Kujiuzulu hakulazimishwi wala kushauriwa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kujiuzulu hakulazimishwi wala kushauriwa

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kilimasera, Feb 26, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Feb 26, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  MILIPUKO ya mabomu kambi la Jeshi la Wananchi Gongo la Mboto ni moja ya matukio yaliyoshtua Watanzania na hata nchi jirani. Wenye machozi ya haraka mpaka sasa wanaendelea kulia.

  Yapo matukio yaliyowahi kushtua kwa mfano ya ajali kama zile za MV Bukoba iliyotokea mapema 1996, au ile ya Reli ya Kati huko Gulwe Dodoma ambako watu karibu 100 walifariki na hata la milipuko ya mabomu Mbagala iliyotokea mwaka jana, lakini tukio la Gongo la Mboto linasababisha maneno mengi kwa sababu kadhaa.

  Moja ni kutokana na ukweli kwamba kwa jinsi jeshi lilivyo makini, ni vigumu kuamini kwamba milipuko hiyo ilitokea kwa ajali.

  Pamoja na kwamba katika ajali zilizotangulia yalisemwa maneno, lakini hayakuwa mengi kama ya kipindi hiki cha milipuko ya Gongo la Mboto.

  Tukio hilo limesababisha maneno yenye kauli mbalimbali zikiwemo za kuliwaza, kusikitisha, kumshukuru Mwenyezi Mungu na zingine za kejeli dhidi ya baadhi ya watu. Tukio la Gongo la Mboto limeshtua Watanzania wote wakiwemo wanajeshi, raia, viongozi, na wananchi kwa ujumla.

  Sababu za kushtua ni tukio lenyewe kwamba linasababisha kiwewe kutoka na makombora kulipuka kwake kusiko na mwelekeo wa kutua.

  Lakini pia, Watanzania hususan wakazi wa Dar es Salaam walishaonja adha ya milipuko hiyo mwaka juzi iliyotokea Mbagala wilayani Temeke.

  Hivyo tukio la sasa ambalo linaelezwa kuua watu zaidi ya 20 na kujeruhi wengine zaidi ya 300 lazima lichambuliwe kwa undani.

  Penye tukio hapakosi maneno. Kauli inayotawala sasa ni ya watu wa kawaida kutaka Waziri wa Ulinzi Dk Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange wajiuzulu.

  Waziri Mwinyi kwa upande wake amesisitiza waziwazi kwamba hawezi kujiuzulu. Hali kadhalika Mkuu wa Usalama na Utambuzi jeshini, Brigedia Jenerali Paul Mella aliwaambia waandishi wa habari kwamba Jeshi halina kitu kitwacho kujiuzulu.

  Kwa upande wa jeshi sitaki kujadili wala kuhoji kwani ni kweli kwamba wana utaratibu wao, hali kadhalika suala la watu kumtaka Waziri ajiuzulu kwa maoni yangu ni kauli tata na isiyo na maana.

  Neno kujiuzulu kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu toleo la pili, maana yake kuacha kazi kwa hiari walau kwa kuandika barua yenye kueleza nia hiyo.

  Kujiuzulu kwa kiongozi maana yake ni kujiondoa mwenyewe kwenye wadhifa fulani ikiwa no moja ya kuonyesha nia ya dhati ya kuguswa na tukio baya lililofanyika.

  Kiongozi anayejiuzulu kwa hiari yake mara nyingi wengi wanamuonea huruma kwa uamuzi wake kwani anawashtukiza na wengine wanakubaliana naye.

  Lakini pia kwa maoni yaongu kiongozi anayejiuzulu kwa mashinikizo kutoka kwa watu, ukweli mtu wa aina hiyo hajajiuzulu bali ametimuliwa na na midomo ya watu.

  Hata kama kiongozi kama Waziri atashauriwa na Rais ajiuzulu kwa uzembe wake, basi waziri huyo hana budi kutambua kwamba Rais ametumia busara tu ya kumfukuza kazi.

  Mtu anayejiuzulu anajivua wadhifa yeye mwenyewe kwanza na anakwenda kutoa taarifa kwa aliyempa kutokana na mambo yaliyotokea.

  Kujiuzulu hakutakiwi kushauriwa au kulazimishwa na mtu yeyote, bali ni hatua inayochukuliwa na mtu muungwana mwenye hisia za kuumia moyoni, mwenye huzuni pale anapowaona watu wengine wakiteseka kutokana na vitendo vilivyofanywa na watu wa chini yake kwa bahati mbaya au makusudi.

  Anayejiuzulu hashurutishwi, bali anaomba mwenyewe kwa aliyemteua.
  Anayejiuzulu anakuwa na moyo wa upendo wa dhati kwa wenzake, ni mwenye huruma ya hali ya juu na hapendi wenzake wapate taabu kwa uzembe.

  Kiongozi anayejiuzulu kwa nia ya kuwajibika bila ya kutakiwa na vyombo vya juu au vikundi vya watu atangaze hayo, ni mtu mwenye dalili za kuwa kiongozi bora, mwenye busara na ana uwezo wa kuwa mnkali kwa wazembe kama atakuwa mkuu .

  Hivyo pamoja na ukubwa wa tukio la Gongo la Mboto, jinsi lilivyomaliza maisha ya Watanzania na kuwahangaisha lakini upo uwezekano mkubwa kwamba halijagusa mioyo ya baadhi viongozi na kuwafanya waone huruma ya kutaka kujiuzulu wenyewe.

  Kwa hali hiyo siyo jambo la busara kuwalaumu au kutaka watu wajiuzulu kwa lazima.
  Lakini pia wapo wanaowalaumu wakazi wa Gongo la Mboto kwa kuamua kuishi karibu na kambi za jeshi. Kwa kweli hoja hiyo haifai kwani mabomu yaliweza kufika hata umbali wa zaidi ya kilometa 10 .

  Wengine wanataka makambi ya jeshi yaondoke mijini, eti yaende porini, jamani ukweli ni kwamba makambi yapo kwa malengo maalumu.

  Mpaka sasa nadiriki kusema kwamba maisha ya jeshi si popote, bali ijulikane wazi kwamba mahali wanapoonekana wanajeshi, basi ipo sababu maalumu ya kiusalama kwa nchi au taifa.

  Lakini pia wanajeshi ni Watanzania wenzetu kutoka kona zote za nchi. Wapo wanajeshi wanaotoka vijiji vya mikoa yote na wilaya zote zikiwemo za Biharamulo, Mbinga, Nkasi, Newala, Kisarawe, Kondoa, Iramba, Geita, Rombo, Mbulu, Chunya, Bunda, Kahama, Sikonge na Njombe, Kilombero, Handeni, Kinondoni na Sumbawanga.

  Wapo wanajeshi wengi kutoka mikoa yote ya Pemba na Unguja zikiwemo wilaya zote na vijiji vilivyoko Dole, Mkanyageni, na Micheweni, hivyo si busara wenzetu kuwaona kama wanastahili kuishi porini.

  Tanzania ni yetu sote wakiwemo viongozi wakuu, wa kati, wa kawaida na na hata raia, hivyo kuishi na wanajeshi ni kujihakikishia amani na ulinzi. Siyo jambo la busara kutoa kauli za kutaka kuwatenga. Lakini pia ikumbukwe wazi kwamba suala la kujiuzulu linatekelezwa na mtu muungwana.
   
Loading...