KWA miaka mingi tokea uhuru wa Tanganyika 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar 1964 viongozi walijitahidi kuwafundisha vijana kwa wazee umuhimu wa kusema ukweli hata pale ukweli huo unapokuwa mchungu kama shubiri.
Tulishuhudia viongozi wakiwaeleza vijana kwa wazee ukweli kuhusu matukio makubwa kama njaa, uchaguzi mkuu, machafuko ya kisiasa, vita na hali mbaya ya kiuchumi. Vingozi hawakuongopa pale nchi ilipokumbwa na njaa.
Watu waliambiwa ukweli. Na kwa kumbukumbu yangu nakumbuka kuna Waziri wa Kilimo alipoteza kazi kwa ‘kupika' au kukubali kuwasilisha takwimu ‘zilizopikwa' ili kuonyesha kuwa hakukuwa na upungufu wa chakula nchini ili tu asionekane ameshindwa kazi!
Machafuko ya kisiasa yalipotokea tulielezwa bila kumung'unya maneno na aliyehusika alikuwa anaadhibiwa bila kujali nafasi yake katika jamii. Mambo ya huyu ni mwenzetu hayakupewa nafasi kwenye mambo ya msingi.
Balaa la njaa lilipoikumba nchi (hasa ile miaka ya 70) watu waliambiwa kuna njaa, wekeni akiba, matumizi ya nafaka kutengeneza pombe yakapigwa marufuku na ukaletwa unga wa ‘yanga' wakala hadi wachaga na wahaya ambao walikuwa wanajinadi kwa kutokula ugali!
Nduli Idi Amini alipovamia nchi yetu watu wakaambiwa ukweli; lazima muende vitani! Mimi nilikuwa ndiyo nimetoka JKT (Operesheni Chama Kimoja). Nilikuwa Mamlaka ya Pamba Mradi wa Pamba Geita. Siku moja isiyo na jina nikiwa kijiji cha Katoma mpakani mwa Wilaya enzi hizo Geita na Chato nikaona gari ya Mkuu wa Wilaya, mzee Mikongoti inakuja pale kijijini nilipokuwa nafanya usoroveya (survey) na kugawa mashamba kwa wanakijiji.
Ilikuwa muda wa saa 11 jioni nimekaa nje ya hema chini ya mti mkubwa! Landrover iliposimama akatoka Mkuu wa Wilaya na kunisabahi; mimi karoho kaliniruka kidogo kwa kuwa ndani ya Landrover (pick up) niliona kuna watu kama 6 hivi lakini nyuso zinasimamzi!
Mkuu wa Wilaya akaniambia ‘kuanzia sasa wewe unaenda vitani'! Kwa kweli sikushtuka sana kwa kuwa mchana ule pale mpakani mwa Geita na Sengerema ilitua helikopta na wanakijiji walioenda waliniambia alikuwa ni Rashidi Mfaume Kawawa ametua! Nikajua shughuli imeiva kwani ni wiki chache tu nimetoka JKT.
Nikaambiwa nikabidhi vifaa vya kazi na mahema kwa Mwenyekiti wa Kijiji kwani nitaondoka na Mkuu wa Wilaya. Nilipomaliza kukabidhi nikaingia kwenye Landrover ndipo nilipogundua wale wenzangu ni waalimu na mabwana shamba nao wamesombwa ! Kwa hakika Mkuu wa Wilaya hakudanganya ! Alituambia ukweli na ukweli ulituweka huru ! Njiani zikaanza kuanguka nyimbo za JKT ! 'Alisemaaa, alisemaaa, alisema Nyerere Vijana wangu wote mmelegea, sharti kufanya mchakamchaka ! Aliselema alijaaa, aliselema alijaaaa, kaburu matata hia, hiaaaaa, hiaaa' Basi tukaenda hivyo mwendo mdundo hadi Geita !
Kufika Mkuu wa Wilaya akashuka na kutuambia ‘hamtaruhusiwa kwenda majumbani mwenu bali leo mtalala kambini na alfajiri mtapelekwa Old Shinyanga, Chui Brigade' ! Hakutuficha ! Tukapelekwa kwenye ghala la RTC pale Geita tukalala hadi saa 10 alfajiri safari ya Old Shinyanga ikawiva.
Kote huko tuliambiwa ukweli mtupu ! Kwamba vita si lelemama, kuna kufa, kuna kujeruhiwa kuna kulemaa! Na baada ya vita ya kumg'oa Nduli tukaambiwa bila kumung'unya maneno itabidi kufunga mikanda kwa miezi 18!
Wenye akili tukaelewa tunaambiwa tufunge mikanda kwa muda mrefu! Wasio na kili baada ya miezi 18 wakakumbushwa muda bado, endeleeni kufunga mikanda !
Kiongozi aliyeingia madarakani kwa ridhaa si hadaa, hapati tabu sana kuwaambia ukweli anaowaongoza. Ukweli ni bidhaa adimu sana kwa kiongozi aliyeingia madarakani kwa hadaa au kwa ‘njia za panya' !
Ukweli si sifa ya kiongozi aliyeingia madarakani kwa kugawa fedha, kuchonganisha watu kwa misingi ya kabila au dini, kupikia watu pilau, kutoa na kutetea takrima, kuiba kura, kutukana au kunyanyasa wapinzani wake, n.k. Ni sawa na kutegemea kibaka aendeshe misa au sala! Hiyo sifa hana hata kama anaijua sana kurani na biblia!
Kwa bahati mbaya sana nchini mwetu Tanzania si tu kumezuka ukame wa viongozi wasema ukweli bali sasa tumekuwa na utitiri wa viongozi wasema uongo tena uongo wa kupindukia! Ni bora muwe na viongozi wasiosema ukweli, lakini mkishakuwa na viongozi wasema uongo ujue taifa limeangamia!
Ni hivi:
Mmnaweza kuwa na baba ambaye anajua humu ndani hamna chakula lakini akakaa kimya asiwaambie kuwa hamna chakula mpaka mkagundua wenyewe kwamba leo humu ndani pamenuna. Baba huyu hajasema ukweli, kaficha ukweli! Ila baba huyohuyo akawaambia leo mtakula hadi msaze huku akijua ndani hata panya wamehama kwa kuwa hamna chakula na nyie mkakaa mkao wa kula halafu usiku ukaingia jiko limenuna huyu atakuwa baba mbaya sana! Ni baba msema uongo! Nafikiri nimeeleweka ninaposema bora kiongozi asiyesema ukweli kuliko msema uongo!
Hapa nitarejea matukio machache kuonyesha jinsi viongozi wetu (baada ya kupita wale wasema ukweli japo mchungu) walivyoona ni vyema wawe wasema uongo!
Takrima:
Baada ya ujio wa vyama vingi na chaguzi zake baadhi ya viongozi wetu waliingiwa hofu ya kupoteza nafasi zao. Wakaja na hoja ya takrima. Tukaelezwa eti takrima ni hulka na desturi ya Kiafrika!
Hawakutueleza kabla ya uongozi wao hulka na desturi hiyo ilienda likizo au vipi ? Mbona enzi za Abeid Karume na Mwalimu Nyerere desturi hii ya Kiafrika haikuzingatiwa? Matokeo yake tukashuhudia ugawaji mkubwa wa fedha kana kwamba sisi tuna utamaduni wa fedha zaidi ya wazungu!
Katika kugawa fedha tukawazidi hata waliogundua fedha! Desturi ya ajabu kabisa hii ya Kiafrika! Badala ya viongozi wetu kuwa wakweli na kutuambia sasa ruksa kuhonga wao wakajificha nyuma ya mila na desturi za bandia!
Maji yalipozidi unga wakaja na uongo mwingine! Wakatuletea sheria eti itamaliza matumizi mabaya ya fedha na mali katika chaguzi! Sheria ikatumika lakini kila mmoja wetu anajua badala ya kupunguza ikaongeza tatizo!
Wenye serikali iliyotunga sheria hiyo wakaongoza katika kuikiuka! Hawakuwa na sidhani wanao ujasiri wa kusimama na kutuambia ukweli kuwa sheria imeshindwa! Tutaingia uchaguzi 2015 na sheria iliyoshindwa na hakuna atakayekuwa na ujasiri wa kutuambia ukweli kwamba JAMANI TUMESHINDWA SASA RUKSA KUHONGA! Bora kuhonga kulikoruhusiwa kuliko kuhonga kusikoruhusiwa!
Ni maajabu ya firauni eti leo kiongozi alitetea ujio wa takrima ndiye anayelalama kuwa rushwa imekithiri katika uchaguzi! Mwalimu alisema adhabu nyingine hufungiwa ndani ya kitendo kiovu!
Uchaguzi wa Spika:
Kumekuwa na kelele za muda mrefu baada ya ujio wa vyama vingi kuwa ni vyema Spika asitokane na chama chochote ili awe huru katika kuendesha Bbunge. Na hii haihitaji digrii ya uzamili kuona hivi ndiyo sahihi!
Badala yake tukaletewa uongo kwamba sifa kuu ya Spika ni maumbile! Uongo huu ukaua ndege wawili kwa jiwe moja! Badala ya mjadala kuwa Spika asitokane na chama chochote ikawa watu wanajadili maumbile ya mtu alivyoumbwa na mola wake! Na hapohapo yule ambaye angalau wengi waliamini ameendesha Bunge kwa kiwango cha kuridhisha lakini wakubwa wakawa hawamtaki akaenguliwa kwa kuwa tu havai sketi!
Viongozi wakashindwa kutuambia ukweli kwamba LAZIMA SPIKA ATOKE CHAMA CHETU au HUYU WA KASI NA VIWANGO HATUMTAKI!
Hawa nao kama ilivyo katika takrima adhabu yao imehifadhiwa ndani ya kitendo! Ipo siku wapinzani wao watakuwa wengi bungeni na wingi wao utawafanya wawe na uwezo wa kumchagua spika kutoka upande wao! Tutasikia kelele za mtu mzima kubanwa na mlango!
Babu Loliondo:
Kukawa mchana kukawa usiku akazuka mzee mmoja akadai ameoteshwa tiba ya magonjwa sugu ukiwamo UKIMWI! Viongozi wetu badala ya kueleza umma ukweli kuwa taratibu za tiba haziruhusu upatikanaji wa tiba kwa njia za ndoto au njozi, wao wakawa wa kwanza kufuata tiba, kuitukuza na kupeleka miundo mbinu!
Baadhi walikuwa wanajua wafanyalo! Kuhamisha mjadala juu ya ufisadi na kuuelekeza kwenye tiba ya ndoto! Wengi wa hao viongozi wao walikuwa wanajua utaratibu wa serikali kupata tiba ila wakaona hii ndiyo njia muafaka kutangaza imani yao ya kidini! Wakanasa watu wengi!
Wote tu - mashahidi ya madhila yaliyowapata wagonjwa kwa wazima, wazee kwa vijana, waislamu kwa wakristo na hata wasio wa imani yoyote! Hatimaye serikali ikatoka kwenye uongo na kuingia kwenye ukweli japo shingo upande!
Ikatangaza hakuna ushahidi wa kimaabara kuhusu tiba hiyo! Ni kweli serikali hii haikuona umuhimu wa kuwaambia watu ukweli kuwa TIBA HII SI RASMI UKIUMIA USIRUDI KULALAMIKA KWETU! Yenyewe ikasimamia na kuhamasisha uongo! Leo hii, nani anajua alipo mzee yule aliyeota dawa? Ipo siku mbele ya safari watu watadai fidia kwa kupotoshwa na serikali yao!
Nawashangaa watetezi wa haki za binadamu na wanasheria hapa si kuna tenda ya kutosha? Saidieni waathirika wapate haki yao na ili iwe fundisho na kinga kwa siku za baadaye!
Sasa kwenye mitandao ya kijamii tunaambiwa eti kuna hawa manabii wa uongo ‘waliona' ajali ya ndege ya Malaysia na wanajua ilipo! Ee mungu, tuepushe, kwani wanaweza kutokea viongozi wakaunga mkono hoja hii ili kutuhamisha kwenye mjadala wa Katiba!
Mchakato wa Katiba:
Serikali iliunda yenyewe Tume ya Katiba na ikamteua Jaji Joseph Warioba na wazee wenzake na wasomi wenye heshima kubwa nchini kuiendesha. Hakuna aliyewalazimisha japo ilitokana na shinikizo la kilio cha kudai katiba mpya.
Mzee wa watu na timu yake wakafanya kazi safi na kuikabidhi. Viongozi badala ya kusifia kazi hii sasa wanashindana kuikosoa na kusema uongo! Wanafikia hata hatua ya kukosoa takwimu na kuja na takwimu zao! Kama kulikuwa na njia nyingine ya kupata takwimu waliteua tume ya nini?
Kama hakubaliani na takwimu kwa nini hawakuhoji walipokabidhiwa Ripoti na Tume? Kwa nini walingoja kuja kutoa maoni yao bungeni?
Kwa kuwa uongo huzaa uongo, sasa kuna mheshimiwa waziri anashadidia kuwa ikiwa itaamuliwa serikali tatu eti jeshi litapindua nchi?! Anarudia hoja hii kwa mfumo wa ‘his masters voice? Tena hawa ni wale wa mwanzo mwanzo kabisa kukimbilia kwenye tiba ya ndoto Loliondo! Hawana hofu ya kushtakiwa kwa kupotosha wagonjwa lakini ipo siku!
Huu ni uongo wa muongo mzoefu. Wanataka tuamini jeshi letu halijawahi kutwaa madaraka kwa vile eti tuna serikali mbili! Na eti tuamini kuwa mapinduzi ya kijeshi nchini Nigeria, Ghana, Togo, Guinea, Mali, Chad na kwingineko, yametokana na uwepo wa serikali tatu katika nchi hizo! Huu si sawa na kusema uongo msibani? Inachukiza na kukinaisha!
Hawa wanajua mwaka 1964 kulikuwa na uasi Tanganyika? Je, ulitokana na uwepo wa serikali tatu? Wanataka kutuaminisha eti sasa hivi jeshi halitaki kutwaa madaraka kwa kuwa wameridhika na mishahara inayolindwa au inayotokana na uwepo wa serikali mbili?! Mwe! Sijui wanajeshi wetu wanachukuliaje kauli hii? Si dhihaka kwao?
Hivi wanaona shida gani kusema ukweli wa chama chao kuwa SISI CCM HATUTAKI SERIKALI TATU TUNATAKA MBILI bila kuingiza uongo? Waseme tu serikali mbili zinawahakakishia kubakia madarakani na zinaenzi fikra za waasisi wa vyama vyao! Uongo wa nini?
Hivi wale ‘disciplined propagandists' wa Kivukoni na Murutunguru au Patrice Lumumba kule USSR wameisha CCM siku hizi?! Wamefungua chuo cha LIARS and LIES wapi?
Magari ya kifahari:
Mara kwa mara tumesikia ngonjera kutoka kwa viongozi kupiga marufuku ununuzi wa magari ya kifahari kwa matumizi ya serikali hasa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa sasa. Lakini nadhani hata yeye anajua analosema ni uongo mweupe! Tembelea ofisi yoyote ya serikali ujionee mwenyewe ‘showroom' ya magari ya kifahari! Hivi tunamdanganya nani hasa! Anayepiga marufuku manunuzi ya magari ya kifahari ofisi yake inanunua magari ya bei mbaya kama haina akili nzuri! Utadhani proceurement officer wake ni kiziwi au kipofu! Hasikii maagizo ya bosi wake!
Ipo mifano mingi ya viongozi wetu kugeuza uongo kuwa ndio utamaduni wa taifa lakini kwa leo niishie na mifano hii michache.
Inapaswa viongozi wetu watambue kwamba taifa likishamilikishwa utamaduni wa kusema na kuamini uongo linakuwa taifa liloangamia kabisa! Leo ukiwasikiliza vijana wetu wamekuwa mafundi mchundo wa kutengeneza, kusema, kusimamia na kutekeleza uongo!
Uongo umegeuka kuwa utamaduni wa Taifa! Wanaosema uwongo wanazawadiwa nafasi kubwa kabisa za uongozi! Uongo umegeuka kuwa ajira yenye kipato cha uhakika! Sasa vijana wamegeuka wajasiriamali wa uongo!
Fuatilia mikutano ya siasa, mikutano ya kampeni, mijadala bungeni (hata Bunge la Katiba), mahojiano kwenye vipindi vya TV utasikia UONGO, UONGO, UONGO!
Kuna mwanafalsafa mmoja alisema UONGO NI SUMU YA JAMII! Uongo ukikithiri, chuki hutamalaki, matusi hujizatiti na hatimaye vurugu huchomoza! Na vurugu zinaposhamiri huwaathiri wote, waliosema uongo, walioshadidia uongo na walioongopewa!
Nawaasa viongozi wetu na Watanzania (hasa vijana) kuwa bora kusema ukweli kwa kuwa ukweli hata ukiuficha hujichomoza wenyewe na kumsumbua anayeukwepa! Ukweli humweka mtu na jamii huru! Ukweli hudumisha amani na utulivu.