Kupambana na Rushwa na Haki ya Kupata Habari: Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2007

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
102
250
Muhtasari

Hivi sasa mlipuko wa rushwa unaendelea kuidhoofisha Tanzania. Kwa mujibu wa Faharasa ya Utambuzi wa Rushwa ya mwaka 2008 (CPI) ya shirika la kimataifa linalopambana na rushwa, Transparency International (TI), Tanzania ni nchi ya 102 kati ya 180 zilizofanyiwa utafiti na kupata alama 3 katika kipimio cha 10, huku alama 10 inaashiria nchi safi—hakuna rushwa—na alama 0 ni ishara ya rushwa iliyokithiri (TI, 2008).

Waraka huu wa sera unaeleza hali ya sasa ya rushwa nchini Tanzania, athari zake, vyanzo vyake na ufumbuzi wa kisera. Kwa usahihi zaidi, baada ya kuchambua athari za rushwa kwa taifa la Tanzania, unaonesha namna ambavyo sababu za rushwa za kisheria, kimfumo, kijamii na kiuchumi zinavyoweza kushughulikiwa na kuondolewa kwa sheria inayotafuta haki ya kupata habari.

Maana ya Rushwa Kitabu cha Kudhibiti Rushwa: Mwongozo kwa Mbunge4 kilichotumiwa na Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Kupambana na Rushwa (APNAC) kimeifafanua rushwa kama ni “matumizi mabaya ya wadhifa kwa manufaa binafsi” (Asasi ya Kimataifa ya Wabunge Dhidi ya Rushwa5 (GOPAC), 2005).

Rushwa inaweza kugawanywa katika makundi mawili: rushwa ndogo na kubwa. Rushwa ndogo ni ile rushwa ya kiwango kidogo inayotokea kila siku kati ya maofisa wa Serikali wa ngazi ya chini na wananchi, “katika hatua za utekelezaji wa masuala ya siasa” (U4, Faharasa ya Rushwa;6 GOPAC).

Hapa ndipo kuna uwezekano mkubwa wa kutoa au kupokea rushwa katika kununua bidhaa na huduma za serikali—mikataba ya serikali, leseni, huduma za afya, uandikishaji wa wanafunzi, kupunguziwa kodi au jambo lolote la kuharakisha huduma za umma. Kwa sababu hufanyika mahali ambapo umma unakutana na utawala , mara nyingi huitwa rushwa ya urasimu.

Kinyume chake, rushwa kubwa hutokea katika ngazi za juu kabisa za serikali, “katika hatua za utungaji wa sera katika siasa” (U4, Faharasa ya Rushwa; GOPAC).

Hii hujali zaidi mamlaka kuliko fedha, aina hii ya rushwa inatokea wakati watu waliokabidhiwa mamlaka ya umma ni mafisadi na hutumia nafasi hiyo kudumisha mamlaka yao na utajiri kwa kupuuza au kukiuka sheria, ushawishi wa kibiashara au upendeleo, kubadilisha upangaji wa rasilimali, au kampeni za kuharibu na uchaguzi. Kutokana na hali hii rushwa kubwa aghalabu hufungamana na rushwa ya kisiasa (U4, Faharasa ya Rushwa; GOPAC).

Athari za Rushwa Watanzania wote wanakabiliwa na rushwa, hasa rushwa ndogo, katika shughuli mbalimbali za maisha ya kawaida ya kila siku. Mara nyingi haki za msingi na huduma huwa hazipatikani bila ya makubaliano ya rushwa ama hongo—fedha, zawadi za vitu au upendeleo, ngono au aina nyingine. Zaidi ya upungufu uliopo wa huduma za afya, mtu analazimika kulipia zaidi kuonana na muuguzi au daktari, kutibiwa, kupewa kitanda au kupata dawa.

Huduma za nyumbani—maji, umeme, simu—zinaweza kupatikana tu baada ya kuwapa rushwa maofisa wanaohusika au wanaotoa huduma. Wakati wa kumpeleka mtoto shule ya sekondari, mtu anatakiwa ampe mkuu wa shule malipo yake maalumu. Kupata nyaraka au vibali vya kawaida kama vile kujenga nyumba ya kuishi, kufungua biashara ndogo au hata kupata cheti halali, maofisa wa serikali ni lazima kwanza walipwe.

Wakati wa kushughulika na polisi, mtu anajikuta kuwa yuko tayari kutoa rushwa kupita katika kituo cha ukaguzi wa magari, kukwepa kutozwa faini au kukamatwa kiholela. Ukifika, wakati wa uchaguzi wanasiasa wananunua kura kwa fedha, soda, vyakula au zawadi nyingine. Ni orodha ndefu (REPOA, 2006; U4, Vyanzo na Matokeo ya Rushwa7).

Taasisi ya Kuzuia Rushwa, chombo cha Serikali ya Tanzania, imetaja athari za rushwa ndogo na kubwa kama ifuatavyo:

• Serikali kushindwa kufikia malengo yake
• Kuongezeka kwa gharama za kiutawala
• Kupungua kwa ukusanyaji wa mapato
• Kukosekana kwa ujasiri na kushindwa kufuata kiwango cha juu cha uadilifu
• Kupunguza heshima kwa mamlaka
• Kupoteza tija kwa sababu muda na nguvu hupotea kwa kuiibia au kuitapeli serikali kuliko kuimarisha malengo yake
• Kupungua kwa uwekezaji wa nchi za nje
• Kwa kuwa rushwa inawakilisha kutotenda haki kwa taasisi, bila shaka husababisha madai na mashtaka ya kusingiziwa ambapo hata ofisa mwaminifu anaweza kutishwa ili kupata fedha, na hivyo hali ya kukosa haki inajitokeza.

Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji Tanzania, au NACSAP, ni mkakati wa kupambana na rushwa, ulioanzishwa mwaka 1999, nao pia unaorodhesha “dhihaka kwa mfumo wa mahakama wa nchi” na “uamuzi unaopimwa kwa fedha kuliko maadili ya binadamu” kama athari zaidi za rushwa (Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,8 1999).

Utafiti mkubwa uliofanyika mwaka 2003 na Transparency International kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania unahakiki na kuzidi kufafanua kwa undani zaidi matokeo yaliyotajwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP. Kwa sababu rushwa ni matumizi mabaya ya mamlaka kwa manufaa binafsi, husababisha pengo kubwa la kiuchumi kati ya “walionacho” na “wasionacho” kwa vile wale wenye mamlaka wanajilimbikizia utajiri mwingi zaidi na kuwaachia masikini kiduchu zaidi.

Ongezeko hili kubwa la umasikini hupunguza mshikamano wa kijamii na kuongeza ukosefu wa amani na utulivu wa umma. Utafiti huo umeona kuwa “ongezeko la vurugu na wizi wa kutumia silaha mijini, ukiwemo ule wa benki jijini Dar es Salaam na Arusha” (TI, 2003, uk. 13) husababishwa na rushwa. Hawa “walionacho” waliopata utajiri wao kwa njia ya rushwa ndio haohao wanaohonga mahakama kwa kununua uhuru wao toka hatiani na hivyo “kuudhihaki mfumo wa mahakama wa taifa” uliotajwa hapo juu (TI, 2003).

Kwa kuwa maofisa wanatumia muda na nguvu nyingi katika kupata manufaa ya kifisadi, tija ya serikali kwa jumla hushuka kwani uwezo wa kutimiza malengo yake ya kuhudumia wananchi na kupambana na umaskini hupungua. Rushwa ya kisekta inayotolewa kwenye huduma za jamii, husababisha kushindania rasilimali chache ambapo raia wanajihusisha na rushwa kwa kukiuka taratibu sahihi na kuwahonga watoa huduma, “kama ilivyo katika uandikishaji wa wanafunzi na kulazwa katika kliniki na hospitali” (TI, 2003, uk. 13).

Hii hugeuka kuwa hali ya kawaida kwa watoa elimu na wafanyakazi wa huduma za afya kuomba rushwa. Na kwa sababu rushwa huchota fedha kutoka katika bajeti za utawala, serikali hulazimika kupandisha kodi, bila kuonesha ufanisi wowote wa huduma (TI, 2003).

Hali kadhalika kuna suala la kimazingira ndani ya rushwa wakati biashara chafu zinaruhusiwa kuanzishwa na kuendelezwa kupitia ukiukaji wa Tathmini za Athari za Mazingira kwa kutumia fedha (TI, 2003).

Kwa ujumla, rushwa huwafanya wananchi “wapoteze imani kwa uongozi wao” (TI, 2003, uk. 13), huathiri mamlaka na uhalali wa serikali yao. Kwa hiyo, wakati serikali inachukua hatua ya kuzuia rushwa, inashindwa muda mfupi tu kwa sababu imetambuliwa kuwa haina mamlaka (TI, 2003). Ni dhahiri kwamba athari za rushwa huongeza madhara kiuchumi, kijamii, kisiasa na kisaikolojia.

Vyanzo vya Rushwa

Kutambua vyanzo vya rushwa ni suala tata kama ilivyo kuzielezea athari zake, kama siyo zaidi. Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP hutoa tathmini ya kwa nini rushwa ipo nchini Tanzania. Taasisi ya Kuzuia Rushwa imebainisha vyanzo vya rushwa kubwa na ndogo kama ifuatavyo:

• Udhaifu na kukosa ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi
• Miundo ya kisheria, kiutawala na kisiasa inatoa mazingira muafaka ya kutoa au kupokea rushwa
• Hali ngumu ya uchumi inayowalazimisha watu kutafuta namna ya kujikimu: Hii inachangiwa na mishahara midogo kwa watumishi wa umma na kuongezeka kwa kasi kwa gharama za maisha.
• Taratibu zinazochukua mlolongo mrefu na mgumu (urasimu)
• Kutokuwa na uhakika wa kipindi cha ajira
• Kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza maamuzi
• Kukosekana kwa utashi wa kisiasa
• Kumomonyoka kwa maadili ya uongozi
• Kuibuka kwa matumizi ya kifahari

Vyanzo hivi na vile vya NACSAP vinajadiliwa kwa kirefu hapa chini. NACSAP inawasilisha mchoro ufuatao ili kuonyesha kile kinachoitwa “mtazamo wa kiuchanganuzi” wa vyanzo vya rushwa:

1583833595514.png
Tunaweza kuvipanga vyanzo hivi vingi vilivyotolewa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa na NACSAP katika makundi manne: muundo wa sheria, masuala ya mfumo, mazingira ya jamii na hali ya uchumi.

Tukianza na muundo wa sheria, mapambano yanayoendeshwa dhidi ya rushwa ni dhaifu mno na kwa hiyo, husababisha kuwapo na mazingira mazuri zaidi ya kuendeleza rushwa. Utafiti wa mwaka 2003 wa Mifumo ya Uadilifu ya Taifa uliyofanywa na Transparency International kuhusu Tanzania unasisitiza kwamba sheria zilizopo zinahitaji ushahidi mwingi ili kuweka na kufanya mashtaka dhidi ya maofisa wanaotuhumiwa kula rushwa kuwa na uwezekano mdogo wa kufanikiwa.

Katika tabia inayozidi kuwa na ujanja, utata na usiri zaidi, rushwa inazidi kuwa vigumu kuikabili kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Masuala ya mfumo yanajumuisha mambo mengi yanayochochea rushwa. Mifumo ya kisheria, kisiasa na kiutawala kuwa chini ya serikali kuu ina maana kwamba upangaji wa rasilimali unadhibitiwa na viongozi wachache wenye mamlaka makubwa. Uhuru wa kiutawala wa mamlaka yao unaongezwa zaidi na maofisa wasiofaa na hata wala rushwa katika ufuatiliaji na ukaguzi (TI, 2003).

Kwa uwazi na uwajibikaji mdogo katika mfumo, matumizi mabaya haya ya madaraka hayaepukiki mbele ya uroho na umaskini. Taratibu na miongozo katika mifumo hii huchukua muda mrefu, huchosha na si wa kifanisi. Pamoja na ushawishi wa fedha wa kukubali kupokea rushwa kutoka kwa mtu au kikundi kinachotafuta kukiuka sheria, kuachana na urasimu na kanuni huwashawishi maofisa wa serikali na kuiharibu zaidi (TI, 2003).

Aidha, baadhi ya vipengele vya mazingira ya kijamii ya Tanzania vinachochea rushwa. Uhusiano wa familia pana au makabila huzaa upendeleo kwa misingi hiyo. Dhana ya mafanikio inayozidi kutafsiriwa na mali na matumizi kuliko huduma bora kwa manufaa ya wananchi inapesababisha maafisa wengi wa serikali katika harakati za kujitafutia wao wenyewe mamlaka, fedha na hadhi. Wakati rushwa inaweza kuchangia katika utafutaji huo, vitendo vingi zaidi vya rushwa hujitokeza; uadilifu wa uongozi huzidiwa na uroho wa binadamu.

Viwango vidogo vya uelewa wa wananchi na udhaifu wa jamii za kiraia katika uwanja wa siasa-jamii pia unawezesha rushwa kushamiri bila kipingamizi. Ni siku za hivi karibu tu ndipo vikundi vya asasi za kiraia vilipoanza kuzungumzia rushwa (TI, 2003).

Mwisho, kutokana na hali ya uchumi, Taasisi ya Kuzuia Rushwa inazungumzia kuhusu kutokuwa na uhakika wa ajira na mishahara midogo. Kutokuwa na uhakika wa muda wa ajira huwasababisha viongozi kujinufaisha zaidi na mamlaka waliyonayo kazini kwa kuendeleza rushwa.

Mishahara midogo inayotokana na uwepo wa sekta kubwa ya umma wakati rasilimali za kuhudumia ni chache mno, huwalazimisha watumishi wa umma kutafuta mapato ya ziada kwa njia nyingine, hasa kupitia hongo (U4, Vyanzo na Matokeo ya Rushwa)

Chanzo: HakiElimu
 

mdudu

JF-Expert Member
Feb 6, 2014
2,367
2,000
Mbona hawa Takukulu wanapingana na Serikali? Serikali wanasema uchumi unakuwa ,umasikini umepungua,wao Takukulu wanasema hali ngumu ya maisha na kipato vimechochea Rushwa,nani yupo sahihi?
 
Nov 21, 2019
79
95
Ktk wote walounga juhudi Abdul ntulia , patrobas katambi, waziri wa tamisemi walimepewa rushwa ya pesa na wengine vyeo ila kwa sababu ya anayetoa rushwa ndio mla rushwa tunafunika kikombe ili kisitumike kunywea pombe 2020 kwani ni haramu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Top Bottom