Kwa majanga kama tetemeko, Mawaziri Mhagama, Simbachawene na Makamba mfanye kazi pamoja

Richard

JF-Expert Member
Oct 23, 2006
14,939
20,400
Kumekuwepo na matukio kadha wa kadha ya baadhi ya viongozi kujitokeza kutoa maoni yao mbalimbali kuhusu nini kifanyike kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.

Waziri Mkuu bwana Majaliwa Kassim Majaliwa tayari amehudhuria msiba wa wale walopoteza maisha wakati wa tetemeko hilo na pia kutoa salamu ya pole kwa wake wahanga wa tukio hilo.

Imetaarifiwa pia kuwa baadhi ya wanasiasa akiwemo mkuu wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe wamekwenda mkoani Kagera kutoa salamu zao za pole kufuatia janga hilo.

Hadi sasa taarifa kamili ambayo imetolewa na serikali ni kwamba idadi ya vifo ni 17, majeruhi ni 169 na wale walotibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitalini ni 83 na hivyo idadi kamili ya majeruhi ni 252.

Nyumba zilizobomoka ni 44 na zile zilizopata nyufa ni 1264 na hivyo kuashiria kuwa wakazi wa nyumba hizo wote wanalala nje ya nyumba zao yaani kwa majirani, marafiki na pia wale walio katika nyumba zenye nyufa bado wanaishi katika mazingira magumu kwa kuzingatia kwamba mvua zinazoendelea kunyesha zinaleta athari ya baridi na uharibifu wa mali na miundombinu iliyopo.

Na taarifa iliyotolewa na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Generali Salum Kijuu imesema pia kuna nyumba 840 zmeharibiwa kabisa na kati ya hizo 733 ni za manispaa ya Bukoba.

Ukiangalia sana utaona kuna tofauti ya uwiano wa taarifa sahihi za kuhusu idadi ya vifo na ile ya uharibifu wa nyumba kutokana na tetemeko hilo na hili linatia dosari juhudi zozote za serikali kujitetea kuwa inajitahidi kutoa msaada wake.

Lakini majanga huwa hayatabiriki na hutokea hata katika nchi zilizoendelea na wananchi kuanza kudai msaada wa haraka ili kuondokana na kero za maafa kama haya.

Nakumbuka miaka mitatu iliyopita nilikuwa nchini Uingereza na kushuhudia mafuriko makubwa ambayo hayakupata kutokea chini humo na watu wengi waliathirika kwa kuharibiwa nyumba zao, na wengine kulazimika kulala nje ya nyumba zao na pia nje kabisa ya eneo hilo.

Lakini wakati vyombo vya utoaji huduma kama zimamoto, magari ya wagonjwa na hata helikopta vikiwa kazini kuhudumia wahanga, mkurugenzi wa mfuko wa maafa au "enviroment agency" yeye alikuwa nchini Dominica kwenye vekesheni huku aliwasiliana kwa simu na maofisa wake wadogo ambao wengine hawakuwa na uzoefu wa kushughulikia maafa hayo kwa kuzingatia hiyo wengine hiyo ilikuwa ni mara yao ya kwanza.

Hatua hiyo ilisababisha malalamiko makali ya wananchi na baada ya siku kadhaa, mkurugenzi huyo akaahirisha vekesheni yake na kurejea nchini Uingereza na moja kwa moja akaingia ofisini na kuanza kuelekeza wapi misaada iende na wapi kwenye mahitaji ya dharura na vitu kama hivyo.

Ukiangalia sana hatua ambazo serikali imechukua katika kujaribu kuwasaidia wananchi waloathirika na maafa haya ya tetemeko la ardhi, utaona wazi kwamba hili pia kwa ujumla ni jukumu la mawaziri Jesta Mhagama, George Simbachawene na Januari Makamba.

Mawaziri hawa wana jukumu kubwa la kuhakikisha wizara zao zinafanya kazi kwa pamoja na kwa uharaka kwa kuzingatia kwamba mara nyingi baada ya tetemeko la ardhi mvua huweza kutokea na hata mafuriko makubwa na mmomonyoko wa ardhi.

Wizara ya mazingira ambayo ipo chini ya waziri January Makamba, bado mpaka leo wamekaa kimya na hawajatoa maelezo yoyote kuhisiana na hali ya mazingira katika neo hilo, na vipi wanashirikiana na mkoa wa Kagera katika kuhakikisha miundo mbinu kama ya maji ambayo ni mahitaji muhimu, hayahitilafiani (contaminated) na uchafu na kemikali zingine hivyo kuzua magonjwa kwa binadamu.

Nikiwa nina nia njema kabisa kuhusu waziri Makamba, ninamshauri azingatie kwamba wizara aliyo nayo si ya kufanya mikutano tu na wageni mbalimbali ofisini kwake, bali ni kuhakikisha mazingira, dalili za mafuriko, shughuli za uzoaji na uchakachaji taka "recycling", na shughuli zingine zinazohusu mazingira anahakikisha anazifuatilia kwa kushirikiana na baraza la mazingira kwa ukaribu kabisa yaani "coordination of highest standard".

Pia Ofisi ya waziri mkuu ambayo ndiyo inacho kitengo cha maafa, kwa kupitia mawaziri wake dada Mhagama na bwana Simbachawene mpaka leo walitakiwa wawe wamekwishatoa tathmini ni kiasi gani cha fedha zimetengwa kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko hilo na ni jinsi gani serikali itahakikisha kuwa eneo hilo lililokubwa na maafa hayo linatathminiwa kama liendelee kujengwa makazi au liwe huru yaani "isolated zone".

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa na ofisi yake wao ndio walio katika eneo la tukio hivyo kuwa na kila aina ya taarifa za maafa hayo, idadi ya waathirika, majengo zikiwemo shule zilozoathirika, kwani kila taarifa itakayotolewa hadi katika vyombo vya habari itategemea sana ushirikiano na ofisi hiyo iliyo chini ya Meja Generali Salum Kijuu.

Ni wakati sasa wa mawaziri vijana na meja generali Kijuu kujitahidi kufanya kazi kwa mipangilio na ushirikiano mkubwa ukizingatia kwamba hili tetemeko ni janga la kwanza kutokea na hivyo kuwa mtihani wao wa kwanza kutaka kuona "organisationa skills", "problem solving" na "coordination" zimekaa vipi.

Hili ni moja tu ya majanga ambayo yanaweza kutokea nchini mwetu kulingana na mwenendo mzima wa hali ya hewa kwa ujumla, maana inaweza kuwa mafuriko makubwa au mmomonyoko wa ardhi.

Mkiacha hali hii iendelee hadi mwezi ufike tangu siku ya tukio basi mtahesabika kuwa ninyi ni "failers" mloshindwa kazi na mnaostahiki kujiuzulu.

Jambo hili pia si la kuingiza siasa kama inavyoonekana kwa bwana Freeman Mbowe na kauli alizotoa kuhusu kufungwa kwa shule, mbunge wa Tarime John Heche ambae ametoa wazo la "kisiasa" kutaka bunge liahirishwe kwa sababu ya maafa ya tetemeko ingawa tayari yeye na wabunge wenzake wa Chadema tayari wametoa 100,000 kila mmoja.

Huu si wakati wa kutaka kutafuta umaarufu wa kisiasa kupitia maafa, bali ni wakati wa kutoa ushauri uwe wa kitaalam au kawaida kabisa ili kusaidia kuwarejeshea wananchi katika hali yao ya maisha ya kawaida waliyokuwa nayo hapo kabla.

Suala la tetemeko ni suala la kisayansi zaidi na kwa kuwa sehemu hiyo ipo karibu eneo la bonde la ufa, basi tutegemee kabisa uwezekano wa matetemeko mengine au pia hata mlipuko wa Volcano kutokea milima Ruwenzori au milima ya Virunga, kitendo ambacho kitasababisha maafa makubwa katika eneo hilo.
 
Back
Top Bottom