Kwa nini mnasema CCM ni wanafiki?

Emashilla

Senior Member
May 24, 2012
138
0
CCM ni wanafiki, wanalia kinafiki

Bwana Mdogo


UNAFIKI ni mbaya, haufai. Kama unafiki ni mbaya basi mnafiki pia ni mbaya na hafai.

Ubaya wa mnafiki ni kwamba unakula naye, unaishi naye, unamwamini sana na unacheza naye.

Mnafiki anakutoa hofu, ikitokea unalia kwa kufiwa au matatizo yaliyokukuta naye atalia sana ili aonekane ana uchungu.

Mnafiki anaweza kuwa kiongozi. Watanzania wameishi na wanafiki kwa muda mrefu na kuwaamini kuwa watu au viongozi wa maana kumbe wapi, wanazuga.

Mfano, hivi sasa Watanzania wana vilio vingi. Wanalia kwa masikitiko na kwa uchungu wa maisha magumu, lakini wanafiki Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanalia na kuteka machungu wakidai wanaleta Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania.

Siku za kuumbuka zimewadia. Kwa muda mrefu kuna kilio cha baadhi ya viongozi wakuu na waandamizi kutorosha raslimali za nchi, wanyama, pembe za ndovu, fedha na kupeleka nje.

CCM wakaonyesha uanafiki wao. Kwanza, mawaziri wa serikali walifanya kazi ya ziada kuzima bungeni hoja ya kufuatilia mabilioni ambayo magazeti ya Ulaya yanadai zinafikia Sh. 300 bilioni. Pili, waliposhindwa katika mkakati huo, sasa wanapita mikoani kueleza ugumu wa kurejeshwa fedha hizo.

Unafiki wa CCM hauko katika mabilioni hayo tu bali hata yale yaliyozamishwa katika miradi kadhaa nchini kama vile Meremeta/ Tangold na hata yaliyochotwa kupitia kampuni ya Kagoda.

CCM hawalii kilio kimoja na wananchi ndiyo maana hawataki kuyapatia ufumbuzi matatizo, kero ya ardhi, wizi wa raslimali ya umma, maliasili na ufisadi katika mikataba ya migodi.

Hebu tujikumbushe tatizo la eneo la Loliondo. Je, una habari kuwa baadhi ya wajumbe wa sekretarieti mpya ya CCM walihusika na matatizo ya kudumu ya wananchi wa Loliondo? Basi jikumbushe.

Mwaka 1988 gazeti la Serikali, Sunday News, liliandika kwa ujasiri mkubwa habari kuhusu uwindaji mbaya uliokuwa ukifanywa nchini Sudan na famila za kifalme kutoka Mashariki ya Kati.

Habari ile ilitabiri ujio wa wawindaji hao wenye wazimu Tanzania. Ilisema pia kuwa wawindaji wale waliua wanyama 200 katika pori la Masai Mara, Kenya, mwaka 1987.

Wafalme walitumia silaha za kivita na magari kufukuza wanyama kwa mbio kiasi cha kuwafanya wanyama waendao kwa kasi sana kama swala na ndege kama mbuni kuchoka hadi kusimama (Sunday News [Dar es Salaam] Februari 21, 1988).

Huo haukuwa utabiri. Tayari wafalme hao walikuwa Tanzania tangu katikati ya miaka ya 1980.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Otterlo Business Corporation Ltd., Isaack Mollel, aliweka bayana jambo hili katika wasifu wa kampuni hiyo aliouandika Februari 2007. Mollel alisema kuwa Mohamed Abdulrahim Al-Ali alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza Septemba 1985.

Alisema Al-Ali alirudi tena Oktoba 1987 na kuwinda wanyamapori kwa siku saba. Julai 1990 Al-Ali alirudi tena kuwinda katika Pori Tengefu la Lolkisale. Alirudi tena Desemba 1990 na safari hii aliwinda katika Pori Tengefu la Longido linalopakana na Pori Tengefu la Loliondo.

Jarida la New York Times liliandaka habari iliyosema kwamba wawindaji kutoka familia ya kifalme ya Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu waliwinda wanyama nchini Tanzania kikatili.

Wanyama hao ni pamoja na waliokuwa katika hatari ya kutoweka kama duma na mbwa mwitu (New York Times [New York] Novemba 13, 1993).

Januari 20, mwaka 1993 gazeti la Mfanyakazi lilichapisha habari yenye kichwa cha habari Tanzania inavyoliwa na Waarabu. Huu ndiyo ulikuwa mwanzo wa makala mfululizo zilizompa umaafuru hayati Stanley Katabalo.

Makala zile ndizo zilionyesha kuhusika kwa viongozi wetu katika ufisadi wa raslimali za nchi kwa kivuli cha uwekezaji.

Katabalo aliandika kwamba tarehe 18 Januari 1993 dege kubwa lenye namba za usajili A6-HRM kutoka Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu lilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Dege hilo, alidai lilikuja kuwachukua wana wa mfalme na mawindo yao pamoja na wanyama waliowakamata wakiwa hai.

Wana wa mfalme hao walisindikizwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakati huo, Abdulrahman Kinana na Meja Jenerali Gideon. F. Sayore.

Ilidaiwa kuwa maafisa hawa waandamizi wa Jeshi na Serikali walikuja 'kulainisha' safari hiyo (Mfanyakazi [Dar es Salaam] Januari 20, 1993).

Alipobanwa na vyombo vya habari, Waziri wa Utalii, Maliasili na Mazingira, wakati huo, Abubakar Mgumia, alikiri kuwa wana wa mfalme wale walifanya uhalifu na uharamia mkubwa.

Alisema waliwinda wanyama wengi kuliko waliokuwa wameruhusiwa na Serikali. Waliwakamata wanyama hai kinyume cha sheria na Mgumia alikiri pia kuwa baadhi ya wanyama wale walifia KIA (Sunday News [Dar es Salaam] Machi 21, 1993).

Ukweli Tarehe 11 Novemba 1992, Waziri Mgumia ndiye alimpa, Brigadia Mohamed Abdulrahim Al-Ali, wa Dubai, kibali cha uwindaji kinyume cha sheria, ili awinde katika Pori Tengefu la Loliondo kwa miaka 10, kuanzia tarehe 1 Januari 1993. Waziri alivunja sheria.

Mkurugenzi wa Wanyamapori wakati huo, Muhidin Ndolanga, alipinga kwa kadri ya uwezo wake uharamia huo na aliapa kwamba atapambana nao hadi mwisho.

Ndolanga alisema haingii akilini kulipokonya shirika la umma ‘Tawico’ eneo, tena kwa kuvunja sheria; yaani kumpa mtu binafsi asiye na kampuni na tena kwa miaka 10. Ndolanga aliapa pia kuwa wanyamapori Loliondo wangeendelea kuwa salama mikononi mwa Tawico.

Ndolanga hakufua dafu, msukumo kutoka Ikulu, wakati ule, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, ulikuwa mkubwa sana. Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipewa amri ili amwamuru Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Leban Makunenge, ahakikishe haraka kuwa vijiji sita vinatia saini mkataba wa kumruhusu Brigadia Al-Ali kuwinda kwa miaka 10 Loliondo.

Tarehe 20 Novemba 1992, ikiwa ni ndani ya siku 10 tu toka Waziri Mgumia alipompa kibali cha uwindaji Brigadia Al-Ali kinyume cha sheria, mkataba uliwekwa saini na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa Mbunge wa kwanza wa Ngorongoro, Moringe ole Parkipuny, viongozi wa vijiji sita walikataa katakata kuridhia Brigadia Al-Ali kuwinda kwenye ardhi ya vijiji vyao.

Ukweli aliyetia saini kwa niaba ya vijiji sita alikuwa Richard Koillah Mbunge wa Ngorongoro. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Leban Makungenge, alitia saini kwa niaba ya Serikali Kuu. Al-Ali aliwakilishwa tu.

Tarehe 1 Aprili 1993, Serikali ilitangaza kuwa Pori Tengefu la Loliondo litakuwa rasmi mikononi mwa Brigadia Al-Ali.

Viongozi wa vijiji sita vilivyopo kwenye Pori Tengefu la Loliondo walikataa kuwa wameridhia uharamia huo. Serikali ilikataa kuwasikiliza. Waziri Mgumia akauambia ulimwengu kuwa Serikali inampa upendeleo maalum Brigadia Al-Ali kwasabubu ni mkarimu sana (Sunday News [Dar es Salaam] Machi 21, 1993).

Tarehe 17 Aprili 1993 Rais Mwinyi alimwondoa Waziri Mgumia kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida na nafasi yake ikachukuliwa na Juma Hamad Omari (Sunday News [Dar es Salaam] Aprili 18, 1993).

Baada ya kifo cha Katabalo, kashfa ya Loliondo ilikosa mwandishi jasiri na karibu ikasahaulika. Aprili mwaka 2000 wafugaji wa jamii ya Kimaasai waliwatuma wajumbe 13 wakiongozwa na kiongozi wa mila, Sandet ole Reya, kwenda Dar es Salaam kukutana na Rais Benjamin Mkapa atatue mgogoro huo.

Wajumbe wale hawakumwona Mkapa. Walipata bahati ya kuzungumza na waandishi wa habari MAELEZO. Jenerali Ulimwengu aliwaalika katika kipindi cha Jenerali On Monday, Channel Ten.

Wazee wale walirejea Loliondo wakiapa kupambana hadi mtu wa mwisho (Guardian [Dar-es-Salaam] Aprili 11, 2000). Waziri wa Maliasili na Utalii, wakati huo Zakia Megji, alikanusha taarifa za vyombo vya habari kuwa OBC inakiuka haki za binadamu, inawinda wanyama kinyume cha sheria na imejenga Loliondo.

Haishangazi kwa nini mwaka jana walitoroshwa ndege na wanyama 130 kwa ndege kubwa ya kijeshi ya Qatar inayojulikana kama Emir Air Force. Serikali na CCM wako kimyaaaaaaaaaaaa ila wanabadili sekretarieti tu.


Source: Tanzania Daima, 28 November 2012
 

Miwatamu

JF-Expert Member
Oct 2, 2012
1,451
1,170
Je, wana kumbukumbu ya haya yote? Kwa kweli makala hii imenikumbusha sana mzee wangu Katabalo (R I P)
 

Emashilla

Senior Member
May 24, 2012
138
0
Naona hapa mambo ni mazito sana. Je! unafiki unatokana na wao kupoteza kumbukumbu au hawajui kuwa mengi yamehifadhiwa tu? Wanalia au wanacheka? Mimi sijui ila swali langu kwenu linabaki kama lilivyo mpaka mnijibu:- KWA NINI MNASEMA CCM NI WANAFIKI?
 

hakisoni

JF-Expert Member
Oct 13, 2012
476
225
mie kwa mtizamo wangu mambo yote yanayofanyika mazuri kwa mabaya katika taifa hili yanaonekana vizuri na wahusika wapo sana nao ni washika dau yaani ni members wa ccm, issue ya unafiki inakuja hivi kwa mtizamo wangu nani amfunge paka kengele?? issue kafanya fulani anajulikana hakuna wa kumsema kama ilivyo wapinzani wanavyoanika uozo huu, Niwakumbushe kidogo mnakumbuka ule usemi wao hapo nyuma kidogo, ccm imeshika hatamu ya uongozi na utamu?
 

cedrickngowi

Senior Member
Jun 9, 2012
148
0
Niliwahi kusema hapa kuwa matatizo yetu kama Tanzania ni mengi kuliko tunavyoyaona,Tatizo ni kwamba kila kitu kilifanyika huku hata wahusika wakijua ni makosa na hasara zake ni zipi.We need active civil society to change this,Tunahitaji kubadili mfumo mzima wa uongozi wa nchi hii hasa chama tawala maana ilipofikia hata wale wasafi hawawezi kukemea chochote kwani dhana ya uwajibikaji bado kwao ni msamiati mgumu sana.Na ndio maana wanahofia chama kingine kuchukua dola maana yote haya yatafufuliwa.Tafakari............
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom