Kuna sababu gani kumpigia kura Mwenyekiti wa CCM?

Allen Kilewella

JF-Expert Member
Sep 30, 2011
18,307
33,925
Agosti 4 2016
NA MARKUS MPANGALA,

JULAI 23 mwaka huu John Magufuli alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama chama Mapinduzi (CCM). Kufuatia kuchaguliwa huko, kumempa kofia mbili; ya uenyekiti wa CCM taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, mgombea wake wa urais anaposhinda kiti hicho pia huchaguliwa kuwa Mwenyekiti wao kitaifa. Hilo ndilo lililoanza kwa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, kisha Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Upo utamaduni wa CCM wa wenyeviti wa taifa kuachiana madaraka kabla ya wakati wao kumalizika. Kwa mfano, Nyerere alikabidhi madaraka ya urais mwaka 1984 kwa Ali Hassan Mwinyi.

Licha ya kumkabidhi nafasi ya urais baada ya uchaguzi mkuu, Mwinyi hakupewa uenyekiti wa CCM mapema. Nyerere aliendelea na uenyekiti wa CCM hadi mwaka 1990. Ni katika kipindi hicho cha miaka sita Nyerere alifanya ziara ya kuzunguka nchi nzima katika mkakati wa kuimarisha chama. Mkakati huo uliitwa ‘Uhai wa Chama”.

Katika mkakati huo ndipo Nyerere alishuhudia makosa mbalimbali ya chama chake, na ambayo yalihitajika kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Hivyo basi, Ali Hassan Mwinyi alikabidhiwa uenyekiti kutoka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1990, wakati ambao alikuwa ameshinda uchaguzi mkuu wa pili katika mfumo wa chama kimoja.

Mwinyi alikiongoza Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka mitano kamili, kabla ya kumkabidhi Benjamin Mkapa ambaye alichaguliwa kuwa Rais mwaka 1995, japo hakupewa mapema.

Mkapa naye alipohitimisha kipindi chake cha madaraka ya urais alimkabidi uenyekiti Jakaya Kikwete bila kulazimishwa wala shinikizo lolote. Kwa mantiki hiyo utaona aliyetumia muda mrfeu hadi kukabidhi nafasi ya uenyekiti ni Mwalimu Nyerere, ambaye alikaa kwa miaka sita.

Kutoka kwa Mwinyi kwenda kwa Mkapa, hadi Kikwete kuna wastani wa miezi sita au mwaka mmoja ndipo mmoja alikabidhi uenyekiti.

Kikwete alipaswa kumaliza kipindi chake cha miaka mitano (5) mwaka ujao 2017 mwishoni. Suala la kumuachia mtu mwingine yoyote ni hiari ya mwenyekiti husika wala sio la kikatiba au lazima.

Utaratibu unaotumiwa na wenyeviti wa CCM taifa kukabidhi madaraka hayo umenipa maswali kadhaa. Kwa mfano, ikiwa suala la kuachia ngazi ya uenyekiti ni hiari, ni kwanini wana CCM wanapiga kura kumchagua mwenyekiti mpya?

Aidha, ikiwa kuchelewa kukabidhiwa Magufuli uenyekiti wa CCM kwasababu ya kupanga mambo yake serikalini, ina maana gani ya kupiga kura?

Hebu tuchukue mfano, ‘utamaduni’ wa CCM umekuwa kuachia madaraka kila unapohitimisha kipindi cha urais. Hii ina maana kama CCM wangemua kufuata katiba yao maana yake Kikwete alipaswa kuachia ngazi mwaka 2017. Hii ina maana Magufuli angekuwa anakabidhiwa rasmi uenyekiti kwa njia ya kuachiwa madaraka siyo kupigiwa kura.

Je kama utamaduni huu umekuwa endelevu na unakubalika na wanachama wote wa CCM takribani milioni 6, kuna maana gani ya kuhangaika kupiga kura kumchagua mwenyekiti?

Vilevile CCM walipokwenda Dodoma walikuwa na azima ya kukabidhi uenyekiti. Kwa maana hiyo hapakuwa na azima ya kupiga kura kwakuwa ni suala la ziada na ambalo halibadilishi chochote katika ‘utamaduni’ wa CCM kukabidhiana madaraka hayo.

Ingeliwezekana kabisa CCM kutumia utamaduni huo kama njia ya kujenga demokrasia inayokubalika bila kuandika katiba kwamba ukomo wa mwenyekiti utafuata kikatiba. Inafaa CCM kuangalia umuhimu wa kupiga kura siku ya kukabidhi uenyekiti na ulazima wa kutekeleza katiba yao kwenye suala hilo.

Ikiwa wenyewe wameweza kudhibiti nidhamu na utamaduni wa kukabidhi madaraka ukakubalika na wanachama wote kwa kauli moja basi hapakuwa na umuhimu wa kumpiga kura Magufuli ama wengine waliopita.

Hivyo basi, CCM wanatakiwa kubadilisha utaratibu, kwamba wanapokabidhi uenyekiti kunatakiwa kuwepo kwa wagombea wa nafasi hiyo. Kwamba wagombea watachuana wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama ili kushinda kiti cha uenyekiti.

Kwanini ninasema hilo la kuchuana? Kwa sababu katiba inaagiza na kuonyesha muda wa kukabidhi madaraka ya uenyekiti. Aidha, katiba inaelekeza kuwa kutakuwa na uchaguzi wa mwenyekiti wa CCM katika mkutano mkuu wa chama.

Kwahiyo, kama katiba hii haifuatwi kadiri inavyoelekeza, ni muhimu basi kwa wana CCM kuamua kuwa mwenyekiti wao hana sababu ya kupigishwa kura kwakuwa hakuna mtu anayeshindana naye. Kwamba CCM inatakiwa kubadilisha utaratibu huo na katiba itamke kuwa mgombea wao wa urais anaposhinda kushika madaraka hayo maana yake ajiandae pia kuwa mwenyekiti wa chama mara baada ya ukomo wa mgombea mwingine (anayemaliza muda wake) au kama anahitaji muda kupanga safu yake serikalini basi uwekwe muda maalumu, kwa mfano miezi sita na zaidi.

Hebu tuchukulie CCM ni chama cha upinzani, kinatakiwa kufanya uchaguzi wa ndani wa kumchagua mwenyekiti wake. Bila shaka utamaduni huu ungelibadilika na kuona kila muda wa ukomo unapofika wanachama kupitia wajumbe wa mkutano mkuu wangelikuwa wanafanya uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti mpya.

Lakini ingelifaa nini kama Katiba imeagiza anayeshika madaraka ya urais, na wakati huo hakuwa rais? Bila shaka utamaduni huu unaweza kuwaletea malumbano ama mjadala usiokuwa na sababu siku za usoni.

CCM watalazimika kuanza kuingia kwenye mchuano wa kuwania uenyekiti, ambao hawakuwahi kuujaribisha. Pia watajikuta wapo kwenye mbio za kunyukana kwa kasi kubwa na kutengeneza makundi ya ndani ambayo yanaweza kukirudisha nyuma au kukiimarisha.

Vyovyote itakavyokuwa, sura iliyopo sasa ya kumwachia mwenyekiti wa zamani kukabidhi uenyekiti kwa mwenyekiti mpya bila kupata mpinzani au mtu wa kuchuana naye halileti tija kwa chama chao.

Wanaweza kujifariji kwamba utamaduni huo ni kitu kilichozoelekea, lakini inafaa nini kujifariji kwenye nyakati ambazo fikra za wanachama zinazidi kupevuka na kutaka kupanua wigo wa uongozi ndani ya chama? Je wanachama wa miaka 30 au 50 ijayo watakuwa na fikra hizo hizo za ‘kurithi utamaduni wa chama’ ambao katiba haiagizi?

Kama wanatakiwa kubadilika basi wanapaswa kuweka utaratibu kwamba katiba iweke utamaduni wa kukabidhi cheo hicho bila kupigiwa kura. Zoezi la upigwaji wa kura kumchagua mwenyekiti mpya ambaye ‘anaachiwa’ nafasi hiyo halina mantiki yoyote.

Ni muhimu basi kukifanya chama chao kibadilike, kwamba kiweke washindani katika nafasi ya uenyekiti kila wakati unapofika, ama wabadilishe utaratibu na kufutwa zoezi la upigwaji kura ili mwenyekiti mpya akabidhiwe katika mkutano mkuu.

Kwamba mkutano huo unaitishwa ukiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wa kikatiba itakayoagiza kuitishwa mkutano mkuu wa makabidhiano ya uenyekiti. Zama zimebaidlika. CCM jiulizeni kama ni muhimu kumpigisha kura mwenyekiti mpya dhidi ya wagombea au mgombea hewa. Muda upo, jadilini.

Chanzo: Gazeti la Rai
 
Back
Top Bottom