Kwa MAONI haya KATIBA MPYA ni ndoto, mpaka KUCHIMBIKE

NYAMKANG'ILI

JF-Expert Member
Apr 1, 2012
223
112
MAONI YANGU KUHUSU KATIBA MPYA

1) MUUNGANO

Hakuna ubishi kuwa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni wa kipekeekatika Afrika na Dunia nzima. Upekee wa muungano huu hautokani tu na nchi kubwa kieneo, Tanganyika, kuungana na nchi ndooogo sana kieneo, Zanzibar, au kwamba ni muungano uliodumu katika Afrika kwa miongo mitano sasa; bali upekee wa muungano huu unatokana na mambo mawili makubwa: (1) muungano kutodhihirisha faida yake yoyote kwa wananchi wasio viongozi na, hata hivyo, bado sehemu kubwa ya wananchi kuendelea kuukubali – hili ni jambo la kipekee; na (2) matatizo lukuki, yamebatizwa jina kero za muungano. Kero za muungano zimekuwa zikijijenga katika ngazi zote za jamii, kutokana na Serikali kuufanya muungano kuwa ‘fumbo la imani’. Muungano ni kero kwa wananchi wa kawaida, wanasiasa, baadhi ya viongozi; na unakera hata imani za kidini za watu wengine wanaoamini kwamba isingekuwa muungano wangekuwa waamini zaidi (hili ni upuuzi mtupu). Kutokana na ukweli kwamba pamoja na muungano kutokuwa na faida yoyote na kuwa na kero lukuki, wana wa Tanganyika na Zanzibar wamekubali au wanaonekana kama wamekubali kuendelea kuishi na muungano mgongoni mpaka mbeleko itakapochanika. Wakati huu tunaposubili mbeleko kuchanika au muungano kushushwa mgongoni ili utembee au uchechemee, Maoni yangu kuhusu muungano ni:

(i) Muungano uwe wa yale mambo 11 tu ya muungano kama yalivyoasisiwa mwaka 1964; (ii) Serikali ya Tanganyika ifufuliwe ili kushughulikia mambo yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanganyika;

(iii) Gharama za kuendesha muungano zieleweke, na kanuni ya kuchangia gharama hizo kati ya Tanganyika na Zanzibar ziwekwe wazi;

na
(iv) Elimu juu ya umuhimu wa muungano, kama umuhimu huo upo kwa wananchi wa kawaida, itolewe ili wananchi wauunge mkono.

2) MAMLAKA MAKUBWA YA RAIS, WAZIRI MKUU ASIYE NA MAMLAKA

Mamlaka na madaraka ya Rais wa Tanzania kwa sasa ni kufuru. Rais ni Mungu mtu. Rais anaumba (mikoa, wilaya, wizara, idara za Serikali na mengine mengi), anaua (anafuta) au akipenda anarefusha maisha (msamaha wa Rais); hashitakiki, akiiba bado atapeta bila tatizo lolote; anaweza kuteua yeyote kuwa mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, Balozi, au Jaji bila hata kuwa mwanasheria: kama atakavyoona inafaa. Madaraka yake ni hatari kwa mustakabali na uhai wa taifa, hasa wakati huu ambapo imedhihirika kuwa u-Rais unanunuliwa gulioni kupitia mitandao ya wanasiasa. Mamlaka ya uteuzi aliyonayo sasa Rais ndiyo yanayosababisha mitandao hii kujijenga. Wakati hali ikiwa hivyo, Waziri Mkuu anashindwa kutekeza majukumu yake kwa kukosa madaraka ya kutekeleza majukumu yake. Maoni yangu ni kuwa hatuwezi kuendelea kuweka nchi rehani kiasi hiki, kwa hiyo:

(i)
Idadi na majina ya wizara za serikali itajwe ndani ya Katiba itakayoundwa. Wizara ziwe 16 tu nazo ni (1) fedha, mipango na uchumi; (2) elimu; (3) mambo ya ndani; (4) ulinzi; (5) afya na ustawi wa jamii; (6) maji, nishati na madini; (7) mambo ya nje; (8) serikali za mitaa; (9) viwanda na biashara; (10) kilimo, ufugaji na uvuvi; (11) maliasili na utalii; (12) utafiti, sayansi na teknolojia; (13) maadili na utawala bora; (14) haki, katiba na sheria; (15) ardhi na ustawishaji makazi; na (16) ujenzi, usafirishaji na miundombinu. Wizara zitaongozwa na waziri mmoja kwa kila wizara na naibu waziri mmoja kwa kila wizara watakaoteuliwa na Waziri Mkuu, na kabla ya kushika madaraka watathibitishwa na Bunge kwa kuulizwa maswali yatakayohusisha taaluma na maadili yao na baadaye kupigiwa kura (siyo kutikia ndiyo au hapana);


(ii)
Rais ateue Waziri Mkuu Mtendaji. Waziri Mkuu awe ndiye kiongozi wa Serikali na awajibike kwa Bunge. Shughuli ya Bunge kuthibitisha mteule wa Rais kuwa Waziri Mkuu ichukue angalau wiki moja, kutokana na unyeti wa kazi za Waziri Mkuu, awekwe kiti moto cha ukweli siyo bora tu aonekane amethibitishwa;


(iii) Kuwepo na Tume ya Ajira itakayohusika na ajira zote katika utumishi wa umma kuanzia kwa mfagizi hadi mkurugenzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP; isipokuwa, makatibu wakuu wa wizara na mabalozi, ambao, napendekeza wateuliwe na Waziri Mkuu kutoka kwenye orodha ya washindani iliyochujwa na Tume ya Ajira na wathibitishwe na Bunge kama ilivyo kwa mawaziri. Kazi zote katika utumishi wa umma zitangazwe na watu washindane kwa uwazi kuzipata;

(iv) Rais ateue wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, kutoka kwenye orodha iliyopendekezwa na Kamati ya Ajira ya vyombo vya ulinzi na usalama, na wathibitishwe na Bunge;

(v) Kusiwepo na wabunge wa kuteuliwa na Rais au na mtu mwingine ye yote;
(vi) Rais asiwe na mamlaka ya kuvunja Bunge isipokuwa tu pale linapokuwa limemaliza uhai wake wa miaka mitano; na
(vii) Rais awe mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu; wakati Waziri Mkuu awe mkuu wa Serikali.

3) VITA DHIDI YA UFISADI

Kwa sasa katika nchi yetu hata jambazi anaweza kabisa kuwa Rais au Mbunge kwa kutumia fedha na mitandao ya kifisadi. Sasa ni wakati muafaka wa kuziba mianya hiyo kupitia mchakato wa Katiba mpya. Maoni yangu kuhusiana na suala hili ni:

(i) Katiba ielekeze vyama vya siasa kuanzisha mchakato wa kupata wagombea wao wa nafasi za u-Rais na u-Bunge miaka miwili kabla ya siku ya uchaguzi mkuu unaofuata ili wananchi wapate nafasi ya kuwajadili, kuwahoji, kuwafahamu, kutambua watu walio nyuma ya wagombea hao – yaani kuweka mambo hadharani. Hili litasaidia kuepuka mitandao ya kifisadi inayofadhili wagombea gizani kwa manufaa yao na kujua mipango ya maendeleo wanayosimamia;

(ii) Sekreteriati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ielekezwe na katiba kuweka wazi taarifa yake ya mwaka itakayoonesha majina ya viongozi ambao hawakuzingatia sheria ya maadili ya umma kila ifikapo Julai mosi ya kila mwaka, na kwa hiyo kwa mujibu wa katiba kukosa sifa za kuwa viongozi, na nafasi zao kuwa wazi. Sekreteriati isipofanya hivyo, katiba itamke kuwa mwenyekiti na wajumbe wake nafasi zao ziwe wazi kuanzia Julai 2. Hayo yakitokea timu mpya ya sekreteriati iundwe ndani ya miezi miwili na timu hiyo itoe taarifa ya maadili ya viongozi ndani ya miezi sita tangu kuundwa kwa sekreteriati mpya;

(iii)
Sekreteriati ianze kujishughulisha pia na maadili ya wakuu wa makampuni na taasisi binafsi; na


(iv)
Katiba ianishe sera za taifa ambazo vyama vya siasa vitatakiwa kutengeneza mikakati ya kuzitekeleza kupitia ilani zao za uchaguzi; ili kuondokana na hali ilivyo hivi sasa ya kila chama cha siasa kutengeneza sera zake jambo ambalo linasababisha ufisadi wa ahadi hewa wakati wa uchaguzi.

4) MAHAKAMA

Mahakama ipo na inafanya kazi nzuri. Ufisadi ndilo tatizo kubwa katika mahakama zetu. Maoni yangu ni:

(i) Nafasi za u-Jaji zitangazwe na watu washindane kupitia mchakato wa wazi kuzipata kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama. Jaji Mkuu anaweza kuteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa majina matatu ya washindani waliopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama;

na
(ii) Kuwepo na mfumo wa mahakama – kwa mambo yasiyo ya muungano – wa Tanganyika kuanzia chini hadi mahakama ya juu kabisa ya rufani, na Zanzibar vivyo hivyo. Kisha kuwepo na mfumo wa mahakama wa Jamhuri ya Muungano utakaohusika na mambo ya muungano tu.

5)
BUNGE

Bunge letu ni kubwa mno. Ukubwa huu umesababisha kuibuka kwa ‘ulipuaji’ wa mijadala kwa lengo la kufanya wabunge wengi zaidi kuchangia, na hivyo tija kutoonekana. Bunge pia limekaliwa kooni na Rais na siasa za vyama vinavyowakilishwa na wabunge husika. Wabunge wanajali sana vyama vyao kuliko wananchi, mwananchi ni mtu wa mwisho kabisa kwa mbunge wa chama. Maoni yangu ni:

(i) Kuundwe Bunge la Tanganyika;

(ii) Watu binafsi waruhusiwe kugombea u-Bunge na u-Rais, isiwe lazima kuwa mtu wa chama kugombea nafasi hizo;

(iii) Idadi ya wabunge iwe 200, watawakilisha wilaya 75 zitakazoundwa Tanzania Bara yaani kila wilaya wabunge wawili (mwanamke na mwanaume – usawa wa kijinsia), na wabunge 50 kutoka Zanzibar;

(iv) Kuwepo na mambo ya kikatiba ambayo Bunge halina mamlaka ya kuyafanyia mabadiliko (The doctrine of basic structures, entrenchment) bali kura ya maoni ndiyo itumike kufanyia mabadiliko mambo hayo. Mambo hayo yajumuishe mambo ya muungano, kuongeza maeneo ya utawala na mambo mengine ya msingi; ili kuondoa uchezeaji wa katiba wa mara kwa mara kwa vyama vinavyokuwa madarakani;

(v)
Spika na Naibu Spika wasiwe wanachama wa vyama vya siasa;

(vi) Mtu aruhusiwe kugombea udiwani, ubunge na urais kwa wakati mmoja na, ikiwa atachaguliwa u-Bunge na u-Rais atachagua nafasi gani aitumikie na ile atakayoiacha wazi itazajwa kwa mujibu wa sheria ; na
(vii) Mbunge akifukuzwa na chama chake aendelee kutumikia wananchi kama Mbunge na iwe hivyo kwa Rais na diwani.

6) SERIKALI ZA MITAA

Serikali za mitaa sasa hivi, kwa jinsi zilivyo, ninazifananisha na mtu mwanaume na mtu mwanamke wanaoamua kufunga ndoa huku mahitaji yao ya kila siku kuanzia chakula, mavazi na malazi yakitolewa na mtu mwingine mwanaume. Ndoa ya namna hiyo inaelea angani, haina msingi na ni dhaifu mno kwa vile wanandoa hawawezi kujiendesha: serikali za mitaa za Tanzania nazo ziko hivyo. Serikali za mitaa, hasa halmashauri zetu hazina uwezo wa kujiendesha kimapato kwa sababu tunaunda vihalmashauri vidogovidogo mno, na sasa vinaundwa hata viwilaya na halmashauri za kabila moja. Nilipata kuambiwa kuwa Waafrika wanamzio (allergy) na vitu vikubwa, eti wao ni wa vitu vidogovidogo. Sasa naamini maneno hayo, kwani watu wanasema ‘Mkoa/Wilaya/kata/kijiji XYZ ni kikubwa mno, kigawanywe.’ Kwa hiyo sisi ni watu wa kugawanya maeneo kila siku ili vipatikane vitu vidogo vidogo saizi yetu, ni hatari. Mtindo huu ni hatari kwa sababu unarudisha ukabila, udini na ukanda kwa kasi ya kutisha. Pia halmashauri hizo hazina uwezo wa kiraslimali wa kujiendesha, na sasa, halmashauri zinategemea bwana mkubwa (big brother) Serikali Kuu ya magogoni kutekeleza majukumu yake. Halmashauri hazina uwezo hata wa kujenga vyumba viwili vya madarasa kutokana na mapato yake kwa mwaka wa fedha wala haziwezi hata kuzoa taka – ni hatari. Maoni yangu ni:

(i) Tanzania Bara nzima iwe na mikoa 15 itakayoongozwa na wakuu wa mikoa wa kuchaguliwa na wananchi kwa kura za wengi. Kila mkoa uwe na wilaya tano tu zitakazoongozwa na wakuu wa wilaya wa kuchaguliwa na wananchi kwa kura. Utaratibu wa sasa wa wakuu hawa kuteuliwa ufe kwani hauna tija kwa taifa;

(ii) Mikoa na wilaya ziwe na mamlaka kamili ya kuendesha shughuli zao kwa kutumia vyanzo na mapato vya maeneo husika. Serikali Kuu itoe ruzuku kwa serikali za mitaa kwa kutumia vigezo vya wazi kama vile idadi ya watu, raslimali za eneo husika, ukubwa wa eneo, umaskini wa wananchi wa eneo husika na vipaumbele na sera za taifa;

(iii)
Kila wilaya iwe na kata tano zitakazotoa madiwani wanne wanne, wanawake wawili na wanaume wawili (usawa wa jinsia), kuwakilisha wananchi katika halmashauri za wilaya. Kila kata iwe na vijiji viwili tu;

(iv) Idadi ya maeneo ya utawala itajwe ndani ya katiba na mabadiliko yake, pale yatakapohitajika, yafanywe kupitia kura ya maoni;
(v) Ngazi ya utawala ya tarafa ifutwe;
(vi) Madiwani walipwe mshahara, posho na marupurupu sawa na ya mkuu wa idara za halmashauri; na
(vii) Meya wa mji, jiji au halmashauri achaguliwe na wananchi kwa kura na yeye ndiye aunde na kuongoza halmashauri.

7) HAKI ZA BINADAMU, ULINZI NA USALAMA

Imedhihirika sasa hivi kwamba Serikali imeviacha vyombo vyetu vya dola kutekeleza majukumu yake kisheria bila aina yoyote ya udhibiti wa nje ya vyombo hivyo. Hilo ni jambo zuri. Hata hivyo, kutokana na uhuru huo, sasa vyombo hivi vinatekeleza asilimia ndogo sana ya kazi za Jamhuri, na muda mwingi wanatumia kusaka pesa zisizo halali. Sasa hivi vyombo vya dola hasa polisi, vinaona kutekeleza shughuli za umma kama vile ni mzigo – siyo kipaumbele chao. Kipaumbele ni pesa. Baada ya kujengeka kwa saikolojia hiyo ndani ya vichwa vyao, sasa askari kwenda kusimamia mkutano wa hadhara anaona ni karaha kwake, anaenda akiwa tayari amekasirika kwa sababu anaona kuwa kazi hiyo kwake haina manufaa, haina pesa. Tabia hii imesababisha kuzuka kwa hali ambayo sasa hivi polisi akiitwa kutekeleza majukumu yake ya kisheria, yeye anaenda kumimina risasi kwa waandamanaji, watuhumiwa wa uhalifu na hata kwa raia wema tu: polisi wanatumia mabavu pasi sababu za msingi. Polisi hawatii sheria, wanahitaji shuruti. Lakini, nani awashurutishe kutii sheria? Tume ya Haki za Binadamu iko katika usingizi wa pono, haitekelezi majukumu yao. Ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama ni za kindugu sana: kama huna ndugu yako TISS basi huwezi kupata ajira humo hata siku moja. Polisi na JWTZ nako hali si shwari, kwenda kamisheni (kupata mafunzo ya nyota) ni kwa kujuana zaidi kuliko uwezo wa mhusika. Maoni yangu ni:

(i) Katiba iunde kamisheni ya malalamiko ya wananchi kwa polisi (Independent Police Complaints Commission – IPCC). Kamisheni hii iwe na mamlaka ya kuchunguza, na kuchukua hatua dhidi ya polisi pale kunapokuwa na malalamiko. Watu wanalalamikia polisi kila siku. Polisi wanaolalamikiwa wanaunda timu za kujichunguza, unategemea nini? Hakuna kitu. Watu wanauwawa na polisi kwa madai kuwa ni majambazi; watu wengine wanabisha kwamba waliouwawa si majambazi: habari inaishia hapo, hakuna mtu wa kutegua kitendawili hiki. IPCC izibe mwanya huu;

(ii) Katiba iunde Kamati ya Ajira ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama yenye majukumu sawa na Tume ya Ajira za serikalini; na

(iii) Nafasi ya IGP itangazwe na watu waombe, mchujo ufanyike na kamati ya ajira kisha rais apelekewe majina matatu ili ateuwe mtu mmoja kuwa IGP.

8) MFUMO WA UCHAGUZI

Kumekuwapo kwa malalamiko mengi kuhusu Tume ya Uchaguzi kuegemea upande wa walio madarakani katika utekelezaji wa majukumu yake. Sababu za malalamiko hayo zianaainishwa kuwa ni pamoja na (1) Rais, mwenyekiti wa chama kimojawapo katika vyama shindani, kuunda na kuteua Tume – yaani timu mmoja kati ya timu shindani kuchagua refa wa kuendesha mchezo, uchaguzi; (2) utaratibu wa kutumia watumishi wa umma (DEDs) ambao ni wateule wa Rais/Waziri Mkuu, ambao ni viongozi wa chama shindani kwenye mchakato wa uchaguzi, kusimamia uchaguzi; (3) utaratibu wa msimu wa kuboresha daftari la wapiga kura, kwa mfano wakati wa chaguzi ndogo, daftari haliboreshwi kabisa na hivyo kunyima watu wengi haki ya kupiga kura. Pia utaratibu huu wa msimu wa kuboresha Daftari umesababisha watu wachache mno kuandikishwa kwani wakati uboreshaji unapofanywa watu huwa hawana hamasa yoyote, au umesababisha kuandikisha watu ambao mwisho wa siku hawapigi kura kwani wakati wanaandikishwa kupiga kura hawakujiandikisha kwa sababu walitaka kupiga kura bali kwa sababu nyingine – hawakuwa na hamasa ya kisiasa; na (4) Tume kutokusimamia vizuri mchakato wa uchaguzi, kwa mfano Tume kushindwa kukemea au kuengua wagombea wanaoendesha kampeni za ubaguzi wa kidini au kikabila au kimaeneo au kikanda. Maoni yangu ni:

(i) Tume ya Uchaguzi iwe huru kwa kutumia taratibu za kupata wajumbe kutoka vyama vya siasa, taasisi za kidini, NGOs, na wengineo kama ilivyofanyika katika kupata wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba inayoongozwa na Jaji Warioba;

(ii) Tume iwe na wafanyakazi wake wasio watumishi wa serikali yaani DEDs wasitumiwe kama wasimamizi wa uchaguzi; na

(iii) Daftari la Kudumu la Wapiga Kura liboreshwe muda wote hadi wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi, yaani kusiwepo na muda au msimu wa kuboresha Daftari.
Ndg NYAMKANG’ILI 15 OKTOBA, 2012
 
Back
Top Bottom