifa letu kwa kuruhusu mfumo wa serikali tatu bila ya kuzingatia kuwa kwa kufanya hivyo tunapunguza nguvu ya taifa na hivyo kuruhusu ukoloni mambo leo kuzidi kupamba kasi.
 
Mueka mada,muungano sio lazima iwe kwa zanzbr tu bali hata msumbiji na malawi mnaweza kuungana nao,miaka 50 tayari na hakuna kimoja cha faida kwa mzanzibr kwenye huu unaouita muungano,tumechoka kutawaliwa na mkoloni tanganyika kupitia koti la muungano,zanzibr kwanza.
 
Back
Top Bottom