Kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha za serikali..!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,422
39,670
Binafsi tatizo nililonalo na bajeti hii si ukubwa, ufinyu, au utegemezi wa bajeti yenyewe!! Ukifikiri sana utaona kuwa licha ya fedha kuongezwa haina maana maisha ya mtanzania yataboreshwa!! Tatizo langu hasa ni juu ya matumizi ya fedha za serikali. Hivi sasa kila mwaka mabilioni ya fedha yanarudishwa hazina (mwisho wa mwaka wa fedha) kwa kutokutumiwa ipasavyo!! na pia pesa nyingi zinapotezwa kutokana nidhamu mbaya ya matumizi ya fedha (angalia taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali!). Binafsi nafikiri Bajeti yetu inaweza kuwa na matumaini endapo mambo kadhaa yatafanyika, miongoni mwao ni haya:

a. Sheria/utaratibu utungwe kulazimisha idara, wizara, na mawakala kuhakikisha kuwa fedha wanazopewa zinatumiwa katika mwaka ule wa fedha. Kushindwa kufanya hivyo, kutapunguza fedha kwa mwaka ujao!!!

b. Sheria ipitishwe inayotaka bajeti ya kila idara, wakala, na wizara lazima ilingane (balanced). Lengo la bajeti siyo tu kuonyesha matumizi ya serikali, bali mapato pia. Bajeti inapoandaliwa iwe na lengo la kulingana. Huwezi kutumia zaidi ya kipato chako!

c. Mawaziri wapewe ripoti kila ndani ya miezi mitatu juu ya mapato na matumizi ya wizara zao na wahakikishe kuwa mapato na matumizi yanalingana!! Kama mapato ni kidogo kuliko matumizi lakini fedha bado zinatumika kuna mahali mtu anakopa au kuiba!! Kama bajeti hailingani kuna tatizo mahali!! Hivi inakuwaje taifa lipoteze shilingi bilioni 140 na hakuna mtu anayegundua!!!

d. Mkaguzi Mkuu wa Serikali apewe nguvu ya kisheria ya kujenga kesi ambayo itaendeeshwa na mwanasheria Mkuu. Katika sheria hii iseme kuwa MMS anapotaja idara, wizara, wakata..n.k kuwa kuna ubadhilifu fulani wa fedha na maelezo ya viongozi wake hayaridhishi hivyo wanaadhimia kufungua mashtaka, basi kiongozi wa eneo hilo anasimamishwa (pending further investigation) na kama zaidi ya kiasi fulani cha fedha kiongozi huyu anajiuzulu automatically!

e. Kila idara, wizara, vitengo...n.k ni lazima viwe na mhasibu wa ndani mwenye shahada ya Uhasibu au Usimamizi wa Fedha, au Utawala wa Biashara (CPA, MBA). Idara yoyote ya serikali inayoshughulikia matumizi ya fedha (Accounting Office) isiongozwe na mtu yeyote asiye na shahada ya Uzamili au CPA. Kuna watanzania wengi ndani na nje ambao wako tayari kuchukua nafasi hizo!! Matumizi mazuri ya fedha yanatokana na nidhamu nzuri ya fedha!!

f. Kiongozi yeyote (nina maana yeyote!) asiyekuwa na maelezo ya kuridhisha ya matumizi ya fedha zilizo chini yake, fedha hizo zitakatwa kwenye mshahara wake kama kiasi kisichoelezeka hakizidi shilingi milioni tano. Na hiyo itaruhusiwa mara moja tu. Ikitokea tena, mtu huyo anajifukuzisha kazi!

g. Fedha zinazotelewa ni lazima zitumikwe kwa malengo yaliyopangiwa. Kiongozi anayetumia fedha za lengo fulani kutimiza lengo jingine bila idhini au kibali kinachostahili anajifukuzisha kazi! Kama kuna kitu kimetudumaza sana kimaendeleo ni mtindo wa fedha za elimu kwenda kwenye maji, fedha za afya kutumika kulipia mafuta, n.k Hili haliwezi kuendelea kuvumiliwa!! Miradi mingi haifanikiwi kwani fedha nyingi zinapelekwa zisikopangiwa!! Bajeti ni kupanga, na ndo maana tuna fedha za "Mengineyo" Lakini isiruhusiwe fedha zilizopangwa kwa matumizi fulani zitumike kwa matumizi mengine isipokuwa pale ambapo Kamati ya Fedha ya Bunge na Rais ameridhia!!

Basi tukijaribu kuyafanyia kazi mapendekezo hayo utaona kuwa tunajaribu kujenga utaratibu mzuri wa matumizi ya fedha za serikali na hivyo, hata kama bajeti ni kiduchu, basi inaweza kufanya vitu vingi kuliko kuwa na bajeti kubwa ya kuvuja utadhania pakacha la maembe!!!
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom