Kumbukumbu ya kweli... | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kumbukumbu ya kweli...

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mzee Mwanakijiji, Oct 8, 2008.

 1. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #1
  Oct 8, 2008
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  “TUJIFUNZE kuwawajibisha viongozi wanaozembea majukumu yao. Watanzania lazima tujifunze kukataa uongozi wa ugoi goi kwa sababu ya kuogopana au kutotaka kuonekana tuna kimbelembele.

  Hadi nani afe kwenye hizi ajali ndipo tutajua kuwa tusisubri mkuki kwa binadamu? Makala yangu ya Aprili 16, 2008, Tanzania Daima.

  Kuna minara mingi ya kumbukumbu ambayo tumeijenga kukumbuka majanga mbalimbali. Mnara wa kumbukumbu wa ajali ya wanajeshi kwenye vilima vya Lukumburu, mnara wa ajali ya mv Bukoba nje kidogo ya Mwanza, na mnara wa vifo vya ajali ya treni.

  Hiyo ni mifano michache tu. Minara hii inatakiwa kutukumbusha matukio yaliyotokea na kumbukumbu ya wale waliopoteza maisha yao katika ajali hizo.

  Lakini ukweli ni kuwa minara hiyo inabakia kama ushahidi wa hatia yetu kuwa hatuna kumbukumbu. Imebakia kuwa minara ya usahaulifu wetu.

  Kabla ya watoto 19 waliokufa kwenye ukumbi wa disko ulio kwenye jengo linalomilikiwa na NSSF hawajazikwa, viongozi wa Mkoa wa Tabora walianza kuzungumzia suala la kujenga mnara wa kumbukumbu ya watoto hao.

  Kwao jambo la maana lilikuwa ni kuonyesha kuwa wanajali na ya kuwa wameguswa na vifo hivyo. Na kwa haraka yao kuanzia rais, NSSF na taasisi ambazo zinahusika moja kwa moja na suala la ukumbi huo wakakimbilia kutoa fedha za ‘pole’.

  Hili tuliliona pia kwenye ajali ya treni kule Dodoma na kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kuliona kwenye kifo cha yule kijana aliyedaiwa kuuawa mikononi mwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ditopile Mzuzuri.

  Lakini, hili la kukimbilia kujenga mnara wa kumbukumbu linanishangaza ni jinsi gani hatuna kipaumbele cha kuwajibika kama ishara ya kwanza ya kuenzi kumbukumbu za watoto hawa.

  Ili watendaji wasilaumiwe na kuwajibishwa, basi wao wenyewe wanakuwa wa kwanza kutangaza mipango yao ya kutaka kujenga mnara wa kumbukumbu.

  Ukiniuliza mimi kitu cha kwanza ambacho kingetakiwa kufanywa ni kubomolewa kabisa kwa jengo hilo na eneo hilo kujengwa bustani ya kuchezea watoto na ukumbi mzuri wa jumuiya (Community Center).

  Jengo hilo litaendelea kubakia kama ishara ya uzembe mkubwa na kutokuwajibika kwa kadiri ya kwamba litaendelea kusimama. Gharama ya kujenga bustani na ukumbi huo ilipwe na NSSF na wakatazwe kabisa kusimamia ujenzi wake na kampuni ya kisasa na ya kimataifa ifanye shughuli hiyo.

  Lakini swali ambalo tunatakiwa kukabiliana nalo ni jinsi gani tutaweza kuwakumbuka watoto hawa ukiondoa hiyo kumbukumbu ya mnara wanaotaka kuujenga hapo Tabora?

  Kwanza kabisa ni kuhakikisha kuwa wahusika wote wanawajibika. Kinachoshangaza ni kuwa watu wanakwepa kuiwajibisha NSSF kwa namna yoyote ile.

  Katika siku chache zilizopita nimegundua hofu ya ajabu watu waliyonayo ya kuinyoshea kidole taasisi hiyo na kutaka uongozi wake kuwajibika kwa kuwekeza katika biashara ambayo haina maana wala mantiki.

  Kwa shirika kubwa kama NSSF ambalo lina majengo makubwa jijini Dar es Salaam, Mwanza na sehemu nyingine nchini, shirika ambalo linatumia fedha za wanachama wake kufanya uwekezaji huo hivi kati ya vitu vyote ambavyo wangeweza kuwekeza na kukodisha ni hili la ukumbi wa disko?

  Hapa nauliza, hekima na busara ya kibiashara ya uongozi wa NSSF chini ya Dk. Ramadhani Dau na Mwenyekiti wa bodi yake Blandina Nyoni, jibu la haraka ambalo linaweza kutokea ni kuwa wao makao makuu hawakujua kuwa jengo lao limepangishwa kuchezesha disko la watoto.

  Kama hilo ni kweli, mbona hadi hivi sasa hatujasikia Meneja wa NSSF Mkoa wa Tabora amewajibishwa kwa kufanya mambo bila kuwajulisha makao makuu?

  Uwezekano wa hilo la wao NSSF makao makuu kutokujua ni finyu mno, kwani kisheria uwezo wote wa kuingia katika uwekezaji au mradi wowote ule ambao unatumia fedha za NSSF uko mikononi mwa bodi, na katika ufuatiliaji wa kila siku wa shughuli za shirika umo mikononi mwa mkurugenzi wake.

  Hivyo, kama nilivyosema nilipopata taarifa za msiba huu ambao watu sasa wameshakinai na umekuwa ‘zilipendwa’ na hasira yake imeanza kutoweka, ni kuwa Mkurugenzi wa NSSF lazima awajibike.

  Kuna baadhi ya watu ambao wanataka tuamini kuwa kuwajibika huku ni lazima kuwe kwa sababu amevunja sheria fulani au shirika lake limefanya jambo fulani la kihalifu.

  Mimi siamini hilo. Ninaamini kuwa kiongozi yeyote anapaswa kuwajibika kwa kupima maamuzi yake, matendo yake na mipango yake hasa pale maamuzi, mipango na vitendo vyake vinaonyesha kuwa hakuwa makini au aliweka faida mbele zaidi kuliko vitu vingine kama masilahi ya kulinda maisha ya watoto.

  Ni kwa sababu hiyo narudia bila kigugumizi, uongozi wa NSSF wajipime wao wenyewe na wafikie uamuzi ambao wanaona unafaa. Na katika hilo, ninaamini wakubali kuwajibika na kuwapisha watu wengine kushika nafasi hizo ili shirika liondokane na kivuli cha uongozi wao na liwe funzo kwa watendaji wengine wote wa ngazi za juu.

  Itakuwa kumbukumbu nzuri kwa watoto hawa kama kuanzia sasa viongozi wa juu wataogopa kufanya maamuzi yasiyo na masilahi, wakijua kwamba ‘kikiungua’ wao wenyewe watawajibika.

  Sasa hivi hakuna hofu ya kuharibu, kwani ni rahisi kumlaumu aliye chini au mtendaji aliyeko mbali (kama Tabora). Ni rahisi zaidi kwa viongozi wa ngazi za juu, meneja wakuu, wakurugenzi, maofisa watendaji wakuu na wengine kufanya mambo yao wakijua ya kuwa itakapotokea suala la kuwajibika, wao wapo mbali, kwani Tanzania hatuna utaratibu wa kuwawajibisha viongozi wa juu wa shirika, idara au taasisi.

  Na pale tunapo wawajibisha tunatengeneza mazingira ya kufanya waonekane mashujaa kama tulivyoshuhudia mapokezi ya kina Edward Lowassa na Andrew Chenge, kana kwamba kujiuzulu kwao kulikuwa ni kitendo cha kishujaa badala ya aibu!

  Lakini la pili ambalo litaonyesha kweli tumeamua kuwakumbuka watoto hawa ni kuhakikisha tunapitisha sheria ambazo zitalazimisha mabadiliko ya ujenzi na sifa za majengo mbalimbali kuwa zile ambazo zinafikia kiwango cha kimataifa.

  Nilipoandika makala ile ya “Taifa lisilojiandaa kwa majanga, limejiandaa kwa maafa” kwenye gazeti hili Aprili mwaka huu, nilisema hivi kuhusu haja ya kubadilisha milango yetu ya kwenye majengo yanayochukua watu wengi kwa wakati mmoja (kama mabweni, kumbi, madarasa) ili kuepukana na vifo vinavyotokana na kukosa nafasi au njia ya kuepukia.

  Ninajinukuu: “Mojawapo ya vitu ambavyo naamini tunaweza kuvifanya na ambavyo si vya gharama kubwa ni kutaka majengo yote yenye watu zaidi ya ishirini kwa wakati mmoja, kama nilivyosema hapo juu, yawe na vifaa vya tahadharai ya moto (VITAMO) au kwa lugha ya kigeni ‘fire alarm systems’.

  “Vifaa hivi mara nyingi si ghali na havitumii umeme bali betri zile ndogo. Si kwenye taasisi tu lakini karibu nyumba zote za umeme zihamasishwe kuwa na vifaa hivi, kwani vinaweza kuokoa nyumba na mali nyingi kama mwenye nyumba ataamka kabla moto haujaenea au kabla majirani hawajaanza kuvunja nyumba hiyo kumuamsha”.

  Katika hili ni kuwa vifaa hivyo vingi siku hizi vinagundua moshi na pia hewa chafu ya carbondioxide. Hewa hii chafu ndiyo ambayo mwanadamu anaipumua na unapokuwa na wanadamu wengi kwenye ukumbi usio na hewa mpya safi zaidi ya ‘viyoyozi’, basi unasababisha kutokuwa na mzunguko wa hewa (air circulation) kwenye ukumbi.

  Matokeo yake ni kuwa wale binadamu waliomo ndani watauana wenyewe kwa sababu wote wanatoa hewa ya sumu ya Carbondioxide.

  Ndiyo maana wengine tunahoji, inakuwaje wataalamu wetu hawa wanakubali jengo lizibwe madirisha yetu na kuwekewa viyoyozi na hakuna sehemu za kuingizia hewa ya kutosha (adequate ventilation system)?

  Hivi ni nani aliyesema kuwa zile ‘air conditioners (AC)’ zinafanya kazi nzuri ya kuzungusha hewa ndani ya ukumbi? AC zinaweza kuwa ni nzuri kwa kupunguza joto (cooling) lakini peke yake haziwezi kupatia kundi la watu wengi hewa mpya ya oksijeni.

  Nitawaachia wataalamu wakosoe kama kufunga madirisha yote na kujaza watu ndani ya ukumbi na kutumia AC kunaweza kutosheleza mahitaji ya hewa ndani ya ukumbi.

  Mara nyingi ili kuwa na mtiririko mzuri wa hewa na kupunguza joto, mbinu mbalimbali zinatumiwa kwa pamoja.

  Sijui kama NSSF Tabora walifanya hivyo kwenye huo ukumbi, labda uchunguzi utaonyesha ingawa kutokana na timu yenyewe iliyoundwa sijui kama ni uchunguzi huru (nilishapinga kwa mkuu wa mkoa ambaye ameonyesha uzembe kuachwa aunde tume nyingine yeye!).

  Hivyo hilo la kutumia vifaa vinavyoweza kugundua uwepo wa hewa ya carbondioxide kwenye mabweni, kumbi na maofisi lifanywe kuwa ni jambo la lazima.

  Kama Bunge lingetoa msamaha wa kodi wa uingizaji wa vifaa hivi na kuhakikisha kuwa bei yake inakuwa ni rahisi, basi watu wengi wangeweza kuzitumia na kuweka kwenye nyumba zao, maofisi, mashule na kwingineko, hivyo kuwa kinga ya kwanza dhidi ya moto na sumu ya carbondioxide.

  Jambo la pili ambalo nililisema kwenye makala ile na hapa ninalirudia vilivyo kuwa itakuwa ni juhudi ya kweli ya kuenzi kumbukumbu ya watoto hawa ni kuwa: “Katika mabadiliko ya sheria ambayo naweza kutolea maoni ni haja ya kuhakikisha vitu vichache vinafanyika ndani ya miaka miwili katika shule, vyuo na majengo yote ambayo yanatumiwa na zaidi ya watu 20 au 30 kwa wakati mmoja.

  La kwanza ni kuhakikisha kuwa milango yote inafunguka kuelekea nje. Ni makazi ya watu ambayo yaweza kuwa na milango inayofungukia ndani lakini maeneo ya kazi, mabweni au madarasa yote yatakiwe kufungukia nje.

  Ninasema hivi kwa sababu madhara ya mlango kufungikia ndani yanaonekana pale watu wanapojaribu kukimbia hatari kwenda nje, kwani inabidi ‘wauvute mlango ndani’ kwanza ili waweze kwenda nje na wakijazana mlangoni nani atakubali kurudi hatua moja nyuma ili mlango ufunguke wakati moto uko nyuma yao?”

  Hili tunaweza kulifanya kama tukitaka. Nilipendekeza kuwa “Hili tunaweza kulifanya kwa kutoa kodi (kama bado ipo kwenye vifaa kama hivyo) ili kufanya upatikanaji wake uwe rahisi na wa bei nafuu.

  Siyo kuondoa kodi kwenye vifaa hivi (vya dharura ya moto), bali kwenye vitasa vya milango ya kusukuma, ambayo inafungukia nje ili ndani ya miaka miwili shule, ofisi na majengo yote ya hadhara yabadilishe milango yao”.

  Haya mawili hatuhitaji kuunda tume kuyagundua au kuyatambua umuhimu wake. Haya mawili ya (ya vifaa na vitasa) hayahitaji ‘Wazungu’ waje kutuambia ndiyo tuone umuhimu wake. Mara mbili sasa tumeshalipia gharama kubwa.

  Shauritanga kama kungekuwa na hivyo vifaa na kama milango ingekuwa inafungukia nje wale watoto wasingelazimika kuuvuta mlango ndani ili watoke nje, wangeweza kuusukuma na kuufungua.

  Milango hiyo unaweza kutia komeo lake ndani na mtu aliye nje asiweze kufungua lakini wewe uliye ndani huhitaji hata funguo unasukuma na mlango unafunguka. Tumelipia Tabora sasa kwa sababu hiyo hiyo.

  Lakini la mwisho katika kuenzi kumbukumbu ya watoto hawa ni kutaka sheria au taratibu kuwa kama kuna ukumbi wowote uliopo ghorofani, lazima uwe na njia zaidi ya moja ya kutokea na lazima iwe inayoweza kutumika (accessible).

  Huwezi kuwa na mlango mmoja kwenye jengo kama hilo na inapotokea dharura watu wote wajaribu kutokea kwenye mlango huo huo mmoja.

  Ndiyo maana hapa narudi tena kwenye NSSF walipokubali jengo lao litumiwe kama ukumbi wa disko, walihakikisha kuwa kuna mlango zaidi ya mmoja kutoka ghorofani baada ya kuziba madirisha yote?

  Hivi walipokubali ukumbi huo utumike wakati mlango (ngazi ni moja) walitarajia nini kama ikitokea dharura? Kwamba watu wataitwa wapange mstari mmoja mmoja na watoke taratibu kama chipukizi?

  Ndugu zangu, tunaposema viongozi hawa wawajibishwe si kwa sababu ya chuki kama wengine wanavyotaka tuamini. Kuanzia tukio hilo litokee nimepata vitisho vingi sana na mojawapo ni kutoka kwa mtu ambaye yuko karibu sana na uongozi wa NSSF.

  Baadhi ya vitisho hivyo ni kunishtumu udini kuwa namuandama Dk. Dau (hasa baada ya kumpinga tena kwenye suala la THI, shirika lake lilipoamuru wagonjwa kuondolewa kwa nguvu bila amri ya mahakama kama ilivyothibitishwa na Mahakama ya Rufaa).

  Watu hao wanaopenda kutoa vitisho wanataka watu waogope kuinyoshea kidole NSSF kwa sababu wataonekana wadini au wana chuki binafsi.

  Msimamo wangu uko pale pale; katika Tanzania ya leo hakuna tena miti mitakatifu na hakuna mtu yeyote ambaye anapaswa kuogopwa au kuhofiwa kwa sababu watu wanafikiria ana uwezo wa kuamuru mbingu na nchi.

  Kama niliweza kupigia kelele kina Lowassa, Hosea na kama tumeweza kumnyoshea kidole hata rais wa Jamhuri yetu pale ambapo tumetokea kuamini kuwa yuko kombo, basi watu wajue kuwa ile hofu ya viongozi haipo tena.

  Tutawaheshimu, tutawaenzi na kuwathamini. Lakini wanapoboronga wasitarajie wananchi watageuza shingo zao kwa aibu na kuinama chini kwa haya. Walitaka uongozi, tumewapa na wao watawajibika kwetu. Vinginevyo wasuse kama alivyosusa jamaa fulani.

  Wale ambao wanatoa vitisho vyao aidha kwa kutumia makuwadi wa ufisadi na rafiki zao ili tusiwanyoshee vidole vya kuwajibika wanafanya makosa.

  Kwani kama nilivyosema katika makala yangu Aprili ninarudia tena bila hofu wala kugwaya mbele ya mwanadamu mwingine yeyote awaye ambaye naye hufa, huoza na kuliwa na funza ‘taifa lisilojiandaa kwa majanga, limejiandaa kwa maafa.’

  Kama hatutaamua kubadilika sasa kabla ya majanga makubwa mbeleni, tusianze kulia kilio cha mbwa pale ambapo tutajikuta tunapata majanga mengine ambayo tungeweza kupunguza ukatili wake na watu watakapoanza kutoa udhuru wa kwa nini wasibebe lawama.

  Kabla ya kujenga mnara wa kumbukumbu, tukumbuke kilichotokea Tabora na tuchukizwe na tuhakikishe kuwa watoto wetu hawajikuti tena kwenye jambo kama hilo.

  Mnara wa kweli, ni kuwajibika. Niseme tena: “Tunapofikia ufisadi hadi kwenye maisha ya watu, si tu tunakuwa ni malaika wa ufisadi, bali tunakuwa ni washirika wa shetani!

  Na kwa wanaotaka tutetemeke mbele zao, ujumbe wangu ni mwepesi; tutaendelea kupaza sauti zetu na kupiga kelele mpaka masikio yao yaliyoziba yafunguke, mpaka ulevi wa ugimbi wao wa madaraka utakapowatoka na mpaka pale watakapoamka kutoka kwenye viti vyao vya uvivu.

  Mpaka pale tutakapoweza kusimika katika ardhi yetu utawala wa kweli wa sheria, wa watu wanaowajibika na hatimaye kujenga kweli “Taifa la watu walio huru na sawa”.

  Mpaka siku hiyo, sauti zetu zitapaa kulikumbusha taifa wito wetu wa kujali utu. Na katika lengo hilo haogopwi mtu, hapendwi mtu na hapendelewi mtu, vyote vinazungumzika!

  mwanakijiji@jamiiforums.com
   
Loading...