Kumuua Ali Hassan Salameh/Abu Hassan

Oct 5, 2015
88
476
Credits;
¶Spies against Armagedon.
by Dan Raviv.

¶An Eye For An Eye". CBS News
¶One day in September
by Simon Reeve

Christopher Cyrilo
Mwaka 1977 kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 29 ya taifa la Israel, chama cha labor (labor party) kilipoteza nafasi ya kuunda serikali. Menachem Begin wa chama cha Likud chenye mlengo wa kulia, akawa waziri mkuu.

Begin, aliwahi kuwa kiongozi wa kikundi cha siri kilichoitwa Irgun, ambacho kilikuwa kikipambana na waarabu na waingereza kabla ya Israel kujitangazia uhuru wake mwaka 1948. Kikundi cha Irgun kilikuwa cha kibabe na chenye msimamo sana kuliko vikundi vilivyoongozwa na David Ben Gurion (The wise man) aliyekuja kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Israel.

Menachem Begin akawa ametoka kuwa kiongozi wa upinzani na kuwa waziri mkuu, huku akiwa na shauku ya kuimarisha na kuitumia jamii ya intelijensia ya Israel vema.

Generali Yitzaki Hofi alikuwa tayari ni mkurugenzi wa shirika la ujasusi wa kimataifa la Israel, Mossad, tangu mwaka 1974 aliposhika cheo hiko kutoka kwa Zvi Zamir. Waziri mkuu Begin akamwachia Generali Hofi nguvu zote za kuiongoza Mossad, na hapo kulikuwa na kazi ya kumalizia. Kazi iliyoshindwa kufanyika hapo awali, kazi ya kumuua msaidizi wa Yesser Arafat, Ali Hassan Salameh.

Salameh ndiye aliyeratibu mauaji ya wanamichezo 11 wa Israel katika michezo ya olimpiki ya mwaka 1972 huko mjini Munich, Nchini Ujerumani.

Ilikuwa Septemba 5, mwaka 1972 wakati kikosi kilichojiita Black September kiliwateka wanamichezo wa Israel waliokwenda nchini Ujerumani kwenye michezo ya Olimpiki. Watekaji walikuwa ni 'magaidi' wa Palestina, wakihitaji kuachiwa kwa wafungwa 250 wa kipalestina kama dhamana ya kuwaachia wanamichezo hao.

Kansela wa Ujerumani magharibi wakati huo, Willy Brandt alikubali ombi maalumu la Israel, la kutumia kikosi maalum cha makomandoo wa Israel kuwaokoa raia wao, lakini mamlaka za serikali ya manispaa ya Munich ilikataa kwa kisingizio kwamba, hakuna uhalali wa kikatiba kuruhusu makomando wa nchi ngeni kufanya misheni ndani ya Ujerumani. Kwa hiyo, maofisa wa polisi wa Ujerumani waliamua kufanya misheni ya kuwaokoa waisrael hao.

Victor Cohen, veterani wa shirika la ujasusi wa ndani la Israel, Shin Bet, alikuwa mjini Munich pamoja na Zvi Zamir aliyekuwa mkurugenzi wa Mossad wakati huo. Cohen alikuwa mahali hapo kwa dhumuni la kufanya mazungumzo na makubaliano (negotiations) na watekaji. Alikuwa mzungumzaji mzuri wa kiarabu na alikuwa nguli wa kazi ya kutafuta maridhiano na maadui.

Baada ya Wajerumani wa Munich kuwakatalia waisrael kujihusisha na ukombozi wa raia wao, wakuu hao wa ujasusi walikaa juu ya mnara wa kuongozea ndege, katika uwanja wa ndege wa Munich, huku Polisi wa Ujerumani wakijaribu bila mafanikio kuwaokoa wanamichezo wa Israel kutoka mikononi mwa watekaji. Watekaji watatu walikufa baada ya kurushiwa risasi na polisi wa kijerumani, waliobaki waliamua kuwamiminia risasi wanamichezo wote 11 wa Israel. Cohen na Zamir, hawakuwa na cha kufanya zaidi ya kuangalia ndugu zao wakiuawa. Haikuwa mara yao ya kwanza; wote wawili wameshuhudia mauaji ya wayahudi sehemu mbalimbali za dunia, hasa Ulaya, ama kwa risasi, au kwa kuchomwa moto.

Jamii ya Intelijensia ya Israel ikagundua kuwa Ali Hassan Salameh ndiye aliyeratibu tukio la mjini Munich. Na kwa taratibu za kijasusi za Israel, alipaswa kutafutwa afe.
Makosa ya mjini Lillehammer:

Miezi tisa baada ya tukio la Munich, July 1973 majasusi wa Mossad walipewa taarifa na mashushu wao wa Ulaya kuhusu uwepo wa Ali Hassan Salameh huko mjini Lillehammer, kaskazini mwa Norway. Michael Harari, aliyekuwa msaidizi wa Zvi Zamir alichukua vijana wake wa kazi na kwenda nchini Norway. Siku chache baadaye, mkurugenzi wa Mossad Zvi Zamir alijiunga na timu hiyo. Ilikuwa ni utamaduni wa wakuu wa vyombo vya dola wa Israel kuwepo mstari wa mbele wakati wa kazi maalum. Ni kwa muktadha huo huo, Yonatan 'Yoni' Netanyahu, kaka wa waziri mkuu wa sasa, Benyamin Netanyahu aliongoza kikosi cha makomandoo cha Sayeret Matkal katika operesheni ya Entebe (Operesheni Thunderbolt) ya kuwakomboa waisrael waliotekwa kwenye ndege, huko Entebe, Uganda. Yonatan alikufa katika misheni hiyo ya mwaka 1976.

Zamir alifuata utamaduni huo huo na kufika nchini Norway ili kumuua Ali Hassan Salameh.
Kwa masaa mengi walimfuatilia mtu waliyeamini ni Salameh. Ilikuwa usiku, lakini binti mmoja aliyeitwa Marianne Gladnikoff, aliyeletwa na Michael Hariri kwenye timu hiyo ya Mossad alishtuka akasema mtu yule hakuwa Salameh, wakampuuza.

Walipomfuatilia hadi sehemu muafaka, Vijana wa Mossad waliofunzwa mahususi kwa kuua, walirusha risasi na kumuua mtu yule, bila kumjeruhi mwanamke aliyekua akitembea naye barabarani. Kisha wauaji walirudi hadi jijini Oslo na kujificha kwenye nyumba salama. Hakukuwahi kufanyika mauaji katika mji wa Lillehammer kwa miaka 40, kwa hiyo ilikuwa tukio la ajabu sana kwa wakazi wa mji huo.

Lakini kesho yake iligundulika kuwa, aliyeuawa sio Ali Hassan Salameh, na mtu mwenye jina hilo hakuwepo nchini Norway. Ilikuwa ni pigo kwa Mossad, lakini pigo kubwa lilikuwa kukamatwa kwa timu yote iliyohusika na mauaji yale, isipokuwa Mkurugenzi Zamir na msaidizi wake Harari ambao walitoroka kwa njia zao binafsi kurudi Israel. Zamir alitumia boti maalum iliyoandalia na muisrael aishiye Norway ,ambaye ni wakala malum wa Mossad. Karibu kila nchi duniani, wapo wakala wa kutoa msaada kwa waisrael, pamoja na kuwasaidia majasusi wa Mossad wanapohitaji msaada. Mawakala hao huitwa 'Sayan' na mara nyingi ni raia wa nchi wanamoishi, lakini wayahudi.

Jamii ya kimataifa ilishangaa, kwamba Mossad inayosifika kwa ufanisi wake imefanya makosa ya kijinga. Lakini zaidi timu iliyohusika na mauaji hayo ilishindwa kujificha na hivyo kukamatwa kirahisi na polisi wa Norway. Pamoja na makosa mengime, kosa la kijinga walilofanya ni kutumia usafiri wa kukodi, badala ya kutumia usafiri wa umma.
Serikali ya Israel haikuwahi kukubali hadharani kuhusika na tukio hilo, lakini ilizungumza na serikali ya Norway namna ya kwasaidia raia wake waliokamatwa huko Norway.

Ahmed Bouchiki, raia wa Moroko aliuawa na Mossad kwa kufananishwa na Ali Hassan Salameh, mwanamke aliyekuwa naye usiku ule, wakitembea barabarani kabla ya kuuawa alikuwa mke wake, raia wa Norway, tena mjamzito. Serikali ya Israel ilimlipa fidia mke wa Ahmed kwa miaka 20.

Ali Hassan Salameh/Abu Hassan.

Yesser Arafat hakuona vema kujiingiza moja kwa moja kwenye matukio ya kigaidi. Kutoka na heshima yake mbele ya jamii ya kimataifa, na jukumu lake la kutafuta amani katika eneo la mashariki ya kati, ilimbidi atumie vijana. Ali Hassan Salameh alikuwa kijana maridadi na mwenye uwezo kazi hiyo. Akiongoza kikosi cha Force 17, chini ya Palestine Liberation Organization (PLO) alitekeleza maagizo ya Yesser Arafat ambayo Arafat hakutaka kujihusisha moja kwa moja. Lengo la Arafat lilikuwa kupata nguvu ya kujiepusha na lawama panapotokea jambo baya.

Mwaka 1969, Salameh alikutana na watu wa shirika la kijasusi la Marekani,CIA, na kufanya mazungumzo.

Mwaka 1978, Salameh alifunga ndoa na mrembo kutoka Lebanon, Georgina Rizk, mshindi wa taji la Miss Lebanon wa mwaka 1970 na baadae miss Universe mwaka 1971 huko Miami Beach, Marekani.

Mwaka mmoja kabla ya ndoa yao, Ali Salameh na Georgina Ritz walidhuru nchi Marekani na kutalii katika maeneo ya Disney Word na Hawaii.

Majasusi wa Mossad walipatwa na sintofahamu; Iweje mtu anayeitwa gaidi, afanye starehe nchini Marekani bila wasiwasi? Iweje awe na mahusiano ya kimapenzi na mtu maarufu kama Georgina? Kwanini?

Mossad hawakujua kuwa Salameh alikuwa mtu wa CIA. Gharama za starehe zote zililipwa na CIA, na alikuwa katika mpango wa kutawazwa rasmi kuwa jasusi wa CIA. Kabla ya hapo, Salameh alishafanya makubaliano na CIA kwamba hakuna mmarekani atakayeguswa na wapiganaji wa Palestina. Na alishaingizwa kwenye Orodha ya malipo, (payroll).

Inawezekana pia, mashushushu wa CIA walimsaidia Salameh kuepuka majaribio manne ya kuuawa yaliyopangwa na Mossad, bila Mossad kujua.
walimtafuta sana, lakini ilikuwa vigumu kumpata. Alikuwa na machale, mjanja na mwenye akili nyingi.

Kifo cha Ali Hassan Salameh.

Baada ya kushika dola, waziri mkuu Menachem Begin akataka kumaliza kazi nyingi za Mossad zilizokuwa zikisuasua. Moja ya kazi hizo ni kumuua Ali Hassan Salameh, mratibu wa tukio la Black September la mjini Munich. Jukumu hilo akakabidhiwa Generali Yitzaki Hofi, naye akakabidhi kwa Michael Harari, kiongozi wa kikosi cha Caesarea.

Katika wanawake ambao shirika la Mossad limewahi kujivunia, ni Erika Chambers.
Erika alizaliwa mjini London mwaka 1948, baba yake alikuwa muingereza, mtu maarufu katika mchezo wa kukimbiza magari wakati huo. Mama yake, alikuwa myahudi wa Czech, aliyekulia mjini Vienna. Mama yake Erika alimlea mwanaye katika maadili ya dini ya kiyahudi na alimuhamasisha kujifunza historia ya uyahudi. Erika alisomea mambo ya nguvu za maji katika chuo kikuu cha Southampton, nchini Uingereza na kisha akaendelea nchini Australia. Mwaka 1972 alisafiri hadi nchini Israel kuendelea na masomo katika chuo kikuu cha Yerusalemu. Kisha, siku moja akapotea.

Erika alikuwa amechukuliwa na Michael Harari, kiongozi wa kikosi maalumu cha operesheni maalum za kijasusi za Mossad. Kikosi hiko cha Caesarea, kilikuwa maalum kwa misheni za siri, kikishirikiana na kikosi maalum cha 'kuua' kilichoitwa Kidon.

Kidon inaundwa na makomandoo maalum kwa ajili ya kuua maadui nje ya Israel. Hawana upendo wala chuki. Hawana furaha na hawana huzuni. Hawana hisia. Ni wavumilivu sana na wana haraka sana. Maisha yao ni kuua. Hata hivyo, wanapostaafu, Katika uzee wao wengi hupatwa na maradhi ya akili.

Erika Chambers alijiunga na Caesarea, ambao kazi yao kubwa ni kuandaa mazingira kwa ajili ya kazi ya kuua itakayofanywa na makomandoo wa Kidon.

Kwanza, Erika alisafiri hadi Ujerumani na kuishi huko kwa muda wa kutosha, ili kuchanganya anuani za chimbuko lake la uingereza. Kisha akaenda Geneva kufanya kazi za kujitolea kuhudumia watoto na wazee. Baadaye, Novemba 1978 aliomba kujitolea kufanya kazi hiyo nchini Lebanon.

Alipanga nyumba mjini Beirut, katika jengo la Anis Assaf, ghorofa ya nane, pembeni ya barabara aliyokuwa akitumia Ali Hassan Salameh Kila siku anapotoka na kurudi nyumbani kwake. Majirani walimtambua Erika kwa jina moja la Penelope, na kwamba ni raia wa Uingereza anayefanya kazi za kujitolea (Charity).

Salameh alijua yupo salama nchini Lebanon, na hivyo hakuona ulazima wa kuwa na ratiba isiyo na mpangilio ili kuwazuga maadui zake. Kosa kubwa alilofanya ni kuwa na ratiba maalum.

Erika, alianza kazi zake za kujitolea kwenye vituo mbalimbali vya yatima. Kwenye baraza la nyumba yake iliyokuwa ghoro ya nane, alijipa kazi ya kuchora picha na kuzipaka rangi. Lakini dhumuni kubwa halikuwa kuchora bali kusoma mazingira. Alijipa ratiba hiyo kwa lengo la kutazama mienendo ya mazingira ya mtaa wa Beka, na mtaa wa jirani wa Rue Verdun, huku akisoma ratiba ya gari analotumia Salameh.

Wakati fulani, Erika alikutana na Salameh katika shughuli za kuwatembelea watoto yatima, akatengeneza urafiki wa muda. Salameh akawa na kawaida ya kumualika Erika katika shughuli mbalimbali, ndipo Erika alipojifunza ratiba mbali mbali za Salameh.
January ya mwaka 1979, Erika alikutana na watu wawili, Peter Scriver na Roland Kolberg.

Mmoja aliingia Lebanon akiwa na pasi ya kusafiria (passport) ya uingereza, mwingine alitumia passport ya Canada. 'Watalii' hao, kutoka Uingereza na Canada walikuwa ni majasusi wa Mossad, kikosi maalum cha kuua maadui nje ya Israel, Kidon.

Kabla ya hapo, 'watalii' wengi waliingia lebanon na kukutana na Erika. Kazi yao ilikuwa ni kuleta kifaa kimoja kimoja kwa ajili ya kutengeneza bomu. Inakadiriwa, majasusi 14 walishiriki mpango huo.

Tarehe 22 Januari, 1979 wakati Salameh akitoka kwenye ofisi za PLO huko Lebanon, akiwa katika njia yake ya kila siku, watu wale wawili walikuwapo kwenye nyumba ya Erika wakiangalia magari yanayopita barabarani.

Salameh, bila kujua aliendelea na safari yake, akitokea kwenye nyumba ya mke wake Gorgina na kuelekea kwa mama zake kwa ajili ya sherehe ya birthday, akiwa na msafara wa magari mawili aina ya Chevrolet Station Wagons.

Pengine alikuwa anamuwaza mrembo wake Georgina, au alikuwa anawaza namna ya kuwateka waisrael wengine, haijulikani. Baada ya kulipita jengo alimoishi Erika, sekunde kadhaa baadaye, kitufe cha rimoti kilibonyezwa. Lilikuwa bomu la kilo 100 lilotegwa pembeni ya barabara muda mfupi kabla ya Salameh kufika eneo lile.

Saa 9:35 mchana wakati mlipuko ukitokea Erika na vijana wake wawili walikuwa ndani ya jengo lile. Haijulikani ni nani aliyebonyeza kitufe cha rimoti kati yao, ingawa majasusi wa MI6 wanadai ni Erika Chambers. Mossad hawakuwahi kusema ni nani kati ya watu wale watatu, Peter Scriver wa Uingereza na Roland Kolberg wa Canada au Erika Chambers wa Uingereza. (Utambulisho wa kughushi). Sio kawaida ya Mossad kutoa ufafanuzi panapoibuka mdahalo unaohusu misheni zao.

Salameh alijeruhiwa vibaya, pia walinzi wake wote wanne na watu wengine wanne; mtawa wa kijerumani na wengine waingereza, waliokuwa pembeni ya barabara walipoteza maisha.

Saa 10:03 jioni, Salameh alifariki juu ya meza ya operesheni katika hospitali ya chuo kikuu cha kimarekani, mjini Beiruti. Kipande cha chuma kilikuwa kimezama kichwani, huku akiwa ameungua kwa sehemu kubwa ya mwili.

Mazishi yalifanyika mbele ya waombolezaji wanaokadiriwa kufika 100,000, wakiongozwa na Yesser Arafat.

Baada ya mlipuko ule, Erika na wenzake waliondoka haraka kurudi Israel kwa boti maalum iliyoandaliwa kwenye fukwe za Lebanon. Kiongozi wa mpango huo Michael Harari alikuwa akisubiri kwenye boti hiyo. Katika jengo lile, Erika aliacha passport yake halisi ya uraia wa kiingereza, na nyaraka za maisha yake akiwa Ujerumani. Inadhaniwa kuwa aliiacha kwa makusudi ili kuwalaghai watakaomfuatilia, wajue ni muingereza wakati yupo Israel. Majasusi wa Ujerumani, BND, wanadai, Chambers alifanya kuacha nyaraka zile kwa makusudi ili kuwalaghai wachunguzi.

Erika alipokelewa na kupangiwa kazi ya kiofisi katika makao makuu ya Mossad.
Hata hivyo hakuipenda. Erika aliamua kuwa mwalimu katika chuo maalum cha majasusi wa Mossad. Kisha alibadili utambulisho wake na kupotea kwenye kumbukumbu za dunia.

Hakuwahi kurudi uingereza, hakuwahi kuwasiliana na mama, baba na ndugu zake, hakuwahi kuwaambia alipo. Alichofanya ni kuwatumia kadi za Krisimasi kila mwaka. Hadi utaratibu huo ulipokoma, ndugu zake wakaamini amekufa.
 

Attachments

  • images (4).jpeg
    images (4).jpeg
    6.5 KB · Views: 180
Imekua kama zali, ndio natoka kuicheki movie ya mauaji ya waizrael Mjini Munich. Tatizo nimeikuta imeanza so hata jina sijalijua.. Ref Azam2
 
Uzi mzuri mkuu hicho kitabu nimewahi kisoma kina matukio ya kustaajabisha sana ila ningependa kukuuliza mtoa mada unisaidie kidogo kwanini pale waisrael wakifanya mission wanaitwa makomandoo ila wapalestina wanaitwa MAGAIDI mpaka leo sijaelewa mkuu naomba unisaidie Christopher Cyrilo
Mkuu, historia inaandikwa na mshindi. Na yeye huamua kuwaita maadui zake majina mabaya .
Wapalestina nawo wakiandika watatumia majina mabaya kwa waisrael.

Ni kama kwenye WWII, akina Hitler wangeshinda wangejiandika kwa majina mazuri mazuri .
 
Uzi mzuri mkuu hicho kitabu nimewahi kisoma kina matukio ya kustaajabisha sana ila ningependa kukuuliza mtoa mada unisaidie kidogo kwanini pale waisrael wakifanya mission wanaitwa makomandoo ila wapalestina wanaitwa MAGAIDI mpaka leo sijaelewa mkuu naomba unisaidie Christopher Cyrilo
Simple tu.

Waisrael na washirika wao wataita watenda kazi wao majasusi na makomandooo huku wakiwaita upande wa maadui zao magaidi.

Wapelestina na washirika wao perhaps na wewe, mtawaida watenda kazi wa kipalestina majasusi na makomandooo huku mkiwaita wa upande wa Israel magaidi walio kubuhu.

Ni hayo tu
 
Simple tu.

Waisrael na washirika wao wataita watenda kazi wao majasusi na makomandooo huku wakiwaita upande wa maadui zao magaidi.

Wapelestina na washirika wao perhaps na wewe, mtawaida watenda kazi wa kipalestina majasusi na makomandooo huku mkiwaita wa upande wa Israel magaidi walio kubuhu.

Ni hayo tu
au utasikia wapiganaji wa kipalestina
Wanamgambo wa Hamas
 
Mkuu, historia inaandikwa na mshindi. Na yeye huamua kuwaita maadui zake majina mabaya .
Wapalestina nawo wakiandika watatumia majina mabaya kwa waisrael.

Ni kama kwenye WWII, akina Hitler wangeshinda wangejiandika kwa majina mazuri mazuri .
Aiseeee"" safi sana
 
Back
Top Bottom