Kwa heri 2013, najua umewatesa vilivyo Watanzania

MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
40,675
2,000

Na Ndyesu


KWA UFUPI

  • Ninasema kwa wiki 51 kati ya 52 mwaka huu nimekuwa nawe bila kukosa. Ni wiki ambazo sikukosa kuwa nawe, ingawa kwa wiki moja sikuonekana.




Ninakamilisha wiki 51 nyingine za mwaka huu, miezi 12 kamili kwa kuwasiliana nawe kwa mara nyingine.

Leo, ninafanya hivyo nikiwa mwenye furaha tele, nakutakia heri ya mwaka mpya, yaani 2014, mwaka ambao panapo majaliwa tutauanza hapo keshokutwa.

Ninasema kwa wiki 51 kati ya 52 mwaka huu nimekuwa nawe bila kukosa. Ni wiki ambazo sikukosa kuwa nawe, ingawa kwa wiki moja sikuonekana.

Ninatambua vizuri wajibu wangu kwako kwani kwa wiki ile moja ambayo hukuwa nami, hakika ulinikosa.

Kwa bahati mbaya, sikupata nafasi ya kukuomba radhi msomaji wangu mtukufu kwa kukunyima uhondo ule wa siku zote ambao kwa zaidi ya miaka minne umeupata kupitia safu hii.

Kwa kipindi hiki cha karibu miaka minne huenda nimekukwaza kwa namna moja au nyingine, naomba unisamehe, kama ambavyo pia ninafanya hivyo kwako.

Kwa pamoja tunaukamilisha mwaka hapo kesho, lakini, ni mwaka ambao kama ilivyokuwa mingine iliyotangulia, tumeshuhudia mambo mengi yakiwamo yale ambayo hakika hayakuwa yenye kupendeza au hata kuvutia. Hata katika familia moja moja, jamii au hata kitaifa, tumepitia katika mambo mengi magumu ambayo siwezi kuyaorodhesha hapa chini.

Kikubwa, kama taifa tulifanikiwa katika moja, lile la kuendelea vyema na mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

Nimeambiwa kuwa leo, mchakato huo unaingia hatua yake ya pili kwa Rais Jakaya Kikwete kupokea rasimu ya pili.

Ninaamini kazi iliyofanywa kwa umakini, umahiri mkubwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba , chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba na wenzake wengi ni ya kupongezwa. Hata hivyo, niitaje kazi ya tume hiyo, nikigusia pia kifo cha mjumbe wake, Dk Edmund Sendongo Mvungi aliyefariki dunia miezi michache iliyopita na kuiacha kazi hiyo ikiwa bado jikoni.

Ninachukua nafasi hii kumwombea pumziko la milele, Dk Mvungi pamoja na Watanzania wengine wote ambao wamepoteza maisha yao, mwaka 2013 kwa sababu zozote zikiwamo za ukatili wetu, sisi binadamu.

Kwa wenzetu, wale ambao wamefariki dunia kwa ajali za aina mbalimbali kama za barabarabani, angani, majini, kwa hakika ninawakumbuka, pia nawaombea pumziko la milele, nikiomba Mwenyezi Mungu awaangazie mwanga wa milele. Ninamkumbuka Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili, Jimbo Katoliki la Zanzibar ambaye aliuawa kikatili kwa risasi, siku ya Jumapili, Februari 17.


Matukio haya ya ukatili yalikuwa mengi, kama nilivyoeleza awali ni pamoja na kuvamiwa, kupigwa, kuumizwa kwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mtanzania linalomilikiwa na New Habari Corporation, Absalom Kibanda.

Kibanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania alivamiwa wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Machi 6, 2013 na kisha kuumizwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na hadi sasa ingawa amepata nafuu baada ya matibabu ya gharama kubwa kule Afrika Kusini, hatuambiwi sababu, chanzo na hata wahusika wa tukio hilo.

Kama vile haitoshi, Padri Anselmo Mwang’amba, pia kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar alivamiwa na kumwagiwa tindikali kama ilivyokuwa kwa katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Soraga karibu na mwisho wa mwaka 2012.

Tukio hilo la Septemba linazidi kutia chachandu matukio hayo mabaya ya kikatili ambayo yameukumba mwaka ambao funguo zake zinawekwa kando, lakini pia unatukumbusha mengi yaliyoitia doa nchi yetu.

Tukio la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wa Kizungu kule Zanzibar, hadi sasa halijawekwa wazi na vyombo vya dola iwe kule visiwani au Tanzania kwa jumla, ni aibu nyingine ambayo nchi yetu haiwezi kujivua.

Wasichana hao,Kirstie Trup na Katie Gee, wenye umri wa miaka 18 walikuwa visiwani humo kwa kazi ya kujitolea, walimwagiwa tindikali Agosti wakati wakiwa matembezi eneo la Mji Mkongwe , Zanzibar.

Jambo la kushangaza ni kuwa tangu wakati ule mbali ya kuhudumiwa katika hospitali zetu, Mnazi Mmoja na Muhimbili, kisha kusafirishwa kwenda kwao, Uingereza walikofanyiwa upasuaji wa kurekebisha sura zao, hatuambiwi nani mhusika.

Nimesoma mahali wasichana hao wanamedhamiria kurudi Zanzibar kuendelea na kazi zao, wanailaumu serikali yaani SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) au ile ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na pia huenda hata ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosimamia vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kulinda raia na mali zao.

Tukio jingine n mfanyabiashara wa Dar es Salaam, ambaye naye alimwagiwa tindikali na kuumizwa vibaya katika mlolongo wa matukio hayo mabaya yanayoupamba mwaka huu.

Tukio hili na jingine la Arusha kwa mfanyabiashara mwingine, pia yote yaliyotangulia limebaki siri baina ya watendaji wake, polisi wanaochunguza na jamii inayosubiri kuona kinachoendelea .

Tumeambiwa kuwa mfanyabiashara huyo na mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad alimwagiwa tindikali kwenye maeneo ya Msasani City Mall, saa 2 usiku ambako inadaiwa kuwa mhusika aliyekuwa na pikipiki alitoka mbio, eti juhudi za mlinzi kujaribu kumkamata zilikwamishwa na utelezi.

Hata hivyo, kama nilivyoeleza mwaka unaisha, lakini cha moto Watanzania walio wengi tumepata.


Hali ya maisha yetu, wengi imeendelea kuwa duni, ngumu, karibu kila kitu kimepanda bei, isipokuwa hewa ambayo Mwenyezi Mungu hugawa bure.

Mategemeo ya wengi kupata hali nzuri, maisha bora ambayo tuliahidiwa na Rais Kikwete wakati ule wa kampeni yake ya kuwania muhula wa pili wa uongozi wake, mwaka 2010 kwa jumla yamebakia ndoto za mchana.

Kisiasa, wananchi tumeendelea kusikiliza ngonjera za viongozi wetu wakiwamo wabunge wakiwa Dodoma ambako hupigana vijembe, kejeli nyingi au kelele lukuki ambazo hazina tija.

Kelele zao (wanasiasa) hazina mwisho ,hazielekei hata siku moja katika kuwafikisha kokote Watanzania hasa katika safari waendako, ile ya kuishi vizuri tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita.

Kama kidonda chetu Watanzania kimetiwa chumvi na ndimu, maisha yetu, wakulima na wafugaji yamewekwa rehani na mapigano baina yetu ambayo yamezikumba wilaya na mikoa mingi nchini.

Uhasama umezidi, wengi wanaishi mtihili ya chui na paka, viongozi wetu wamekosa mbinu za kuimaliza mizozo hii, wameshindwa kuandaa mipango ya kutenga maeneo ya kudumu ya mifugo na kilimo bila bughudha.

Binafsi, nasema yote yanawezekana, endapo kuna dhamira hasa kwa uongozi wetu wa ngazi mbalimbali kujaribu kufanya hivyo. Kama nchi, tujaribu tuone, naamini tunaweza. Kwa heri 2013, najua umewatesa vilivyo Watanzania - Vionjo vya wiki'Mambo halisi' - mwananchi.co.tz


 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Similar Discussions

Top Bottom