Kama kweli Chunya hawakuomba na hawaoni haja ya wao kujitenga na Mbeya basi ni bora wakajenga hoja ya wao kubaki mkoa wa Mbeya! Lakini nionavyo mimi wanafurahia wazo hilo na hata mimi ningefurahia kupewa hadhi hiyo!
Kuhusu wenzetu wa Rungwe ni kweli kama ulivyoeleza katika hoja yako kuwa ni wabaguzi, wakabila na wasiopenda kushirikiana au kuwasaidia wenzao kujikwamua katika lindi la umaskini! Tabia hii si ya leo au jana bali toka enzi za wakoloni! Wanyakyusa hawa wa milimani waliwabagua wenzao wa mabondeni na wakawabagua zaidi watu wa Ileje kiasi kwamba kuna baadhi ya wandali ambao kutokana na ubaguzi huo na kujiona wanyonge wakajibatiza kuwa wanyakyusa au wakabadili lugha yao ili kwa kiasi kikubwa ifanane na kinyakyusa!! Ajabu sana hii!!!
Kwa hiyo kama wenzetu hawa wa Rungwe bado wanang'ang'ania kutaka mkoa basi nashauri wapewe hadhi ya kuwa angalau mkoa mdogo au nusu ili wapate amani ya moyo!! Hii ni kwa sababu naelewa hoja yao ya kutaka kujitenga haijafutwa kabisa kwa kuwa hata katika mkoa huo wa Mbeya walikobakizwa bado wataendeleza hoja hiyo kupitia mlango wa nyuma!!
Umenena vema Ileje. Ni kweli kwamba lengo la uzi huu ambalo pengine halikutegemewa linaweza likawa haja ya kutumbua hiki kijipu cha kuusambaratisha mkoa wetu. Nani hasa mwanzilishi wa wazo hili? Lakini pia kuna faida gani tunapata katika kusambaratika huku. Je serikali imechukua hatua sahihi katika kushughulikia suala la kuusambaratisha mkoa?
Nikubaliane na wewe kwamba Chunya wamekosa miundo mbinu mingi kwa miaka mingi na kuleta shida kwa ndugu zetu Wabungu kuna wakati huwa napata wasiwasi kama wanajisikia ni wakazi wa Mkoa wetu. Nina mdogo wangu anaishi Chunya mjini kajenga kule. Sijawahi kuenda kule kumjulia hali kwa sababu tu ya shida ya usafiri. Lakini hilo la kusahaulika ni kweli kuhusu Ileje Pia. Nina biashara ambayo inanipa nafasi ya kujua kwamba wafanyabiashara wenzangu wanaokaa Chunya na Ileje wanalipia gharama kubwa sana kufadhili safari za mafundi kutoka Mbeya Mjini kwenda ama Chunya, ama Ileje. Fundi wa mashine akisikia neno Chunya, au Ileje, anajua hiyo ni kazi ya siku mbili hadi tatu, wakati ambapo anaweza kwenda Tunduma, Kyela Vwawa--au hata Makambako akafanyakazi na kurudi kulala nyumbani Mbeya.
Nirudi kwenye hoja: Rungwe wanataka kujitenga. Hilo limezaa Wazo la kuitenga Chunya, lakini pia limezaa wazo la Mbozi na Ileje kutaka kujitenga. Kwa mtizamo huo Rungwe wameleta utengano katika mkoa.
Serikali imefanya sawa katika lile ambalo imefanya? Kwa mara ya kwanza naomba niseme ndiyo. Serikali imekwepesha Rungwe ikiwa inajua hilo linaweza kuleta shida kati ya Kyela na Rungwe yenyewe huko mbele. Yanaweza kuzuka masuala ya Ruzuku za Serikali na mtawanyo wa maendeleo watu wakakatana mapanga na kuchomeana nyumba pale. Kwa hiyo dawa ni kuwabakiza hawa katika pool moja inaitwa Mkoa wa Mbeya. Serikali wamefanya sawa kuwanyima Rungwe Mkoa kwa sababu Mkoa huo ungelazimisha Kyela, na pengine Ileje kuwa ndani, na Rungwe wangewasumbua sana Kyela na Ileje kwa misimamo ya wazi na ya siri kuwa wao ndo haswa wakubwa, ambao waliomba mkoa na wakaupewa! Nadhani wewe pia umeafiki mtizamo wa serikali. Hapo tupo pamoja.
Kuhusu Chunya kutengwa ama kujitenga--kama wanataka--hili niseme lingejadiliwa na WanaChunya wenyewe waangalie kama kuna faida kwenye lipi: Pesa za kuugawa mkoa ziboreshe miundombinu Chunya na Ileje hasa, ama pesa hizo zipewa makandarasi wa kujenga majengo ya makao makuu ya Mkoa wa Chunya ili watu wa Ileje wabaki na miundo mbinu mibovu kama ilivyo sasa na kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata makao makuu Chunya.
Binafsi nadhani kitu sahihi ni kuboresha miundombinu kwenye haya maeneo mawili: Hivi Tukiwa na Lami safi kati ya Mbeya Mjini na Chunya Mjini, halafu tukaweka Lami safi kati ya Mbeya mjini na Ileje--hasa kupitia njia mkato inayoanzia Njia panda ya Iyula, kuelekea Idiwili , kupitia Hezya hadi Itumba. Huoni kama Mbeya mjini patafikika kirahisi sana kati kwa kila mtu? Ujue kwa kuweka lami safi kwenye maeneo ambayo nimeyataja, Mtu aliyepo Chunya na Aliyepo Itumba watafika pengine wakati huohuo Mbeya Mjini na mtu ambaye anatakoka Kyela.
Wakati huo huo uboreshaji wa miundombinu--hasa hasa barabara utakuwa na faidi nyingi za ziada ukiachana na hili la kufikika kwa urahisi makao makuu ya mkoa. Wagonjwa watafika Rufaa haraka, wahalifu wa jinai kubwa watafika haraka mahakama kuu Mbeya mjini. Huduma chake zinazolazimika kufanyika mkoani kwa kuwa haziwezekani wilayani zitafuatwa na kufikika kwa urahisi Mbeya mjini.
Mimi kwa kweli nadhani kitu sahihi ni kuboresha miundo mbinu badala yakuongeza gharama za kuendesha serikali kule Mbeya. Kama kuna mtu ana pesa zinamuwasha kujenga majengo na kuajiri rundo la watu Mkwajuni nashauri ajenge lami kwenda Chunya na Ileje na hizo hela.