Kukosekana kwa mvutano wa ardhi (Gravity) nje ya dunia kunamaanisha mwili unapoteza nishati ya kujenga misuli inayohitajika kubeba uzito wa mtu, pia ubongo na masikio hupoteza balansi ya kumuweka sawa.
Nje ya dunia hakuna kuhisi uzito, juu, au chini. Mikao yote mwili unahisi sawa hata kulala mithili ya popo kwenye chombo, huwezi kuhisi umelala tofauti.
Safari ya wiki moja au mbili nje ya dunia inatosha kukusahulisha kumbukumbu ya mfumo wa balansi ya wapi chini na wapi juu na kuhisi kizunguzungu kila ukijaribu kusimama unaporudi duniani.
Hii ndiyo sababu wanaanga wakirudi duniani wanakuwa hawawezi kutembea husaidiwa kubebwa kufikishwa kwenye hema za matibabu.
"Hii inakuwa kama mlevi aliyekunywa kupindukia na kushindwa kutembea, isipokuwa kwa mwanaanga anabaki na akili timamu"
Anapojaribu kusimama anahisi kama kitu kizito kinamkandamiza kurudi chini kwa nguvu au kumbebesha nusu tani ya mizigo.
Kwahiyo usistaajabu mwanaanga kutambaa kama nyoka ingawa huwezi kuwaona sana katika hali hii.
Mwanaanga mmoja alisema baada ya kutua duniani.
"Unaposimama kwa mara ya kwanza, unahisi mzito mara tano kuliko unavyotarajia si ajabu kuhisi kichefuchefu, tena kama umekaa anga hizo miezi sita au zaidi, dalili ni kali zaidi"
Hivyo hutumia muda kadhaa kulala ili mwili kurudisha hali ya mazoea ya dunia kisha kulazimisha kutembea kama mtoto anayejifunza kutembea.
Aidha kuna mambo mengi ya kufurahisha pale mwanaanga anaporudi kutoka kwenye anga za mbali.
Kwasababu ya mvutano dhaifu nje ya dunia, unapoacha kitu hewani huwa kinaelea, basi warudipo duniani, kuvunja vikombe, simu, laptop huwa ni kawaida kwa wiki za mwanzo.
Wengi hujisahau na kuachia vikombe vya udongo au simu hewani na kusituka vikipiga chini.
Mara mtu hujiachia kukaa kwenye kiti akijua ataenda taratibu "slow motion' kama ilivyo nje ya dunia kisha kujikuta anapigiza makalio chini.
Hali hii hudumu kwa siku /wiki kadhaa kisha kurudi kawaida.
Chanzo: NASA/Astronauts tales